HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

Bunge lapitisha Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb) akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 Bungeni mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb) akijibu hoja mbalimbali za Wabunge wakati wa Kikao cha Bunge baada ya kuwasilishwa kwa bajeti ya Wizara Mjini Dodoma.
Hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 mara baada ya kuwasiliswa ilijadiliwa na kuchangiwa na Wabunge mbalimbali na hatimaye kupitishwa na Bunge hilo.
Baadhi ya Waheshimiwa Mabalozi wanaoziwakilisha nchi mbalimbali nchini wakifuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bungeni mjini Dodoma 
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akifurahia jambo na Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Mambo ya Nje na Ushikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Peter Msigwa mara baada ya kuwasilisha hotuba ya bajeti Bungeni mjini Dodoma.
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga, Naibu Waziri Dkt. Susan Kolimba, Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz Mlima na Waziri Kivuli wa Wizara Mhe. Msigwa wakiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi na baadhi ya Wabunge. 
Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga na Katibu Mkuu Balozi Dkt. Aziz Mlima wakishirikishana jambo baada ya kuwasilisha hotuba ya Madirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka 2017/2018 katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma 
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akijibu hoja za wa Bunge Bungeni. 
Waziri Mhe.Dkt. Mahiga na Naibu Waziri Mhe.Dkt. Susan Kolimba wakiwa katika picha ya pamoja na Watendaji mbalimbali wa Wizara mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara Bungeni Mjini Dodoma


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amewasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Mahiga katika hotuba yake aliliomba Bunge kupitisha kiasi cha shilingi150,845,419,000 ambapo katika kiasi hiki cha fedha shilingi142,845,419,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 8,000,000,000 imetengwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

Bajeti hii ya mwaka 2017/2018 pamoja na mambo mengine imepanga kutekeleza malengo makuu muhimu kulingana na majukumu ya Wizara kama ifuatavyo;
  • Kutangaza mazingira mazuri ya nchi yetu kwa ajili ya uwekezaji kutokana na historia yake ya miaka mingi ya amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa;
  • Kuendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi mbalimbali zilizotolewa kwa nchi yetu na nchi wahisani, mashirika ya kikanda na ya kimataifa katika kusaidia utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo;
  •  Kuendelea kuratibu Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali katika kuvutia wawekezaji na watalii, kutafuta nafasi za masomo, ajira na nafasi za kubadilishana uzoefu na kutafuta masoko; 
  • Kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa kati ya nchi yetu na nchi nyingine na ile ya mashirika ya kikanda na kimataifa;
  • Kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya viongozi mbalimbali wa kitaifa;
  • Kuendelea kusimamia balozi zetu katika kutekeleza majukumu ya uratibu hasa kutafuta wawekezaji, fursa za ajira, nafasi za masomo na masoko kwa bidhaa zetu;

  • Kuendelea kufuatilia kwa karibu mageuzi kwenye taasisi za Umoja wa Mataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Baraza la Kiuchumi na Kijamii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo;
  • Kuongeza uwakilishi wetu nje kwa kufungua Balozi mpya na Konseli Kuu na kuendelea kununua, kujenga na kukarabati majengo kwa ajili ya makazi na ofisi za Balozi kwa kadri hali ya fedha itakavyoruhusu; 
  • Kujenga mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa kiuchumi kati yetu na vyombo mbalimbali vya Kikanda na Kimataifa, unaozingatia maslahi ya Taifa letu; 
  • Kuendelea kutetea na kusimamia maslahi ya nchi maskini kwenye mikutano yote mikubwa na hasa ile ya Umoja wa Mataifa na taasisi zake. Vilevile, tutaendelea kufanya mazungumzo na nchi tajiri duniani ili kuhakikisha zinatekeleza ahadi mbalimbali zilizotoa ili kuharakisha maendeleo ya nchi maskini. Kwa mfano, ahadi za G8 na ile ahadi ya kila nchi tajiri kutoa asilimia 0.7 ya pato lake la Taifa kwa nchi zinazoendelea na kutoa asilimia 0.2 ya pato lake kwa nchi maskini sana duniani kama msaada; 
  • Kuendelea kutambua jumuiya za watanzania wanaoishi ughaibuni na kuweka utaratibu utakaowawezesha kuchangia maendeleo ya taifa; 
  • Kuratibu maandalizi na kushiriki kwenye majadiliano katika mikutano ya Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na mikutano ya Vikundi Kazi na Wataalam; 
  • Kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa maamuzi na maelekezo ya Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mabaraza ya Kisekta ya Mawaziri ya Afrika Mashariki, miradi na programu za Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa miaka kumi wa Umoja wa Fedha katika kuelekea kwenye eneo la Sarafu Moja ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu zoezi la mapitio ya Sheria za Tanzania ili kuwezesha Watanzania kunufaika na utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki;
  • Kuratibu majadiliano na kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kuanzisha Eneo Huru la Biashara baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na COMESA na SADC pamoja na Eneo Huru la Biashara la Afrika; 
  • Kuratibu majadiliano kuhusu maeneo ya ushirikiano katika uendelezaji wa miundombinu ya kiuchumi (reli, barabara, bandari, nishati, viwanja vya ndege na hali ya hewa) na kijamii (elimu, afya, mazingira, jinsia na watoto) katika Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha katika biashara baina ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu ushiriki wa Tanzania katika Mikutano ya Bunge la Afrika Mashariki;
  • Kuratibu na kushiriki katika maandalizi ya Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzingatia mfumo wa Confederation; 
  • Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha Baraza la Usalama la Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya Mkataba wa Ulinzi wa Pamoja wa Afrika Mashariki; 
  • Kuratibu na kushiriki katika majadiliano ya kuanzisha Itifaki ya Utawala Bora ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  • Kutoa Elimu kwa Umma juu ya fursa zitokanazo na mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; 
  •  Kuratibu mapitio, utafiti, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki;
  • Kuratibu na kufanya uchambuzi wa utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Taasisi ya TradeMark East Africa Wizarani, Wizara nyingine, Idara, Taasisi za Serikali na sekta binafsi; na 
  • Kukamilisha kuandaa Sera Mpya ya Mambo ya Nje 

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini kufanya ziara ya siku tatu nchini Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga (Mb.), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu Ziara ya Rais wa Afrika Kusini nchini Mhe. Jacob Zuma, ambaye atawasili nchini kwa ziara ya siku 3. Pamoja na mambo mengine, Rais Zuma pia atatembelea Hospitali ya Muhimbili Kitengo cha tiba ya ugonjwa wa moyo (Jakaya Kikwete Cardiac Institute), na pia kufungua rasmi Ubalozi wao hapa nchini. 
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Suleiman Salehe, akimsikiliza Waziri Mahiga (Hayupo pichani) katika mkutano na waandishi wa Habari 
Sehemu ya waandishi wa habari wakinukuu maeneo mbalimbali yaliyotajwa na Waziri Mahiga kwenye mkutano na waandishi wa habari. 
Mkutano na waandishi wa habari ukiendelea. 


Taarifa kuhusu ziara ya Rais wa Afrika Kusini nchini

1. UTANGULIZI

(i) Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Gedleyihlekisa Zuma anatarajiwa kufanya Ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini, kuanzia tarehe 10 hadi12 Mei 2017, kwa mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

(ii) Ziara hii inafanyika baada ya Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa Rais Zuma kukutana mjini Addis Ababa, Ethiopia wakati wa Mkutano wa 28 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU).

(iii) Mheshimiwa Rais Zuma anatarajiwa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere tarehe 10 Mei 2017, jioni na kupokelewa na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Magufuli. 

(iv) Ziara hii itatoa fursa kwa Viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nchi hizi mbili, ya kikanda na kimataifa pamoja ‎na kujadili fursa zaidi za ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji na biashara. Ujio wa Mheshimiwa Rais Zuma ni fursa nzuri sana ya kuendelea kukuza na kuimarisha zaidi mahusiano mazuri naya kihistoria kati ya nchi zetu mbili. 

(v) Mheshimiwa Rais Zuma anafuatana pia na wafanyabiashara takribani 80. Hii ni fursa muhimu sana katika kukuza mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Hivyo, tarehe 11 Mei 2017, kutakuwepo na Kongamano la Wafanyabiashara katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere (JINCC).

(vi) Ziara ya Mheshimiwa Rais Zuma inaenda sambamba na vikao vya Tume ya Pamoja ya Marais (Bi-National Commission - BNC) kati ya Tanzania na Afrika Kusini. Mkutano wa Marais umepangwa kufanyika tarehe 11 Mei, 2017. Mkutano huo utatanguliwa na Kikao cha Mawaziri kitakachofanyika tarehe 10 Mei, 2017 na kikao cha Makatibu Wakuu kitafanyika tarehe 8 na 9 Mei, 2017.


2.0. RATIBA



(i) Wakati wa ziara hiyo, tarehe 11 Mei 2017, Mheshimiwa Rais Zuma atakutana na mwenyeji wake, Mheshimiwa Rais Magufuli kwa mazungumzo ya faragha kabla ya kushiriki mazungumzo rasmi yatakayowahusisha wajumbe wa pande mbili.

(ii) Aidha, Viongozi hao watashuhudia uwekwaji saini wa Mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ya ushirikiano. 

(iii) Siku hiyo hiyo, Mheshimiwa Rais Zuma atashiriki chakula cha mchana na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini katika Hoteli ya Hyatt Regency. Pia, Mheshimiwa Rais Zuma na Mheshimiwa Rais Magufuli watashiriki Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Afrika Kusini litakalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.

(iv) Aidha, jioni ya siku hiyo, Mheshimiwa Rais Zumana ujumbe wake watashiriki Dhifa ya Kitaifa ya Chakula cha jioni kilichoandaliwa Ikulu kwa heshima yake na Mheshimiwa Rais Magufuli.

(v) Tarehe 12 Mei 2017, Mheshimiwa Rais Zuma anarajiwa kufungua rasmi Jengo jipya la Ubalozi wa Afrika Kusini nchini pamoja na kutembelea Taasisi ya Matibabu ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

(vi) Mheshimiwa Rais Zuma na ujumbe wake wataondoka siku hiyohiyo kurejea Afrika Kusini.


3.0. MAHUSIANO BAINA YA TANZANIA‎ NA AFRIKA KUSINI

(i) Mahusiano ya Tanzania na Afrika Kusini ni mazuri na ni ya muda mrefu tangu wakati wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini zilizoongozwa na Chama kikongwe cha African National Congress (ANC). Nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana kwa karibu katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kikanda na hasa ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Kwa sasa, Afrika Kusini ni Mwenyekiti wa SADC na Tanzania ni Mweyekiti wa SADC Organ, hatua inayotoa nafasi ya kushirikiana zaidi. 

(ii) Aidha, ushirikiano baina ya Tanzania na Afrika Kusini umekuwa ukiimarika kila mara kwa Viongozi wakuu kutembeleana na viongozi wa ngazi za juu Serikalini kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi zetu mbili. Kama mtakumbuka Julai 2011, Mhe. Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alifanya Ziara ya Kiserikali nchini Afrika Kusini ambayo ndiyo iliyozaa Mkataba wa Ushirikiano wa Tume ya Marais ambayo ndiyo iliyotuwezesha kukutana leo.

(iii) Uhusiano wa Vyama vya Siasa vya CCM na ANC

Vyama vya ANC na CCM vina mahusiano mazuri na Viongozi wa vyama hivyo wamekuwa wakikutana mara kwa mara kwa ajili ya kujadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano kati yao.

(iv) Mikataba ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini

Tanzania na Afrika Kusini zimekuwa zikishirikiana katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hadi sasa, Tanzania na Afrika Kusini tayari zimetia saini Mikataba ya Ushirikiano (MoU) kumi na tano (15), ambayo inagusa sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, sayansi na teknolojia, uwekezaji, utamaduni na kilimo.

(v) Ushirikiani katika Utatuzi wa Migogoro katika Kanda

Tanzania na Afrika Kusini zimeendelea kufanya kazi pamoja katika juhudi za utatuzi wa migogoro na kuhakikisha kwamba Afrika inakuwa sehemu salama. Nchi hizi mbili zimeshiriki katika kutatua migogoro nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Sudan Kusini. Tanzania na Afrika Kusini zote zimechangia Askari katika Brigedi ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Amani na Usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (United Nation Force Intervention Brigade-FIB) kwa lengo la kutuliza uvunjifu wa amani Mashariki mwa Kongo. Vile vile, nchi hizi mbili kwa pamoja zimekua zikishirikiana katika kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Sudan Kusini.

(vi) Uhusiano katika Nyanja za Uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini

Ø Uhusiano ya uwekezaji kati ya Tanzania na Afrika Kusini umekuwa ukiimarika siku hadi siku. Uhusiano huo mzuri umezidi kuchochea na kurutubisha ushirikiano wetu wa muda mrefu na wa kihistoria. 

Ø Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi zinazochangia idadi kubwa ya wawekezaji wa kigeni nchini Tanzania. Takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Centre-TIC) kimesajili jumla ya miradi 226 kati ya mwaka 1990 hadi 2016. Miradi hiyo ina thamani ya Dola za Kimarekani zipatazo Milioni 803.15 na imetoa ajira zipatazo 20,916.

(vii) Uhusiano katika Sekta ya Biashara

Ø Kiwango cha biashara (volume of trade) imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Mwaka 2007 ilikuwa Tsh Milioni 976,331 na mwaka 2016 ni Tsh 2,402,211.20. Hili ni ongezeko kubwa na linaleta matumaini ya ushirikiano zaidi.

Ø Bidhaa ambazo Tanzania inauza nchini Afrika Kusini ni pamoja na maua, kahawa, wanyama hai, chai, nguo, pamba, vito vya thamani, tumbaku na mafuta ya kupikia. Bidhaa zinazoagizwa kutoka Afrika Kusini ni pamoja na maziwa na mazao yote ya maziwa, matunda aina ya apple, mbegu za mahindi, mafuta ya soya, sukari kwa matumizi ya viwanda, juisi za matunda, mafuta ya kulainisha mitambo, bidhaa za vileo, Acrylic polymers, lami, magari, pampu za maji, bidhaa za chuma, vitabu, mashine, na trela.

(vii) Mchango wa Madawati wa Afrika Kusini kwa Serikali ya Tanzania

Ø Katika kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutatua changamoto mbalimbali za kijamii, kwa kupitia Ubalozi wake hapa nchini, Serikali ya Afrika Kusini iliweza kuchangia jumla ya madawati 1100 kwa shule za Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga na Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma. Madawati hayo yalikabidhiwa kwa Naibu Waziri wa TAMISEMI.

Ø Pamoja na hayo, Serikali ya Afrika Kusini inatarajia kuanzisha programu mahsusi ya kubadilishana walimu na uzoefu kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuinua sekta ya elimu. 

4.0. TAARIFA FUPI KUHUSU TUME YA USHIRIKIANO YA MARAIS (BI-NATIONAL COMMISSION) KATI YA TANZANIA NA AFRIKA KUSINI

Sasa naomba niwape taarifa fupi kuhusu Mkutano wa Tume ya Ushirikiano ya Marais

(i) Tanzania na Afrika Kusini zilisaini Mkataba wa kuanzishwa kwa Tume ya Ushirikiano ya Marais (Bi-National Commission-BNC) tarehe 19 Julai 2011 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi. Tume ya Ushirikiano ya Marais imechukua nafasi ya Tume ya Uchumi ya Pamoja ya Marais (Presidential Economic Commission-PEC) iliyoanzishwa mwaka 2005. Kama nilivyosema awali, Mkataba huu ulisainiwa wakati wa ziara ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tano, Mhshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

(ii) Mkataba wa kuanzisha BNC umeainisha maeneo kumi (10) ya ushirikiano ambayo ni Biashara na Uwekezaji (Trade and Investment), Maendeleo ya Miundombinu (Infrastructure Development), Kilimo (Agriculture), Elimu, Sayansi na Teknolojia (Education, Science and Technology), Ulinzi na Usalama (Defence and Security), Habari, Utamaduni na Michezo (Infrastructire, Culture and Sports), Afya (Health), Nishati na Madini (Energy and Minerals) na Maliasili na Utalii (Natural Resources and Tourism).

(iii) Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Mashirikiano ya Marais (BNC) unatarajiwa kufanyika kuanzia leo, tarehe 8 hadi 11 Mei, 2017. Mkutano wa Marais utatanguliwa na vikao vya Makatibu Wakuu tarehe 8 na 9 Mei, 2017 ukifuatiwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 10 Mei, 2017. Mkutano wa Marais utafanyika tarehe 11 Mei, 2017 ambapo Mheshimiwa Rais Magufuli na Mheshimiwa Rais Zuma watakuwa Wenyeviti Wenza wa Mkutano huo. 

(iv) Wakati wa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Marais, Mikataba ifuatayo inatarajiwa kutiwa saini:-

(a) Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Masuala ya Bio Anuwai na Uhifadhi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini (Memorandum of Understanding between the Government of the United Republic of Tanzania and the Government of the Republic of South Africa on Cooperation in the Field of Biodiversity Conservation and Management);

(b)Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Sekta ya Maji kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini; na

(c) Hati ya Makubaliano katika Sekta ya Uchukuzi kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Afrika Kusini;

(v) Pia kuna Mikataba mingine inaendelewa kufanyiwa kazi na mara itakapokamilika, Mawaziri wa sekta husika watasaini. Mikataba hiyo ni pamoja na wa Sekta ya Utalii, Sekta ya habari, Sekta ya kilimo, sekta ya afya, niitaje hiyo tu kwa sasa.

(vi) Tofauti na Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (BNC) inashirikisha Marais wa Nchi mbili ambapo katika JPC inaishia katika ngazi ya Mawaziri. Ushiriki wa Marais katika Tume ya Pamoja ya Ushirikiano unatoa uzito wa pekee katika utekelezaji wa maeneo ya mashirikiano yaliyoafikiwa.


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, 
Dar es Salaam, 08 Mei, 2017

WAZIRI MAHIGA AFUNGUA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA 69 YA UHURU WA ISRAELI, DODOMA.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akizungumza kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 69 ya uhuru wa Taifa la Israel iliyofanyika kwenye Hoteli Morena Mjini Dodoma 
Meza Kuu wakiwa wamesimama wakati wimbo ya Taifa unakipigwa kweye maadhimisho ya 69 ya uhuru wa Israel 
Balozi wa Israeli nchini mwenye makazi yake Nairobi, Kenya Mhe. Yahel Vilan akizunguza kwenye hafla ya maadhimisho ya 69 ya uhuru wa Israel iliyofanyika mjini Dodoma 
Mhe. Balozi Vilan akisisitiza jambo 
Waziri Mhe.Balozi Dkt. Mahiga akihutubia hadhira iliyo shiriki hafla hiyo 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Ramadhani (Mwinyi kulia) akifuatilia jambo, kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Israel Mhe. Job Masima 
Picha ya pamoja 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga jana alifungua hafla ya maadhimisho ya 69ya uhuru wa Taifa la Israeli yaliyo fanyika mjini Dodoma katika Hoteli ya Morena.

Hafla hiyo ya maadhimisho ya 69 ya uhuru wa Taifa hilo na uhusiono mzuri wa kidiplomasia  baina ya Tanzania na Israeli yaliratibiwa na Ubalozi wa Israel wenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya.  Waziri Mahiga akizungumza katika hafla hiyo aliupongeza Ubalozi wa Israel kwa uamuzi wake wa kufanyia hafla ya maadhimisho ya 69 ya uhuru wao, Makao Mkuu ya Serikali mjini Dodoma.

 Waziri Mahiga aliongeza kusema Mataifa haya mawili Tanzania na Israel yana mahusiano mazuri ya kidiplomasia, ikidhihirishwa wazi na idadi kubwa ya raia wa nchi hizi mbili kutembeleana na kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo utalii. Aidha Mahiga aliipongeza Serikali ya Israel kwa hatua kubwa ya maendeleo waliyofikia katika maeneo mbalimbali ikiwemo sayansi na teknolojia na kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbalimbali.  

Balozi wa Israeli nchini Mhe. Yahel Vilan mwenye makazi yake Jijini Nairobi, Kenya akitoa hotuba yake alisema Ubalozi wa Israeli umechukua maamuzi ya kufanyia hafla hiyo Mjini Dodoma ikiwa nikuunga mkono maamuzi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma. Aliongeza kusema kuwa hafla hiyo ni ishara ya Israel kuanziasha Ubalozi wake nchini Tanzania. 

Balozi Vilan ameihakikishia serikali ya Tanzania kuwa Israel itaendelea kuwa mshirika mzuri wa maendeleo ya Taifa katika maeneo ya kilimo, afya, elimu, sayansi na teknolojia na usalama.Israeli ilifungua kituo cha kushughulikia masuala ya viza nchini Tanzania tarehe 3 Novemba, 2016.


Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa aipongeza Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akisalimiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Antonio Guterres (kushoto) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar Es Salaam jana. Mhe. Guterres alisimama kwa muda katika uwanja huo akitokea nchini Kenya kwa ajili ya kufanya mazunguzmo na Balozi Mahiga. Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, Mhe Guterres aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi zake za kutafuta amani nchini Burundi kupitia kwa Msuluhishi wa Mgogoro huo Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Benjamin Willium Mkapa. Aidha, Dkt. Mahiga aliwasilisha Salamu Maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. 
Waziri Mahiga akizungumza jambo huku Mhe. Guterres akimsikiliza kwa makini. 
Dkt. Mahiga akiendelea kuzungumza na Mhe. Guterres huku Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez (wa pili kutoka kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy wakiwasikiliza kwa makini. 
Picha ya pamoja 
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Bi. Mindi Kasiga naye akiagana na Mhe. Guterres 
Mhe. Guterres akiagana na Dkt. Mahiga mara baada ya kumaliza kufanya mazungumzo yao.
PRESS RELEASE 
UN SECRETARY GENERAL STOPS IN DAR ON HIS WAY TO NEW YORK
H.E. Dr. John Pombe Magufuli, the President of the United Republic of Tanzania has urged the United Nations to continue its support in bringing about political stability in Burundi and the Democratic Republic of Congo.

In his special message to the United Nations Secretary General Mr. Antonio Guterres President Magufuli explained that the recent instability in the two countries has created refugees’ influx in Tanzania and its neighbors, hence the region is committed to ensure political stability is restored. 

Delivering President Magufuli’s message to the United Nations Secretary General Mr. Antonio Guterres, Tanzania’s Foreign Minister Augustine Mahiga said that as the chair of EAC, Tanzania is hopeful with the progress been made in the mediation process in Burundi under the leadership of President Yoweri Museveni of Uganda and facilitated by the former President of Tanzania, H.E. Benjamin William Mkapa. Hon. Mahiga also informed the UN Secretary General that the upcoming EAC Summit is expected to receive a progressive report about the process. 

With regards to the Democratic Republic of Congo, Minister Mahiga revealed that the Southern African Development Community is intending to include the agenda of political transition in DRC, whereby SADC member states are expecting positive deliberations. Tanzania is the current chair of the SADC organ of political, defense and security with the mandate to support the achievement and maintenance of peace and security as well as the rule of law in the SADC region. 

Upon receiving President Magufuli’s message, Mr. Guterres praised Tanzania for its ability to uphold principles of good governance in the country as well as maintaining peace and creating a peaceful environment in the EAC and SADC regions.

Mr. Guterres commended President Magufuli’s efforts in Burundi peace process, and his readiness to host refugees from Burundi, emphasizing the role played by regional communities in Africa in resolving leadership crisis in African countries. 

“The United Nations appreciates the work done by President Mkapa in Burundi under the EAC and its leadership. If the region come together the way EAC has done in the case of Burundi, I am sure together they will be able to establish lasting solutions” he remarked. 

Minister Mahiga told the reporters that President Magufuli met Mr. Guterres during the AU Summit in Addis Ababa earlier this year, where the two leaders exchanged cordial discussions about various issues concerning the region. 

“President Magufuli instructed me to deliver his message to Mr. Guterres, and has also extended an invitation to the Secretary General at an appropriate time to have a working visit in the country” concluded Hon. Mahiga.

Mr. Guterres was met and held talks with Foreign Minister Mahiga at the Julius Nyerere International Airport yesterday night where he was on transit from Somalia and Kenya for a working visit. Also present at the airport was the United Nations Resident Coordinator, Mr. Alvaro Rodriguez and officials from the Ministry of Foreign Affairs including the Director of Multilateral Cooperation Ambassador Celestine Mushy and Ministry’s Spokesperson Ms. Mindi Kasiga. 

Issued by:
Government Communication Unit,
Ministry of Foreign Affairs and East African Cooperation,
Dar es salaam, Tanzania
March 9, 2017.

Waziri Mahiga akutana na Rais wa Mahakama ya Afrika ya haki za Binadamu na Watu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akifafanua jambo alipokutana na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Jaji Sylvain Ore yenye Makao Makuu Jijini Arusha,Tanzania. Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ofisini kwa Mhe. Wiziri Mahiga mjini Dodoma, wamejadili masuala mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya mahakama hiyo ikiwemo majengo ya ofisi ili kuiongezea ufanisi zaidi.
Mazungumzo yakiendelea; Kushoto ni Wafanyakazi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na kulia kwa Rais wa Mahakama, ni Mtumishi wa Wizara Bw. Beatus Kalumuna
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika picha na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Jaji Sylvain Ore mara baada ya mazungumzo
Picha ya Pamoja
Waziri Mhe. Mahiga akiongea na wanahabari (hawapo pichani) mara baada ya mazungumzo
Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Jaji Sylvain Ore akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo

Waziri Mahiga akutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Arkadia Ltd

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ARKADIA Ltd. Dr. Ezio Copat walipokutana kwa mazungumzo ofisini kwake mjini Dodoma.
Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akimsikiliza Dr. Copat walipokutana kwa mazungumzo mjini Dodoma.
Waziri Mhe. Balozi Dkt. Mahiga akifafanua jambo wakati wa mazungumzo.
Mazungumzo yakiendelea.

Wizara ya Mambo ya Nje yahamishia Ofisi zake Dodoma Rasmi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU WIZARA KUHAMIA DODOMA
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inapenda kuufahamisha Umma kuwa tayari imeshahamia Dodoma kuanzia tarehe 17 Februari, 2017.  Hatua hiyo imehusisha Awamu Mbili, Awamu ya kwanza imetekelezwa tarehe 28 Januari, 2017 na Awamu ya Pili imetekelezwa tarehe 17 Februari, 2017.
Miongoni mwa Watumishi waliohamia Dodoma katika awamu hii ya kwanza (Awamu ndogo ya kwanza tarehe 28 Januari, 2017) nipamoja na Viongozi Wakuu na Watumishi wa Wizara wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.  Dkt. Augustine P.Mahiga na Naibu Waziri Mhe. Dkt. Susan A. Kolimba pamoja na Watumishi Kumi (10) waliofuatana nao. Awamu ndogo ya kwanza ilifuatiwa na (Awamu ndogo ya Pili tarehe, 17 Februari, 2017) iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Balozi Dkt. Aziz P.Mlima na Naibu Katibu Mkuu Balozi Ramadhan M.Mwinyi wa kiongozana na Watumishi 33 wa Wizara ya Mambo ya Njena Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Katika Uhamisho huo wa Awamu ya Kwanza, jumla ya Watumishi 43 wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wameungana na Viongozi wao Wakuu.
Mawasiliano ya Wizara yatakayotumika kuanzia sasa nikama ifuatavyo:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Barabara ya Makole,
S.L.P 2933,
Jengo la LAPF, Ghorofaya6,
DODOMA.
Namba za Simu: +255 (0) 262323201-7,
Nukushi           :  +255-26-2323208,
Barua pepe      :   nje@nje.go.tz  Tovuti             : www.foreign.go.tz
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dodoma, 27 Februari, 2017.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Ofisini kwake Mjini Dodoma. Waziri Mahiga leo ameutangazi Umma wa Watanzania kuwa Wizara imehamia rasmi Dodoma. 
Waandishi wa habari wakifuatilia hotuba ya Mhe. Waziri Balozi Dkt. Mhaiga 
Walio keti ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (katika), Naibu Katibu Mkuu Balozi Ramadhani Mwinyi (wa kwanza kulia) Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bw. Nigel Msangi (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu Bw.Hamid Mbegu wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wizara Mjini Dodoma