Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi kwa kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Kupitia banda la NBAA, wananchi, wanafunzi, wahitimu na wadau mbalimbali wanapata fursa ya kujifunza kuhusu Taaluma ya Uhasibu, pamoja na kupata huduma mbalimbali za kitaaluma zinazotolewa na Bodi.
Huduma zinazotolewa katika banda hilo ni pamoja na usajili wa mitihani ya Certified Public Accountant (CPA), usajili wa uhamaji wa madaraja kwenda Associate Certified Public Accountant (ACPA) na Associate Certified Public Accountant in Public Practice (ACPA-PP), usajili wa kampuni za Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu, kozi za muda mfupi za maendeleo endelevu ya Taaluma, pamoja na ushauri kuhusu fursa mbalimbali zinazotolewa na NBAA.
Aidha, wanafunzi wanaotamani kujenga Taaluma ya Uhasibu wanapatiwa elimu kuhusu hatua za kuanza safari ya kuwa Wahasibu na Wakaguzi wa hesabu waliosajiliwa, sifa zinazohitajika pamoja na fursa za maendeleo ya kitaaluma zinazopatikana kupitia NBAA.
Ushiriki wa NBAA katika maonesho hayo ni sehemu ya jitihada za Bodi za kuendelea kuwafikia wananchi, kuongeza uelewa kuhusu huduma zake na kuhamasisha vijana wengi zaidi kujiunga na taaluma ya uhasibu ili kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi.
Maonesho ya Nanenane 2026 yanaendelea na kaulimbiu ni"Tambua Soko, Ongeza Tija, Kuendeleza Dira ya Taifa 2050." NBAA imewahimiza wananchi kutembelea banda lake ili kupata elimu, ushauri wa kitaaluma na huduma mbalimbali zinazotolewa na Bodi.
Watumishi wa NBAA wakiwa kwenye picha ya pamoja kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya akitoa elimu kwa mwananchi aliyetembelea Banda la Bodi hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) 2026
Mfanyakazi wa NBAA Happiness Mwamwembe akitoa elimu kwa wananchi waliofika katika Banda la Bodi hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) 2026



No comments:
Post a Comment