Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, akibadilishana nyaraka na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania,Chansa Kapaya(kulia) zenye makubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa mkoani Kigoma.Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere,jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye, akibadilishana nyaraka na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Chansa Kapaya (kulia) zenye makubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa mkoani Kigoma.Katikati ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi, Harrison Mseke, akifafanua vipengele vilivyopo kwenye Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa mkoani Kigoma, kabla ya kutiwa saini.Wanaosikiliza meza kuu toka kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Chansa Kapaya na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Burundi,Abel Mbilinyi.Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Wajumbe kutoka Serikali ya Burundi wakiongozwa na Balozi wa Burundi nchini Tanzania,Gervais Abayeho wakiwa katika Mkutano wamakubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa mkoani Kigoma.Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki,Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Wajumbe kutoka Mashirika mbalimbali ya kimataifa wakiwa katika Mkutano wa makubaliano juu ya Mpango wa Kuwarejesha Wakimbizi wa Burundi wanaohifadhiwa mkoani Kigoma.Makubaliano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki, Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
Wakimbizi wa Burundi waliokimbia machafuko nchini kwao wataanza kurejea nchini kwao ifikapo Septemba 7 hadi Desemba 31, mwaka huu mara baada ya pande tatu ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Burundi na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), kutiliana saini Mpango wa Kuwarejesha wakimbizi baada ya mkutano uliochukua takribani siku tatu katika kuandaa mpango huo.
Wakitiliana saini makubaliano hayo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki,Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) nchini Tanzania, Chansa Kapaya, mwishoni mwa wiki wote walikubaliana kutekeleza vipengele vilivyopo katika makubaliano hayo yakiwa na lengo la kuwarudisha wakimbizi walioomba kurejea nchini Burundi, baada ya hali ya Amani na utulivu kurejea.
Akizungumza baada ya kutiliana saini makubaliano hayo Waziri Mwigulu, alisema umefika wakati wa wakimbizi wa Burundi kurudi nchini kwao kuungana na familia zao na ndugu waliobaki ili kusaidia kujenga uchumi wa nchi yao baada ya kuwa katika machafuko yaliyosababisha kukimbia nchi yao kwa muda mrefu.
“Mimi kama mwanauchumi ninaona madai yao ya kurudi nchini Burundi kujishughulisha na shughuli za kilimo ni maamuzi mazuri huku pia wakisisitiza kurejea kwa Amani na Utulivu nchini kwao kuwa ni sababu ya msingi ya kufikia kuomba kurejea, sisi kama Serikali tutahakikisha zoezi hilo la urejeaji nchini kwao linaenda salama tukishirikiana na Serikali ya Burundi kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchini Burundi,” alisema Mwigulu.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo kutoka nchini Burundi, Pascal Barandagiye, amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania na Watanzania wanaoishi kwenye maeneo yaliyotumika kuwahifadhi wakimbizi kwa ukarimu wao walioonyesha muda wote kwa raia kutoka nchini Burundi huku akisisitiza kurejea kwa hali ya Amani na utulivu ambao hapo mwanzoni ilitoweka.
“Nawaomba wananchi wetu warejee nchini ili tuweze kuijenga Burundi yetu ambayo hivi sasa kuna Amani na utulivu, pia naishukuru Serikali ya Tanzania na Watanzania ambao wamekua wakiwaonyesha ukarimu wakimbizi kutoka Burundi na kuwapa hifadhi nchini hapa,”alisema Barandagiye.
Kwa upande wao Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) kupitia kwa Mwakilishi wao nchini,Chansa Kapaya, wameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha wakimbizi wa Burundi 6,800 walioomba kurejea nchini kwao wanasahiliwa na kurejeshwa kwao katika hali ya utu na usalama huku shirika hilo likizishukuru Serikali za Tanzania na Burundi kwa msaada wao walioupata katika kushughulikia masuala ya wakimbizi.
No comments:
Post a Comment