HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

CUF KUIFIKISHA KORTINI WAKALA WA USAJILI, UFILISI NA UDHAMINI (RITA)

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi(CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu madai ya muendelezo wa hujuma dhidi ya chama hicho zinazofanywa na ofisi ya msaji wa vyama vya siasa nchini. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Seveline Mwijage.
Maofisa wa Chama hicho wakiwa meza kuu wakati wa mkutano na wanahabari.
Wabunge wa chama hicho wakiwa kwenye mkutano huo.
Baadhi ya wanahabari wakiwa kwenye mkutano huo
Wapiga picha kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo. 

Na Dotto Mwaibale

CHAMA cha Wananchi (CUF), kinatarajia kumfikisha mahakamani Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA)kwa kukiuka taratibu za sheria ya wadhamini kwa kutojiridhisha juu ya uhalali wa majina ya Bodi ya Wadhamini yaliyofikishwa kwake kama yalipitishwa na kikao halali cha chama kwa mujibu wa katiba.

Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif jijini Dar es Salaam leo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema wanachukua hautua hiyo kutokana RITA kushindwa kutumia mwongozo na weledi katika kutekeleza majukumu yao na badala yake wamesukumwa na utashi binafsi kwa ajili ya hujuma dhidi ya chama hicho.

Chama chetu kimepatwa na mshituko mkubwa sana, kuona taasisi kubwa nan yeti yenye dhamana kubwa katika nchi inaweza kufanya vitendo vya ovyo. RITA ni taasisi inayobeba maisha ya watu ya kila siku. 



Licha ya kusajili Bodi za Wadhamini, inasajili vizazi na vifo, ndoa, talaka na inatunza wosia kwa ajili ya mirathi,” alisema Maalim.Alisema michakato wa kufungua kesi hiyo inaanza leo ambapo alieleza kuwa tayari wamekwisha agiza mwawakili kulishughulikia. 

Kutokana na matarajio ya ufunguzi wa kesi hiyo watawasilisha maombi mbele ya Mahakama Kuu kuitaka isimamishe kesi nyingine zote walizofungua kuhusiana na kadhia hiyo hadi hapo shauri linalohusu uhalali wa maamuzi ya RITA litakapoamuliwa.

Maalim alisema kusajiliwa kwa bodi hiyo ambayo aliiita kuwa ni bodi feki, alieleza kwamba ni mwendelezo wa kukihujumu na kukidhoofisha chama kunakofanywa dola kupitia kwa Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na Profesa Ibrahim Lipumba na kundi lake.

Alitaja mambo manne ambayo yalikuwa msukumo wa kusajiliwa kwa bodi hiyo. Alisema kuwa ni kwa ajili ya kufuta kesi zote zilizofunguliwa na ambazo zinawaelemea licha ya kutumia nguvu kubwa ya dola, kufungua akaunti mpya ya benki ili kumwezesha Profesa Lipumba kupata ruzuku.

Aliongeza mengine kuwa ni Bodi hiyo kuwezesha udhibiti wa Ofisi za Makao Makuu, Zanzibar pamoaja na kumwondoa madarakani Katibu Mkuu Maalim Seif Hamad na hivyo kufanikisha njama za kuwapokonya haki Wazanzibar kwa maamuzi yao ya Oktoba 25 mwaka 2015.

Hamadi alisema kamwe haki ya Wazanzibar haitapotea na kuahidi kuwa ndani ya miezi mitatu haki hiyo itakuwa imepatikana.

Msajili wa Vyama Azungumzia Sakata la Maalim Seif Kufungua Ofisi Mpya za CUF

Kutokana na Chama cha Wananchi (CUF) kufungua ofisi mpya za chama hicho katika eneo la Mtaa wa Idrisa Kata ya Mzimuni, Magomeni wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Msajili wa Vyama vya Siasa amesema anaamini chama hicho kinafanya mambo yake kwa kuzingatia sheria.

Jana  Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema hajapata taarifa yoyote ya chama hicho, kufungua ofisi mpya zaidi ya kuona katika vyombo vya habari.

“Ukiondoa taarifa za kwenye media sijapata taarifa yoyote kutoka CUF labda wawe wameleta leo (jana), lakini naamini chochote wanachofanya wanaelewa taratibu wataleta taarifa, “ alisema Jaji Mutungi.

Jaji Mutungi alisema sheria inawataka wanapofungua ofisi watoe taarifa ndani ya siku 14, ambazo hazijaisha hivyo anaamini wanajua hilo. 

Upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad wamefungua ofisi hizo, baada ya tukio la kuvamiwa katika Ofisi Kuu za Buguruni na kundi la Profesa Ibrahim Lipumba.

Jaji Mutungi alisema atakapopokea taarifa rasmi ataangalia kama taratibu zilifuatwa kwani ufunguaji wa ofisi mpya una taratibu zake. 

“Nikiletewa taarifa ndio nitajua kama walifata taratibu au la, ufunguaji wa ofisi una taratibu zake najua wanazijua pia, “ alisema Jaji Mutungi.

Alisema taarifa hiyo ataipata kutoka kwa mwenyekiti au msemaji wa chama, ambaye ni katibu mkuu ambao wanatambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa. 

Akizindua ofisi hiyo Juni 4 mwaka huu, Maalim Seif alisema ofisi hiyo imetolewa na wabunge 40 wa CUF.

Alisema uamuzi wa wabunge hao kumpatia ofisi ya kufanyia kazi hapo ni kitendo cha kiungwana na kiungwe mkono na wanachama wote. 

Alisema kwa miezi 10 sasa, wamekuwa wakishindwa kufanya kazi kwa upande wa Tanzania Bara, jambo ambalo limewaathiri hivyo kupatiwa ofisi kutamsaidia kutimiza majukumu bila hofu yoyote.

Katibu huyo alisema ana imani na mahakama kuwa itawapatia haki stahiki hivyo kuwataka wanachama kuendelea kuwa na subira.

CUF Ya Maalim Seif Yazindua Ofisi Magomeni Jijini Dar Es Salaam

IKIWA ni takribani miezi 10 sasa kwa Chama cha Wananchi (CUF), upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad kuvamiwa katika Ofisi Kuu za Buguruni na kundi la Profesa Ibrahim Lipumba chama hicho kimezindua ofisi mpya za chama hicho katika eneo la Mtaa wa Idrisa, Kata ya Mzimuni, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aidha, Seif amesisitiza kuwa hatarajii kukutana na Profesa Lipumba kwa kile alichodai kuwa hatambuliki katika chama na hana sifa hizo kwa sasa.

Akizindua ofisi hiyo ambayo lengo kubwa ni kwa ajili ya wabunge 40 wa CUF, Seif alisema uamuzi wa wabunge hao kumpatia ofisi ya kufanyia kazi hapo ni cha kiungwana na kinahitajika kuungwa mkono na wanachama wote.

Alisema kwa muda wa miezi 10 sasa wamekuwa wakishindwa kufanya kazi hasa upande wa Tanzania Bara jambo ambalo limewaathiri sana hivyo kupatiwa ofisi kutamsaidia kutimiza majukumu yake vilivyo bila hofu yoyote.

Maalim Seif alisema kukosa ofisi kumewaathiri sana katika baadhi ya mambo hivyo anaamini kwa sasa akifikia Dar es Salaam anamahali pa kukutana na wakurugenzi wake.

“Nimekuwa ni kija hapa nakosa sehemu ya kukutana na wakurugenzi, viongozi mbalimbali wanachama ila hiki ambacho wabunge wamefanya ni cha kuungwa mkono sijawahi kufanya kazi na wabunge wanao kipenda chama kama kipindi hiki,” alisema.

Katibu huyo alisema atahakikisha kuwa anaanza kazi haraka iwezekanavyo kwa kukutana na wakurugenzi wake ili waweze kutekeleza majukumu ya chama.

“Hakuna shaka kuwa huu unaoitwa mgogoro umeturudisha nyuma sana hivyo naamini wakati wa kufanyakazi umerejea na hawa wabaya wetu hawata ambulia kitu kwani CUF ni chama imara hakitikisiki,” alisema.

Maalim Seif alisema jitihada zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukimaliza chama ni kubwa lakini hawataweza kufikia lengo hilo kutokana na misingi ya chama hicho.

Alisema kwa sasaa atafanya kazi katika ofisi hiyo ambayo amepewa na wabunge hadi hapo muafaka wa ofisi kuu Buguruni utakapopatikana huku akisisitiza kuwa haki haipotei ila inachelewa.

Katibu huyo alisema anaimani na mahakama kuwa ita wapatia haki stahiki hivyo kuwataka wanachama kuendelea kuwa na subira.

Aidha, alisema kupitia mgogoro huo hadi sasa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini inashikilia zaidi ya sh. bilioni 1.2 ambazo ni ruzuku ya chamahicho.

Maalim Seif alisema fedha hizo ni pamoja na zile ambazo ofisi ya msajili ilimpatia Lipumba hivyo waamini mgogoro ukiisha wata pata haki yao.

Kwa upande mwingine Katibu huyo alisema hana mpango wa kukutana naLipumba kuhusu mgogoro unaondelea ndani ya chama hicho kwa kile alichodai kuwa si kiongozi wala mwanachama wa chama hicho.

Alisema CUF haimtambui Lipumba kwa sifa yoyote tofauti na kumfukuza uanachama hivyo yeye hawezi kukukutana na mtu kamahuyo.

Maalim Seif alisema pamoja na kuwa hawamtambui Lipumba kama kiongozi au mwanachama ila akiomba msamaha wapo tayari kumsamehe.

Akizungumza baada ya kuzinduliwa ofisi hizo Mbunge wa Viti Maalum na Kiongozi wa Wabunge wa CUF bungeni, Riziki Ngwali alisema wamelazimika kufungua ofisi nyingine ili wapate mahali pa kukutana wakiwa nje ya Bunge.

Ngwali alisema kupitia ofisi hiyo wataweza kujadiliana mambo mbalimbali yanayo wahusu wabunge na wananchi na kuja na ufumbuzi.

Kwa upande wake Mbunge wa Temeke CUF, Abdallah Mtolea alisema katika ofisi hiyo wanatarajia kuajiri wataalam mbalimbali ambao watasaidia kufanya tafiti na kupitia tarifa mbalimbali za Bunge ili kuwarahisishia katika uchangiaji bungeni.

Alisema katika ofisi hizo wameingia mkataba wa kulipa sh. milioni 18 kwa mwaka ambazo zitatolewa na wabunge wenyewe kwa maslahi ya chama chao.

Maalim Seif akutana na Gwajima


Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameutua mgogoro wa chama che kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima huku kiongozi huyo wa kidini akitangaza kuwa atamlipua Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba Jumapili ijayo.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati alipomtembelea Askofu Gwajima, Maalim Seif alibainisha kwamba amemweleza kiongozi huyo mambo mbalimbali ikiwemo suala la mgogoro ndani ya CUF, aliodai umesababishwa na Lipumba.

Alisema kuwa ameamua kwenda kwa Askofu Gwajima kumweleza hayo kwa sababu ni rafiki yake na hawajaonana siku nyingi lakini pia kiongozi huyo alikuwa haelewi mgogoro wa CUF umesababishwa na nani.

"Nimemweleza Askofu Gwajima mambo mengi hususani mgogoro wa CUF hivyo ataamua mwenyewe nini afanye kutokana na niliyomweleza,"alisema.

Aliongeza kuwa mbali na kwenda kwa Gwajima  pia ameshazungumza na viongozi wengine wa dini husuani ya Kiislamu.

Kwa upande wake, Askofu Gwajima alisema kuwa ameshafahamu chanzo cha mgogoro huo kwa kuwa Maalim ni rafiki yake wa siku nyingi lakini Lipumba hana urafiki naye.



"Mimi huyu ni rafiki yangu kwa hiyo nilitaka kujua Professa Lipumba anafanya nini kuvuruga CUF, hivyo nilitaka kujua Lipumba amepatwa na nini mpaka amevuruga chama chako na kiukweli mimi nilikuwa siufahamu vizuri huu mgogoro ila saizi Seif ameniambia kwa hiyo na mimi nataka nitafakari alichoniambia rafiki yangu ni ‘digest’ baada ya hapo nitajua nafanya nini” alisema Gwajima

Alipoulizwa kama watu watarajie chochote kutokea kuhusu CUF, Maalim Seif na Lipumba kwenye ibada Jumapili ijayo, Gwajima alijibu: “Kumbe mnajua, subirini Jumapili ifike nitamlipua na tutajua amekula maharage ya wapi.”

Lowassa, Maalim wajadili migogoro ya CUF

Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa amekutana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif katika ofisi ya Lowassa iliyopo Mikocheni jijini hapa leo mchana.
Katika mkutano huo Lowassa na Maalim wamejadiliana masuala ya siasa ikiwamo migogoro ya ndani ya CUF na namna ya kuimarisha umoja na mshikamano wa umoja wa vyama vya upinzani.
Maalim Seif, ni Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu wa Zanzibar na Lowassa ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema.

PROFESA LIPUMBA ATINGA MAHAKAMANI

Mgororo wa ruzuku ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) unazidi kupamba moto baada ya mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kwenda kuitetea mahakamani.
 
Profesa Lipumba na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa chama hicho, Thomas Malima wamefungua maombi Mahakama Kuu wakiomba waunganishwe kwenye kesi iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa CUF, walio upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
 
Katika kesi ya msingi ya ruzuku namba 21 ya mwaka 2017, wadai wanaiomba Mahakama imzuie msajili kutoa ruzuku kwa CUF na imuamuru Sh360 milioni alizozitoa kwa kina Profesa Lipumba zirejeshwe kwenye akaunti rasmi ya chama. 

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini Profesa Lipumba na Malima wamewasilisha maombi mahakamani nao waunganishwe kwenye kesi hiyo upande wa wadaiwa.
 
Maombi hayo yalitajwa jana na Malima aliieleza mahakama wakiwa viongozi halali wa chama hicho, wanaomba kujumuishwa kwenye shauri hilo kwa kuwa wana masilahi na shauri hilo.
 
Wakili wa CUF upande wa Katibu Mkuu, Juma Nassoro na Wakili wa Serikali, Hang Chang’a waliieleza mahakama kuwa bado hawajapewa hati za maombi hayo.
 
Jaji Wilfred Dyansobela aliamuru waombaji hao (kina Lipumba) kuwapatia nyaraka hizo na amepanga kusikiliza maombi hayo Juni 6, siku ambayo kesi ya msingi itatajwa.

Maalim Seif: Hakuna CUF ya Maalim wala CUF ya Lipumba

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema chama hicho kitaendelea kufanya mambo kiungwana kwa kuwa Tanzania ni nchi ya amani na kuwa hakuna CUF ya Maalim Seif wala CUF ya Lipumba.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Maalim Seif alisema CUF inatimiza wajibu wa kutunza amani na iwapo kingetaka kuleta machafuko basi kingefanya hivyo tangu zamani.
“CUF ni moja. Ni kweli sisi tumekuwa wapole na waungwana, sisi si tunaambiwa hii nchi ya amani, sisi tunatimiza wajibu wetu wa kutunza amani. Hakuna chama kinachotunza amani kama CUF” alijibu mara baada ya kuulizwa na waandishi wa habari.
“The struggle we continue, mtatia ndani Maalim Seif, mtatia ndani Mtatiro lakini there are so many Maalim Seif’s. Kuna Maalim wengine ni vichaa,” alisema
Wakati huhuo Maalim Seif aionyooshea kidole Rita
Katibu Mkuu wa CUF , Maalim Seif Sharif Hamad amezungumza na waandishi wa habari leo na kusema Wakala wa Usajili wa vizazi na vifo, (RITA) utakuwa umekiuka sheria iwapo utaisajili na kuitambua bodi ya wadhamini iliyoundwa na Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba.
“Sisi tumekuwa wapole sana, tunaona katiba inavunjwa, lakini niseme kwamba, kama Rita wataisajili bodi ya Lipumba, watakuwa wamekiuka sheria yao wenyewe. Bodi ipo na imesajiliwa 1993 na tunacho cheti cha kusajiliwa” alisema
Alisema ni utaratibu kuwa kila kipindi fulani marekebisho hufanywa lakini bodi haifi.
Alisema bodi ya CUF ipo na kama ofisa Mtendaji mkuu wa Rita ataisajili basi ajue anavunja sheria.

MAALIM SEIF: LIPUMBA HANA UWEZO WA KUNIVUA UKATIBU MKUU CUF

Sarakasi za kisiasa zinaendelea kutawala ndani ya chama cha CUF baada ya Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kudai kuwa Profesa Ibrahim Lipumba anatumiwa kukihujumu chama hicho.

Maalim Seif alimtuhumu Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa anakihujumu chama ili kishindwe kudai haki waliyoipata katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka juzi.

Aliyasema hayo jana katika kijiji cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja alipozungumza na wanachama wa chama hicho, ikiwa ni ziara maalumu ya uimarishaji wa chama katika mikoa yote ya Kisiwa cha Unguja.

Maalim Seif alisema pamoja na Profesa Lipumba kupata nguvu kutoka vyombo vya dola na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kukihujumu chama hicho, lakini hawataweza kufikia malengo hayo.

Alisema taasisi hizo kwa pamoja zimekuwa zikimuunga mkono Lipumba kwa kumpa kila nguvu anayohitaji ili kuona anafanikisha malengo ya CCM ya kuitawala nchi bila ya kuwepo kwa chama kikuu pinzani, ila nguvu zao hizo zitagonga mwamba.

“Nashangaa sana kuona Lipumba amekubali kutumika na CCM kwa kukihujumu chama kwa masilahi binafsi, lakini nataka muelewe wananchi kuwa pamoja na nguvu zao zote hizo katu hawataweza kuwakatisha tamaa Wazanzibari ya kudai haki yao waliyoipata katika uchaguzi uliopita,” alisema.

Alishangazwa kuona Ofisi ya Msajili kwa kushirikiana na vyombo vya dola badala ya kufuata Katiba na sheria za nchi, wao wamekuwa wakikihujumu chama hicho.

“Pamoja na hujuma hizi zinazofanywa na Lipumba katika chama chetu, lakini nashangaa Rais (John) Magufuli anatumbua watendaji wabovu, lakini humu mrajisi (Msajili) wa Vyama vya Siasa anamuachia,” alisema.

Kuhusu kuondolewa kwenye nafasi yake, Maalim Seif alisema kwa mujibu wa katiba ya CUF, Lipumba hana uwezo wa kumvua nyadhifa hiyo hata kama angekuwa ni mwenyekiti halali.

Alisema kwa mujibu wa katiba yao ili Katibu avuliwe wadhifa wake lazima mkutano mkuu uhudhuriwe na zaidi ya nusu ya idadi wajumbe.

Alisema kikao kilichofanyika chini ya Profesa Lipumba kilihudhuriwa na wajumbe wasiokuwa na ujumbe kihalali, ambao walipandikizwa kuonesha kama kikao hicho kilikuwa halali.

“Ikiwa mimi nimefukuzwa chama kutokana na madai kuwa sihudhurii vikao vinavyofanywa na ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam, mbona yeye Lipumba tangu mwaka 2015 hawajawahi kuja ofisi kuu ya chama ambayo ni mtendeni hadi leo, kwa hiyo naye alitakiwa kufukuzwa,” alihoji.

Maalim Seif alisema kuwa kinachosikitisha ni kuona Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nayo kuidhinisha kuwa wamekubaliana na mageuzi hayo yaliyofanywa na Lipumba kwa kushirikiana na wajumbe wake.

“Ninachokifahamu mimi ndani ya katiba yetu inasema kuwa ili uamuzi wa kuvuliwa nafasi ya uongozi ni lazima anayedaiwa kufanya kosa aitwe na uongozi kujieleza, lakini mimi sijaitwa kujieleza,” alihoji Maalim Seif.

Akizungumzia madai ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliopita, Maalim Seif alisema waliwataka wananchi wa Zanzibar kutokata tamaa na haki yao, huku akidai hivi karibuni dola ya Zanzibar itakuwa chini ya CUF.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema uongozi wa CUF unasikitika kuona vyombo vya dola vikiingilia mamlaka ya chama hicho na kusahau wajibu wao.

Alisema kuwa wajibu wa vyombo hivyo ni kusimamia amani ya wanachama na viongozi wake, lakini ni jambo la kushangaza kwa viongozi wa vyombo hivyo kuwa ni miongoni mwa wanaongoza kuonesha chuki dhidi ya CUF.

Alisema pamoja na hujuma hizo, lakini viongozi wakuu wa chama hicho chini ya Maalim Seif, hawatosita kudai haki yao hadi kieleweke.

Akijibu tuhuma hizo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara na anayemuunga mkono Profesa Lipumba, Magdalena Sakaya alimtuhumu Maalim Seif kuwa ndiye anakula njama za kukidhoofisha chama.

Alisema Seif amekataza ruzuku zisifike kwenye wilaya, hakuna mikutano na hakuna hata pikipiki huku wenzao Chadema waliokuja juzi wamekuwa chama kikuu cha upinzani kutokana na kuwa wamoja.

“Malalamiko anayotoa ajikite kwenye katiba, aichambue kifungu kwa kifungu atabaini anakosea wapi.

“Hii ni taasisi  ya chama, siyo kampuni ya mtu, lazima tufuate katiba tuliyojiwekea ambayo ipo wazi inatoa maelekezo ya kila kitu, anayekengeuka anafanya makusudi na sisi hatuwezi kukaa kimya bila kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuteua watakaofanya kazi alizotakiwa kufanya yeye,” alisema Sakaya.

Alieleza kuwa badala ya kujenga chama, ameamua kukidhoofisha na anatumiwa kufanya hivyo akijificha kwenye mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Amekuwa bwana kesi, kila kukicha anafungua mpya, mimi nina kesi, Lipumba ana kesi, Msajili wa Vyama ana kesi, mwanasheria ana kesi, akae kimya asubiri ziishe, ”alisema Naibu katibu mkuu huyo.