HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» » NBAA YAZINDUA MFUMO WA KUKUSANYA TAARIFA ZA FEDHA ILI KUSAIDIA WADAU KUFANYA MAAMUZI SAHIHI


Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imezindua rasmi mfumo mpya wa kukusanya taarifa za fedha zilizokwisha kukaguliwa na Wakaguzi wa Hesabu, ambao utaanza kutumika rasmi kuanzia Julai 1, 2025.

Mfumo huu unalenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za kifedha kwa matumizi ya mamlaka ya mapato (TRA), taasisi za kifedha, wadau wa mikopo, taasisi za serikali na binafsi, na mashirika mbalimbali, kwa ajili ya kufanya maamuzi muhimu ikiwemo utoaji wa mikopo na tenda kwa wazabuni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam alipotembelea banda la NBAA katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu, alisema mfumo huo ni hatua kubwa katika kuhakikisha taarifa za fedha zinakuwa na uwazi, uaminifu na uhalali wa kitaaluma, hasa kwa wale wanaohitaji kuzitumia katika maamuzi ya maendeleo ya kiuchumi na kibiashara.

“Kuanzia sasa, taarifa zote za fedha zilizokaguliwa zitakuwa zinaletwa moja kwa moja kwenye mfumo wa NBAA. Hii itasaidia taasisi kama TRA, taasisi za fedha, na wadau wengine kuhakikisha taarifa wanazozipokea ni sahihi, zimetolewa na wakaguzi walioidhinishwa, na zinaweza kutumika kama msingi wa kufanya maamuzi makubwa kama utoaji wa mikopo au kandarasi,” alieleza Prof. Temu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika wa NBAA, CPA Kulwa Emmanuel Mandeleja, alisema mfumo huu utarahisisha sana mchakato wa uthibitishaji wa taarifa kwa taasisi mbalimbali, hasa zile zinazohitaji uthibitisho wa hali ya kifedha ya kampuni au taasisi kabla ya kutoa huduma au mikopo.

“Mfumo huu utahakikisha taarifa zote za kifedha zilizokaguliwa zinahifadhiwa sehemu moja salama na ya kuaminika. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kufanya tathmini, kuzuia taarifa za kughushi na kuimarisha mchakato wa maamuzi ya kifedha katika taasisi nyingi,” alisema CPA Mandeleja.

NBAA imetoa wito kwa taasisi zote, watoa huduma za ukaguzi, na wahasibu kuhakikisha wanatumia mfumo huo mpya ipasavyo na kuhakikisha taarifa zote zinaingizwa kwa wakati kama sehemu ya uwajibikaji na weledi wa kitaaluma.

Kwa maelezo zaidi, wadau wanakaribishwa kutembelea banda la NBAA katika jengo la Wizara ya Fedha na Mipango katika viwanja vya Sabasaba au kutembelea tovuti ya NBAA: www.nbaa.go.tz.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Sylvia Temu akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Bodi hiyo lililopo ndani ya  jengo la Wizara ya Fedha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Sylvia Temu akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Bodi hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Sylvia Temu akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa NBAA alipotembelea banda la Bodi hiyo lililopo ndani ya jengo la Wizara ya Fedha. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Huduma za Shirika kutoka NBAA CPA Kulwa Malendeja.

«
Next
This is the most recent post.
»
Previous
Older Post

No comments: