HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

Lema ahoji kushikiliwa mmiliki wa shule ya Lucky Vincent

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amehoji sababu za polisi kumshikilia mmiliki wa shule ya Lucky Vincent badala ya trafiki waliokuwa barabarani siku ya ajali iliyoua watu 35.
Akiomba mwongozo wa Spika kuhusu jambo hilo leo, amesema katika eneo husika kuna vizuizi vya ukaguzi vinne lakini trafiki hawakuona kuwa basi hilo lilikuwa kimezidisha watoto na hawakuwa wamefunga mikanda.
Amesema badala ya trafiki hao kuchukuliwa hatua, anakamatwa mmiliki ambaye hakuwapo.
Akijibu mwongozo huo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema suala hilo halijatokea bungeni.

SAKATA LA GODBLESS LEMA KUBAGULIWA JANA MSIBANI LATUA BUNGENI

Wabunge wawili wa Chadema, Peter Msigwa wa Iringa Mjini na Godbless Lema wa Arusha Mjini wameomba mwongozo wa Spika kuhusu ubaguzi wa kisiasa uliotokea kwenye msiba mjini Arusha Jumatatu.

Jana Jumatatu jijini Arusha ilikuwa inaagwa  miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa Shule ya Lucky Vincent waliopoteza maisha katika ajali ya gari.

Wa kwanza kusimana alikuwa Msigwa ambaye amehoji kama ni haki kutowapa fursa Meya wa Arusha, Calist Lazaro na Mbunge wa jimbo hilo, Lema kutoa salamu za rambirambi.

Lema kwa upande wake amesema hata magari mawili ya kubeba wagonjwa yaliyotolewa na yeye na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari yaliondolewa kwa sababu yana majina yao.

Amesema ni kwa sababu walimheshimu makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, vinginevyo mambo kama hayo huwa hayatokei mbele yao.

Mwenyekiti wa Bunge  Najma Giga amesema atatoa mwongozo huo baadaye.

Kauli ya Godbless Lema kuhusu wabunge CCM waliokwenda kumsalimia gerezani kuitwa wasaliti

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ameibuka na kueleza kushangazwa na kauli ya Rais Dk. John Magufuli kwamba wabunge wa CCM waliotaka kwenda kumwona gerezani walikuwa wasaliti.

Lema alisema anatarajia Spika wa Bunge, Job Ndugai, atatoa msimamo juu ya kauli ya kiongozi huyo wa nchi.

Kauli hiyo ya Lema imekuja siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kuripotiwa na chombo kimoja cha habari  kwamba alishangazwa na hatua ya baadhi ya wabunge wa CCM waliounda kamati ya kutaka kwenda kumtembelea Lema gerezani.

Katika mkutano wake na wabunge hao juzi uliofanyika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma, Rais Magufuli alisema amekuwa akielezwa kuwa kamati hiyo ilikuwa imepanga safari za kutaka kwenda kumwona Lema alipokuwa gerezani jambo ambalo alilifananisha ni sawa na usaliti kwa chama chake.

Katika taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, Lema alisema kitendo cha wabunge hao kutaka kumtembelea si usaliti bali ni upendo ambao ni muhimu kwa binadamu yeyote pale anapokuwa na matatizo.

Lema alikaa gerezani kwa muda wa miezi minne kwa kukosa dhamana kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.

“Mheshimiwa Rais Magufuli nakusalimu. Nimetoka gerezani hivi karibuni ambako nilikuwa huko kwa zaidi ya miezi minne kwa kunyimwa masharti ya dhamana kwa dhamana iliyokuwa wazi.

“Nimeona kwenye vyombo vya habari leo kwamba wale wabunge waliokuwa wanataka kunisalimia nilipokuwa magereza ni wasaliti wa chama cha CCM.

“Mheshimiwa Rais wengi walinisalimia wakiwemo wachungaji, masheikh, wabunge na viongozi mbalimbali, sidhani kama hatua hii ilikuwa ni usaliti isipokuwa upendo ambao ni muhimu kwa binadamu yeyote pale anapokuwa na matatizo.

“Mheshimiwa  Rais nimeogopa sana kwa kauli hii, je Taifa linakwenda wapi? Hivi kweli sisi wabunge ni maadui? Kama viongozi tutafikiri utengano ni moja ya njia ya kuimarisha vyama vyetu, bila shaka tutakuwa tunalitendea Taifa ubaya,” alisema Lema.

Mbunge huyo alisema dhambi hiyo ikikomaa ni wazi kwamba lugha za kidini, ukanda na ukabila hazitaacha kukomaa.

Alisema ni muhimu sasa wakajenga utamaduni wa kuhimiza mshikamano wa kitaifa bila kujali itikadi kama kweli wanapenda masikini na wanyonge.

“Nawaomba wabunge wenzangu walionijali wakati niko gerezani wasijisikie vibaya kwani walifanya jambo jema na muhimu kwa wakati muhimu sana katika maisha yangu ninatarajia kuwa Spika wa Bunge atatoa neon juu ya kauli hii ya Rais.

“Mheshimiwa Rais wakati wa msiba wa Christina Lissu dada yake na Tundu Lissu, nilikuona katika msiba ule wewe na mama yetu mke wako, je wewe ulikuwa unasaliti chama chako?

“Meshimiwa Rais neno la Mungu linasema wapendeni maadui zenu, waombeni wanaowadhi, wabarikini wanaowaonea kwani kufanya hivi ni kuishi kwa thawabu za Mwenyezi Mungu,”alisema Lema.

Mbunge huyo alisema pamoja na hali hiyo ya kuzuiwa lakini aliwashukuru wabunge wa CCM kwa kwenda kumjulia hali, akiwa nyumbani kwake baada ya kutoka gerezani.

“Sina la kusema katika hili kama Rais alikuwa anajua hawakuja kuniona gerezani lakini niwashukuru wabunge wa CCM wote waliokuja kunijulia hali nyumbani. Sisi kama nchi tunatakiwa kuwa na umoja badala ya kuanza kubaguana kwa itikadi zetu za vyama.

“Mdogo wangu wa kike amepata mchumba lakini familia ya huyo mchumba wake inatokana na CCM je tuvunje vikao vya harusi kwa sababu ya tofauti ya vyama?

“Jibu ni hapana sisi ni Watanzania ni lazima tuishi kwa kupenda na kwa umoja kama ambavyo utamaduni wetu unatutaka na si vinginevyo,” alisema.

Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka jana mjini Dodoma nje ya viwanja vya Bunge na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Novemba 4 mwaka jana akikabiliwa na kesi mbili namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Katika kesi ya kwanza ya jinai namba 440, anadaiwa kati ya Oktoba 22 mwaka jana maeneo ya Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro, katika mkutano wa hadhara alitoa maneno yenye kuleta tabaka miongoni mwa jamii kwa kutoa matamshi yenye chuki, kuibua nia ovu kwa jamii.

Katika kesi ya pili namba 441, alidaiwa kwamba, Oktoba 23, mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa, Lema  alitoa maneno kuwa:

“Kiburi cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni Mungu, nimeota  Mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshamchukua maisha yake,”.

Februari 27,  mwaka huu, Mahakama ya Rufaa Tanzania ilifuta rufaa mbili za Jamhuri dhidi ya Lema baada ya mawakili wa Serikali kuieleza mahakama  hiyo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hana nia ya kuendelea na rufaa, hivyo kuiomba mahakama kuzifuta rufaa hizo zilizokuwa zinahusu dhamana ya mbunge huyo.

LEMA: ASEMA MADIWANI WA CHADEMA WAOGA YUPO TAYARI KUWAKANA MBELE YA WANANCHI

Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika shule katika viwanja vya Ngarenaro Jijini Arusha.
Wapili kutoka kushoto ni mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema ,wakwanza kulia ni mbunge wa Simanjiro James OLemilya akifuatiwa na aliyeko kulia kwake ni Meya wa jiji la Arusha Kalisti Lazaro, akifuatiwa na Wema Sepetu,na wakwanza kulia ni mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Arusha Derick Magoma
Wema Sepetu akisaliamia wananchi wa jiji la Arusha waliofika kwenye mkutano huo
Mamia ya wananchi waliohudhuria katika mkutano huo leo jijini Arusha.

Na,Vero Ignatus ,Arusha.
Mbunge wa Arusha mjini Godbless Jonathan Lema amefanya mkutano wake wa kwanza kwa kuzungumza na wananchi wa Arusha baada ya kutoika rumande alipokuwa ameshikiliwa kwa miezi minne

Akizungumza katika mkutano huo Lema amesema kuwa madiwani wa chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema watakao kuwa waoga yupo tayari kuwakana mbele ya wananchi na kama hawawezi kuwa majasiri waachanae na chama hicho. 

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwemo madiwani wote wa chama hicho katika jiji la Arusha pamoja na wabunge wa simanjiro na yule wa Monduli.

Aidha mbunge huyo amesema kuwa yupo kwenye harakati za kukamisha kukiandika kitabu chake kitakachotoka hivi karibuni chenye historia ya maisha halisi ya wafungwa waliopo gerezani bila hatia,sambamba na wale waliobambikiziwa kesi mbalimbali.

Ameataka madiwani kuwa sambamba na yeye na kuachana na kauli wanayoisema ya kuwa wapo nyuma yake kwa kila kitu anachokifanya .

WEMA SEPETU ATEMBELEA GODBLESS LEMA BAADA YA KUTOKA GEREZANI

Msanii wa filamu nchini Wema Sepetu ambaye hivi sasa amehamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ametimiza hadi yake kwenda kuonana na Mbunge wa Arusha mjini Mhe. Godbless Lema ambaye amepata dhamani siku ya Ijumaa na kutoka gerezani.

Wema Sepetu juzi alisema atakwenda Arusha kuonana na Mbunge huyo ambaye amekaa ndani kwa zaidi ya miezi mitatu na kusema ni faraja kwao saizi kuona ametoka na kuja kuendeleza mapambano

"Ni faraja kwetu kwamba sasa umerudi mtaani kuendeleza mapambano, kwenye mapambano haya hautakuwa mwenyewe, mdogo wako Wema nitakuunga mkono mpaka kieleweke. For that sake, kesho (jana) i'll be in Arusha kuonyesha Solidarity" alisema Wema Sepetu

Baada ya Wema Sepetu kufanikiwa kuonana na Mbunge wa Arusha Gobless Lema amefunguka na kusema saizi anajisikia furaha na amani kuwa ndani ya chama hicho
"Finally Met my brother, aisee Chadema inanipa furaha mimi. Nina amani ya moyo... Ona Venye nacheka .... It was A Good Day...." aliandika Wema Sepetu

BREAKING NEWS: MBUNGE WA ARUSHA GODBLESS LEMA AACHIWA KWA DHAMANA

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Jonathan Lema akiwa kwenye gari baada ya kuachiwa kwa dhamana leo.

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema, ameachiwa kwa dhama leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Lema ameachiwa kwa dhamana ikiwa ni takribani miezi minne tangu awekwe rumande kwa kesi ya uchochezi.
Polisi wa kutuliza ghasia walijaa mahakamani hapo wakiwafukuza wafuasi wa Lema waliojaa katika viwanja vya mahakama hiyo.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe walikuwepo mahakamani hapo leo.

Lowassa, Sumaye Wawasili Mahakamani Kusikiliza kesi ya Lema

Viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa Katibu Mkuu wa Chadema Dr Vicent Mashinji, Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Edward Lowasa, Waziri Mkuu Msaatafu Sumaye na Meya wa Jiji la Arusha Mjini Kalisti Lazaro wakiwa mahakamani kusikiliza uamuzi wa Mahakama kuhusu dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema unaotolewa leo
Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless  Lema akishuka kwenye gari kuingia mahakamani.

LEMA NA MKEWE WAKANA MASHITAKA DHIDI YAO

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) jana alikana tuhuma za makosa ya jinai kwa pamoja na mkewe, Neema, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Nestory Barro, Lema na Neema walikana mashtaka ya kutuma ujumbe mfupi wa simu ya mkononi wenye matusi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Awali akiwasomea maelezo ya kesi hiyo Wakili wa Serikali Alice Mtenga alidai kuwa Lema na Neema, Agosti 20 mwaka jana, ndani ya Jiji la Arusha, walimtumia ujumbe wa simu ya kiganjani kwa mkuu huyo wenye lugha ya matusi, huku wakijua ni kosa kisheria.

Ilidaiwa kuwa ujumbe huo ulitumwa kutoka simu namba 0764-150747 kwenda namba 0766-757575 uliokuwa ukidai, “Karibu, tutakudhibiti kama Uarabuni wanavyodhibiti mashoga.”

Baada ya kuwasomea maelezo hayo ya awali, washtakiwa hao kwa pamoja walikiri kuwa ni wakazi wa Arusha na Lema ni Mbunge wa Arusha Mjini ila walikataa kusambaza ujumbe huo wa kumtukana Gambo na tarehe ya kukamatwa kwao.

Hakimu Barro aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 3, ambapo upande wa Jamhuri utaanza kuwasilisha ushahidi wake Gambo akiwa wa kwanza.

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, wakili wa Lema, John Mallya aliiambia mahakama wanatoa notisi ya kuwasilisha pingamizi la mdomo kwa kuwa hati ya mashtaka ina mapungufu, na baadaye wataomba mahakama iitupilie mbali hati hiyo.

Hata hivyo, Hakimu huyo alisema hoja za awali za pingamizi hilo zitasikilizwa Februari 3 pia.

Mbali na Mkuu wa Mkoa, Jamhuri inakusudia kuita mashahidi wengine wanne, ilielezwa.

Kwa mujibu wa Wakili wa Serikali Mtenga upande wake pia utakuwa na vielelezo vitatu vitakavyotolewa
mahakamani hapo.

Alisema mashahidi watano watakaotoa ushahidi wao ni Gambo, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO), George Katabazi, (ASP) Damasi Massawe, mhusika kutoka kampuni ya simu ya Vodacom pamoja na mtaalamu wa picha.

Pia alivitaja vielelezo watakavyovitoa katika kesi hiyo kuwa ni nakala ya taarifa za mawasiliano ya simu kutoka kampuni ya Vodacom, simu ya mshtakiwa mke wa Lema na taarifa ya uchunguzi kutoka kitengo kinachoshughulikia masuala ya kiuchunguzi (Forensic Bureau).

Wakati huo huo, wakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, John Mallya amemuomba Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Bernard Nganga kutoanza kusikiliza kesi ya kuhamasisha maandamano Septemba Mosi (Ukuta) inayomkabili Lema peke yake.

Akitoa ombi hilo jana, Mallya alidai kuwa kesi hiyo ya kuhamasisha maandamano kwa njia ya mtandao wa kijamii kisha kuusambaza Agosti Mosi hadi Agosti 26 mwaka jana, haifai kusikilizwa katika mahakama hiyo sababu kuna hoja za Kikatiba.

Alisema shahidi aliyeandaliwa kwa ajili ya kutoa ushahidi wake ambaye ni RCO, George Katabazi hapaswi kutoa ushahidi mahakamani hapo, sababu kesi hiyo ina hoja za kikatiba.

“Mheshimiwa kesi hii ukiiangalia ipo kikatiba zaidi na kwasababu ipo kikatiba basi sisi tunaenda Mahakama Kuu ikasikilizwe na majaji watatu ili tupewe tafsiri ya vifungu vya sheria," alisema Mallya.

Alisema kwa Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977 inampa haki kiongozi au mwanasiasa kufanya shughuli za kisiasa.

"Kuwakataza au kuingilia kati tunataka kujua huko Mahakama Kuu ya Katiba, nani ana mamlaka ya kuzuia maandamano."

Naye wakili wa Serikali Mtenga alimuomba hakimu kutupa pingamizi la Mallya alilolitoa mahakamani hapo, badala yake kesi hiyo iendelee kusikilizwa kwani upande wa Jamhuri tayari ulishamuandaa
shahidi wake.

Hakimu Nganga alisema amesikia hoja za mawakili hao wa pande zote mbili na yeye anaendelea na kesi hiyo baada ya aliyekuwa
 
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Augutino Rwezile kupanda cheo na kuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kitengo cha biashara.

Alisema atatoa uamuzi wa kesi hiyo, kusikilizwa au kwenda kwa majaji watatu Februari 8.