HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » NEC YATOA ONYO KALI DHIDI YA UKIUKWAJI WA MAADILI KIPINDI HIKI CHA KAMPENI

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.



Kama mnavyofahamu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani zimeanza tangu tarehe 22 Agosti, 2015 na zinaendelea hadi tarehe 24 Oktoba, 2015.
Ni jambo linaloeleweka kwamba mchakato wa Kampeni na wa Upigaji Kura unatawaliwa au kuongozwa na Sheria, Katiba na Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.
Katika kipindi hiki tangu Kampeni zianze, nafurahi kusema kwa niaba ya Tume kuwa kwa ujumla, Kampeni zimeenda vizuri. Karibu mikutano yote imefanyika katika hali ya utulivu na amani. Hatujapata taarifa ya mkutano wa Kampeni ambao umevurugwa kwa fujo zozote. Kwa hilo napongeza Vyama vyote vya Siasa.
Hata hivyo, kutokana na mikutano hiyo nchini ya Kampeni, ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani yamejitokeza mambo ambayo ni kinyume kabisa na Mwongozo wa Maadili ya Uchaguzi wa Rais Wabunge na Madiwani wa mwaka 2015 uliotiwa saini na Vyama vyote vya Siasa tarehe 27 Julai, 2015.
Yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo yamejitokeza katika Kampeni hizo:-
(i) Kutozingatia muda wa kumaliza Mikutano ya Kampeni
Kuna baadhi ya Vyama ambavyo katika mikutano yao vimekiuka Kipengele hiki kwa kufanya mikutano zaidi ya saa 12.00 jioni. Kuendelea kufanya Mkutano wa Kampeni zaidi ya muda huo ni ukiukwaji wa Kipengele cha 2.1 (c) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 kinafafanua kuwa Mikutano yote ya Kampeni itafanyika kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni.


(ii) Kubandika mabango ya Kampeni, matangazo au Mchoro wowote kwenye maeneo yasiyoruhusiwa au bila idhini ya wahusika
Baadhi ya Vyama vimeanza kubandika mabango, michoro na picha za Wagombea wao katika majengo au vyombo vya usafiri vya watu binafsi au Taasisi mbalimbali bila idhini ya wamiliki husika.
Napenda kuwakumbusha kuwa, kwa mujibu wa Kipengele cha 2.2. (g) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, hairuhusiwi kufanya hayo bila idhini ya wamiliki husika.
(iii) Kuchafua, kubandua au kuharibu matangazo au picha za Kampeni za Vyama vingine
Tume imeanza kupokea malalamiko kutoka baadhi ya Vyama kuwa, mabango au picha za Kampeni za Vyama vyao yanabanduliwa au kuchafuliwa na wafuasi wa Vyama vingine.
Ni vema Vyama vya Siasa na Wagombea wakumbuke kuwa Kipengele cha 2.2 (f) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, kinapiga marufuku Chama kingine kuchafua, kubandua au kuharibu matangazo au picha za Kampeni za Vyama vingine.
(iv) Matumizi ya lugha zisizo za staha
Tume imepokea malalamiko kuwa, katika Mikutano mbalimbali ya Kampeni katika ngazi zote, kumeanza kujitokeza baadhi ya viongozi wa Vyama, Wagombea au wafuasi wao kutumia lugha zisizo za staha wakati wa Mikutano ya Kampeni katika ngazi mbalimbali.
Lugha zisizo za staha zinajumuisha matusi, kejeli, kashfa n.k. Kipengele cha 2.2 (b) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, kinakataza Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wao kutumia lugha zisizo za staha katika harakati zote za Kampeni hadi upigaji Kura.
Wajibu wa Vyama vya Siasa na Wagombea
Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wana wajibu wa Kisheria wa kuyaheshimu, kuyasimamia na kuyatekeleza Maadili hayo kwa mujibu wa Kipengele cha 2.1. (b) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015. Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wagombea wana jukumu la kuwaelimisha, kuwahamasisha na kuwasisitiza wanachama wao kutekeleza Sheria ya Uchaguzi (ikumbukwe kuwa Maadili ya Uchaguzi yametungwa chini ya Kifungu cha 124A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343)
Adhabu za ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi
Napenda kuwakumbusha Vyama vya Siasa na Wagombea kuwa, ukiukwaji wa aina yoyote wa Maadili unaweza kusababisha Chama au mgombea kupewa adhabu kama zilivyoainishwa katika Kipengele cha 5.10 (a-f). Adhabu hizo ni pamoja na:
1. Chama au Mgombea aliyekiuka maadili kuelekezwa kuomba msamaha hadharani.
2. Kupewa onyo au karipio.
3. Kumtangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari na taarifa kwa Umma mgombea au Chama kilichokiuka Maadili.
4. Chama au Mgombea kusimamishwa kuendelea kufanya Kampeni.
5. Chama au Mgombea kuzuiliwa kutumia vyombo vya habari.
6. Chama au Mgombea kulipa faini kuanzia kiwango cha 100,000/- 500,000/- na 1,000,000/- kutegemea ngazi ya Kamati husika.
Katika kipindi hiki cha Kampeni, Chama au Mgombea akipewa mojawapo ya adhabu hiyo kunaweza kuathiri Kampeni zake za kuelekea Uchaguzi wa Rais, Wabunge au Madiwani.
Hitimisho.
Napenda kunukuu Kipengele cha 1.4 cha Maadili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 ili kila Chama kione umuhimu wa kuwahimiza wagombea na wanachama wao kuzingatia Maadili katika harakati zao za kujinadi. Nanukuu:
“[……] kila mgombea atajaza Fomu Na. 10 kuthibitisha kuwa ataheshimu na kutekeleza Maadili ya Uchaguzi. [….] Mgombea atakayekataa kusaini Maadili haya atakataliwa au kuondolewa kushiriki katika Uchaguzi kama Mgombea.”
Maana yake ni kwamba kila Chama, Mgombea na Wanachama kwa ujumla wana wajibu kuheshimu taratibu zote za Kampeni hadi kupiga Kura.
Yote yaliyokatazwa katika Maadili yazingatiwe na Vyama vyote. Kama nilivyosema hapo awali Tume imepata malalamiko kuwa baadhi ya Vyama na Wagombea wamekiuka Maadili ama kwa kuzidisha muda wa Kampeni, au kuchana na kuharibu mabango, au kutumia lugha chafu isiyo na staha; Haya yote Tume inakemea kwa nguvu sana na kusihi Vyama vyote na Wanachama wao wote kuheshimiana, waeleze sera zao bila kukashifiana.
Lengo na matumaini ya Tume ni kuwa na Kampeni za utulivu na hatimaye wananchi kuwa na hali ya utulivu na amani ili Uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu. Kwenye hali ya utulivu na amani wananchi wataweza kupiga Kura ya utulivu ili kuamua viongozi wanaowataka. Hiyo ndiyo Demokrasia.
Nimalizie kwa kuwakumbusha Vyama vyote kuzingatia Maadili ya 2015. Tume isilazimishwe kuchukua hatua za kutoaadhabu kwa Vyama na Wagombea. Busara itumike katika mikutano yote ya Kampeni.
Inawezekana, wote tukidhamiria, “Play your Part”.
Jaji (Mst.) Damian Z. Lubuva
MWENYEKITI
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: