Polisi imemkabidhi mfanyabiashara Yusuf Manji (41) na wenzake watatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kumaliza kuwahoji kuhusu kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.
Jana, Septemba 4 Mahakama iliruhusu washtakiwa kwenda kuhojiwa polisi kwa ajili ya kukamilisha upelelezi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi amedai wamewarudisha washtakiwa kama walivyoamriwa na Mahakama. Upande wa mashtaka ulitakiwa kuwarudisha muda wa kazi baada ya kuhojiwa polisi.
Mbali na Manji, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Meneja Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda (28), mtunza stoo, Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43), mkazi wa Chanika wanakabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi.
Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi ameahirisha kesi hadi Septemba 8.
Mahakama ilitoa ruhusa ya washtakiwa kwenda kuhojiwa polisi baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa waliomba hati ya kuwatoa washtakiwa mahabusu ili kuhojiwa katika kesi namba 33/2017, hivyo wakabidhiwe polisi.
No comments:
Post a Comment