HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» » » WAZIRI MAHIGA AAGANA NA BALOZI WA CHINA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga akimkabidhi tuzo ya kutambua mchango wake katika kuendeleza ushirikiano baina ya Tanzania na China Balozi wa China aliyemaliza muda wake nchini Dkt. Lu Youqing alipotembelea ofisi kwake leo Jijini Dar es Salaam. Na: Mpiga Picha Wetu 

Na: Bushiri Matenda- MAELEZO 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga ameagana na Balozi wa China aliyemaliza muda wake chini Dkt. Lu Youqing. 

Katika hafla fupi iliyofanyika leo kwenye ukumbi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Dkt. Mahiga alimshukuru Balozi Dkt. Lu kwa kuendeleza ushirikiano kati ya Serikali ya nchi yake na Tanzania kwa muda wote alipokuwa nchini akitekeleza majukumu yake. 

Dkt. Mahiga alimueleza Balozi huyo kuwa Tanzania na China ni ndugu kwani tangu Tanzania ilipopata Uhuru imekuwa ikishirikiana na nchi hiyo yenye maendeleo makubwa kiuchumi. 

“Kwa muda mrefu wizara zetu zimekuwa zikifanya kazi kwa karibu sana ambapo sasa tumekuwa washirika wa karibu. Wewe Balozi umekuwa kielelezo tosha cha kutekeleza tafsiri ya sera nzuri ya nchi yako kwa mataifa mengine ikiwamo Tanzania” alisema Dtk. Mahiga. 

Aidha, Dkt. Mahiga alisifu utendaji wa balozi huyo kuwa wa ni wa kipekee kwani amekuwa mnyenyekevu, msikivu na anafanya kazi zake kwa utaratibu na uhakika. 

Alimshukuru balozi huyo kwa jitihada zake za kuhakikisha watushishi wa wizara kuendelea kupata mafunzo nchini China na kuomba kuendelea kushirikiana katika masuala ya tafiti mbali mbali baina chuo cha Diplomasia nchini na vyuo vyao vya Diplomasia vya China. 

Waziri Mahiga alitumia fursa hiyo kumshukuru Balozi Lu kwa jitihada zake za kuhakikisha maombi mbali mbali ambayo Serikali imekuwa ikiomba Serikali ya China katika sekta mbalimbali na kutolea mfano ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) ambapo ulikamilika kwa wakati. 

Aidha, aliishukuru serikali ya China kwa kukubali kujenga jengo la ofisi za wizara yake huko Dodoma ombi ambalo waziri Mahiga alilotoa kwa waziri wa China alipotembelea nchini hivi karibuni. 

Kwa upande wake Balozi Dkt. Lu ameishukuru wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki chini ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli kwa ushirikiano wanaoendelea kutoa kwa Ubalozi na serikali ya China 

“Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ni familia yangu, kwa muda wote nimekuwa mwenye furaha na ari kufanya kazi na nyinyi kwa maslahi ya nchi zetu hivyo nawashukuru sana kwa ushirikiano wenu”Dkt Lu alisema. 

Alimueleza Dkt. Mahiga kuwa anajisikia furaha kuona Sera ya Serikali ya kuliletea taifa maendeleo na wananchi wake kwa ujumla inatekelezwa kwa vitendo hivhyo kuongeza kasi ya maendeleo hadi Tanzania sasa inaweza kuuza bidhaa zake nchi za nje. 

“Narudi nyumbani China lakini naahidi nitakuwa balozi wenu huko nyumbani, Ubalozi wa China hapa nchini utaendelea kushirikiana na wizara na Serikali kwa kila hali” alisisitiza Dkt. Lu 

Balozi Lu pia ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa mchango wake katika ukombozi wa nchi za Afrika ikiwemo Afrika ya Kusini na jitihada za wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili watanzania wanaoishi nchi za nje. 

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Bw. Rogers William Sian’nga amemshukuru Balozi Lu kwa ushirikiano wake na Mamlaka hiyo ambapo Ubalozi wa China umetoa vifaa mbalimbali wenye lengo la kuongeza ufanisi na kutoa fursa za watumishi kwenda China kupata mafunzo ili yaweze kuwasaidi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini. 

“Serikali ya China naifananisha na mshumaa kwani inamulika Tanzania katika mapambano dhidi ya madawa haramu ya kulevya, Mamlaka imepata kibali kwenda China kutembelea magereza yote ili tuweze kuwahoji wafungwa wote kwa lengo la kubaini wafanyabiasha wakubwa wanaofanya biashara hii haramu” alisema Bw. Sian’ga. 

Katika hafla hiyo Waziri Mahiga alimkabidhi Balozi Lu zawadi kinyago cha Ujamaa kinachoashiria udugu na mshikamano wa Watanzania na picha yenye mchoro wa Tembo na Mlima Kilimanjaro wenye ishara ya kutambua mchango wa Balozi huyo katika mapambano dhidi ya ujangiri na wizi wa Maliasili nchini. 

Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers William Siang’a kwa niaba ya Mamlaka yake alimkabidhi Balozi Lu zawadi ya ngozi ya pundamilia kwa kutambua mchango wake wa kupambana na madawa ya kulevya nchini ambapo serikali ya China ipo mstari wa mbele katika mapambano hayo. 

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: