Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.
Kaimu wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Selemani Mzee (katikati) ambaye pia
ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo akifungua mdahalo wa wazi juu ya amani
wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu unaofanyika katika
ukumbi wa chuo Kikuu Huria (OUT)mjini Iringa. Kutoka kushoto walioketi
na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilolo Martin Mlwafu, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Iringa ACP Ramadhani Mungi, Mwenyekiti wa
ICISO Alexander Kisinini na Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa
Iringa, Wilfred Myuyu. Mdahalo huo uliandaliwa na Iringa civil society
organization (ICISO-Umbrella) kwa kushirikiana na Asasi ya Foundation
for Civil Society (FCS) jana. (Picha na Friday Simbaya)
Na Friday Simbaya, Iringa
WAKATI zimebaki siku chache kabla ya
uchaguzi mkuu kufanyika Oktoba mwaka huu, Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa
Iringa, Wilfred Myuyu amesema ameanza kupokea vifaa vya
uchaguzi.
Mratibu huyo alisema hayo wakati wa
mdahalo wa wazi juu ya amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba
mwaka huu uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Huria (OUT) mjini
Iringa jana.
Mdahalo huo uliandaliwa na shirika
lisilo la kiserikali la Iringa Civil Society Organization
(ICISO-Umbrella) kwa kushirikiana na asasi ya ‘The Foundation for
Civil Society (FCS).’
Myuyu ambaye pia ni Katibu Tawala
Msaidizi (Sehemu ya Serikali za Mitaa) alisema kuwa baadhi ya vifaa
vilivyopokelewa ni pamoja na maboksi 5,995 ya kupigiakura, taa
mbalimbali na daftari la kudumu la wapigakura.
Alisema kuwa uchaguzi ni mchakato na
tayari Mkoa wa Iringa umeanza maandalizi na utakuwa na jumla ya vituo
vya kupigiakura 1,641 na kuongeza kuwa kila kituo kitakuwa na
wapigakura wasiozidi 500.
Wilfred Myuyu alisema kuwa mkoa
umeandikisha jumla ya wapigakura 526,006 kwa kuvuka lengo la matarajio
la 521,491 na kufikia asilimia 100.8.
“Vituo vile vilivyotumika
kujiandikisha wapigakura ndivyo vitakavyokuwa vituo vya kupigiakura na
kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na wapigakura wasiopungua 500 na
kama kituo kile kilikuwa na wapigakura 1,000, basi kituo hicho
kitagawanywa na kuwa vituo viwili vya kupigiakura ambapo vitakuwa ‘A’
na ‘B’, ” alisema Myuyu.
Alisema kuwa vituo vyote vya
kupigiakura vitafunguliwa kuanzia saa 1 asubuhi na kufungwa saa 10
jioni ambapo vitageuzwa kuwa vituo vya kuhesabia kura.
Aidha, alisema kuwa orodha ya majina
ya wapigakura itabandikwa siku nane kabla ya uchaguzi mkuu, ili kuwapa
fursa watu kuangalia majina yao katika vituo
walivyojiandikishia.
Alisema kuwa kanuni za uchaguzi mkuu
za mwaka 2015 zinavitaka vyama vya siasa kuwaelimisha wanachama wake
namna ya kupigakura na baada ya kupigakura hawaruhusiwi kusubiri
matokeo ili kuepusha msongamano.
Mkoa wa Iringa ulianza uandikishaji ya
wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura Aprili 29 na
kukamilika Mei, 29 mwaka huu.
“Kwa mujibu wa sheria, matokeo ya
udiwani yanatangazwa na msimamizi msadizi wa kata, ya ubunge msimamizi
wa wilaya na urais ni tume,” alisema.
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), Damian Lubuva aliagiza waratibu na wasimamizi
wa uchaguzi pamoja na makamanda wa polisi kutenda haki wakati wa
Uchaguzi Mkuu kwa kuwa usalama wa Taifa upo mikononi mwao na kuonya
kuwa kosa lolote linaweza kuiingiza nchi matatizoni.
NEC ilisema hayo katika kikao
kilichohudhuriwa na wasimamizi wa uchaguzi wa halmashauri zote nchini
pamoja na makamanda wa mikoa wa Jeshi la Polisi, ambalo liliongozwa na
mkuu wake, IGP Ernest Mangu, pamoja na makamishna wake- Diwani
Athumani (Upelelezi wa Makosa ya Jinai), Paul Chagonja (Operesheni),
Mussa Ali Mussa (Polisi Jamii) na Suleiman Kova (Kanda Maalumu Dar es
Salaam) pamoja na baadhi ya wakuu wa vikosi.
No comments:
Post a Comment