Rais wa Rwanda, Paul Kagame (kushoto) akitembea pamoja na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza (katikati) na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete (kulia) Walipowasili kwenye Mkutano wa 14 wa EAC wa Viongozi wa Mataifa ya Ushirikiano huo jijini Nairobi, Novemba 30, 2012
Katika siku za hivi karibuni hali ya wasiwasi imeibuka kuhusu uimara na mshikamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Tanzania na Burundi, nchi mbili kati ya nchi tano wanachama wa jumuiya hiyo, zimetoa malalamiko kuwa zinatengwa na nchi wenzake wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kenya, Uganda na Rwanda, hasa baada ya marais wa Kenya, Uganda na Rwanda kukutana mara mbili kwenye mikutano iliyobeba jina la jumuiya.
Wa kwanza ni ule wa Entebbe tarehe 24 na 25 Juni, ambapo marais Uhuru Kenyatta, Yoweri Museveni na Paul Kagame mbali na mambo mengine walifikia makubaliano ya kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa Kenya, kupitia Kampala Uganda hadi Kigali Rwanda. Mwingine ni ule wa tarehe 28 Agosti marais hao watatu walikutana mjini Mombasa nchini Kenya kuendelea na ufuatiliaji wa yale waliyokubaliana mjini Entebbe. Hali hii imeleta maswali kuhusu uimara wa jumuiya ya Afrika, mshikamano kati ya nchi wanachama, mwelekeo wa jumuiya hiyo, na hata kuonesha dosari zilizopo ndani ya jumuiya hiyo zinazotakiwa kushughulikiwa.
Ili tufahamu vizuri undani wa kinachotokea sasa, ni vizuri tukiangalia hali halisi ya kiuchumi katika nchi za jumuiya hiyo, na tuelewe ni kwanini mikutano kadhaa imefanyika bila Tanzania na Burundi kualikwa. Kwanza ni vema tukitambua wazi kuwa, kwa sasa Kenya ni nchi yenye uchumi imara zaidi kati ya nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika na uchumi wake wa soko umekomaa zaidi kuliko ule wa Tanzania. Kukomaa kwa mfumo wa soko kunahitaji milango ya jumuiya iwe wazi zaidi, ili uchumi inufaike na fursa zinazotokana na matunda ya soko la jumuiya. Kwa Kenya mikutano mwili iliyofanyika bila kuwahusisha marais wa Tanzania na Burundi, kimsingi inalenga hilo. Bila shaka Uganda na Rwanda pia zinajua kuwa zitanufaika, kwa hiyo kimsingi nazo pia zina maslahi ya kiuchumi.
Lakini tukiangalia kwa upande wa Tanzania, ambayo uchumi wake unachukua nafasi ya pili katika jumuiya ambao kwa kiasi fulani unaanza kuonekana kutishia nafasi ya ule wa Kenya, hatua ya Kenya kuamua kwa ghafla kujenga reli kutoka Mombasa kupitia Kampala hadi Kigali, ni jaribio la kujihami kutokana na ushindani utakaoletwa na bandari ya kisasa inayojengwa Bagamoyo. Sio siri kuwa, kama bandari ya Bagamoyo ikikamilika na kuendeshwa kitaalamu bila “uswahili” kama ilivyo kwa bandari ya sasa ya Dar es salaam, bandari ya Mombasa itachukua nafasi ya pili katika jumuiya. Hali hiyo itakuwa ndoto ya jinamizi kwa Kenya, kwa hiyo kwa kutumia jicho la hatua za kujihami, hatua ya Kenya kwa upande fulani inaeleweka.
Hata hivyo, tukiangalia nyuma zaidi tunaweza pia kuona kuwa siku zote uhusiano kwenye mambo ya uchumi kati ya Kenya na Tanzania umekuwa ni mwongozo wa maendeleo ya jumuiya ya Afrika Mashariki, na vizuri tukiwa wakweli kuwa mambo hayo ndio yatakayoimarisha na ndio yaliyoivunja jumuiya. Kama uhusiano kati ya nchi hizo mbili kiuchumi unaendelea vizuri, basi kwa ujumla mambo ya jumuiya yataendelea vizuri, na kama kukiwa na mivutano kati ya nchi hizo mbili kiuchumi, basi jumuiya pia inatetereka. Kwa sasa hakuna haja ya kuwa na wasiwasi kama ilivyokuwa mwaka 1967, wakati jumuiya ilikuwa ni mali ya serikali na marais wa nchi, na uhai wake kutegemea zaidi nia yao, kwa sasa jumuiya ni mali ya watu, na hasa kwa wakenya na watanzania ambao wamekuwa na maingiliano makubwa.
Tanzania imekuwa inashiriki kwenye jumuiya ya Afrika Mashariki kwa jicho la tahadhari kubwa. Kila mara inatafakari kwa makini na hata kuchelewa kusaini au kupitisha mikataba ya ushirikiano, kama inahisi kuwa hatua hiyo italeta matata kwa maslahi ya nchi na wananchi wake. Na uzuri ni kuwa kwa sasa Tanzania ina mibadala mingi ya uchumi, kwa hiyo haiko kwenye mkao wa kuburutwa. Katika miaka iliyopita Kenya imekuwa ikilalamika mara kwa mara kuwa Tanzania inachelewesha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa nchi wanachama, na Tanzania imekuwa ikitoa maelezo mengi ya hali hiyo na kufikia hata kutosaini baadhi ya vipengele vya ushirikiano, kwa kusema inahitaji muda wa kujiandaa na kuwa na uwezo wa kushiriki kwenye vipengele hivyo. Chelewa chelewa hii ya Tanzania imewafanya wajumbe wengine waone kuwa Tanzania inawachelewesha, ndio maana wamekosa uvumilivu na kuamua kutangulia.
Tofauti za kiuchumi kati ya nchi wanachama, ilikuwa ni moja ya sababu kubwa zilizochangia kufa kwa Jumuiya ya Afrika ya kwanza mwaka 1967. Kimsingi muundo wa uchumi wa nchi za Afrika Mashariki bado haujabadilika sana, kwa hiyo changamoto zilizosababisha jumuiya ya kwanza kufa [Kenya kupiga hatua zaidi kiviwanda vingi na kunufaika zaidi na soko la jumuiya kuliko nchi nyingine, watu wake kuwa na viwango vya juu vya elimu na mafunzo ya kazi kuliko wa nchi nyingine na kunufaika zaidi na soko la ajira, na kutokana na msingi mzuri wa uchumi inapata vitega uchumi vingi kutoka nje kwa kutumia jina la jumuiya kuliko nchi nyingine wanachama, na kutokana na kukusanya mitaji mingi ya ndani inaweza hata kuwekeza katika nchi wanachama], kama hazitashughulikiwa kwa makini huenda zitaendelea kuwa changamoto kubwa kwa jumuiya ya sasa.
Kumekuwa na hali fulani ya kujidanganya kwa sisi watanzania na kwa kudanganywa na wakusanya takwimu za uchumi wa jumuiya kutoka Kenya, kuwa na sisi watanzania sasa tunanufaika na soko la jumuiya kwa kuwa exports zetu zinazokwenda kwenye soko la jumuiya zimeongezeka. Pamoja na kuwa kuna ka-ukweli fulani kwenye takwimu hizo, kimsingi bado Tanzania ni soko la Kenya, kwa mitaji, bidhaa na hata nguvu kazi, na mitaji, bidhaa na nguvu kazi kutoka Tanzania ni kama havionekani nchini Kenya. Kwa hali yoyote ile hali hii haikubaliki na hii si maana ya jumuiya, au sio lengo la jumuiya. Na kama hali hii ikiendelea kwa muda mrefu bila shaka kwa Tanzania jumuiya haitakuwa na maana iliyotarajiwa.
Huna haja ya kuwa Profesa wa uchumi kujua ni vipi Kenya inanufaika na raslimali za Tanzania au za Jumuiya kwa ujumla, na vipi Tanzania inajikongoja au kuinufaisha zaidi jumuiya kuliko kunufaika yenyewe. Katika mkoa wowote, wilaya yoyote na mji wowote wa Tanzania, ukienda supamaketi, dukani, kwenye kioski na hata kwa mama ntilie, huwezi kukosa bidhaa za Kenya. Kuanzia chumvi, mafuta, sabuni, dawa, vyombo vya usafi na vyombo vya kupikia nk, vingi vinatoka Kenya. Ukivuka mpaka na kuingia Kenya huwezi kuona bidhaa yoyote kutoka Tanzania, kama ukiipata labda utapata sigara au pombe, vilivyoingia kwenye sehemu za mpakani za Kenya kwa njia za panya.
Hata hivyo kuna mambo mapya yaliyotokeza kabla ya jumuiya mpya kuanzishwa yanayoifanya Kenya isiwe na furaha, ambayo yanaitaka ifanye juhudi zaidi ya kupanua wigo wake wa ushirikiano ili inufaike zaidi na soko la Jumuiya. Mwaka 2000 wakati jumuiya mpya ya Afrika Mashariki inafufuliwa, Tanzania ilikuwa kwenye jumuiya nyingine ya uchumi (jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC), uanachama wa Tanzania kwenye jumuiya ya SADC hauifurahishi Kenya na mara kwa mara Kenya imekuwa ikiishawishi Tanzania ijitoe SADC. Uanachama Tanzania kwa SADC umeifanya Tanzania iwe wazi kwa bidhaa kutoka Afrika, hali hii inafanya viwanda vya Kenya vikabiliwe na changamoto kubwa zaidi. Hali hii pia inaihimiza Kenya kuchukua hatua za kuhakikisha inakuwa na nguvu ya ushindani kwenye soko la Afrika Mashariki.
Kwenye upande wa siasa, kwa sasa hali kwa ujumla ni nzuri. Nchi zote wanachama zinatambua kuwa jumuiya ni muhimu kwao, na kauli zinazotolewa na pande zote licha ya kuonesha hasira na kejeli. Watanzania na wakenya, wanajua kuwa marais wao wa sasa wataondoka madarakani baada ya vipindi vyao vya miaka 10 kumalizika, kwa hiyo wanachoangalia ni vipi jumuiya iendelee kama taasisi, na sio kama gari linalotegemea watu wawili. Ndio maana msemaji wa Ikulu ya Tanzania hivi karibuni alinukuliwa akisema Tanzania haina wazo la kujitoa kwenye jumuiya hiyo.
Hata hivyo jinamizi la tofauti binafsi kati ya waliokuwa marais wa nchi wanachama wa jumuiya ya kwanza (Jomo Kenyatta, Idd Amini na Julius Nyerere) zilichangia sana kuifanya jumuiya ivunjike. Na sasa kuna tofauti za wazi kabisa kati ya Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete na Rais wa Rwanda Paul Kagame, hasa baada ya Rais wa Tanzania kuishauri Rwanda kufanya mazungumzo na waasi wa kundi la FDLR walioko nchini DRC wanaoipinga serikali ya nchi hiyo, na Rais wa Rwanda kukataa kufanya mazungumzo na waasi wa kundi la FLDR. Tofauti hizo zilianza kujionesha kwenye mambo ya uchumi, baada ya Rwanda kuamua kuyatoza ushuru mkubwa malori yanayoingia katika nchi hiyo kutoka Tanzania, na baadaye kuacha kutumia bandari ya Tanzania na kuanza kutumia bandari ya Mombasa. Jambo hili ambalo nchi tatu waanzilishi wa jumuiya zilisema halitatokea tena, sasa linaonekana kuleta kivuli cha yaliyotokea mwaka 1967.
Mbali na changamoto kubwa ya uchumi na tofauti za kisiasa, tatizo kubwa linaloisumbua jumuiya kwa sasa ni kuwa imefikia kwenye hatua ya utekelezaji wa vipengele ambavyo ni changamoto kubwa kwa maslahi makuu ya nchi (prerogatives of states). Pamoja na kuwa viongozi wa nchi za Afrika Mashariki wanajua kuwa siasa za umoja na ushirikiano ni nzuri na zina manufaa, ukweli ni kwamba umoja na ushirikiano ukihimizwa kwa kasi unakuwa na madhara ya muda mfupi ambayo baadhi ya watu hasa wale wasiojua undani wake hawakutarajia. Matokeo yake ni kuwa wakati wa kupiga hatua za utekelezaji wa mambo ya kuelekea shirikisho la kisiasa, baadhi wanaanza kushtuka na kusema, kama Jumuiya ina maana kuwa hatutapata import tax toka kwa nchi inayouza bidhaa nyingi Tanzania basi kuna dosari, kama jumuiya ina maana matajiri kutoka nchi nyingine ya jumuiya watakuja kuvamia ardhi yetu kwa kisingizio cha jumuiya basi kuna dosari, kama jumuiya ina maana watu kutoka nchi nyingine watakuja kuchukua ajira zetu na sisi hatuwezi kupata ajira kwao basi hatutaki, kama jumuiya ina maana jina la nchi yetu litatumiwa kuomba fedha kwa ajili ya miradi ya kuzinufaisha nchi nyingine basi hatutaki, kama jumuiya ina maana wahalifu kutoka nchi moja wataingia kwa urahisi katika nchi nyingine basi ni tatizo, kama jumuiya ina maana kuna wakati tutakuwa na wanachama ambao tuna tofauti za kisiasa, basi haifai.
Haya ni mambo ambayo yalitokea na bado yanatokea hata kwenye jumuiya kubwa kama Umoja wa Ulaya na hata shirikisho la Marekani, kwa hiyo ni mambo ambayo yalitakiwa kuzingatiwa na kupatiwa majibu kabla ya kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini inaonekana kuwa hadi sasa baadhi ya watu hawajui, ndio maana sauti za manung’uniko zimeanza kusikika. Labda tunaweza kusema tuliingia kwenye jumuiya kutokana na kushawishiwa, kuiga mkumbo lakini sio baada ya kutafakari kwa makini na kuangalia pande zote za shilingi.
Ukweli ni kuwa, kutokana na kutojiandaa vya kutosha changamoto hizo zitaendelea kuwepo na zitazidi kuwa kubwa kadiri maingiliano ya kiuchumi yanavyozidi kuongezeka. Lakini ikilinganishwa na manufaa ya kiuchumi kwa nchi zote wanachama, bado jumuiya ni muhimu sana kuliko changamoto hizo zinazoweza kuondolewa moja baada ya moja na hatua baada ya hatua. Pamoja na kuwa rais Jakaya Kikwete alisema bungeni kuwa Tanzania haifikirii kujitoa, kauli za kutishia kujitoa kwenye jumuiya zilizotolewa na baadhi ya wanasiasa ni dalili ya woga, kutokuwa wawajibikaji na kukwepa ukweli.
Pia ni kuchafua sura ya Tanzania na hata sifa ndogo ya Tanzania iliyobaki kwa sasa, na kuonekana kuwa sisi ni “quitters” na sio “fighters”. Tanzania inatakiwa ipigane ndani ya jumuiya, na kuifanya iwe mwanachama wa kweli. Wanasiasa wetu wafanye kazi ya kujenga uchumi wenye nguvu ya kushindana, wafanye kazi ya kuweka yanayohitajika ili Tanzania iweze kuwa mwanachama wa kweli.
Kibaya zaidi ni pale unaposikia kauli kuwa kama kutakuwa na haja ya kujitoa swala hili litajadiliwa na wabunge. Tatizo ni kuwa mwamko, uelewa na elimu kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa watanzania bado viko chini sana. Kila mara nikipata bahati ya kuongea na wakenya wa kawaida na watanzania wa kawaida kuhusu jumuiya, ninachogundua ni kuwa wakenya wengi hata wale wa mitaani wenye elimu ndogo kabisa, wana mwamko mkubwa kuhusu jumuiya ya Afrika mashariki na wanajua ni vipi jumuiya itawanufaisha, na wanaiunga mkono serikali yao kwa hatua inazochukua kuhusu jumuiya.
Wanaelewa maana ya soko huria (duty free trade on member states) na maana yake kiuchumi kwa uchumi wa nchi yao, hata ukiwauliza maana ya rules of origin na manufaa yake kwa Kenya wanaweza kukueleza ni nini, kwa ujumla unaweza kuona hata wana uchangamfu (enthusiasm) na jumuiya. Lakini ukiwauliza watanzania walio wengi (bahati mbaya sana hata baadhi ya tuliowachagua kuwa wawakilishi wetu, na wale walioteuliwa kuongoza idara mbalimbali) hawajui jumuiya ya Afrika Mashariki ni nini zaidi ya kujua jina.
Hawajui inaweza kuwa na hatari gani na manufaa gani kwa usalama wa kiuchumi wa Tanzania, wengine hata hawajui kama wanaiunga mkono serikali au kuipinga inapofanya maamuzi kuhusu jumuiya ya Afrika Mashariki, na wengine wanafanya hivyo kwa ushabiki tu. Kwa hiyo wakati tunafufua jumuiya tukawa tunasikia tu hiki kimepitishwa kile kimepitishwa, na tumekuwa ndani ya jumuiya. Lakini kilichokuwa kinaonekana wazi ni kuwa, hata wanasiasa wetu waliokuwa wanashiriki kwenye vikao, ni kama walikuwa wanalazimika kuridhia, lakini economic realities za Tanzania zilikuwa zinawasuta.
Lakini jambo la muhimu ambalo sisi watanzania tunatakiwa kujiangalia na kulipatia ufumbuzi, ni “uswahili” na siasa za “uswahili”. Siasa za uswahili zinaendelea kuitafuna nchi yetu, na ushahidi upo kwenye taasisi, idara, makampuni, familia, vikundi na vyama na mashirika mengi tunayoyaendesha. Pamoja na kuwa tunatumia maneno “urasimu” na “ukiritimba”, lakini kikubwa zaidi ya hayo ni “uswahili” na “ushkaji”.
Inaweza kuonekana kuwa hatuna tafsiri sahihi ya maneno “uswahili” na “ushkaji”, na hakuna utafiti uliofanyika hadi sasa kuhusu mambo haya na madhara yake kwa siasa, uchumi na jamii ya Tanzania, lakini watanzania wengine wanaofuatilia uongozi na uendeshaji wa taasisi zetu hapa Tanzania wanajua mambo haya ni nini. Kwa sasa elimu, uzoefu, ujuzi, uchapaji kazi, sio tena misingi wa uongozi Tanzania, badala yake mambo ambayo kwa ujumla wake tunaweza kuyaita uswahili ndio yanatawala mambo hapa Tanzania. Kwa wakenya kukataa uswahili, si jambo baya, sidhani kama ni busara kwa wao kukumbatia hasa kutokana na kuona jinsi unavyoitafuna Tanzania.
CHANZO: FIKRA PEVU
No comments:
Post a Comment