HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

Jeshi la Polisi Lasema Linawashikilia Watu 3 Kwa Kuvamia Mkutano wa CUF na Kuwapiga Watu

Saa  tatu baada ya viongozi wa CUF kukutana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuhoji sababu za kutokamatwa watu waliofanya vurugu kwenye mkutano wa waandishi wa habari na viongozi wa chama hicho wa wilaya ya Kinondoni, Jeshi la Polisi limetangaza kushikilia watu watatu.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho Julius Mtatiro, viongozi hao waliwaeleza wanahabari kuwa ni ajabu kuona  Polisi haijachukua hatua huku ikijulikana wazi kuwa watu hao walijeruhi wanahabari na viongozi wa chama hicho katika tukio ambalo liliripotiwa na vyombo vya habari.

Viongozi hao walikutana na Sirro jana saa 5 asubuhi na kuzungumza kwa takribani saa moja, na kisha saa 8 mchana Kamanda huyo alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kukamatwa kwa watu hao, wakituhumiwa kuhusika katika tukio hilo.

Jumamosi iliyopita takribani watu watano wakiwa kwenye gari lenye nembo na bendera za CUF, walivamia mkutano huo uliokuwa ukifanyika kwenye hoteli ya Vinna, Mabibo wilayani Kinondoni na kufanya vurugu.

Miongoni mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso kininja alichomoa bastola na kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na wenzake, jambo lililosababisha wananchi wamzingire na kumshushia kipigo.

Katika ufafanuzi wake, Mtatiro alisema tukio hilo ni la 13 dhidi ya upande unaomwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad lakini vyombo vya Dola viko kimya.

“Baada ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa kimya ili kuona kama polisi watasema chochote ila imekuwa tofauti. Wako kimya tu,” alisema Mtatiro.

Akieleza kilichowapeleka kituoni hapo, alisema: “Tulitaka kujua yule mvamizi aliyekuwa na bastola mpaka sasa yuko wapi. Mvamizi mmoja tunajua alikamatwa na wananchi, akapigwa kidogo na kuokolewa. Tulitaka kujua alitoa maelezo gani.”

Alisema baada ya tukio hilo, Mkuu wa Upelelezi aliwapigia simu viongozi waliovamiwa akiomba waende kituo cha Polisi Magomeni  wakapatanishwe.

“Tulishangazwa na taarifa hiyo, kwa watu waliovamiwa kwenda kupatanishwa. Tulijihoji kama Jeshi la Polisi linaweza kupatanisha watu wenye makosa ya jinai, kwani mtu wa makosa hayo upelelezi unapokamilika hupelekwa mahakamani,” alisema Mtatiro.

Alisema sababu nyingine ya kwenda kituoni hapo ni kutaka kufahamu kama watu wanaofanya matukio hayo wako juu ya sheria.

“Tulimwonya Kamanda Sirro kwamba sisi (upande wa Maalim) tuna nguvu kuliko Lipumba na kuiomba Polisi kutekeleza majukumu yake kwa kuchukua hatua dhidi ya wavamizi hao,” alisema.

Katika mkutano wake na wanahabari, Sirro alisema Polisi inashikilia watu watatu wakituhumiwa kufanya vurugu kwenye mkutano huo.

“Tulipata taarifa ya kuvamiwa kwa mkutano wa wanachama wa CUF na watu wasiofahamika wakiwa na silaha. Baada ya taarifa hizo kupokewa askari walifuatilia na kukamata watu watatu,” alisema Sirro.

Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitafuatwa.

Alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa waliohusika watasakwa kokote watakokuwa.

KAMANDA SIRRO AWATAKA WANANCHI KUTOJICHUKULIA SHERIA MIKONONI

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Simon Sirro amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi badala yake waviachie vyombo husika ili viweze kufanya kazi yake.

Ameyasema hayo Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari. Amesema kuwa wananchi kujichukulia sheria mikononi pindi wawakamatapo watuhumiwa ni kinyume cha sheria hivyo wanatakiwa kuacha mara moja tabia hiyo.

“Ni vyema wananchi wakaacha  tabia ya kujichukulia sheria mikononi ili vyombo usika vifanye kazi yake,”amesema Sirro.

Aidha, amesema kuwa wananchi kuwauwa watuhumiwa ni kosa kisheria kwani watakao bainika kufanya hivyo sheria kali dhidi yao zitachukuliwa.

Hata hivyo, ameongeza kuwa ni bora wananchi waache tabia hiyo ya kujichukulia sheria mikononi kwani vyombo husika kama Polisi na Mahakama vipo kwa ajili ya shughuli hiyo.

WAZIRI NCHEMBA AWASILI ENEO YALIPOTOKEA MAUAJI YA POLISI WANANE

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amewasili eneo yalipotokea mauaji ya askari wanane katika kijiji cha Jaribu, Wilayani Kibiti.
Waziri Nchemba ameambatana na naibu wa wizara hiyo, Mhandisi Hamad Masauni.
Nchemba atatembelea kambi za askari polisi wa kanda ya Pwani na katika kata ya Bungu wilayani Kibiti.

WATU WATATU WANAODHANIWA KUWA NI MAJAMBAZI WAULIWA KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI

Watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi  wameuwa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kukaidi amri ya kutakiwa kusimama eneo la kizuizi cha Mwembe Muhoro wilayani Rufiji, mkoani Pwani.

Watu hao walikuwa wamepakiana kwenye pikipiki moja huku wakiwa wamevaa hijabu.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo, kamanda wa Polisi mkoani Pwani ,Onesmo Lyanga alisema pikipiki nyingine mbili zilifanikiwa kukimbia.

Akielezea juu ya tukio hilo alifafanua,lilitokea Aprili 2 mwaka huu majira ya mchana ,Muhoro ,Rufiji barabara kuu ya Dar es Salaam Lindi.

“Siku ya tukio askari walipata taarifa kuwa kulikuwa na pikipiki tatu zikitokea Kibiti kwenda mikoa ya Kusini zikiwa zimebeba watu watatu kila moja “

“Miongoni mwa pikipiki hizo kati yake mbili wamebebwa watu waliovaa hijabu,” alisema Lyanga.

Alisema askari wa barabarani walipewa taarifa katika kizuizi cha Mparange na kuwasimamisha ili wawahoji lakini walikataa na kupita ambapo waliwajulisha wenzao kwenye kizuizi cha Ikwiriri lakini walikaidi kusimama.

“Baada ya hapo walifika kizuizi cha Ikwiriri lakini bado walikaidi kusimama na kuendelea kukimbia ndipo walipofika kituo cha Muhoro “

“Hata hivyo hawakusimama na askari waliokuwa doria wakiwa kwenye gari waliwafuatilia na wakavuka daraja la Mkapa na waliwapa onyo kwa kupiga risasi hewani,” alisema Lyanga.

Aidha alibainisha baada ya hapo watu hao waliruka kwenye pikipiki na kuanza kukimbilia msituni na ndipo askari walipowapiga risasi za miguu na kiunoni na kufanikiwa kuwakamata.

“Majeruhi hao walijulikana ni wanaume hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika na walikuwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 272 BLW aina ya Boxer yenye rangi nyeusi”

“Watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi  kwa mwonekano wao walijaribu kuwawahisha hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alisema Lyanga.

Lyanga alisema walipofikishwa hospitali daktari alithibitisha kuwa watu hao wamefariki dunia .

Hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika huku pikipiki nyingine mbili zilitoroka na kuelekea mkoa wa Lindi na taarifa zimetolewa polisi ili wawakamate.

Aliwataka wananchi kuwa watulivu pale wanaposimamishwa na askari polisi badala ya kujaribu kutoroka na kwa sasa jeshi hilo limeimarisha doria katika kukabiliana na uhalifu.

WAZIRI MWIGULU AWAASA ASKARI KUTOWABAMBIKIZIA WATU KESI

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi.
Mzee John Samwel Malecela akizungumza wakati wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi nchini Ernest Mangu Akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Jordan Lugimbana akitoa salamu za Mkoa wa Dodoma wakati wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
 Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi.
SACP Ramadhani Mungi Msimamizi wa bandari Tanzania na Kamanda wa polisi mkoa wa Lindi Renata Mzinga wakifatilia kwa makini kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akisalimiana na Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Samwel Malecela mara baada ya kuwasili katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe Mwigulu Lameck Nchemba akisalimiana na baadhi ya Maafisa wa jeshi la Polisi mara baada ya kuwasili katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha Mwaka 2017 cha Maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi.

Na Mathias Canal, Dodoma
Askari na Maafisa wa jeshi la Polisi nchini wameaswa kutotumia madaraka yao vibaya kwa kuwabambikizia wananchi kesi kwani kufanya hivyo ni kushindwa kusimamia dhamira njema ya Mhe Rais ya kuwapatia wananchi wanyonge haki zao stahiki.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe Mwigulu Nchemba wakati akifungua kikao cha kazi cha Siku tatu cha mwaka 2017 kwa maafisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa/Vikosi kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa LAPF Mjini Dodoma.
Mhe Mwigulu amesema kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kuwabambikizia kesi, Kuwabadilishia watu kesi zao za msingi kwa sababu ya kushindwa kutoa rushwa hivyo kikao hicho kinapaswa kuwa na maamuzi na maadhimio yenye dira na taswira njema kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesisitiza pia Askari na Maafisa wa Polisi kutotumia taarifa za watu wanaohasiana kuwa ndio chanzo pekee cha msingi wa shtaka badala yake kufanya uchunguzi kwa kina na kujiridhisha vyema ili kufikia hukumu yenye tija Na haki kwa mtuhumiwa kwani kufanya hivyo kutaimarisha amani na jeshi la Polisi kupata taarifa nyingi za uhalifu kutoka kwa wananchi endapo watajikita katika haki.
Akizungumzia Vita dhidi ya Dawa za Kulevya Mhe Nchemba alisema kuwa serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukamata na kuziteketeza Dawa za kulevya zilizopo mashambani ambapo ametilia msisitizo zaidi kwa Askari na Maafisa wa Jeshi la Polisi kuendelea kupambana ili kuzikamata Dawa za kulevya zilizopo katika viwanda.
Amesisitiza pia Jeshi la Polisi kuendelea kupambana na kubaini uhalifu sambamba na kushirikiana na vyombo vingine ili kuhakikisha lengo mahususi la serikali ambalo ni kuzuia uhalifu linafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Mhe Mwigulu amesema kuwa kauli mbiu ya Mwaka 2017 inayosema "ZINGATIA MAADILI TUNAPOPAMBANA NA UADILIFU ILI KUIMARISHA USALAMA KWA MAENDELEO YA TAIFA" endapo kama itatekelezwa kwa vitendo itaijenga nchi na kuzidi kudumisha zaidi amani iliyopo kwa wananchi.
Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi nchini Ernest Mangu alisema kuwa kikao hicho cha kazi kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi kina dhamira kubwa ya kufanya Tathmini ya utendaji wa mwaka 2016 na kuandaa mikakati mizuri ya mwaka 2017 na kupata fursa ya kubadilika kiutendaji kwa kuzingatia dhamira ya serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Hata hivyo amesisitiza zaidi askari wote nchini kutofanya kazi kwa mazoea, Kuacha Urasimu na kujenga uaminifu na weledi katika kazi.
Mangu amesema matendo ya Askari Polisi nchini yanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa katika jamii hivyo askari Polisi hapaswi kuwa chanzo cha vurugu au kujihusisha na matendo ovu yasiyostahili katika jamii.
Ameongeza kuwa miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaombele kwa kujadiliwa katika Kikao hicho itakuwa ni pamoja na Vita dhidi ya Dawa za Kulevya, Vita dhidi ya Magendo, Vita dhidi ya ujangili na Uvuvi sambamba na Vita dhidi ya Ubambikizaji wa kesi kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Jordan Lugimbana akitoa salamu za Mkoa wa Dodoma kabla ya kumkaribisha Waziri Mwigulu Nchemba kuzungumza na askari hao amelipongeza jeshi la Polisi kwa kazi kubwa linayofanya ambapo pia ameeleza mpango wa Mkoa katika kupambana na migogoro ya ardhi kwa kuanzisha kamati maalumu ya wataalamu wa sheria kutoka chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) Kupitia na kushauri ili kuweza kumaliza haraka migogoro hiyo.
Naye Makamu wa kwanza wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Samwel Malecela alisema kuwa jambo la msingi ambalo askari Polisi wanapaswa kulifanya ni pamoja na kuhakikisha kila mwananchi anapata Uhuru wake na kama jambo hilo likitekelezwa ipasavyo Fikra za Hayati Mwalimu J.K Nyerere zitakuwa zimeenziwa kwa weledi.

SIRRO: MBOWE ASIPORIPOTI TUTAMFUATA

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kama Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe hataripoti bila kutoa taarifa yoyote ya hudhuru atafuatwa kwa kuwa jeshi hilo linahitaji kumhoji.
Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro amesema hayo leo muda mfupi baada ya Mbowe kueleza kuwa hataripoti polisi kutokana na wito wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Pia Sirro amesema askofu wa kanisa la ufufuo na uzima Josephat Gwajima na mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji walilala polisi kwa kuwa bado upelelezi dhidi yao unaendelea..
"Oparesheni ya dawa za kulevya bado inaendelea na kuanzia sasa hatutaruhusu mkusanyiko wa wananchi karibu na kituo cha polisi hiki watakaoonekana watashughulikiwa na asije akalaumiwa Kamishina Sirro kwa kuwa tayari nimeshatoa taarifa."

Chanzo: Mwananchi

MSAKO DAR WANASA WATUHUMIWA 590

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


JESHI la Polisi katika Kanda Maalumu Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa 586 kwa makosa mbalimbali katika msako uliofanyika kwa siku kumi kuanzia Novemba 22 mwaka huu.

Hayo yalisemwa jijini humo na Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro.

Alisema watuhumiwa hao wamekamatwa maeneo mbalimbali kwa nyakati tofauti kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu, kuvunja nyumba usiku na kuiba, wizi kutoka maungoni, kucheza kamari, kubughudhi abiria, wizi wa magari, shambulio la aibu na la kawaida, kutengeneza, kuuza na kunywa pombe haramu ya gongo pamoja na uvutaji bangi.

Aliongeza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa baada ya operesheni iliyofanyika maeneo ya Buguruni na Magomeni ambapo walikamatwa jumla ya watuhumiwa 257, walikamatwa kwa makosa mbalimbali na jumla ya lita 405 za Pombe haramu za gongo zilikamatwa, mitambo miwili ya kutengenezea gongo na bangi.

Kamanda Sirro alisema baadhi ya watuhumiwa hao walikutwa na silaha ndogo ndogo za kufanyia uhalifu kama visu, nyembe, bisibisi. Katika tukio jingine , Polisi Kanda Maalum Dar es salaam kupitia kikosi kazi cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha, mnamo Novemba 29, mwaka huu majira ya saa nne na nusu Kijichi Neluka Mbagala lilifanikiwa kukamata gari lililobeba mali za wizi.

Sirro alisema gari hilo lilikamatwa baada ya majambazi watatu wakiwa na gari Toyota Noah lenye rangi ya fedha lililosajiliwa kwa namba za usajili T 129 DDS, kuvamia baa moja inayofahamika kwa jina la Whatsapp na kuvunja, kisha kuiba vitu mbalimbali vikiwemo seti ya televisheni aina ya Samsung, king’amuzi kimoja cha startimes kimoja, radio moja, spikambili aina ya Sony, na katoni tatu za glasi.

GARI LA WIZI LAMPONZA PADRI WA KANISA KATOLIKI SUMBAWANGA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Kikosi Kazi cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam cha kuzuia wizi wa magari kimeendelea na kazi ya kudhibiti vitendo hivyo kwa kumkamata Padri wa Kanisa Katoliki Sumbawanga Demestrious Apolinary kwa tuhuma za kuhusika na ununuzi wa gari ya wizi.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro amesema mnamo Novemba, 11 baada ya padri huyo kununua gari aina ya Toyota L/cruiser T616 DCH mali ya Joseph Kayawaya lililoripotiwa kuibiwa Dar es Salaam na nyaraka za kughushi na kuuzwa jijini Arusha.

Amesema padri huyo anafanyiwa mahojiano na kwamba upelelezi utakapokamilika atapelekwa mahakamani ili kuona kama ni mnunuzi asiye na hatia au alishiriki kwa namna moja au nyingine katika wizi huo.

Kamanda Sirro amesema pia Jeshi la Polisi linashikilia watuhumiwa wengine wanne aliowataja kwa majina ya Aman Dickson, Exaud Martin, Rashid Haruna na Mzee Nasibu kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa magari katika matukio mawili tofauti.

Katika tukio lingine, Kamanda Sirro amesema Jeshi la Polisi linashikilia majambazi watano na vifaa mbalimbali walivyopora maeneo ya Tuwangoma mtaa wa Masaki, Mbagala.

WALIMU WATATU WATIWA MBARONI KWA KUWAZUIA WANAFUNZI KUFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


POLISI mkoani Dodoma inawashikilia walimu watatu wa shule za sekondari kwa tuhuma ya kuwazuia wanafunzi wa kidato cha nne, kufanya Mtihani wa Taifa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema kwamba walimu hao wa shule za sekondari za Zoissa na Mnyakongo wilayani Kongwa, walikamatwa Novemba Mosi mwaka huu.

Kamanda Mambosasa alisema kwamba, wakati wa mtihani wa somo la Kiingereza, walimu hao walimzuia mwanafunzi Amina Said wa shule ya sekondari Zoissa kwa madai ya kuwa ni mjamzito na kumpeleka kituo cha afya, kupimwa muda wa mtihani, lakini majibu yalionesha hakuwa na ujauzito.

Aidha, mwanafunzi Bahati Ntigonza wa shule ya sekondari Mnyakongo, alizuiliwa kuingia katika chumba cha mtihani kwa kuwa hakuvaa sare ya viatu, hivyo alirudishwa nyumbani kuvaa viatu huku wenzake wakiendelea na mtihani.

Kamanda Mambosasa aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Lukonge Mwezo ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Mnyakongo, Omari Athumani Mkuu wa Shule ya Sekondari Zoissa na Daud Suleimani John aliyekuwa mwalimu wa zamu katika shule ya sekondari Mnyakongo.

RPC KINONDONI ATOA TAHADHARI KWA WAMILIKI WA MAGARI JIJINI DAR ES SALAAM

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


RPC Suzan Kaganda
Na Dotto Mwaibale


WAMILIKI wa magari wametakiwa kuchukua tahadhari ya kuzima na kufunga milango magari yao pale wanaposimama kwa dharura kupata mahitaji mbalimbali ili kuyanusuru kuibwa.



Mwito huo umetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Suzan Kaganda wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam kuhusu tukio la kuibwa kwa gari la Kapteni Innocent Dallu maeneo ya Mbezi Juu huku akiwemo mtoto wake Lightness.



"Napenda kutumia fursa hii kuwaomba wamiliki wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari ya kuzima magari yao na kufunga milango wanaposimama maeneo yoyote kupata mahitaji yao kwani si rahisi kumbaini mhalifu kwani wapo kila sehemu" alisema Kaganda.



Alisema katika tukio la kuibwa kwa gari la kampteni Dallu alikuwa amesimama maeneo ya Mbezi Juu bila ya kulizima akinunua mahitaji ambapo walitokea vijana wakaondoka na gari hilo aina ya Toyota Harrier baada ya kumtelemsha mmoja wa watoto aliyekuwemo ndani ya gari hilo aitwaye Philip huku wakiondoka na mdogo wake Lightness.



Alisema watuhumiwa hao walimtelekeza mtoto huyo maeneo ya Golden Bridge katika baa moja na kisha kuondoka na gari hilo ambalo lilipatikana baada kukamatwa na polisi Kiwangwa mkoani Pwani ambapo  kijana mmoja Ezekiel Daud anashikiliwa na polisi kwa mahojiano.



Alisema ni vizuri wamiliki wa magari kuzingatia jambo hilo ili kuepusha matukio kama hayo ambayo yanapoteza muda mwingi wa kuyatafuta kwani tukio kama hilo lilitokea hivi karibuni maeneo ya Kinondoni ambapo wahalifu waliweza kuiba gari aina ya Noah lililosimamishwa bila ya kuzimwa na kuondoka nalo na alijapatikana mpaka leo hii.

POLISI ARUSHA YATOA ONYO KWA WANAOLIMA BANGI

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Mkuu wa Kikosi cha kutuliza Ghasia mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Ramadhani Giro akiwa anaonyesha burungutu la madawa ya kulevya aina ya bangi ambalo lilikuwa limehifadhiwa kwenye moja ya magunia yaliyopatikana katika kijiji cha Kismiri Juu wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Mkuu wa Operesheni mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) James Manyama akiwa ameshikilia ndoo lenye mbegu za mmea wa bangi mara baada ya operesheni iliyofanywa na jeshi la Polisi kijiji cha Kismiri wilayani Arumeru kumalizika. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)

Jeshi la Polisi mkoani hapa lipo kwenye mkakati wa kuwachukulia hatua viongozi wote wanaoishi au kufanyia kazi katika maeneo ambayo yatabainika wananchi wa maeneo yao wanalima bangi bila wao kuwachukulia hatua zozote au kutoa taarifa kwa vyombo husika.

Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu kamishna (DCP) Charles Mkumbo alipokuwa anaongea na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya operesheni iliyofanyika katikati ya wiki iliyopita katika kijiji cha Kismiri Juu, kata ya Uwiro tarafa ya King’ori wilayani Arumeru,

“Mara kadhaa tunapofanya operesheni hizo wananchi wa eneo hilo huwa wanakimbia na kuacha nyumba zao huku viongozi wao kutoonekana kabisa au kutoa taarifa zozote juu ya uhalifu huo, sasa tutawachukulia hatua kwani wao ni sehemu ya uwajibikaji katika kuzuia vitendo vya uhalifu”. Alisema Kamanda Mkumbo.
Katika operesheni hiyo, jeshi la Polisi lilifanikiwa kupata jumla ya magunia 22 ya bangi yaliyokuwa yamehifadhiwa katika nyumba za wakazi hao na kwenye makorongo yanayozunguka kijiji hicho pamoja na kilogramu 80 za mbegu za mmea huo ambazo zote ziliharibiwa kwa kuchomwa moto.

Kamanda Mkumbo aliendelea kueleza kwamba, katika operesheni hiyo pia walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aitwaye Raphael Laizer (33) mkazi wa Kismiri Juu akiwa na magunia matatu ya bangi huku taratibu za kumfikisha mahakamani zikiwa zinaendelea.

Kamanda Mkumbo aliongeza kwa kusema kwamba, imekuwa vigumu kuwakamata watuhumiwa kutokana na jiografia ya eneo hilo ambapo kila kunapokuwa na operesheni askari wanapokwenda, wananchi hao wanawaona kirahisi au kusikia miungurumo ya gari na kisha hukimbilia milimani na kuwaacha wazee na watoto.

“Japokuwa operesheni hizo ambazo tunazifanya mara kwa mara zimekuwa za mafanikio lakini changamoto zilizopo ni pamoja na miundo mbinu ya eneo hilo si rafiki kwa magari hasa uwepo wa milima mirefu na ubovu wa barabara”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.

Operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia saa 12:00 asubuhi mpaka saa 7:30 mchana ilijumuisha askari wa vikosi na vitengo mbalimbali huku ikisimamiwa na Mkuu wa Operesheni mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) James Manyama.
Mmoja wa askari wa Jeshi la Polisi akiwa anaendelea na zoezi uchomaji wa bangi katika kijiji cha Kismiri Juu, wilayani Arumeru wakati wa operesheni iliyofanyika katika eneo hilo.
Askari wa Jeshi la Polisi wakivusha moja ya gunia la bhangi lililofichwa katika korongo wakati wa operesheni ya bangi iliyofanyika kijiji cha Kismiri wilayani Arumeru. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha).

BABA AUA MWANAWE KISA KUFUNGUA REDIO KWA SAUTI KUBWA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


BABA mmoja mkazi wa Kijiji cha Maji ya Moto, Wilaya ya Arumeru mkoani hapa, Wilfred Kivuyo amemuua mtoto wake baada ya kumchoma kisu tumboni, kwa kosa la kufungulia redio kwa sauti ya juu.

Kabla ya tukio hilo inadaiwa yalitokea mabishano ya kugombea kupunguza sauti ya redio kati ya baba na mtoto, ambapo baba aliamua kumchoma kisu tumboni mtoto wake na utumbo kutoka nje.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema, tukio hilo lilitokea Oktoba 23, mwaka huu saa tatu usiku katika Kijiji cha Maji Moto na kumtaja marehemu kuwa ni Abraham Wilfred (22), ambaye kabla ya mauti alikuwa nyumbani akiendelea na shughuli zake huku akiwa amefungulia redio.

Alisema siku ya tukio mtuhumiwa huyo alifika nyumbani akiwa amelewa na kumkuta mtoto wake amefungulia redio kwa sauti ya juu, ambapo alimtaka kupunguza sauti hiyo lakini mtoto huyo aligoma.

“Baada ya hapo mabishano na kutoelewana kulijitokeza baina yao wakaanza kupigana, baba alipozidiwa nguvu na mtoto wake alichomoa kisu cha kukunja kwenye mfuko wa suruali kisha akamchoma tumboni na kumsababisha utumbo kutoka nje.

“Mara baada ya tukio hilo mtoto huyo alichukuliwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu, lakini hata hivyo alifariki wakati madaktari wakiendelea kuokoa maisha yake,” alisema Kamanda Mkumbo.

Kamanda Mkumbo alisema Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka mtuhumiwa huyo ambaye baada ya tukio alikimbia ili hatua zaidi za kisheria zisichukuliwe dhidi yake

WATU 6 WANASWA NA SILAHA KWA MGANGA WA KIENYEJI MWANZA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Taarifa Ya Jeshi La Polisi Mkoa Wa Mwanza Kwa Vyombo

Kwamba Tarehe 18.10.2016 Majira Ya Saa 13:00hrs Katika Eneo La Buswelu Kata Ya Buswelu Wilaya Ya Ilemela Jiji Na Mkoa Wa Mwanza, Askari Wakiwa Katika Misako Na Doria Walifanikiwa Kuwakamata Watu Sita Wakiwa Na Silaha Mbili Zilizotengenezwa Kienyeji Pamoja Na Risasi Ishirini Na Tatu, Ambazo Walikuwa Wakizitumia Katika Matukio Ya Unyang’anyi Wa Mali Na Uporaji Hapa Jijini Mwanza Na Mikoa Mingine.

Aidha Tukio Hilo Limefanikiwa Baada Ya Kupokea Taarifa Kutoka Kwa Raia Wema Kuhusu Uwepo Wa Wahalifu Hao, Ndipo Askari Walifanikiwa Kumkamata Kwanza Jeremiah Maligia @ Mkumbo Miaka 25, Mnyiramba, Fundi Seremala Mkazi Wa Malega – Singida Ambaye Alipohojiwa Alikiri Kuhusika Na Kutaja Wenzake Waliokuwa Wakishirikiana, Na Kuwa Silaha Wamezificha Kwa Mganga Wa Kienyeji Aitwaye Leornad Litta @ Makai Anayeishi Mtaa Wa Kagida – Buswelu.

Askari Walikwenda Mahali Hapo Na Kufanikiwa Kumkamata Mganga Huyo Wa Kienyeji Bwana Leornad Litta Miaka 39, Akiwa Na  Silaha Hizo Mbili Zilizotengenezwa Kienyeji Hapo Nyumbani Kwake Na Risasi Ishirini Na Mbili Zinazotumiwa Na Bunduki Ya Aina Ya Short Gun Na Risasi Moja Ya Rifle Aina Ya Mark Iv.

Aidha Katika Kuhojiwa Zaidi  Na Askari Watuhumiwa Tajwa Hapo Juu Waliwataja Washirika Wao Wanne Ambao Walikuwa Wakishirikiana Katika Kufanya Uhalifu Ambapo Askari Walifanikiwa Kuwakamata, Ambao Ni 1. Kamgisha Jovini Kamhambwa Miaka 40, Mlinzi Na Mkazi Wa Iloganzala, 2. Juma Yusuph @ Jimi Miaka 35, Mkazi Wa Bwani Kinondoni, 3. Samweli Peter Miaka 36, Mkazi Wa Busweli Na 4. Shabani Hussein Miaka 26, Fundi Viatu Na Mkazi Wa Nyasaka Msumbiji.

Watuhumiwa Wote Walipofanyiwa Mahojiano Walikiri Kwamba Silaha Hizo Walizitumia Katika Unyang’anyi Wa Mali Na Uporaji Katika Maeneo Ya Jiji Na Mkoa Wa Mwanza, Aidha Jeshi La Polisi Kwa Sasa Linaendelea Na Uchunguzi Kuhusiana Na Tukio Hilo Na Matukio Waliyokuwa Wameyafanya, Pindi Uchunguzi Ukikamilika Watuhumiwa Wote Watafikishwa Mahakamani.

Kamanda Wa Polisi Mkoa Wa Mwanza Naibu Kamishina Wa Polisi Ahmed Msangi Anatoa Wito Kwa Wakazi Wa Jiji Na Mkoa Wa Mwanza Akiwataka Kuendelea Na Tabia Ya Kutoa Ushirikiano Kwa Jeshi Lao La Polisi, Ili Tuweze Kudhibiti Uhalifu Katika Mkoa Wetu., Lakini Pia Anatoa Angalizo Kwa Wananchi Haswa Vijana Akiwataka Kuacha

Tabia Ya Kujihusisha Na Uhalifu Bali Wajikite Katika Kufanya Shughuli Halali Za Maendeleo, Kwani Jeshi La Polisi Lipo Vizuri

Kuhakikisha Ulinzi Na Usalama Upo Kwa Raia Wote Wa Jiji Na Mkoa Wa Mwanza.

Katika Tukio La Pili
Mnamo Tarehe 18.10.2016 Majira Ya Saa 14:00hrs Mchana Katika Eneo La Ilemela Wilaya Ya Ilemela Jiji Na Mkoa Wa Mwanza, Askari Walifanikiwa Kuwakamata Watu Wawili Ambao Ni 1. Rahim Feka Miaka 28, Mkazi Wa Ilala – Dar Es Salaam, 2.  Ally Kawalale Miaka 32, Mkazi Wa Jetrumo – Arport Dar Es Salaam, Wakiwa Wanataka Kuuza Gari Lenye Namba T.778 Azv Aina Ya Toyota Land Cruiser Lililokuwa Wameliiba Huko Ilala Jijini Dar Es Salaam.

Aidha Watuhumiwa Hao Walikamatwa  Baada Ya Kupokelewa Taarifa Ya Kuibiwa Kwa Gari Hilo Huko Dar Es Salaam Na Kwamba Kuna Uwezekano Kuwepo Eneo La Kanda Ya Ziwa, Ndipo Ulifanyika Upelelzi Kuhusiana Na Taarifa Hiyo, Na Kufanikiwa Kuwakamata Watuhumiwa Tajwa Hapo Juu Wakiwa Na Gari Hilo.

Watuhumiwa Wote Wapo Chini Ya Ulinzi Wa Jeshi La Polisi Wakiendelea Na Mahojiano , Huku Taratibu Za Kuwasafirisha Kwenda Dar Es Salaam Wakiwa Chini Ya Ulinzi  Wa Askari Polisi Zikiwa Bado Zinaendelea.

Kamanda Wa Polisi Mkoa Wa Mwanza Naibu Kamishina Wa Polisi Ahmed Msangi Anatoa Rai Kwa Wakazi Wa Jiji Na Mkoa Wa Mwanza Akiwataka Kuacha Tabia Ya Kununua Vitu Vya Wizi, Bali Pindi Wanapoona Biashara Za Wizi Zinataka Kufanyika Au Zinafanyika Watoe Taarifa Polisi Ili Watuhumiwa Waweze Kukamatwa Na Kufikishwa Mahakamani.

Katika Tukio La Tatu
Kwamba Tarehe 18.10.2016 Majira Ya Saa 23:00hrs Katika Kitongoji Cha Ibungiro Kijiji Cha Sagani Kata Ya Kandawe Wilaya Ya Magu Mkoa Wa Mwanza, Mtu Mmoja Msichana Aliyejulikana Kwa Jina La Dema Charles @ Bulayi Miaka 20, Mkazi Wa Kandawe, Ameuawa Kwa Kukatwa Na Vitu Vyenye Ncha Kali Sehemu Za Kichwani Na Kiunoni

Akiwa Amelalala Na Watu Wasiojulikana, Huku Wenzake Wa Wili Wakijeruhiwa Sehemu Mbalimbali Za Miili Yao.

Majeruhi Waliojeruhiwa Katika Tukio Hilo Ni 1.mariam Lucas @ Kapele Miaka 26, Mkazi Wa  Kijiji Cha Sagani Aliyejeruhiwa  Shingoni Na Kwenye Kiganja Cha Mkono Wa Kulia, 2. Kapelele Makubi @ Salulo Miaka 90, Ambaye Ni Baba Mwenye Nyumba/ Mji, Aliyejeruhiwa Mgongoni, Kichwani Na Kiunoni.

Inadaiwa Kuwa Wauaji Hao Walifika Katika Nyumba Hiyo Majira Tajwa Hapo Juu Na Kuwakuta Wenye Mji  Wakiwa Wamelala, Ndipo Waliingia Ndani Na Kufanya Mauaji Hayo, Hadi Sasa Hakuna Mtu Yeyote Aliyekamatwa Kuhusiana Na Tukio Hilo.

Aidha Uchunguzi Wa Awali Umebainisha Kuwa Mauji Hayo Yametokana Na Kulipiza Kisasi, Jeshi La Polisi Kwa Sasa Lipo Katika Upelezi Pamoja Na Uchunguzi Kuhusiana Na Tukio Hilo, Majeruhi Wapo Katika Hospitali Ya Wilaya Ya Magu Wakiendelea Kupatiwa Matibabu Na Hali Zao Zinaendelea Vizuri.

Kamanda Wa Polisi Mkoa Wa Mwanza Naibu Kamishina Wa Polisi Ahmed Msangi Anatoa Wito Kwa Wakazi Wa Jiji Na Mkoa Wa Mwanza Akiwataka Kutoa Ushirikiano Kwa Jeshi La Polisi Ili Watuhumiwa Wa Mauaji Hayo Wawezwe Kukamatwa Na Kufikishwa Katika Vyombo Vya Sheria.

Imetolewa Na:
Dcp: Ahmed Msangi
Kamanda Wa Polisi (M) Mwanza