Kashfa imeikumba
Hospitali ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kutokana na tuhuma za mmoja
wa wauguzi wake kumuuzia dawa 'feki' mgonjwa ambaye anaendelea kupatiwa
matibabu katika taasisi hiyo ya Serikali.
Mtumishi wa ORCI katika kitengo cha
dawa, Almasi Matola anatuhumiwa kudai fedha kwa mmoja wa wagonjwa wa
satarani (jina tunalihifadhi kwa sasa), lakini akampa dawa feki baada ya
kupewa fedha.
Mgonjwa huyo alipewa rufaa kwenda
Ocean Road Novemba mwaka jana akitokea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
baada ya kubainika kwamba alikuwa na saratani ya titi.
Baada ya kufika ORCI, ilibainika
kwamba mgonjwa huyo alikuwa akihitaji tiba ya kuua vijidudu vya saratani
inayojulikana kitaalamu kwa jina la chemotherapy au chemo kwa kifupi na
ndipo alipokutana na Matola.
"Huyu Almasi (Matola) alisema
anahitaji apewe fedha za dawa moja kwa moja kupitia akaunti yake ya NMB
yenye namba zinazoanzia 206016024** (namba mbili za mwisho tumehifadhi),
ambako tuliweka kiasi cha Sh340,000," alisema mgonjwa huyo.
Almasi alikiri kuwekewa fedha katika akaunti yake, lakini akakanusha kuomba fedha hizo kama ujira wa kumpa mgonjwa huyo dawa.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
"Huyo mgonjwa unayemsema ninamkumbuka
ijapokuwa jina lake limenitoka. Lakini ni kweli sijawahi kuonana naye
uso kwa uso isipokuwa nilikuwa nawasiliana naye kupitia kwa mfanyakazi
mwenzangu ambaye ni ndugu yake. Huyo ndiye alikuja kwangu na kutaka
nimsaidie ndugu yake," alisema Matola.
Kwa mujibu wa taratibu za OCRI,
wagonjwa wanaokwenda hospitalini hapo kwa rufaa kutoka hospitali
nyingine hawapaswi kutozwa fedha zozote kwa ajili ya matibabu.
Mmoja wa madaktari wa OCRI, Dk Steven
Shadrack alisema utaratibu wa wagonjwa wengi waliogundulika na saratani,
kwa kawaida hutokea Muhimbili ambako huwa wamefanyiwa uchunguzi.
Dk Shadrack alisema mgonjwa anapopewa
rufaa kwenda OCRI, hatakiwi kulipia hata senti tano na kama kuna kifaa
kilichoharibika ndipo hutakiwa kupimwa nje ya hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa madaktari, mgonjwa wa
saratani anayehitaji tiba ya chemo, hutakiwa kupewa dozi hiyo kulingana
na hatua ya saratani na aina ya dawa aliyoandikiwa.
Ilikuwaje
Mgonjwa huyo alisema Matola alimwambia
kuwa tiba yake inahitaji dozi sita za dawa ambazo gharama yake ni zaidi
ya Sh2 milioni kwa maana kwamba kila dozi inagharimu Sh340,000.
Alisema kabla ya kuanza kupewa tiba,
alielekezwa atoe damu kwanza, ambayo ingepimwa na majibu kutoka siku
inayofuata, hivyo angeanza kupewa tiba siku ya tatu.
"Siku ya kwanza ilikuwa Novemba 3,
2013 nilipotolewa damu na nikaenda siku ya tatu kupewa tiba ya chemo,"
alisema mgonjwa huyo. Alisema alipokwenda kwa ajili ya kupewa dozi ya
pili, Matola alimchukua damu na hapohapo akamwekea dripu ya dawa.
Alisema licha ya kupewa tiba hiyo,
alikuwa akisikia maumivu makali kwenye titi lililoathirika huku sehemu
ya uvimbe ikitoka damu na maji kwa wingi na uvimbe huo ambao ulikuwa
mdogo, uliendelea kusambaa kuelekea mabegani, chini ya kwapa hadi kwenye
tumbo. "Nilikuwa kwenye maumivu makali sana. Halafu, ndani ya dakika
10, nguo yangu ilikuwa inalowa kwa maji kutoka kwenye titi," alisema
mgonjwa huyo.
Katika awamu ya pili na ya tatu ya
tiba, mgonjwa alisema alikuwa akimpatia Matola mkononi Sh340,000 kwa
kila awamu na kwamba alikuwa akiweka fedha hizo mfukoni, taarifa ambazo
hata hivyo, Matola alizikanusha.
Wasiwasi wa tiba
Kwa maelezo ya Dk Shadrack, kwa kawaida dawa za saratani hasa chemotherapy zina madhara mbalimbali kwa watumiaji wake.
"Kwa mfano, mgonjwa baada ya kupata
chemo, anaweza kuharisha, kutapika, damu kupungua na wakati mwingine
kupata kizunguzungu," alisema Dk Steven na kwamba dalili kubwa kwa
wanaopata tiba hiyo huwa ni nywele kunyonyoka.
Lakini, licha ya mgonjwa huyo kupewa dozi tatu za chemo, hakuwahi kupata athari zozote kama hizo.
Mgonjwa huyo alisema ulipofi ka awamu
ya nne ya kupewa dawa hiyo Januari 15 mwaka huu, alimwambia Matola
kwamba hali yake inazidi kuwa mbaya hivyo alitaka kwenda kwa daktari
bingwa, lakini alimkataza akisema hiyo ni hali ya kawaida tu.
"Baada ya kuniambia hivyo alisema kwa
dozi ya nne na kuendelea atanipunguzia bei ya dawa na sasa nitakuwa
nikilipa Sh320,000 kwa dozi na kama kawaida nilimkabidhi na akaziweka
mfukoni kwake."
Alisema alikwenda kwa daktari bingwa,
Dk Dominista Kombe na kumwelezea hali yake. "Ni kama alishtuka hivi na
alisema inashangaza kama nilikuwa nimepata dozi nne lakini nywele zangu
zilikuwa hazijanyonyoka," alisema
Alisema daktari huyo alionekana kushangazwa na kiasi kikubwa cha fedha alizokuwa akitozwa na kumwagiza amwite Matola.
"Wakati tukielekea kwa daktari, Matola
alikuwa akilalamika kwamba 'nimeshaharibu mambo'. Hata hivyo,
sikuruhusiwa kuwepo wakati wa mazungumzo kati ya daktari na Matola,"
alisema.
Alisema baadaye Dk Kombe alimwambia ni vyema aanze tiba upya kwani dawa alizopewa ni feki.
Daktari huyo alimwandikia dawa nyingine na kumwelekeza aende katika duka la dawa ambako alizinunua kwa Sh26,000.
Alisema baada ya dozi ya kwanza tu,
aliona dalili zote za kufanya kazi kwa tiba hiyo ukiwamo uvimbe kuanza
kunywea, damu na maji kukauka.
Utetezi wa Matola
Lakini Matola alidai kuwa mgonjwa huyo alitoa fedha kama asante.
"Baada ya kuwa nimewapatia dawa, yule
mfanyakazi mwenzangu aliniambia kwamba mgonjwa anataka namba yangu ya
simu au akaunti ya benki ili anipe asante na mimi niliwapa ila sikujua
waliweka shilingi ngapi," alisema Matola.
"Nilipokwenda benki nilikuta fedha
zimeongezeka, lakini sikujua ni shilingi ngapi ila yule mgonjwa aliwahi
kunipigia simu akaniambia kwamba aliniwekea asante, sijui Sh300,000 au
330,000 au sijui 340,000..."
Matola alisema hakuwahi kumwomba fedha mgonjwa huyo na kwamba hakuwahi kuchukua fedha mkononi kama anavyodai.
Dk Kombe anena
Dk Kombe alikiri kukutana na tukio
hilo na kusema baada ya kuona hali ilivyo kwa mgonjwa, alimwandikia dawa
nyingine ili aendelee na matibabu.
"Nakumbuka hiyo kesi lakini simkumbuki
mtu mwenyewe, ila ninachojua ni kuwa, yeye mwenyewe (mgonjwa) alimpa
mtu hela mkononi. Yalikuwa ni makosa yake kwa upande mwingine, dawa
hazinunuliwi sasa utampaje mtu hela mkononi?" alihoji daktari huyo.
Dk Kombe, ambaye alisema hakumbuki ni
mhudumu gani aliyefanya hivyo, alionyesha kuhofia maisha ya mgonjwa au
wagonjwa ikiwa taarifa hizo zitatolewa gazetini.
"Unajua wataendelea kupata tiba kwa
muda mrefu hapa na hii ni hatari kubwa kwao, huwezi kujua nini kinaweza
kuwapata. Cha muhimu wameandikiwa dawa nyingine na wanaendelea nazo, ni
bora wangekaa kimya," Dk Kombe.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Ocean Road,
Dk Twalib Ngoma alisema mgonjwa aliyefanyiwa hayo aende kushtaki kwenye
vyombo vya sheria badala ya vyombo vya habari.
"Anakuja kwako kulalamika wewe
umsaidie nini? Anatakiwa kwenda katika vyombo vya sheria ili apewe haki
yake, wewe utamsaidiaje?" alihoji Dk Ngoma.
Alisema kama mgonjwa amefanyiwa unyama kama huo, anatakiwa alipwe fidia na hakuhitaji maswali zaidi ya hapo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Mussa Wambura alisema watashughulikia suala hilo kwa kupata vithibitisho vyote
Chanzo MjengwaBlog
Chanzo MjengwaBlog
No comments:
Post a Comment