Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema gharama za matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya zimefikia Sh412.7 milioni.
Lissu ambaye ni mwanasheria wa chama hicho, amelazwa hospitalini hapo tangu Septemba 7 aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa maeneo ya nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.
Mbowe akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Oktoba 17, 2017 jijini Dar es Salaam, Tanzania amesema gharama ni kubwa, ila anawaomba Watanzania wasichoke kuchangia kwa kuwa Lissu atarudi barabarani.
“Tunaishukuru sana familia ya Lissu, imekuwa na msimamo kama Lissu mwenyewe. Tumefanya kazi na familia na tutaendelea kufanya kazi na familia. Tutakapokwenda katika matibabu ya tatu, tutaiacha kwa familia iwe msemaji wa kwanza, mgonjwa anaweza kuongea na kujitambua,” amesema.
Kuhusu mchanganuo wa michango, Mbowe amesema wabunge wa Chadema wamechanga Sh48.4 milioni.
Amesema wananchi wamechangia Sh24.2 milioni kupitia simu ya Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko.
“Watu mbalimbali wakiwemo wanachama wa Chadema wamechanga Sh90 milioni kupitia akaunti iliyofunguliwa katika Benki ya CRDB,” amesema.
Mbowe amesema wabunge wote wakiwemo wa Chadema wamechanga Sh43 milioni na kwamba, Watanzania walio nje ya nchi wamechanga kupitia Go fund me Dola 29,000 za Marekani.
Kiongozi huyo wa Chadema amemshukuru Mange Kimambi kwa kufanya kazi kubwa ya kuhamasisha michango.
Mbowe amesema wafanyabiashara wakihamasishwa na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema wamechanga Dola 18,000.
Amesema wana orodha nzima ya wote waliochangia na amewaomba Watanzania waendelee kuwapigania.
No comments:
Post a Comment