HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

BALOZI SEIF AKUTANA NA MKUU WA JESHI LA POLISI NCHINI

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake Vuga kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifafanua tatizo la Udhalilishaji dhidi ya Wanawake na Watoto linaloonekana kuathiri Jamii wakati akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro.



Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro amesema mwamko mdogo wa kielimu walionao Wananchi wengi ndio unaopelekea ongezeko kubwa la vitendo vya udhalilishaji vinavyoendelea kushuhudiwa kufanyika kila kukicha katika maeneo mbali mbali hapa Nchini .

Alisema baadhi ya Watu wakorofi wamekuwa wakitumia udhaifu huo kwa kuendeleza vitendo viovu dhidi ya Wanawake na Watoto ambao huathirika kiakili na kimwili na kuwapa wakati mgumu wa kuendelea na maisha yao ya kawaida ndani ya Jamii inayowazunguuka.

IGP Simon Sirro alieleza hayo wakati alipofika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.

Kamanda Sirro alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba katika kukabiliana na vitendo hivyo viovu vinavyoonekana kuleta fadhaa inalazimika kwa Jamii wakati huu kubadilika kwa kuwa tayari kutoa ushahidi pale wanaposhuhudia vitendo hivyo.

Alisema kesi yoyote inategemea kuendeshwa katika misingi na taratibu za Kisheria kwa kuzingatiwa ushahidi unaotolewa na mashahidi ili haki inapotolewa iende sambamba na stahiki ya pande zote husika.

Kamanda sirro aliitahadharisha Jamii inayopenda kulalamika zaidi kwamba nje ya kukosekana kwa ushahidi wa tuhuma zozote zinazowasilishwa Polisi na hatimae kwenye Ofisi ya Muendesha Mashtaka maana yake hakuna kesi itakayoendelea hata kama kuna mtu aliyedhulumiwa.

Alisema zipo kesi nyingi za udhalilishaji hasa zile za utelekezaji wa familia zinazofanywa na baadhi ya Wanaume zaidi upande wa Tanzania Bara zinazofikia zaidi ya asilimia 80% na kusababisha familia husika kukosa matunzo jambo ambalo huchangia ongezeko la Watoto wa Mitaani wanaokosa malezi ya Familia.

“ Tunafarajika kuona kwamba ipo Sheria ya adhabu dhidi ya Watu wanaotupa na kutelekeza Familia zao kwa upande wa Tanzania Bara ambayo imekuwa ikitumika na kupunguza matukio kama hayo ”. Alisema Kamnada Simon Sirro.

Akizungumzia hali ya Amani Nchini Tanzania Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Tanzania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Nchi bado iko shwari licha ya matukio ya hapa na pale yanayoshuhudiwa katika Maeneo ya Rufiji.

IGP Sirro kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi waendelee kushirikiana na vikosi vya ulinzi katika kutoa Taarifa za matukio ya uhalifu, Ujambazi na Uhujumu Uchumi kwenye maeneo yao ili vyombo vya Ulinzi vitumie maarifa yake katika kuwasaka wahalifu hao.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alilishauri Jeshi la Polisi kuongeza nguvu katika ujenzi wa Makaazi ya Askari wake ili kuondosha mfumo uliopo hivi sasa wa Askari wengi kuishi Mitaani pamoja na Raia.

Balozi Seif alisema kitendo hicho cha Askariu kuishi Mitaani kinaleta muhali sana kwao na kushindwa kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya Jamaa na marafiki pale wanapofanya makosa na baadae kuwasilishwa kwao.

Akigusia janga la Dawa za Kulevya Nchini Balozi Seif alimueleza Kamanda Sirro kwamba tatizo hilo Bado linaonekana kuleta madhara hasa kwa upande wa Visiwa vya Zanzibar kutokana na Vijana wengi kuonekana watumiaji wakubwa wa Dawa hizo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/6/2017.

BALOZI SEIF ASHIRIKI MAZIKO YA MZEE KHAMIS JUMA MKADARA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Tatu kutoka Kulia akijumuika pamoja na Viongozi na Wananchi katika kumsalia Mwanasiasa Mkongwe wa Kisiwani Pemba Mzee Khamis Juma Mkadara kwenye Msikiti wa Ijumaa Wawi Chake chake Pemba.  Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Juma {Mabodi } na kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Kilimo, Mali Asili, Mifugo na Uvuvi Mh. Hamad Rashid Mohamed.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mtaa wa Wawi Chake chake wakiwa miongoni mwa wananchi waliomsalia Kiongozi huyo nguli wa Kisiasa Kisiwani Pemba Mzee Mkadara.
Balozi Seif akimimina mchanga katika Kaburi la Mzee Khamis Juma Mkadara aliyezikwa katika Mavani ya Familia yake yaliyopo Mashariki ya Msiku wa Ijumaa wa Wawi Chake chake.
Balozi Seif wa Pili kutoka Kulia akiwa sambamba na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Juma { Mabodi } wakiwafariji wanafamilia ya Mwanasiasa Mkadara Nyumbani kwake Wawi Chake chake.
Baadhi ya Wanafamilia ya Mzee Khamis Juma Mkadara wakionyesha sura za majonzi na huzuni kufuatia kuondokewa na mpendwa wao aliyekuwa kiungo katika familia hiyo.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Mabodi wa Pili kutoka Kulia akiwataka kuwa na moyo wa subra Wajukuu wa Mzee Mkadara. Picha na – OMPR – ZNZ.                                                                                                    


Mwanasiasa Mkongwe wa Zanzibar Mzee Khamis Mkadara aliyefariki Dunia mapemba jana asubuhi amezikwa Kijijini kwake Wawi Mkoa wa Kusini Pemba maziko yaliyohudhuriwa na Mamia ya Waumini wa Dini ya Kiislamu, Wananchi pamoja na Viongozi wa Kiserikali na Kisiasa. 


Mzee Khamis Mkadara alikuwa akisumbuliwa na Maradhi ya kawaida pamoja na uzee alifariki nyumbani kwake Mtaa wa Wawi Wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika mazishi hayo aliiwakilisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Chama cha Mapinduzi akijumuika na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Mabodi na baadhi ya watendaji wa Serikali.

Marehemu Mzee Khamis Juma Mkadara alizaliwa Mwaka 1927 na kuanza elimu ya Quran katika Madrasa mbali mbali za Wilaya ya Chake chake ambapo baadaye katika ujana wake akajishughulisha na masuala ya Kisiasa katika dhana nzima ya kudai Uhuru wa Visiwa vya Zanzibar.

Katika kipindi hicho ya kutaka kujikomboa Mzee Mkadara alikuwa muanzilishi wa Chama cha Shirazy Association na baadaye kukiunganisha na chama cha African Association na Kuzaliwa kwa Chama cha Afro Shirazy Party.

Katika utumishi wa Chama Mzee Khamis Juma Mkadara aliwahi kuwa Mwenyekiti wa ASP wa Wilaya ya Chake chake mwaka 1973 na baada ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi mwaka 1977 aliendelea na wadhifa huo hadi mwaka 1997.

Mbali ya wadhifa huo wa Kichama Mzee Mkadara pia aliwahi kuwa Diwani wa Wadi ya Wawi mwaka 1995.

Mwanasiasa huyo mkongwe Kisiwani Pemba alikuwa mstawi wa mbele katika utetezi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akiwa miongoni mwa Wazee waliotumikia kwa kiindi kirefu Taifa hili la Tanzania.

Utumishi huo uliweza kumpatia fifa na ushujaa uliopelekea kutunukiwa nishani na Rais Mstaafu wa Tanzania Awamu ya Nne Dr. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Sita Dr. Aman Abeid Karume.

Mzee Khamis Juma Mkadara aliyefikisha umri wa Miaka 90 ameacha Kizuka Mmoja, Watoto Wanane na Wajukuu 33.

Mwenyezi Muungu ailaze roho ya Mwanasiasa huyo Mkongwe Mzee Khamis Juma Mkadara mahali pema peponi. Amin.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
8/6/2017.



BALOZI SEIF ATAKA UFUMBUZI WA KUDUMU UPATIKANE BAINA YA MWEKEZAJI NA WANANCHI WA ENEO LA PWANI YA MTONI

Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud kati kati akimuonyesha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi maeneo yalioathirika na mawimbi la Maji ya Bahari katika Pwani ya Mtoni.
Balozi Seif Ali Iddi akikagua baadhi ya maeneoyaliyoathirika na kasi ya maji ya Bahari na kusababisha mmong’onyoko wa ardhi ulioathiri baadhi ya Nyumba za Mtaa huo wa Asili.
 Sheha wa Shehia ya Mtoni Bwana Hassan Zaid Ali wa kwanza kutoka Kushoto akielezea athari za mmong’onyoko wa ardhi zinazolikumba eneo la Pwani ya Mtoni toke asili.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Tathmini ya Athari zaKimazingira Ndugu Ali Vuai Pandu akitoa ufafanuzi wa tathmini ya awali iliyofanywa na Wataalamu wa Kitengo chek katika eneo la Pwani ya Mtoni mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Mzee wa Mtaa wa Pwani ya Mtoni Bwana Yussu Amour Abdulla akimueleza Balozi Seif changamoto zinazowakumba Wananchi wa eneo hilo za kuongezeka kwa kina cha Maji ya Bahari na kuathiri makaazi yao.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameziagiza Taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa Mazingira, Halmashauri ya Wilaya pamoja na Wananchi wa Mwambao wa Pwani ya Mtoni kukaa pamoja na Muwekezaji wa mradi wa Hoteli ya Kimataifa inayojengwa Mtoni Marine ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la athari ya maji ya Bahari yanayolikumba eneo hilo.



Alisema hatua hiyo itatoa muelekeo mzuri wa pamoja utakaoepusha migogoro kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili ile ya Muwekezaji pamoja na Wananchi wa Eneo la Pwani ya Mtoni.


Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo alipofanya ziara fupi ya kukagua eneo la Pwani ya Mtoni na kusikiliza malalamiko yaWananchi wa sehemu hiyo kufuatia maji ya bahari kuvamia maeneo yao na kuleta athari kubwa ya kimazingira bila ya kujua hatma yao ya hapo baadae.


Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari kupokea ushauri wa pande hizo pamoja na kusubiri ripoti ya awali ya Kitaalamu inayofuatilia mwenendo mzima ya athari za kimazingira katika eneo hilo katika kipindi cha Miaka Kumi iliyopita.


Balozi Seif aliwataka ma kuwaomba Wananchi hao kuwa na subra wakati

Serikali yao ikiendelea kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo linalohitaji umakini mkubwa hasa ikizingatiwa mabadiliko ya kimaumbile ya mazingira yanayojitokeza na kuathiri mambo mbali mbali Nchini.


Mapema akitoa ushauri wa athari zinazolikumba eneo hilo na mabadiliko

yake yanayojitokeza Mzee Yussuf Amour Abdulla alisema Mji wa Pwani ya
Mtoni upo tokea Karne ya 18 wakati eneo hilo lilikuwa njia ya Reli.


Mzee Yussuf alisema zipo nyumba zilizoathirika kwa kukatika na nyengine kubomoka kutokana na kasi ya maji ya Bahari katika kipindi hichi jambo ambalo limewatia wasi wasi wa hatma yao na vizazi vyao hapo baadae.


Alisema ipo mito miwili iliyokuwa akiingiza na kutoa maji ya habari

 wakati wa maji Makuu lakini kilichojitokeza wakati huu ni sehemu ndogo
iliyosalimika na maji ya bahari kutokana na uwepo wa miti ya Mikoko.


Mwakilishi huyo wa Wananchi wa Mtaa wa Pwani ya Mtoni aliishukuru na

kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Viongozi wake kwa umakini wake mkubwa inayoendelea kuuchukuwa wa kuwajali Wananchi wake inaowaongoza.


Alisema kitendo cha Viongozi hao kuanzia ngazi ya Juu, Kati, Mkoa hadi Wilaya kimethibitisha hali hiyo jambo ambalo kwao limekuwa likileta

faraja na kuwapa muelekeo wa maisha ya matumaini.


Akitoa ufafanuzi wa Kitaalamu Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Tathmini ya Athari za Kimazingira Ndugu Ali Vuai Pandu alisema uchunguzi wa awali

uliofanywa na Wataalamu kuhusu athari za Kimazingira wa eneo hilo
umeonyesha dalili zitazojichomoza za athari za Mazingira katika Pwani
ya Mtoni.


Nd. Ali alisema kipimo cha madhara ambayo yanajitokeza wakati wa uendelezaji wa mradi kwa mujibu wa Mikataba inayofungwa kinamuwajibika

muwekezaji kuondosha kasoro zinazojichomoza ambazo zina muelekeo wa
kuathiri jamii ya eneo husika.


Hata hivyo Kaimu Mkuu huyo wa Kitengo cha Tathmini ya Athari za Kimazingira alifafanua wazi kwamba Hali ya Hewa ya Kimaumbile nayo

imekuwa ikichangia madhara yanayojichomoza sehemu mbali mbali
kunakosababisha na mabadiliko ya Tabia Nchi.


Mapema Sheha wa Shehia ya Mtoni Bwana Hassan Zaid Ali alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba hali ya mmong’onyoko wa ardhi katika Pwani ya Mtoni umekuwepo tokea asili.


Bwana Hassan alisema mmong’onyoko huo ulikuwa akisababishwa na kasi ya

maji ya bahari kulingana na Bamvua la msimu wa mabadiliko ya upepo, lakini hivi sasa kasi ya Mmong’onyoko huo inaonekana kuongezeka zaidi
na kutia wasi wasi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/6/2017.

BALOZI SEIF ASHIRIKI MSIBA WA MAMA MZAZI WA NAIBU KATIBU MKUU MSTAAFU WA CCM ZANZIBAR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimfariji Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai aliyefiwa na Mama yake Mzazi Bibi Mwanaisha Hassan Vuai aliyezikwa kijijini kwao Bwejuu Mkoa wa Kusini Unguja.
Waumini wa Dini ya Kiislamu wakimsalia Bibi Mwanaisha Hassan Vuai katika Msikiti wa Ijumaa Bwejuu aliyefariki Dunia jana katika Hospitali ya Global alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu na Viongozi wa Serikali na Kisiasa wakimuombea Dua Marehemu Bibi Mwanaisha Hassan Vuai baada ya kumsalia kwenye Msikiti wa Ijumaa wa Bwejuu Mkoa Kusini Unguja.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu na Viongozi wa Serikali na Kisiasa wakimuombea Dua Marehemu Bibi Mwanaisha Hassan Vuai baada ya kumsalia kwenye Msikiti wa Ijumaa wa Bwejuu Mkoa Kusini Unguja.
Balozi Seif Ali Iddi kushoto akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa Kusini Unguja Nd. Ramadhan Abdullah Ali wakati wa msiba wa Mama Mzazi wa Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Zanzibar hapo Bwejuu Mkoa Kusini Unguja.

                                                     Picha na – OMPR – ZNZ.

BALOZI SEIF AREJEA ZANZIBAR AKITOKEA JORDAN

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na baadhi ya Mawaziri na Watendaji Wakuu wa Serikali mara alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume akitokea Nchini Jordan kushiriki Mkutanowa Jukwaa la Dunia la Uchumi akimuwakilisha Rais wa Jamuhuri ya Mauungano wa Tanzanmia Dr. John Pombe Magufuli.
Balozi Seif Kushoto akibadilishana Mawazo na Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika chumba cha Watu Mashuhuri {VIP} Kongwe. Picha na – OMPR – ZNZ.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewasili Zanzibar akitokea Mjini Amman Nchini Jordan kuhudhuria Jukwaa la Dunia la Uchumi World Economy Forum - WCF} la Siku Tatu litakalohudhuriwa na zaidi ya Wajumbe 2,000 kutoka Nchi 58 Duniani.




Balozi Seif alimuwakilisha Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwenye Jukwaa hilo la Kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika lililoshirikisha Viongozi Wakuu wa Nchi, Wafanyabiashara,wamiliki wa Makampunni ya Kimataifa, Wawakilishi wa Taasisi za Kiraia, Mashirikia ya Kimataifa, Wana Habari pamoja naVijana wapatao 2,000.


Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipokewa na baadhi ya Mawaziri, Watendaji Wakuu wa Serikali pamoja naViongozi wa Kisiasa. 



Katika Mkutano huo wa Jukwaa la Dunia la Uchumi Balozi Seif aliongozana na Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Balozi Amina Salum Ali, pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa


Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed.


Katika Mkutano huo wa Jukwaa la Dunia la Uchumi Balozi Seif na Ujumbe wake alishiriki Washa ya Utalii iliyojikita zaidi katika masuala ya Kujenga Uchumi kwa Mataifa yaMashariki ya Kati na yale ya Kanda ya Afrika ili kuona njia gani


zinaweza kutoa fursa za ajira kwa Vijana kwa kutumia Teknolojia ya Kisasa


Mkutano huo wa Jukwaa la Uchumi Duniani ulifunguliwa na Kiongozi wa Jordan Mfalme wa Pili Abdullah Bin Al-Hussein kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa King Hussein Bin Talal katika Bahari Nyeusi.



Jukwaa la Uchumi la Dunia { World Economy Fforum - WCF} limeasisiwa Mwaka 1971 chini ya Muanzilishi na Mwenyekiti wake Profesa Klaus Schwab huko Davos, Switzerland.


Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

24/5/2017.




BALOZI SEIF AFUNGUA TAMASHA LA TANO LA ZAHILFE

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Tamasha la Tano la Michezo ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar { ZAHILFE} kwenye Uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amani Zanzibar Riziki Pemba Juma kulia akiteta na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Mashindano ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} hapo katika uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amani Zanzibar Riziki Pemba Juma akitoa salamu za Wizara kwenye Tamasha la Mashindano ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} hapo katika uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Viongozi wa Michezo na Serikali walioshuhudia ufunguzi wa Tamasha la Mashindano ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} hapo katika uwanja wa Amani.
Kutoka Kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar {BTMZ}, Mkuu wa Mkoa Mjini Maghribi Ayoub Mohamed Mahmoud na Mkuu wa Wilaya ya Mjini Marina Joel Thomas.
Balozi Seif akisalimiana na wachezi wa Timu ya Soka ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere { MNMA} waliopambana na Mabingwa watetezi wa Kombe la ZAHILFE Timu ya ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu.
Mabingwa watetezi wa Kombe la ZAHILFE Timu ya soka ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu { ZU} wakisalimiana na Balozi Seif ambae ni mgeni rasmi kwenye pambano lao dhidi ya Timu ya Soka ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere { MNMA}
 Mashabiki wa Timu ya soka ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu { ZU} wakishangiria kwa kujiamini wakati Timu yao ilipotoa kichapo cha Paka mwizi cha Goli 4 kwa Bila dhidi ya Timu ya Soka ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

Picha na – OMPR – ZNZ.

Mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya juu Zanzibar { ZAHILFE} Timu ya Soka ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu {Zanzibar University - ZU} jana ilidhihirisha ubabe wake baada ya kuitandika bila ya huruma Timu ya soka ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere { MNMA} Magoli 4-0.


Mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua kwa muda wote wa dakika 90 ulifungua pazia la mashindao ya Tamasha la Michezo la Shirikisho hilo uliorindima ndani ya Uwanja wa Michezo wa Amani Mjini Zanzibar ambapo Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Watetezi hao ZU walionyesha dalili za mapema za ushindi wa mchezo huo licha ya kuwa mpaka wanakwenda mapumziko hakukuwa na timu iliyoona mlango wa mwezake huku washabiki wa Timu zote mbili wakishindwa kukaa kwenye majukwa ya uwanja huo.

Kipindi cha pili kilianza kwa mikiki mikiki kwa timu zote mbili lakini uzoefu na utaalamu wa Timu ya ZU ukajidhihirisha pale wanandinga hao walipoanza kumimina karamu ya Magoli ndani ya kimia cha MNMA na hadi mwisho wa mchezo huo ZU 4 na MNMA 0.

Akiizindua michezo hiyo ya Tamasha la Tano la Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} tokea kuanzishwa kwake Mwaka 2013 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema utunzwaji wa vipaji vinavyoibuliwa ndani ya mashindao hayo lazima uendelezwe ili kupata wanamichezo bora watakakidhi kiwango cha Kitaifa na Kimataifa.

Balozi Seif alisema mashindano ya Tamasha la Shirikisho la Zahilfe ni mwanzo wa kuelekea njia sahihi ya kupata vipaji hivyo sambamba na kuchangamsha akili za Wanafunzi katika kukabiliana vyema na masomo yao ya kila siku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Sera ya Michezo Zanzibar ya Mwaka 2007 imeweka umuhimu wa kuimarisha Sekta ya Michezo Vyuoni na Maskulini Unguja na Pemba.

Alisema Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA} kupitia Sera hiyo kimeanzisha mafunzo maalum yalaiyowezesha kutoa Wahitimu 9 wa Stashahada ya Michezo ambao tayari wameanza kusomesha katika maskuli mbali mbali Nchini.

Balozi Seif alihimiza umuhimu wa kuimarishwa michezo Maskulini na Vyuoni kwa vile inasaidia kupatikana kwa matokeo mazuri ya Wanafunzi hasa kwenye mitihani yao pamoja na kuimarika kwa nidhamu miongoni mwa wanafunzi na walimu wao.

Alisema nidhamu inamuwezesha mtu sio mwanafunzi pekee kufanya kazi zake kwa mipango maalum na akafarajika na utaratibu wa kuanzishwa kwa mashindano ya Zahilfe yatakayofungua njia sahihi ya kudumisha nidhamu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo na Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Amali Zanzibar kwa jitihada za watendaji wake kuwaweka pamoja Wanamichezo hapa Nchini.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pemba Juma ameipongeza Benki ya Biashara ya NMB kwa moyo wa kizalendo wa kuamua kwa makusudi kusaidia Sekta ya Elimi Visiwani Zanzibar.

Waziri Riziki alisema Benki ya NMB mbali ya kusaidia Sekta ya Michezo lakini pia juhudi zake za kusaidia Kompyuta 50 pamoja na Vikalio 450 kwa Skuli za Zanzibar ni ushahidi wa wazi unaothibitisha kwamba Uongozi wa Benki hiyo unaendelea kujali umuhimu wa Sekta ya Elimu inayofinyanga wataalamu wa fani zote.

“ Benki ya NMB imekuwa mshirika mkubwa wa Sekta ya Elimu Nchini, mbali ya kusaidia michezo lakini pia kuongeza nguvu zake katika kupunguza uhaba wa Vikavio na vifaa muhimu maskulini kama Kompyuta”. Alisema Waziri wa Elimu Zanzibar.

Akitoa salamu katika uzinduzi huo wa Tamasha la Michezo ya Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} Afisa Mkuu Wateja wadogo wadogo na wa kati pamoja uendeshaji Matawi ya Benki ya NMB Bwana Abdulmajid Nsekela alisema Taasisi hiyo ya kifedha itaendelea kusaidia huduma za Kijamii kadri mapato ya makusanyo yake yanavyoongezeka.

Bwana Nsekela alisema wadau wakuu wa Taasisi hiyo wengi wao ni Wananchi, hivyo hakuna budi wala kigugumizi kwa Uongozi wa Benki hiyo kuzipa kisogo changamoto zinazowakabili Wananchi hao katika maeneo yao wanayoishi.

Hilo ni Tamasha la Tano la Michezo inayoandaliwa na Shirikisho la Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar {ZAHILFE} tokea kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2013.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

15/5/2017.













BALOZI SEIF AONGOZA DUA MAALUM YA KULIOMBEA AMANI TAIFA

Waumini wa Dini ya Kiislamu wakisoma Dua maalum ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu pamoja na kujiandaa kuukaribishwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani iliyofanyika katika Msiki wa Ijumaa Malindi Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akijumuika pamoja na Waumini mbali mbali wa dini ya Kiislamu Nchini katika Dua maalum ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu pamoja na kujiandaa kuukaribishwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kulia ya Balozi Seif ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Ka’abi pamoja na Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam Sheikha Alhad Mussa Salum.
Mufti Mkuu wa Tanzania Bara Sheikh Abubakar Zubeir Ali wa kwanza kutoka Kushoto, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji pamoja na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud walikuwa miongoni wa Viongozi walioshiriki Dua
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Madhehebu ya Shia Kutoka Nchni Iran waliojumuipa pamoja na Waumini wa Zanzibar katika Dua ya kuliombea Taifa Aman.
Maulamaa na wahadhiri kutoka Nchini Misri nao walikuwa miongoni mwa washiriki wa Dua hiyo iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa Malindi.
Baadhi ya Maimamu wa Misikiti mbali mbali ya Mkoa wa Mjini Magharibi wakisoma Dua hiyo maalum ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu pamoja na kujiandaa kuukaribishwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa nasaha ya kuwataka waumini na Wananchi kuendelea kudumisha Amani kwenye Dua ya Kuliombea Taifa amani. Picha na – OMPR – ZNZ.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mkusanyiko wa Waumini wa Dini ya Kiislamu katika mfumo wa kushikamana bila ya kufarakana daima huzaa baraka zinazootesha neema na kheir miongoni mwa Umma huo mtukufu mbele ya Muumba wao Mwenyezi Mungu.


Alisema Vitabu vya Dini na Miongozo yote iliyotolewa katika Vitabu hivyo imekuwa ikielekeza na kusisitiza umuhimu wa Binaadamu hasa Wale walioamini Vitabu hivyo kushikamana pamoja ili lile lengo lao la kumuabudu Mwenyezi Muungu likamilike bila ya kutetereka kwa kitu chochote kile.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa Dua Maalum ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu pamoja na kujiandaa kuukaribishwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaokaribia kuingia wiki chache zijazo dua iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa Malindi Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na Mamia ya Waumini wa Dini ya Kiislamu, Wananchi pamoja na baadhi ya Viongozi wa Serikali na Kisiasa.

Alisema Waumini na Wananchi wote wanapaswa kuzingatia umuhimu wa suala la Amani iliyopo Nchini kwani kwa kufanya hivyo kutatoa fursa kwa Waumini hao kutekeleza kwa utulivu Ibada zao sambamba na Wananchi kuendelea na harakati zao za Kimaisha za kila siku.

Aliwahimiza Waumini wa Dini zote hapa Nchini kuendeleza Dua mbali mbali ambazo ndio ufunguo wa Ibada yoyote ile inayomuelekeza Mja kudumu katika ucha Mungu unaotakiwa kudumishwa katika mazingira yanayomzunguuka ya kila siku.

Balozi Seif aliwashukuru Wananchi wa Kisiwa cha Pemba kwa mshikamano wao waliouonyesha ndani ya kiindi hichi cha Mvua za Masika zilizoleta maafa na kusababisha Mamia ya Wakaazi wake kukosa sehemu za Kuishi baada ya nyumba zao kujaa maji na nyengine kuanguka kabisa.

Alisema kitendo hicho cha mshikamano kimerejesha mafungamano ya Wananchi hao kilichokosekana kwa kipindi kirefu kutokana na itikadi zao tofauti za Kisiasa zilizosababisha kutengana na kuleta athari kubwa hata kwenye maeneo ya Ibada katika kumcha Mwenyezi Mungu.

Akizungumzia ujio la Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuingia wiki chache zijazo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alitoa wito kwa Wafanyabiashara wote hapa Nchini kuacha tabia ya kupandisha bei za bidhaa muhimu zinazotumiwa kwa wingi na waumini wa Dini ya Kiislamu katika kipindi hicho cha saumu.

Alisema tabia hiyo mbaya ni dhambi kubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitakuwa na huruma katika kuwachukulia hatua za kisheria wafanyabiashara wowote watakaopandisha bei bidhaa zao bila ya sababu za msingi zitakazokubalika.

Balozi Seif alisema ni vyema kwa Wafanyabiashara kuwaonea huruma Waumini watakaofunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambao wengi kati yao wanaeleweka upatikanaji wa kiato chao unakuwa na mazingira ya mashaka.

Mapema Mufti Mkuu wa Tanzania Bara Sheikh Abubakar Zubeir Ali alisema Dua ni fursa kubwa inayompa fursa Mwanaadamu kumuomba Mungu amuelekeze katika njia ya Amani.Sheikh Zubeir alisema Mwenyezi Muungu muda wote hutarajia kuombwa na waumini wake vyenginevyo anaondosha baraka zake na kutowajaalia kheir na hatma njema waombaji hao anayoisisitiza kila siku kufanywa na waja wake.

Hata hivyo Mufti Mkuu huyo wa Tanzania alitahadharisha wazi kwamba zipo ishara zinazoanza kujichomoza za mmong’onyoko wa Maadili unaotishia kutetereka kwa Amani jambo ambalo kila Muumini na Mwananchi anapaswa kuliondoa au kulikemea lisije kuleta athari hapo baadae.

Akimkaribisha Mgeni rasmi katika Dua hiyo Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud aliipongeza Kamati ya Amani ya Kitaifa Zanzibar kwa juhudi inazochukuwa za kuhakikisha kwamba Taifa la Tanzania linaendelea kuwa na utulivu.

Mh. Ayoub alisema Dua hiyo ni tukio muhimu kwa Mustakabala wa Taifa hili na aliwaomba Waumini na Wananchi wote popote pale walipo kuendelea kuwaombea dua Viongozi wao waliojitolea kusimamia mapambano dhidi ya Dawa za kulevya na Mmong’onyoko wa Maadili unaooneka kuliathiri Taifa hasa kundi kubwa la Vijana.

Katika shughuli hiyo ya dua Maalum ya kuliombea Taifa Amani na Utulivu pamoja na kujiandaa kuukaribishwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Masheikh na Maulamaa wa Mkoa Mjini Magharibi wametoa zawadi Maalum kwa Rais wa Zanzibar Al – Hajj Dr. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud.

Zawadi hizo wamezitoa kutokana na mchango mkubwa wa Viongozi hao katika kusimamia suala la Amani, mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya Nchini pamoja na kuzuia mmong’onyoko wa Madili ulioonekana kupotea siku za nyuma.

Dua hiyo ya Ighaathatul – Mustaghiith ambayo pia husomwa kila jumatano baada ya sala ya Ishaa katika Msikiti huo wa Ijumaa wa Malindi iliongozwa na na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Kitaifa Zanzibar Sheikh Salim Mohamed Hassan.

Othman Khamks Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

14/5/2017.

BALOZI SEIF AKUTANA NA MWAKILISHI WA KAMPUNI YA UJENZI YA GARWARE YA INDIA

Kaimu Balozi wa Tanzania Inchini India Balozi Mohamed Hija kulia akifafanua jambo wakati wa mazungumzo ya Viongozi wa Kampuni za Kimataifa ya Ujenzi ya GARWARE na Taasisi inayojishughulisha na Masuala la Sekta ya Elimu ya Arun (U) ltd ya Nchini India walipokutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayojishughulisha na Masuala la Sekta ya Elimu ya Arun (U) ltd ya Nchini India Bwana Jatinder Sehgal na wa kwanza kushoto ni Balozi Seif.
Balozi Seif akibadilishana mawazo na Ujumbe huo wa Makampuni na Taasisi za Uwekezaji kutoka Nchini India mara baada ya mazungumzo yao.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya GARWARE ya Nchini India Bwana Kedar Chapekar amesema Zanzibar ina uwezo wa kuwa kituo cha Kimataifa cha Kibiashara kinachofanana na Dubai kutokana na rasilmali ya kimazingira iliyonayo.


Bwana Kedar alieleza hayo akiambatana na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayojishughulisha na Masuala la Sekta ya Elimu ya Arun (U) ltd ya Nchini India Bwana Jatinder Sehgal wakati wakizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Viongozi hao wa Taasisi za Uwekezaji za Nchini wapo Zanzibar kwa ziara ya Wiki moja kuangalia fursa mbali mbali za Uwekezaji zilizopo Zanzibar kufuatia mualiko wa Balozi Seif wakati wa ziara yake ya hivi karibuni Nchini India.

Alisema Zanzibar iko katika mazingira mazuri ya Kibiashara ndani ya mwambao wa Afrika Mashariki pamoja na Ukanda wa Kusini Mashariki mwa Bara la Afrika ambayo bado haijatumika vyema kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Bwana Kedar alimueleza Balozi Seif kwamba Taasisi zao za uwekezaji zimepata fursa nzuri ya kuangalia hali halisi ya kimazingira iliyopo Zanzibar na Uongozi wa Taasisi hizo utaangalia maeneo ambayo wanaweza kuwekeza Visiwani Zanzibar.

Naye Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayojishughulisha na Masuala la Sekta ya Elimu ya Arun (U) ltd ya Nchini India Bwana Jatinder Sehgal alisema upo uwezekano wa Zanzibar kuwa na Ukumbi mkubwa wa Kimataifa unaoweza kutoa huduma za Mikutano ya Kimataifa.

Bwana Jatinder Sehgal alisema ukumbi huo kwa upande mwengine unaweza kuhamasisha kasi ya uwekezaji ambayo tayari imeshachaguliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa muhimili wa Uchumi wake utakaoweza kusaidia kunyanyua Mapato ya Taifa.

Akitoa shukrani zake kufuatia ujio wa Ujumbe huo wa Wawekezaji kutoka Nchini India kufuatia ziara yake ya hivi karibu Nchini India Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanziba imejiwekea malengo ya kuwa kituo na kitovu cha Utalii katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Balozi Seif alisema uimarishaji wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar pamoja na miundombinu ya mawasiliani ya bara bara ni jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuona Sekta hiyo inaanza muelekeo mzuri wa kuimarika Kiuchumi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza Taasisi na Makampuni ya Nchini India yaliyoonyesha nia ya kutaka kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi Visiwani Zanzibar katika azma yao ya kuunga mkono jitihada za SMZ za kuimarisha mipango ya Maendeleo.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

8/5/2017.