Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kuonesha dhamira yake ya kurejesha kwa jamii kwa kushiriki katika zoezi la uchangiaji damu pamoja na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Prof. Siasa I. Mzenzi, amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Bodi kurudisha kwa jamii kupitia ushirikiano kati ya NBAA, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, pamoja na wahasibu waliokuwa kwenye mafunzo yanayoratibiwa na Bodi hiyo.
Alieleza kuwa wahasibu hao walijitokeza kwa wingi kushiriki katika uchangiaji wa damu salama kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo muhimu.
“Katika kuendeleza juhudi za kuwafikia wananchi, NBAA imetoa msaada wa vifaa muhimu ikiwemo pampers na mahitaji mengine kwa ajili ya watoto wanaopatiwa matibabu hospitalini hapa. Hatua hii inalenga kuboresha huduma na kuwafariji wagonjwa pamoja na walezi wao,” alisema CPA Prof. Mzenzi.
Aidha, wahasibu waliokuwa wakihudhuria mafunzo, wakiwemo washiriki wa Warsha ya Uendelevu ya IPSAS, walichangia fedha kwa ajili ya kusaidia kugharamia vipimo na dawa kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama hizo.
Mchango huo uliwakilishwa na CPA Sura Sabas Kimboka, ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Usaidizi katika Mahakama ya Rufani za Kodi (TRAT), kwa kushirikiana na washiriki wengine wa mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Dkt. Zaid Kihando, Mratibu wa Huduma za Tiba aliyemwakilisha Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, aliishukuru NBAA pamoja na wahasibu kwa kuendelea kuona umuhimu wa kusaidia jamii kupitia utoaji wa misaada na uchangiaji damu.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya dhamira ya NBAA ya kuchangia maendeleo ya jamii na kusaidia sekta ya afya sambamba na majukumu yake ya kitaaluma. Wananchi na wadau mbalimbali wameipongeza Bodi hiyo kwa moyo wa kujitolea na mshikamano uliooneshwa, wakieleza kuwa ni mfano bora wa taasisi kushiriki katika shughuli za kijamii.
Kupitia juhudi hizi, NBAA inaendelea kudhihirisha kuwa mchango wake hauishii kwenye taaluma pekee, bali pia unalenga kuboresha maisha ya jamii kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Siasa I. Mzenzi akishuhudia makabidhiano ya misaada kati ya Mkurugenzi wa Huduma za Viwango vya Kiuhasibu, Utafiti na Huduma za Ufundi wa NBAA, Angyelile Tende pamoja na Dkt. Zaid Kihando, Mratibu wa Huduma za Tiba aliyemwakilisha Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.Baadhi ya watumishi wa NBAA, wahasibu pamoja na madakatari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kukabidhi misaada hiyo katika hospitali hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Siasa I. Mzenzi akizungumza kuhusu namna walivyoguswa kuja kutoa misaada katika
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro
Dkt. Zaid Kihando, Mratibu wa Huduma za Tiba aliyemwakilisha Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro akiwakaribisha wageni kutoka NBAA wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo CPA Prof. Siasa I. Mzenzi pamoja na Wahasibu waliofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kutoa misaada.
Mkurugenzi wa Huduma za Usaidizi katika Mahakama ya Rufani za Kodi (TRAT), CPA Sura Sabas Kimboka ambaye aliwawakilisha washiriki wengine wa mafunzo ya NBAA akizungumza namna walivyoweza kufanya malipo ya matibabu kwa ajili ya baadhi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.











No comments:
Post a Comment