Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.

Harakati za
makada wa CCM wanaowania urais kusaka wadhamini mkoani zinaendelea kukumbwa na
vituko baada ya wanamgambo wa chama hicho, maarufu kama Green Guards,
kumshushia mkong’oto Dk Mussa Muzamill Kalokola aliyeingilia mkutano
ulioandaliwa kwa ajili ya mgombea mwingine.
Tukio hilo
lililotokea juzi, ni mwendelezo wa matukio kadhaa ambayo yamekuwa yakitokea
kwenye mchakato huo, yakiwamo ya wanachama kutaka kuchana fomu za mgombea baada
ya kunyimwa ‘posho’ na kada mwingine kukosa wadhamini na kulazimika kuomba
chakula cha mchana kutoka kwa mkuu wa wilaya.
Katika tukio
la Tanga, Dk Kalokola, ambaye pia anadaiwa kushawishi wanachama wasimdhamini
mgombea mwingine wa urais, Bernard Membe, alidaiwa kuvamia mkutano ulioandaliwa
kwa ajili ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kutaka kulazimisha apewe
kipaza sauti kwa ajili ya kuomba wanachama wamdhamini, kitu ambacho viongozi wa
CCM wa wilaya hawakukubaliana nacho na alipoendelea kung’ang’ania ndipo Green
Guards walipoamriwa wamuondoe eneo hilo.
Picha za
video za tukio hilo ambazo zimesambazwa mitandaoni zinawaonyesha vijana hao wa
Green Guards wakimsomba mzobemzobe mgombea huyo, kumuangusha kwa kumpiga ngwala
na mkoba wake wenye stika ya fomu za mgombea urais, ukionekana kuzagaa chini.
Alipoulizwa
na Mwananchi kuhusu mkasa huo, Dk Kalokola alikiri kupigwa katika tukio hilo
lilitokea mchana Jumatano ya Juni 17, 2015 alipofika kwenye ofisi za CCM za
Wilaya ya Tanga Mjini, siku ambayo mgombea huyo anadai alipangiwa na katibu wa
wilaya.
Dk Kalokola
alisema baada ya kukabidhiwa fomu za kuomba kuteuliwa na CCM Julai 15 mwaka huu
mkoni Dodoma, alikwenda mkoani Tanga ili kupata wadhamini.
“Tulielekezwa
kuwa makatibu wa CCM wa mikoa ndiyo watakaotutafutia wadhamini siyo sisi
tutafute hivyo mimi tarehe 16 nilikwenda ofisi za CCM kuripoti kwa katibu wa
Mkoa,” alisema.
Hata hivyo,
alisema hakuweza kuonana na Katibu huyo baada ya kuambiwa kuwa hayupo na
amemwachia majukumu hayo katibu wa CCM wa Wilaya ya Tanga Mjini.
Alisema siku
hiyo alikuta wagombea wawili waliofika ofisi hizo wakitaka kupewa wadhamini
ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na
Balozi Amina Salum Ali.
“Hawakutaka
hata kunisikiliza shida yangu. Mimi nikaamua kutoa taarifa makao makuu ya CCM,”
alisema.
Hata hivyo,
baadaye saa 12:00 jioni alipigiwa simu na katibu wa CCM wilaya hiyo ya Tanga,
akielezwa kuwa aende siku inayofuata asubuhi yaani Alhamisi.
“Nilienda
pale nikasaini kitabu nikawaeleza kuwa mimi jana (juzi) nilikuwa na kesi ya
kupinga Katiba jijini Dar es Salaam kwa hiyo ningeomba nipate wadhamini siku
hiyo hiyo ili nisafiri,”alisema Dk Kalokola ambaye amefungua kesi akitaka
Mahakama Kuu itangaze kuufuta mchakato wa kupata Katiba mpya kinyume cha utashi
wa chama hicho tawala ambacho kinajisifu kwa kufanikisha mchakato huo.
Dk Kalokola,
ambaye wakati anachukua fomu pia aliiponda CCM akidai inaiba sera za wapinzani,
alisema siku iliyofuata alikubaliwa na kutakiwa kurejea saa 6:00 mchana.
“Nilipofika
nikakutana na vijana wa Green Gurd wakiwa mlangoni, wakanipiga ngwala
wakiniambia huu ni mkutano wa Lowasa, nikawaambia kuwa mimi nakwenda kumuona
Katibu nina ahadi naye,” alisema.
“Wakaendelea
kunipiga lakini kinachonisikitisha vijana hawa wamekuwa wakija nyumbani kwangu
kuniomba msaada, hata sare walizovaa niliwanunulia mimi… sasa cha kushangaza
wagombea wako 37 kama kila mgombea mmoja siku moja katika kila mkoa tutamaliza
lini zoezi hili?” alihoji.
Alisema
kutokana na kipigo hicho, hajaweza kupata wadhamini kwenye mkoa huo ambao
alipanga kuanzia kutafuta wadhamini.
“Kesho (leo)
ndiyo nitaanza tena baada ya kutoka mahakamani juzi (Alhamisi). Hadi sasa
sijapata wadhamini hata kwenye mkoa mmoja,”alisema.
Dk Kalokola
alisema tukio hilo mbali ya kulitolea taarifa makao makuu ya CCM, pia
ameliripoti kituo cha Polisi cha Chumbageni.
Lakini
katibu mwenezi wa CCM wa Wilaya ya Tanga, Lupakishyo Kapange alisema kuwa
alilazimika kuwaamuru Green Guard wamuondoe kwa sababu mtangazania huyo alikuwa
aking’ang’ania kupewa kipaza sauti ili azungumze katika mkutano uliokuwa
umeandaliwa kwa ajili ya Lowassa.
“Alikuja
hadi nilipokuwa nikitangaza, akataka kuninyang’anya kipaza sauti, nilipomuomba
afuate taratibu za kuandaliwa mkutano wake kwa sababu huu ulikuwa wa
mtangazania mwingine, hakutaka kunielewa akang’ang’ania nikaamua kuwaita Green
Guards wa CCM hapa Tanga wamuondoe,” alisema Kapange.
Katibu wa
CCM wa wilaya, Lucia Mwilu alisema Dk Kaloloka, ambaye ni mkazi wa Tanga,
alifika ofisini kwa mara ya kwanza Juni 15 wakati wa mapokezi ya Membe na
alikuwa akiwazuia wanachama waliokuwa wakitaka kumdhamini mgombea huyo.
“Nilimwita
na kumuomba afuate taratibu zilizopo kwenye fomu za wagombea urais, lakini
nikakubaliana naye tukutane Juni 16 mchana ili anipe fomu zake hatimaye
niweze kumuandalia taratibu za kudhaminiwa. Hakufanya hivyo badala yake
akamvamia katibu mwenezi,” alisema Mwilu.
Alifafanua
kuwa tukio la kumondoa Dk Kalokola lilitokea saa 7:50 mchana wakati wanachama
wa CCM wakimsubiri Lowassa nje ya jengo la chama hicho la mkoa wa Tanga, lakini
waziri huyo mkuu wa zamani na timu yake aliwasili Tanga saa 12:00 jioni.
Alipoulizwa
kuhusu tukio hilo, kamanda wa polisi wa mkoa, Zubery Mwombeji alisema Dk
Kalokola alitaka kutumia jukwaa la Lowassa kuwapata wadhamni, wakati ni kinyume
na taratibu za CCM.
Alisema
baada ya hapo alikwenda kituo cha polisi kuomba aruhusiwe kutumia jukwaa hilo,
lakini ofisa upelelezi alimtaka aende kuonana na viongozi wa CCM Kwa sababu
suala hilo haliko chini ya polisi.
Watu
walioshuhudia tukio hilo waliieleza Mwananchi kusitikishwa kwao na kitendo cha
kada huyo kushambuliwa, lakini wamesema baadhi yao walimsihi Dk Kalokola afuate
taratibu lakini hakutaka kuwasikiliza.
“Sikufurahishwa
na alivyofanyiwa Dk Kalokola lakini naye kwanini avamie mikutano ya wenzake?
Juzi aliwazuia wana-CCM wasidhamini Membe, leo tena kaja hapa kuleta
tafrani,”alisema Mwahija Omari mkazi wa Tanga.
CHANZO: MWANANCHI



No comments:
Post a Comment