HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» » WAKULIMA WATAKIWA KUTUMIA FURSA YA KUFUTWA TOZO NA ADA KUBORESHA KILIMO

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba

Jovina Bujulu-MAELEZO
Sekta ya kilimo nchini ni kitovu cha maendeleo ya viwanda kwa kutoa masoko na malighafi za viwandani ambapo inaajiri Watanzania wengi takribani zaidi ya asilimia 67.

Katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo, Serikali inaendelea kuimarisha mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya kilimo ikiwemo kuimarisha masoko ya kilimo ili sekta hiyo iendelee kuwa na tija kwa wakulimananchi na taifa kwa ujumla.

Hivi karibuni Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilitangaza kufuta ada na tozo mbalimbali katika baadhi ya mazao ya biashara ili kumpa unafuu mkulima wakati wa kuuza mazao yake.

Hatua hiyo ni mwanzo mzuri wa kuimarisha sekta hiyo hasa wakati huu ambapo Serikali ya Awamu ya Tano imetangaza nia yake ya kuimarisha uchumi wa kati na viwanda.

Serikali iliamua kufuta na kupunguza ada na tozo imedhamiria kumaliza kero na kilio cha muda mrefu cha wakulima ambao wamekuwa wakilalamikia tozo hizo kwa madai kuwa zinawanyonya.

Aidha, uamuzi huo unategemea kuwapunguzia mzigo mkubwa wa malipo ambao umekuwa ukiwaelemea wakulima hao, hivyo kuwapa unafuu mkubwa na kuwapatia faida.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba alizitaja baadhi ya tozo zilizofutwa katika zao la tumbaku kuwa ni mchango wa ushirika wa mkoa, mchango kwa ajili ya gharama za masoko ya ushirika na chama cha msingi cha ushirika, dhamana ya benki kuu ya Tanzania na fomu ya maombi ya leseni za tumbaku.

Ada na tozo nyingine zilizotajwa kuwa ni kodi ya leseni ya kununua tumbaku kavu na mbichi kiwandani, leseni ya kuuza tumbaku nje ya nchi na tozo ya Baraza la Tumbaku.

Pamoja na kufuta tozo na ada katika baadhi ya mazao, Serikali pia imetoa punguzo katika zao la tumbaku ambapo kodi ya leseni ya tumbaku kavu itakuwa dola za kimarekani 2,000 badala ya dola 4,000.

Aidha, leseni ya kusindika tumbaku imepungua kutoka dola za kimarekani 10,000 hadi 5,000 ambapo Serikali imechukua hatua hizo ili kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo wakiwemo wakulima wadogo.

Kupitia bodi ya mazao, Serikali itaendelea kuimarisha soko la mazao ya asili hasa mazao ya jamii ya mikunde ili kukidhi mahitaji ya zao hilo katika soko la India na zao la muhogo kwa ajili ya soko la China.

Tozo na ada nyingine zimepunguzwa katika zao la kahawa, ambapo ada ya leseni  ya ghala la kahawa, leseni ya kukoboa kahawa, kuuza nje ya nchi kahawa iliyosindikwa na leseni ya kununua kahawa kwa kampuni na vyama vya ushirika zimefutwa.

Tozo nyingine zilizopunguzwa kwenye zao la kahawa ni ya fomu ya kuomba leseni ya kuuza kahawa ya kijani, leseni ya ghala na leseni ya kukoboa na kusindika kahawa pia zimefutwa.

Kwa upande wa zao la sukari jumla ya ada 17 zimefutwa ambazo baadhi ni ada hizo ni ya leseni ya uingizaji sukari ya viwandani, ada ya leseni kamili ya uzalishaji sukari mkubwa na mdogo, leseni ya muda ya uzalishaji sukari uwekezaji mdogo, leseni ya marudio kila baada ya miaka mitatu na ada ya leseni ya kuchakata miwa.

Vilevile ada ya kusajili kwa waagizaji wakubwa  na wa kati, na ya wafanyabiashara wa sukari ya matumizi ya kawaida ikiwa ni pamoja na ada ya kupata kibali cha kuingiza sukari ya viwandani zimefutwa pia.

Mazao ya pamba, chai na korosho pia yamo katika kufutiwa tozo na ada. Hii ni pamoja na tozo ya kituo cha kununulia pamba katika ngazi ya Halmashauri na tozo ya maendeleo ya elimu katika Halmashauri ya Meatu.

Katika zao la chai, tozo kwa ajili ya gharama ya uendeshaji wa vyama vya wakulima na ada ya leseni ya kununua korosho zimefutwa, ambapo wakulima na wafanyabiashara watapata unafuu wakati wa kuuza mazao yao.

Katika kuhakikisha wakulima wanaendelea kunufaika na kilimo, Serikali pia imefuta baadhi ya ada katika pembejeo ya mbolea ambapo wafanyabiashara wa mbolea hawatalipia usajili wa mbolea, ada ya leseni na usajili wa mzalishaji.

Akizungumzia kufutwa kwa tozo na ada hizo, wakati wa maonesho ya kilimo (Nanenane) yaliyofanyika Kitaifa hivi karibuni katika viwanja vya Ngongo mkoani Lindi, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. William Tate Ole Nasha alisema kuwa Serikali ilifikia hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa tozo hizo hazikulenga kuwakwamua wakulima katika wimbi la umaskini badala yake ziliwazidishia umaskini.

Aliendelea kusema kuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliamua kufuta tozo na ada hizo ili kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha inaondoa vikwazo vyote vilivyokuwa vikiwakabili wakulima ili kuwainua na kukuza uchumi.

Aidha, Serikali za Mitaa zimeagiza kuacha kutoza ushuru kwa mazao yanayosafirishwa kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine ili kurahisisha  na kuwapunguzia  wakulima mzigo wa kulipa kodi.

Kutokana na kupunguza kodi, tozo na ada mbalimbali  katika mazao hayo ya biashara wakulima wanatakiwa kuitumia nafasi hiyo kwa manufaa yao kwa kujiongezea faida ikiwa ni pamoja na kuzingatia kilimo bora chenye tija kwa ajili ya kujipatia mazao bora yanaweza kukabiliana na soko la ushindani ndani na nje ya nchi hatua itakayowasaidia kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: