HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

Gwajima awajibu waliomtabiria kifo

Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema hatakufa hadi pale atakapotimiza lile lililomleta duniani.
Ameyasema hayo leo wakati wa ibada ya Jumapili kanisani kwake ikiwa ni siku chache baada ya mhubiri mmoja wa kimataifa kutabiri kuwa Gwajima atakufa ifikapo 2018.
“Mungu ndiye anajua siku saa na dakika ya kufa kwangu si mwanadamu,” amesema Gwajima

Askofu Gwajima akemea wanaoizungumzia nchi vibaya

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amewaonya baadhi ya watu wanaoiongelea vibaya nchi akiwataka waache mara moja kwa kuwa wanachochea uvunjifu wa amani.
Askofu Gwajima amesema kinachotakiwa watu waizungumzie nchi vizuri kwa kuwa amani itakuwepo na uchumi wa nchi utaendelea kukua.
"Namkemea yule mtu ambaye anaiongelea vibaya nchi yetu huwezi ukawa unatoa kinywa kinachoashiria uvunjifu wa amani,"
"Huwezi kila siku unalaani kwa kuiongelea vibaya nchi yetu lazima nikemee ili nchi yetu iweze kuendelea kuwa na amani,"amesema Gwajima katika mahibiri kanisani kwake leo.

Maalim Seif akutana na Gwajima


Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameutua mgogoro wa chama che kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima huku kiongozi huyo wa kidini akitangaza kuwa atamlipua Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba Jumapili ijayo.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati alipomtembelea Askofu Gwajima, Maalim Seif alibainisha kwamba amemweleza kiongozi huyo mambo mbalimbali ikiwemo suala la mgogoro ndani ya CUF, aliodai umesababishwa na Lipumba.

Alisema kuwa ameamua kwenda kwa Askofu Gwajima kumweleza hayo kwa sababu ni rafiki yake na hawajaonana siku nyingi lakini pia kiongozi huyo alikuwa haelewi mgogoro wa CUF umesababishwa na nani.

"Nimemweleza Askofu Gwajima mambo mengi hususani mgogoro wa CUF hivyo ataamua mwenyewe nini afanye kutokana na niliyomweleza,"alisema.

Aliongeza kuwa mbali na kwenda kwa Gwajima  pia ameshazungumza na viongozi wengine wa dini husuani ya Kiislamu.

Kwa upande wake, Askofu Gwajima alisema kuwa ameshafahamu chanzo cha mgogoro huo kwa kuwa Maalim ni rafiki yake wa siku nyingi lakini Lipumba hana urafiki naye.



"Mimi huyu ni rafiki yangu kwa hiyo nilitaka kujua Professa Lipumba anafanya nini kuvuruga CUF, hivyo nilitaka kujua Lipumba amepatwa na nini mpaka amevuruga chama chako na kiukweli mimi nilikuwa siufahamu vizuri huu mgogoro ila saizi Seif ameniambia kwa hiyo na mimi nataka nitafakari alichoniambia rafiki yangu ni ‘digest’ baada ya hapo nitajua nafanya nini” alisema Gwajima

Alipoulizwa kama watu watarajie chochote kutokea kuhusu CUF, Maalim Seif na Lipumba kwenye ibada Jumapili ijayo, Gwajima alijibu: “Kumbe mnajua, subirini Jumapili ifike nitamlipua na tutajua amekula maharage ya wapi.”

Askofu Gwajima amwomba Spika kuahirisha Bunge kwa ajili ya msiba

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephath Gwajima amemtaka Spika wa Bunge kuahirisha kikao cha Bunge siku ya kuaga miili ya watoto waliofariki kwa ajali jana.
Amesema kama Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliamuru viongozi kusimama kuwakumbuka watoto hao itakuwa ajabu kwa Bunge kuendelea na vikao vya Bunge.
Amesema Spika akiahirisha Bunge kwa siku moja itatoa nafasi kwa wabunge hao kwenda Arusha ili kuomboleza pamoja.

Gwajima afutiwa mashtaka ya kutoa lugha chafu

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeifuta kesi ya kutoa lugha chafu inayomkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Josephat Gwajima.
Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha aliifuta kesi hiyo leo chini ya kifungu cha 225 cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai (CPA).
Kesi hiyo imefutwa baada ya Wakili wa Serikali, Joseph Maugo kueleza kuwa hawakuwa na shaidi na kuomba wapewe ahirisho.
Katika uendeshwaji wa kesi hiyo upande wa mashtaka uliita ushahidi mmoja kwa miezi 14.
Katika kesi hii, Gwajima anadaiwa kuwa kati ya Machi 16 na 25,2015 Tanganyika Packers Kawe alitumia lugha chafu na kumdhihaki Muhadhama wa Kanisa Katoliki Askofu Kardinal Polcarp Pengo.

VIDEO: GWAJIMA AWASILI CLOUDS NA KUWAPA POLE

Askofu wa kanisa la Ufufuo na uzima Joseph Gwajima amezungumza na waandishi wa habari wa Clouds Media Group na kusema kilichomfanya afike katika ofisi hizo ni kutoa pole kwa kuwa yeye ni sehemu ya sababu za uvamizi huo.
“Isingekuwa busara watu wavamiwe na mimi ni mhusika mkuu halafu nisije kutoa pole,” alisema
Hatua ya Gwajima imekuja baada ya tukio la kituo hicho kuvamiwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda akiwa na polisi wenye silaha.
Gwajima amewasilia saa 4:00 asubuhi akiwa na msafara wa magari zaidi ya manne na walinzi wake takribani 30 na alipofika alipokelewa na Mkurugenzi wa vipindi na Uzalishaji Ruge Mutahaba na kufanya mazungumzo na waandishi wa habari na baadaye na uongozi wa kituo hicho.
Amewataka Clouds kuendelea na kazi zao za kawaida na kutaka suala hilo lisichukuliwe kisiasa huku akikisitiza kuwa Mkuu wa mkoa alikosea.

Gwajima amshambulia tena Makonda

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ametaja makosa ya kisheria yaliyomfanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kukimbilia Afrika Kusini.
Akizungumza leo kanisani kwake, Ubungo, jijini hapa, Gwajima alidai kosa la kwanza la Makonda ni kughushi cheti ambacho kinaonyesha yeye ni Paul Makonda wakati akifahamu kuwa yeye ni Daudi Bashite.
“Kosa hilo kwa mujibu wa Gwajima ni kifungo cha miaka saba.Kosa jingine ni kula kiapo cha ukuu wa wilaya na ukuu wa mkoa akisema yeye ni Makonda wakati akijua yeye ni Bashite,” alisema
Gwajima alisema kosa la hilo la kula kiapo na cheti feki ni kifungo cha miaka mitatu.
Kosa jingine alisema ni kupokea mshahara na posho kwa jina la Makonda wakati akifahamu si yeye na kuongeza kuwa kosa hilo likithibitika atatakiwa kurudisha mishahara na posho zote alizochukua.

POLISI WATINGA NYUMBANI KWA GWAJIMA, AGOMA KUFUNGUA MLANGO

Jeshi  la Polisi kwa mara nyingine jana lilizingira nyumba ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kwa kile lilichodai kuwa lilifika kufanya uangalizi.

Taarifa ambazo zimethibitishwa na Askofu Gwajima mwenyewe, zinaeleza kuwa polisi walifika nyumbani kwake wakiwa katika gari lao.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, polisi hao walipojaribu kutaka kuingia nyumbani kwa askofu huyo, walizuiwa mlangoni kwa sababu hawakuwa na kibali chochote wala maelezo yanayojitosheleza ya kutaka kukutana na kiongozi huyo wa kiroho.

Askofu Gwajima  jana alikiri polisi hao kumfuata nyumbani kwake na hivyo kulazimika kumtafuta wakili wake mara moja.

“Ni kweli walikuja wakiwa na gari la polisi, lakini walipofika nami nilimpigia mwanasheria wangu ambaye aliniambia tuwaulize wametumwa na nani na kama wana ‘search warrant’ (kibali cha kufanya upekuzi) au ‘arrest warrant’ (kibali cha kukamata),” alisema.

Askofu Gwajima alisema walipowauliza, walimtaja Afande Kingai kama ndiye mtu aliyewatuma, lakini hawakuwa na kibali chochote.

Kwa mujibu wa Askofu Gwajima, mwanasheria wake alifanya mawasiliano ya simu na Afande Kingai ambaye amepewa jukumu la kuwafuatilia wale wote waliotuhumiwa katika sakata la dawa za kulevya na kumuuliza sababu za kumfuata nyumbani.

“Afande Kingai amemweleza mwanasheria wangu kuwa walikuwa wamekuja kwa ajili ya ‘observation’ (uangalizi) tu, kwa hiyo mwanasheria wangu akasema kama ni ‘observation’ tu tusiwaruhusu kuingia ndani kwa sababu sheria ya hivyo hakuna, na sisi tumewazuia hawakuingia ndani,” alisema Askofu Gwajima.

Alipoulizwa kama kufuatwa kwake sasa na polisi kuna uhusiano wowote na kauli alizozitoa kanisani kwake hivi karibuni kuhusu elimu ya Paul Makonda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Askofu Gwajima alisema huenda ikawa hivyo, lakini akasisitiza kuwa hana uhakika kwa sababu hajazungumza na askari waliomfuata.

Na alipoulizwa kama anadhani ujio huo pia unatokana na andiko ambalo linasambaa kwenye mitandao ya kijamii ambalo linasema Jumapili ijayo mwalimu aliyemfundisha mtu mmoja anayetajwa kwa jina la Bashite atakuwapo kanisani kutoa ushuhuda, Askofu Gwajima alikana akisema andiko hilo si lake.

Pamoja na hayo, Askofu Gwajima alikwenda mbali na kuhoji: “Hata kama ni kweli, sasa unaogopa mwalimu kuja… kanisani kwangu wapo watu wengi waliosoma naye Bashite kuanzia shule ya msingi na Sekondari ya Pamba… vyeti kama huna huna tu.”

Alipoulizwa haoni kauli yake kwamba Rais Magufuli ni tofauti kabisa na Makonda ilikuwa na nia ya kuwatenganisha viongozi hao, Askofu Gwajima alisema aliyemtaja kwa kumshambulia ni Makonda na si Rais.

“Aliyenitaja kwa kunishambulia katika sakata la dawa za kulevya ni Makonda na si Rais, mimi nimemuongelea Makonda, mimi ni mtumishi wa Mungu siwezi kuongozwa kwa ‘speculation’, si unajua hata Yesu alisema kama wewe huna dhambi basi uwe wa kwanza kushika jiwe,” alisema Askofu Gwajima.

Alipoelezwa kuwa katika mahubiri yake ni kama anaonekana kumshtaki Makonda, askofu huyo alisema: “Nilisema nitamshtaki kwa mahakama iliyo juu yake na nilisema Makonda aombe radhi, angekuwa mstaarabu baada ya sakata lile yeye mwenyewe angenipigia simu na kuniambia Gwajima nilikengeuka, lakini hajafanya hivyo.”
 
Pamoja na hayo, Askofu Gwajima alisema kwa aliyoyafanya Makonda tayari amekwishamsamehe na ndiyo maana hajampeleka mahakamani.