HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AKABIDHIWA VIFAA TIBA VYA UZAZI ZAIDI YA 200 NA BALOZI WA KUWAIT HAPA NCHINI

Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan akitazama moja ya Dawa,mara baada ya kukabidhiwa mapema leo Ikulu jijini Dar,vifaa tiba vya uzazi zaidi ya 200 na Balozi wa Kuwait hapa nchini,Mhe,Jasem Al-Najem,vifaa hivyo vitasambazwa katika hospitali mbalimbali kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Balozi wa Kuwait hapa nchini Jasem Al- Najem amemkabidhi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan vifaa tiba vya uzazi zaidi ya 200 ambavyo vitasambazwa katika hospitali mbalimbali kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Makabidhiano ya vifaa hivyo vya uzazi yamefanyika leo Ikulu ya Dar es Salaam ambapo Balozi wa Kuwait hapa Nchini Jasem Al- Najem amesema Serikali ya nchi hiyo imetoa vifaa hivyo kama hatua ya kuendelea kudumisha na kuendeleza mahusiano mazuri kati ya nchi hiyo na Tanzania.

Amesema kuwa Serikali ya Kuwait imetoa vifaa hivyo ikiwa ni awamu ya kwanza na lengo ni kutoa vifaa hivyo zaidi ya 1000 vyenye thamani ya shilingi milioni 40 kwa wanawake wajawazito na waliojifungua katika hospitali mbalimbali nchini.

Mara baada ya kupokea msaada huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameishukuru Serikali ya Kuwait kwa msaada huo ambao utasambazwa katika hospitali mbalimbali kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema msaada huo utasaidia sana wanawake wajawazito na waliojifungua kupata vifaa za uzazi ambavyo vinahitajika wakati wanamke mjamzito anapojifungua na baada ya kujifungua.

Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa vifaa hivyo vitaanza kusambazwa kuanzia mwezi huu na mchakato wa kuainishwa hospitali zitakazopata msaada huo unaendelea.

Makamu wa Rais pia amesisitiza kudumishwa kwa mahusiano mazuri yaliyopo kati ya nchi ya Kuwait na Tanzania kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande zote Mbili.

Aidha Balozi huyo wa Kuwait hapa nchini Jasem Al- Najem amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa Serakali ya Kuwait itaendelea kusaidia Serikali ya Tanzania katika uimarishaji wa sekta ya afya na elimu nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za msingi


WAZIRI MAHIGA AFUNGUA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA 69 YA UHURU WA ISRAELI, DODOMA.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 69 ya uhuru wa Taifa la Israel iliyofanyika kwenye Hoteli Morena Mjini Dodoma 
Meza Kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo ya Taifa unakipigwa kweye maadhimisho ya 69 ya uhuru wa Israel 
Balozi wa Israeli nchini mwenye makazi yake Nairobi, Kenya Mhe. Yahel Vilan akizunguza kwenye hafla ya maadhimisho ya 69 ya uhuru wa Israel iliyofanyika mjini Dodoma 
Mhe. Balozi Vilan akisisitiza jambo 
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akihutubia hadhira iliyo shiriki hafla hiyo 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhani (Mwinyi kulia) akifuatilia jambo, kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe. Job Masima 
Picha ya pamoja 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga jana alifungua hafla ya maadhimisho ya 69ya uhuru wa Taifa la Israeli yaliyo fanyika mjini Dodoma katika Hoteli ya Morena.

Hafla hiyo ya maadhimisho ya 69 ya uhuru wa Taifa hilo na uhusiono mzuri wa kidiplomasia  baina ya Tanzania na Israeli yaliratibiwa na Ubalozi wa Israel wenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya.  Waziri Mahiga akizungumza katika hafla hiyo aliupongeza Ubalozi wa Israel kwa uamuzi wake wa kufanyia hafla ya maadhimisho ya 69 ya uhuru wao, Makao Mkuu ya Serikali mjini Dodoma.

 Waziri Mahiga aliongeza kusema Mataifa haya mawili Tanzania na Israel yana mahusiano mazuri ya kidiplomasia, ikidhihirishwa wazi na idadi kubwa ya raia wa nchi hizi mbili kutembeleana na kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo utalii. Aidha Mahiga aliipongeza Serikali ya Israel kwa hatua kubwa ya maendeleo waliyofikia katika maeneo mbalimbali ikiwemo sayansi na teknolojia na kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbalimbali.  

Balozi wa Israeli nchini Mhe. Yahel Vilan mwenye makazi yake Jijini Nairobi, Kenya akitoa hotuba yake alisema Ubalozi wa Israeli umechukua maamuzi ya kufanyia hafla hiyo Mjini Dodoma ikiwa nikuunga mkono maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma. Aliongeza kusema kuwa hafla hiyo ni ishara ya Israel kuanziasha Ubalozi wake nchini Tanzania. 

Balozi Vilan ameihakikishia serikali ya Tanzania kuwa Israel itaendelea kuwa mshirika mzuri wa maendeleo ya Taifa katika maeneo ya kilimo, afya, elimu, sayansi na teknolojia na usalama.Israeli ilifungua kituo cha kushughulikia masuala ya viza nchini Tanzania tarehe 3 Novemba, 2016.


Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia atumia Sikukuu ya Muungano kutangaza Utalii

Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Hemed Mgaza, kushoto akifurahia jambo katika Sikukuu ya Muungano wa Tanzania iliyoadhimishwa nchini humo kwa kukutanisha Watanzania wanaoishi Saudi Arabia, wazawa na viongozi mbalimbali kama sehemu ya kuitangaza vyema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hisani ya Ubalozi wa Tanzania Saudi Arabia.

Na Mwandishi Maalum, Riyadh Saud Arabia
SHEREHE za Sikukuu ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimetumika kama sehemu ya kutangaza utalii wa Tanzania katika tukio maalum lililoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wan chi hiyo.

Akizungumza hivi karibuni katika sherehe hizo za Sikukuu ya Muungano wa Tanzania, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Hemed Mgaza, alisema kwamba Tanzania ni eneo zuri la uwekezaji kutokana na sera zake nzuri pamoja na dhamira njema za viongozi chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli kwa Tanzania Bara pamoja na Dr Ali Mohamed Shein kwa upande wa Visiwani Zanzibar.
Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Hemed Mgaza wa nane kutoka kushoto mstari wa mbele akiwa na wageni mbalimbali katika maadhimisho ya Sikukuu ya Muungano nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kusherehekea pamoja katika siku hiyo muhimu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Picha kwa Hisani ya Ubalozi wa Tanzania Saudi Arabia.
Balozi Mgaza akiwa na mgeni rasmi Prince Muhammad bin abdullahman wakikata keki ya sherehe.
Balozi Mgaza kushoto akikata keki
Balozi Mgaza akihutubia katika hafla hiyo

Alisema kutokana na sera hizo pamoja na kusimamia vyema rasilimali za utalii kama vile Mlima Kilimanjaro, mbuga mbalimbali za wanyama ni sehemu thabiti ya utalii kwa wageni, wakiwamo wananchi wa Saudi Arabia.

“Nchi yetu ina mbuga za wanyama 16 ambazo zimekuwa zikitunzwa na kuhifadhiwa vema kama sehemu ya kuhakikisha kwamba rasimali hiyo inakuza uchumi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Nchi yetu ina wakaribisha wote kutembelea kujionea mambo mbalimbali yanayovutia katika utalii pamoja na kuwekeza katika sekta muhimu zikiwamo za viwanda ambazo ndio agenda kuu kwa sasa nchini mwetu,” Alisema Balozi Mgaza.

Sikukuu ya Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeadhimishwa wiki iliyopita Aprili 26 ambayo hutumiwa kama kioo cha kuangalia matunda yanayojitokeza kutokana na Muungano huo kati ya Tanzania Bara na Visiwani.

Taarifa Potofu Zinazomuhusisha Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza Dr Asha Rose Migiro

Ubalozi wa Tanzania London umepokea Habari inayozagaa kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa instagram ikiwa na nukuu ifuatayo:


''Binafsi bado sijaona umuhimu na mafanikio ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zaidi ya vingozi kujikusanyia mali na utajiri mkubwa sambamba na kung'an'gania madaraka kwa nguvu. Mfano uchaguzi uliofanyika mwaka 2015 kwa yaliyotokea Zanzibar ni miongoni mwa Athari mbaya kabisa zinazotokona na Muungano,nadhani kila Mtanzania aliyaona"

Ukurasa huo wenyewe jina la UKUTA inaihusisha nukuu hiyo na jina la Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Dkt Asha Rose Migiro. 

Ubalozi wa Tanzania London unapenda kutumia fursa hii, kuwajulisha Watanzania Waishio Uingereza na Watanzania kwa ujumla kuwa Balozi Migiro ahusiki na nukuu hiyo kama inavyosambazwa.Hivyo ni wazi kuwa wanayoisambaza wana malengo ya kulichafua jina la Balozi Migiro kwa sababu wanazozijua wao. 

Ubalozi wa Tanzania London unaendelea kutoa wito kwa Watanzania Waishio Uingereza kutumia muda wao na mitandao ya kijamii kutoa mawazo chanya yatakayo imarisha Muungano wa Taifa letu na mustakabali wa maendeleo ya Nchi yetu na Watanzania wa pande zote za Muungano. 

Ubalozi wa Tanzania London 
29 Aprili 2017.

WABUNGE WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WATINGA UBALOZI WA TANZANIA WASHINGTON, DC


Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo siku ya Jumatatu April 24, 2017 wametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na kukutana na Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico Mhe. Wilson Masilingi. Katika picha toka kushoto ni Mkuu wa Utawala na Fedha Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani Bi. Swahiba Mdeme,Mwambata wa Jeshi Ubalozi wa Tanzania na Canada Col. Adolph Mutta, Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Bajeti Mhe. Hawa A. Ghasia, Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico Mhe. Wilson Masilingi, Mbunge Mhe. Janeth Z. Mbene, Mhe. Josephat S. Kandege, Afisa wa Ubalozi Bwn. Dismas Assenga na Afisa wa Bunge Bwn. Godfrey Godwin. Wabunge hao wa Bunge la Jamhuri ya Muungano waTanzania walikuja Washington, DC kuhudhuria mikutano ya kipupwe ya Benki ya Dunia na IMF
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico Mhe. Wilson Masilingi. Katika picha toka kushoto ni Afisa wa Bunge Bwn. Godfrey Godwin, Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Bajeti Mhe. Hawa A. Ghasia, Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico Mhe. Wilson Masilingi, Mbunge Mhe. Janeth Z. Mbene, na Mhe. Josephat S. Kandege.

BALOZI WA MSUMBIJI AKUTANA NA TCCIA KUIMARISHA MAHUSIANO YA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA MSUMBIJI

Balozi wa Msumbiji nchini Bi Monica Patricio Clemente akizungumza na viongozi wa TCCIA walioongozana na Makamu wa Rais-Viwanda Bw. Octavian Mshiu wa kwanza kulia, Mkurugenzi Mtendaji Bw. Gotfrid Muganda pamoja na viongozi wa TCCIA Mtwara Bw. Swallah S. Swallah-Mwenyekiti na Muhidin Swalehe. 

Mkutano huo ulihudhuriwa na Makamu wa Rais wa TCCIA mwenye dhamana ya Viwanda Bw. Octavian Mshiu akiambatana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA Bw. Gotfrid Muganda pamoja na viongozi wa TCCIA Mkoa wa Mtwara Bw. Swallah S. Swallah ambaye ni Mwenyekiti na Bw. Muhidin Swalehe- Afisa Mtendaji.Akizungumza katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa TCCIA- Viwanda Bw. Octavian Mshiu amesema mapendekezo ambayo TCCIA imewasilisha kwa Balozi wa Msumbiji nchini yanalenga kutoa ushirikiano wa karibu kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili ambao utawezesha uanzishwaji wa vituo katika mkoa wa Mtwara ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na misaada ya haraka kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Makamu wa Rais wa TCCIA-Viwanda Bw. Octavian Mshiu akimkabidhi Balozi Monica Clemente nyaraka maalum baada ya mkutano na Balozi huyo ofisini kwake mapema wiki iliyopita.

Balozi Bi. Monica Patricio Clemente amesema amefurahishwa na ugeni alioupata wa uongozi wa TCCIA na kwamba mapendekezo chanya yaliyoletwa na TCCIA yana nafasi sahihi na muhimu katika kuboresha ushirikiano wa wafanyabiashara wa Mtwara na Mikoa jirani ya Msumbiji kwani mahusiano ya aina hiyo yana nafasi kubwa ya kunufaisha jamii ya wafanyabiashara, kuongeza pato la nchi zote mbili na pia kukuza uchumi wa maeneo husika.
Balozi Monica ameahidi kuyafanyia kazi majadiliano na mapendekezo ya TCCIA kwa haraka ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa mikoa inayofanya biashara pamoja ambayo matokeo yake yataleta tija kwa maslahi ya Tanzania na Msumbiji kwa ujumla
Viongozi wa TCCIA wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa ubalozi wa Msumbiji nchini baada ya mkutano wa Balozi na uongozi wa TCCIA jijini.

Katika mkutano huo wajumbe kutoka ubalozini humo wamesema moja ya changamoto kubwa inayowakumba wafanyabiashara wengi ni lugha ambapo wamependekeza pia kuwepo kwa vituo maalum ambavyo vitakuwa vikitoa elimu ya lugha kwa wafanyabiashara hao ili kuondoa changamoto hiyo.Mwenyekiti wa TCCIA Mtwara Bw. Swallah S. Swallah ameshukuru ubalozi wa Msumbiji kwa ukarimu na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya wafanyabiashara wa Cape Delgado nchini Msumbiji na Mtwara nchini Tanzania. Pia alieleza juhudi za Chemba ya Mtwara katika kukabiliana na changamoto ya lugha na kwamba mjini Mtwara tayari kuna kituo kikubwa cha lugha kinachofundisha watanzania lugha mbalimbali ikiwemo Kireno ambacho sasa kinatiliwa mkazo zaidi.
Viongozi wa TCCIA wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa ubalozi wa Msumbiji nchini baada ya mkutano wa Balozi na uongozi wa TCCIA jijini.

MHESHIMIWA BALOZI WILSON MASILINGI, AWASILISHA HATI ZA UTAMBULISHO KWA MHESHIMIWA ENRIQUE PEÑA NIETO, RAIS WA MEXICO.

Tarehe 11 Aprili, 2017, Mhe. Balozi Wilson Mutaganywa Kajumula Masilingi aliwasilisha hati za utambulisho kwa Mhe. Enrique Peña Nieto, Rais wa Mexico, Ikulu Katika Jiji la Mexico. Hafla hiyo ilishuhudiwa na Mhe. Luis Videgaray Caso, Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Mexico na mke wa Mhe. Balozi, Marystella Masilingi. 
Wakati wa kuwasilisha hati hizo, Mhe. Balozi alipata fursa ya kuongea na Mhe. Rais wa Mexico na kumpa salam kutoka kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Enrique Peña Nieto, Rais wa Mexico akimpokea Mhe. Balozi Wilson M. K. Masilingi, Balozi mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Mexico. Katikati akitizama ni Mhe. Luis Videgaray Caso, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico.
Mhe. Enrique Peña Nieto, Rais wa Mexico na Mhe. Balozi Wilson M. Masilingi, Balozi mpya wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, nchini Mexico.
Kutoka kushoto, Mhe. Balozi Wilson M. Masilingi na Mhe. Enrique Peña Nieto, Rais wa Mexico; Mke wa Balozi Bi. Marystella E. Masilingi na Mhe. Luis Videgaray, Waziri wa Mambo ya Nje wa Mexico.
Mhe. Balozi Wilson M. K. Masilingi na Mke wake Bi. Marystella Masilingi (kulia) na Bi. Swahiba Mndeme, Mkuu wa Utawala wa Ubalozi (kushoto)

RAIS DKT MAGUFULI AKUTANA NA BALOZI WA ISRAEL NCHINI MHE. YAHEL VILAN, IKULU, DAR ES SALAAM LEO

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akifanya mazungumzo na Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Yahel Vilan alipokutana naye Ikulu jijini Dar es salaam leo April 6, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipokea ujumbe maalumu toka kwa Waziri Mkuu wa Israel Mhe. Benjamin Netanyahu uliowasilishwa kwake na Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Yahel Vilan alipokutana naye Ikulu jijini Dar es salaam leo April 6, 2017.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimsindikiza baada ya mazungumzo na Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Yahel Vilan alipokutana naye Ikulu jijini Dar es salaam leo April 6, 2017.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiagana na Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Yahel Vilan baada ya kutana naye kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo April 6, 2017.

PICHA NA IKULU