Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa akizungumza na Viongozi wa Serekali pamoja na Watendaji waTanesco, REA. katika kikao cha maendeleo ya usambazaji umeme kilichofanyika , leo (Jumamosi, Januari 13, 2018)Ofisini kwake, Mjini Dodoma (PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Nishati ijiridhishe na ubora wa vifaa vinavyotumiwa na wakandarasi katika miradi ya umeme.
Pia iwasimamie wakandarasi hao kwa ukaribu ili kuhakikisha thamani ya miradi inayotekelezwa inalingana na kiasi cha fedhawanacholipwa wakandarasi hao.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Januari 13, 2018) wakati akizungumza katika kikao cha maendeleo ya usambazaji umeme kilichofanyika , Ofisini kwake, Dodoma.
Waziri Mkuu amesema wakati huu ambao Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakiendelea na miradi ya usambazaji umeme, ni vema wizara hiyo ikajiridhisha na ubora wa vifaa.
“Wasimamieni wakandarasi kikamilifu na kama hamjaridhishwa na kazi wanayofanya msisite kuwachukulia hatua, tunataka wananchi wapate umeme.”
Amesema Rais Dkt. John Magufuli amedhamilia kuona umeme unasambazwa kwenye vijiji vyote nchini kwa lengo la kuboresha maendeleo ya wananchi.
Hivyo, Waziri Mkuu amesisiza kwamba ni lazima wakandarasi waliopewa jukumu hilo wasimamiwe kikamilifu ili mradi hiyo iweze kuwa na ubora unaostahili.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema tayari wakandarasi wanaotekeleza mradi wa REA namba tatu wameshaanza kazi.
Amesema kwa wakandarasi ambao bado hawajaanza wamekubaliana kwamba wataanza wakati wowote na wa mwisho ataanza Machi 2, 2018.
Dkt. Kalemani amesema wizara yake itahakikisha miradi yote ya kusambaza umeme inasimamiwa kikamilifu na inakamilika kwa wakati na katika ubora unaostahili.
Kikao hicho kilihudhuliwa na Waziri wa Nishati Dkt.Kalemani, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Nishati Bibi Subira Mgalu, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bibi Maimuna Tarishi.
Wengine ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Mtendaji Mkuu wa REA, Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Kamishna Msaidizi-Bajeti.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, JANUARI 13, 2017.
No comments:
Post a Comment