HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

VIDEO: POLISI WAUA MAJAMBAZI JIJINI MWANZA.

Jeshi la polisi mkoani Mwanza limepambana na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi ambapo katika mapambano hayo, wapo waliouawa.
Tazama video hapo chini

WATU WATATU WANAOTUHUMIWA KUHUSIKA NA MAUAJI YA VIONGOZI WA VIJIJI NA ASKARI MKOANI PWANI WAMEUAWA.

Jeshi la polisi mkoani Pwani limewaua kwa kuwapiga risasi watu watatu wanaodhaniwa kuwa wali husika na mauaji ya viongozi wa vijiji na vitongoji na askari polisi katika wilaya za Mkuranga,Kibiti na Rufiji.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani ONESMO LYANGA amesema katika taarifa yake kuwa watu hao wamefariki dunia wakati wakipelekwa hospitali ya Mission ya Mchukwi kwa matibabu baada ya kujeruhiwa kwa risasi miguuni na kiunoni walipojaribu kukimbilia porini wakiwa kwnye pikipiki baada ya kukaidi amri halali ya polisi iliyowata ka  wasimame kutokana na kuwatilia mashaka.

Amesema polisi waliokuwa katika doria walipata taarifa kutoka kwa wa safiri  kuwa waliona pikipiki tatu zilizokuwa zinatokea Kibiti kupitia barabara kuu ya Dar es salaam -Lindi zinepakia watu watatu kila mmoja na pikipiki mbili kati ya hizo ziliwabeba waliovalia hijabu ndipo walipowapa taarifa askari wa usalam barabararni walioko katika kizuizi cha Mparange ili wawasimamishe na kuwatambua lakini hawakutii.

Amesema askari wa kituo cha Mwembe,Muhoro waliwasinamisha lakini hawakutii amri na kuongeza kasi,ndipo askari waliwafuatilia hadi kuvuka daraja la Mkapa  na wakatoa onyo kwa kufyatua risasi hewani lakini waliendelea kukaidi.

Amesema baadaye watu hao waliamua kuruka kutoka kwenye pikipiki  zao na kukimbilia msituni,kitendo kilichowafanya polisi kuwafyatulua risasi za miguuni na kiunoni na kuwakamata lakini walifariki dunia wakati wakikimbizwa hospitali ya Mission ya Mchukwi ambako daktari alithibitisha watu hao walikuwa wameshafariki.

Kamanda amesema majeruhi hao waliovalia hijabu baadaye walitambukiw kuwa walikuwa wanaune waliotumia pikipiki aina ya BOXER yenye namba za usajili MC 272 BLW.

CHANZO: ITV TANZANIA

Jinsi mauaji ya kutisha ya polisi nane yalivyofanyika

Wakati Taifa likiwa katika simanzi na taharuki baada ya askari wanane kupoteza maisha katika shambulizi lisilo la kawaida dhidi ya Jeshi la Polisi, mashuhuda wa tukio hilo wanasema wauaji walijipanga katika maeneo matatu tofauti katika eneo la tukio kabla ya kufanya shambulizi hilo.
Habari za shambulio hilo la aina yake lililotokea juzi ziliripotiwa na gazeti hili pekee jana na hali ya simanzi ilitawala jana wakati Jeshi la Polisi likitoa taarifa kuhusu tukio hilo, huku Rais John Magufuli akiongoza waombolezaji.
“Baada ya kusikia hili tukio nilikaa kama dakika kumi natafakari bila kupata majibu. Hivi haya matukio yanafanywa na kina nani? Wanafanya kwa malengo gani?” alihoji Othman Juma, aliyekuwa anafuatilia mkutano huo wa Jeshi la Polisi katika ukurasa wa Mwananchi.
Wauaji hao walimshambulia kwa risasi tano dereva wa gari aina ya Toyota Landcruiser (pickup) na wakati askari walipokuwa wanajariku kuruka kujinusuru, watu hao waliwatungua kwa risasi wakati gari likienda kunasa pembeni ya barabara.
Watu hao walilifuata gari hilo liliposimama na kuwavua fulana za kuzuia risasi kisha kuwamalizia tena kwa risasi kabla ya kuchukua silaha saba walizokuta, tatu zikiwa za masafa marefu.
Waandishi wetu waliofika eneo la tukio wamesema hofu imezidi kutanda kwenye vijiji vya Wilaya ya Kibiti, na hasa Kijiji cha Jaribu ambako viongozi wao hawaonekani na wakazi hupotea inapofika nyakati za usiku kuhofia maisha yao.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, aliyeomba jina lake lihifadhiwe, aliiambia Mwananchi kuwa washambuliaji hao walikuwa watatu na walijificha katika maeneo matatu kando ya Barabara ya Dar-Kibiti kuhakikisha hawawezi kulikosa kwa risasi gari hilo la Jeshi la Polisi.
Alisema wakati gari hilo likipita kwa mwendo wa kasi majira ya saa 12 jioni eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa, likiwa limetokea Jaribu Mpakani, kijiji kilichopo takriban kilomita tatu kutoka eneo la tukio, washambuliaji hao walianza kufyatua risasi mfululizo, hasa kumlenga dereva.
“Wauaji hao walifanya mashambulizi hayo wakitokea vichakani kwa kuwa eneo hilo ni pori. Lakini eneo walipouawa askari hao lilikuwa limefyekwa vizuri kwa miti yote na majani kukatwa,” alisema.
Alisema baada ya dereva kushambuliwa, gari lilianza kuyumba na kupoteza mwelekeo na askari waliokuwa ndani walianza kuruka nje ya gari ili kujiokoa au kurudisha mashambulizi na kila waliporuka walikumbana na risasi.
Shuhuda huyo alieleza kuwa baada ya gari kusimama, watu hao walienda kwenye gari hilo lililokuwa limeegemea kwenye ukingo ulio kando ya barabara na kuwamalizia kwa risasi askari hao wanane na mmoja alijeruhiwa mkono wake wa kushoto.
Askari huyo alimudu kuwatoroka wavamizi hao baada ya kutambaa kupanda gema lililokuwa karibu na eneo ambalo gari liligota na kuibukia upande wa pili ambao una mtaro.
“Sielewi. Ni Mungu tu,” alisema askari huyo aliyetambulishwa kwa jina la PC Fredrick ambaye amejeruhiwa mkono wa kushoto.
Lakini dereva wa gari hilo, ambaye pia alijaribu kutoroka eneo hilo, alionekana kirahisi na washambuliaji kwa kuwa alikimbia kunyoosha njia kulingana na mwelekeo wa barabara hiyo na hivyo kushambuliwa kwa risasi nyingine.
Waandishi wetu waliofika eneo la tukio kuanzia jana asubuhi wameeleza kuwa wananchi walisikia milio ya silaha nzito majira ya saa 12:15 jioni, lakini walishindwa kusogelea kutokana na vitendo vya mauaji vinavyoendelea maeneo yao.
Wakazi wa eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa walisema walisikia milio ya silaha nzito tofauti na milio ya bunduki za kawaida na hivyo kuamua kutotoka nje.
Mkazi wa Mkengeni, Rashid Mohamed alisema hofu imezidi kijijini hapo na wanashindwa kufanya biashara zao kama walivyokuwa wakifanya awali, na hivyo maisha yanazidi kuwa magumu.
Mohamed alisema juzi walisikia milio ya bunduki na risasi moja iliangukia kwenye paa la duka lake. Alisema ana hofu kwa sababu biashara yake haiendi vizuri kwa kuwa watu hawaendi kazini kwa kuhofia usalama wao.
“Leo watu wengi hawajaenda kabisa mashambani. Kila mtu ana hofu. Unaweza kwenda halafu ukakutana na hao wauaji. Hali si nzuri kabisa, sijui hatima yangu ni nini,” alisema mfanyabiashara huyo.
Mkazi mwingine wa Kijiji cha Bungu, ambako kuna kambi maalumu ya polisi, Mwajuma Said alisema kwa sasa hawana viongozi kwa kuwa wote wamekimbia baada ya kutishiwa maisha.
Alisema kutokana na kukosa serikali tangu Februari mwaka huu, walianza kupeleka matatizo yao Kituo cha Polisi cha Bungu. Alisema baada ya tukio la juzi hawajui watapeleka wapi shida zao kwa sababu polisi ambao wanawategemea nao wanauawa.
“Walikuja wakatupa vipeperushi kwenye ofisi ambavyo waliandika kwamba wamefika kijiji chetu kwa ajili ya kumuua mwenyekiti, mjumbe na mtendaji wa kijiji. Baada ya vitisho hivyo, viongozi hao walikimbia kijiji hiki, mpaka sasa hatuna serikali,” alisema mwanamke huyo.
Mwalimu mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema wauaji hao wamekuwa wakielekeza mashambulizi yao kwa watumishi wa umma, jambo ambalo linampa hofu.
“Hatujui hatima yetu itakuwaje. Baadhi ya walimu wanaomba uhamisho ili waondoke eneo hili. Polisi tunao wa kutosha lakini yanapotokea mauaji kama haya tunashindwa kujua ni nguvu gani waliyonayo wauaji hao,” alisema mwalimu huyo mkazi wa Kijiji cha Bungu.
Hali ilivyokuwa jana
Mwananchi ilikuta polisi wakiwa eneo la tukio majira ya saa 4:30 asubuhi, wakichukua vipimo, huku baadhi yao wakiwa wameficha sura kwa kuvaa kinyago kinachoruhusu macho pekee kuonekana.
Eneo hilo ni kilomita tatu kutoka kituo cha ulinzi ambako askari hao walibadilishana lindo na kuanza safari ya kurudi kambini Bungu.
Eneo la tukio hilo ni mteremko uliopo Kijiji cha Mkengeni kilichopo kati ya Mkuranga na Rufiji.
Askari mmoja wa kambi maalumu iliyopo Bungu aliiambia Mwananchi kuwa risasi tano zilipigwa mfululizo upande wa dereva kabla gari hilo halijaacha njia na kwenda kuegemea kwenye ukingo wa bonde dogo lililo pembeni ya barabara.
“Sehemu lilipotokea tukio ni kama ina kichaka na askari aliyenusurika alitambaa kwa tumbo kwenye kichaka cha upande wa kulia kama unaelekea Rufiji na kufanikiwa kujinusuru, ingawa alikuwa ameshapigwa risasi ya mkono,” alisema askari huyo.
Alieleza zaidi kuwa baada ya gari kupinduka na askari hao kupigwa risasi, bado walivuliwa vikinga risasi na kupigwa risasi nyingine.
Akizungumza eneo la tukio Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alimwambia Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba kuwa washambuliaji hao walijipanga maeneo matatu na walikuwa wanafahamu wanachofanya.
“Wangemkosa hapa, wangempata pale au pale. Lengo lao ilikuwa kumshambulia dereva,” alisema Ndikilo huku akionyesha kwa mikono aliposimama mshambuliaji mmoja baada ya mwingine.
Wananchi katika kijiji cha Mkengeni walikuwa wamesimama katika makundi na wengine wakiwa kwenye vibanda vya kahawa wakijadiliana kuhusu tukio hilo na wengi hawakutaka kuongea na waandishi wakionekana kuhofia maisha yao.
Baada ya Waziri Mwigulu kuwasili eneo la tukio na kupokea maelezo kutoka kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, msafara huo ulielekea Kijiji cha Bungu kuona kambi hiyo maalumu.
Kambi hiyo imetengenezwa kwa maturubai sita ambayo wanaishi askari hao.
Shambulio hilo ni mwendelezo wa matukio kadhaa dhidi ya askari wa Jeshi la Polisi ambayo yamekuwa yakitokea tangu mwaka juzi. Januari 20, 2015, watu wasiojulikana walivamia Kituo cha Polisi cha Ikwiriri wilayani Rufiji na kuua askari wawili waliokuwepo kituoni hapo na kuondoka na silaha walizokuta.
Uvamizi kama huo ulifanyika Februari 3, 2015 wakati kundi la watu wasiojulikana lilipovamia Kituo cha Polisi cha Mgeta wilayani Kilombero na kuchukua bunduki aina ya SMG iliyokuwa na risasi 30.
Tukio jingine lilitokea Julai mwaka juzi wakati watu wasiojulikana walipovamia Kituo cha Polisi Sitakishari, Ukonga, Dar es Salaam na kuua askari wanne na raia watatu na baadaye kupora silaha ambazo idadi yake haikuwekwa bayana.
Katika shambulizi jingine lililofanyika Agosti mwaka jana, polisi wanne waliuawa wakiwa Benki ya CRDB, Mbagala, Dar es Salaam ambako walikuwa wakibadilishana lindo. Watu wasiojulikana waliowasili eneo hilo kwa pikipiki tatu, waliwafyatulia risasi askari hao na kuwaua baadaye kuondoka na bunduki mbili.
Polisi pia wameuawa katika matukio ambayo walijaribu kupambana na watu hao, likiwamo la Vikindu ambako ofisa wa polisi wa cheo cha ASP, Thomas Njuki alipigwa risasi wakati polisi ilipoenda kukamata watuhumiwa wa ujambazi.
“Tumeshapoteza askari zaidi ya 10. Ninaamini wanatosha. Sasa tunaenda kwenye operesheni maalumu, hatutakuwa na mzaha wala msamaha,” alisema kamishna wa operesheni na mafunzo wa Polisi, Nsato Marijani alipoongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
“Tutawapata popote walipo, tutawashughulikia kikamilifu hakuna atakayebaki. Mapambano haya hayana mwisho, huu ni mwanzo usio na mwisho,”alisema.
Alisema baada ya mauaji hayo ya polisi, operesheni kali ilifanikisha kubaini maficho ya muda ya watu hao.
Kamishna Marijani aliwataja askari waliouwawa katika shambulio hilo kuwa ni Peter Kigugu, ambaye ni mkaguzi msaidizi wa polisi, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zacharia, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub.
Alisema katika msako huo, polisi waliwaua watu wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi na kukamata bunduki nne, mbili zikiwa zile zilizoporwa kwa askari.
Alisema watu hao walifanikiwa kuua askari wengi kwa sababu walikuwa pamoja ndani ya gari, na si kwa sababu wana ujuzi wa kipekee.
Alipoulizwa kuhusu uhusiano wa shambulio hilo na ugaidi, Kamishna Marijani alisema: “Wale ni majambazi, hawana lolote. Si chochote. Hatuwezi kuweka kanda maalum kwa sababu yao. Wameamua kupambana na Jeshi la Polisi kwa sababu tunawazuia. Huu si ugaidi, ni ujambazi.”
Alisema matukio ya uhalifu yametawala mkoani Pwani kutokana na kuwa na mapori yanayowavutia wahalifu na kuweka maficho yao.
Kamishna Marijani aliwataka wananchi kuliunga mkono Jeshi la Polisi katika operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa.
Kamishna pia alipiga marufuku pikipiki kuonekana Kibiti, Mkuranga na Rufiji kuanzia saa 12:00 jioni.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema watu hao waliiba silaha saba, nne zikiwa ni bunduki aina ya SMG na bunduki tatu za masafa marefu.
Alisema bunduki nyingine mbili aina ya SMG zilizokuwa sehemu ya mbele ya gari la polisi zilipatikana kwa kuwa washambuliaji hao hawakuziona.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alitembelea eneo hilo na kusema wanaofanya mauaji hayo watashughulikiwa.
“Hatukubaliani na jambo hilo, halina nafasi. Mkuu wa Mkoa pokeeni pole na fungeni mikanda upya ili tuunganishe nguvu kukabiliana na uhalifu huu,” alisema Mwigulu akiwa katika kambi maalumu ya Bungu muda mfupi baada ya kuwasili eneo la tukio saa 7:00 mchana.
Waziri Mwigulu aliwapa pole polisi na kuwataka kusonga mbele ili kuhakikisha silaha zilizoibwa zinarudishwa.
Akizungumzia zaidi tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ndikilo alisema ni tukio zito kwa mkoa kupoteza askari wanane wakati mmoja. “Ni tukio zito na mtihani mkubwa kwa wananchi, hasa wanapoona askari walioletwa kuwalinda nao wamefariki,” alisema Ndikilo.
Aliwataka wananchi wawe na subira wakati serikali ya mkoa ikiendelea kulifanyia kazi suala hilo.


Chanzo: Mwananchi

MAJAMBAZI YALIYOUA POLISI 8 KWA RISASI NAYO YAMEUAWA

Jeshi la Polisi Tanzania limesema limewaua majambazi wanne ambao walikuwa ni sehemu ya kundi la majambazi lililowashambulia na kuwaua askari 8 wilayani Kibiti mkoani Pwana jana usiku.

Akizungumza na wanahabari leo, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Nsato Marijani amesema kuwa mara baada ya kundi hilo kuwashambulia askari, kikosi kingine cha askari kilifanya msako na kubaini maficho ya majambazi hao.

Amesema baada ya kuwabaini, yalifanyika mashambulizi ya kurushiana risasi, ambapo majambazi wanne waliuawa pamoja na kukamata bunduki 4 zikiwemo SMG mbili zilibainika kuwa kati ya zile zilizoporwa na majambazi hao.

Akielezea tukio hilo lilivyokuwa, Kamishna Marijani amesema kundi la waharifu walikuwa na silaha za moto na ambao idadi yao haikujulikana liliweka mtego na kufanikiwa kuishambulia kwa risasi gari iliyokuwa na askari 9 waliokuwa wakitoka katika malindo kurudi kambini, na kuwaua askari 8 kati yao huku mmoja akijeruhiwa mkononi.

Amewataja askari waliuawa kuwa ni pamoja na Mkaguzi Msaidizi Peter Kiguu, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub, ambapo pia walipora bunduki 7 zikiwemo SMG 4.

Kufuatia tukio hilo, Kamishna Marijani ametangaza vita na waharifu wote katika maeneo hayo, ambapo amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinaanza oparesheni maalum katika mkoa wa Pwani, kuhakikisha vinawasaka na kukomesha mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua.

"Mpaka sasa jeshi limekwisha poteza skari zaidi ya 10, inatosha…. Tunakwenda kwenye oparesheni maalum, hatutakuwa na mzaha, tutawasaka popote walipo na kuwashughulikia kikamilifu, ,,, watajua tofauti ya moto na maji… mpaka jana idadi ilikuwa ni 8 kwa nne, lakini nawahakikishia kuwa ndani ya wiki moja idadi hiyo itakuwa imebadilika, na tutakuwa na hesabu tofati” amesema Marijani

Kuhusu hofu ya ugaidi, Kamishna Marijani amesema tukio hilo siyo la kigaidi bali ni uhalifu wa kawaida, huku akibainisha kuwa Tanzania hakuna ugaidi

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limepiga marufuku uendeshaji wa pikipiki katika maeneo yote ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji zaidi ya saa 12:00 jioni. Amesema usafiri wa boda boda utaruhusiwa kati ya saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.

CHANZO: EATV 

WATU WATATU WANAODHANIWA KUWA NI MAJAMBAZI WAULIWA KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI

Watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi  wameuwa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kukaidi amri ya kutakiwa kusimama eneo la kizuizi cha Mwembe Muhoro wilayani Rufiji, mkoani Pwani.

Watu hao walikuwa wamepakiana kwenye pikipiki moja huku wakiwa wamevaa hijabu.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo, kamanda wa Polisi mkoani Pwani ,Onesmo Lyanga alisema pikipiki nyingine mbili zilifanikiwa kukimbia.

Akielezea juu ya tukio hilo alifafanua,lilitokea Aprili 2 mwaka huu majira ya mchana ,Muhoro ,Rufiji barabara kuu ya Dar es Salaam Lindi.

“Siku ya tukio askari walipata taarifa kuwa kulikuwa na pikipiki tatu zikitokea Kibiti kwenda mikoa ya Kusini zikiwa zimebeba watu watatu kila moja “

“Miongoni mwa pikipiki hizo kati yake mbili wamebebwa watu waliovaa hijabu,” alisema Lyanga.

Alisema askari wa barabarani walipewa taarifa katika kizuizi cha Mparange na kuwasimamisha ili wawahoji lakini walikataa na kupita ambapo waliwajulisha wenzao kwenye kizuizi cha Ikwiriri lakini walikaidi kusimama.

“Baada ya hapo walifika kizuizi cha Ikwiriri lakini bado walikaidi kusimama na kuendelea kukimbia ndipo walipofika kituo cha Muhoro “

“Hata hivyo hawakusimama na askari waliokuwa doria wakiwa kwenye gari waliwafuatilia na wakavuka daraja la Mkapa na waliwapa onyo kwa kupiga risasi hewani,” alisema Lyanga.

Aidha alibainisha baada ya hapo watu hao waliruka kwenye pikipiki na kuanza kukimbilia msituni na ndipo askari walipowapiga risasi za miguu na kiunoni na kufanikiwa kuwakamata.

“Majeruhi hao walijulikana ni wanaume hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika na walikuwa kwenye pikipiki yenye namba za usajili MC 272 BLW aina ya Boxer yenye rangi nyeusi”

“Watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi  kwa mwonekano wao walijaribu kuwawahisha hospitali ya Misheni ya Mchukwi,” alisema Lyanga.

Lyanga alisema walipofikishwa hospitali daktari alithibitisha kuwa watu hao wamefariki dunia .

Hata hivyo majina yao hayakuweza kufahamika huku pikipiki nyingine mbili zilitoroka na kuelekea mkoa wa Lindi na taarifa zimetolewa polisi ili wawakamate.

Aliwataka wananchi kuwa watulivu pale wanaposimamishwa na askari polisi badala ya kujaribu kutoroka na kwa sasa jeshi hilo limeimarisha doria katika kukabiliana na uhalifu.

MAJAMBAZI YAPORA MILIONI 25 KWENYE FOLENI JIJINI DAR

Watu  wanaodaiwa majambazi wamepora kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 25 katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere, eneo la Tazara, Dar es Salaam.

Tukio hilo lilitokea  jana saa 4 asubuhi wakati gari hilo likiwa kwenye foleni ya magari eneo hilo la taa za Tazara. Watu hao wameporwa katika eneo ambalo huwa askari doria wametanda, lakini wakikamata pikipiki zinazotokea eneo la Buguruni.

Aidha taa za Tazara yaliko makutano ya barabara kutokea Buguruni, Temeke, Kariakoo/Posta na Gongo la Mboto ndilo eneo lenye askari wengi wakiwemo wa usalama barabarani.

Wakati tukio likifanyika kulikuwepo askari wenye magwanda maalumu ya askari doria zaidi ya watano wakivurumushana na waendesha pikipiki upande wa Barabara ya Mandela kutokesa Buguruni. Hata hivyo imeelezwa kuwa watu hao waliokuwa wakipeleka benki hawakuwa na ulinzi kama inavyoshauriwa na Jeshi la Polisi.

Majambazi hao waliokuwa watatu, walipora fedha hizo katika gari ndogo aina ya Toyota Rav4 yenye namba za usajili T 455 DFN mali ya kampuni ya kutengeneza mabati ya Sun Share iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aliyejitambulisha kwa jina la Richard Charles.

Kwenye gari pia alikuwepo mfanyakazi mwingine wa kampuni hiyo, mwenye asili ya China, aliyetambulika kwa jina la Cheng Deng.

Kwa mujibu wa dereva wa gari hiyo, Charles, walikuwa wakizipeleka fedha hizo benki eneo la Quality Centre na ndipo walipovamiwa na watu hao wakiwa na pikipiki aina ya boxer wakati magari yakiwa kwenye foleni wakisubiri taa ziwaruhusu kupita kutoka barabara ya Mandela.

Charles alisema majambazi hao walimwamrisha kufungua mlango na kuwapatia begi la fedha lililokuwa limewekwa katika kiti cha nyuma huku wakimtishia kwa bastola kabla ya kuvunja kioo cha nyuma cha gari hilo na kubeba fedha hizo na kutokomea nazo.

“Kwa kweli hata sielewi mpaka sasa hivi kilichotokea. Walikuja watu wawili mmoja upande wangu mwingine wa bosi wangu wakinitishia kwa bastola nifungue mlango niwape begi la fedha. Ghafla mtu mwingine akavunja kioo cha nyuma kwa kutumia kitako cha bastola na kubeba begi la fedha na kutokomea” alisema Richard.

Askari wenye silaha walifika katika eneo la tukio dakika 20 baada ya tukio hilo wakaishia kuhoji. Hata hivyo askari mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake alilaumu tabia ya baadhi ya watu kusafirisha kiasi kikubwa cha fedha pasipo kuomba ulinzi wa polisi jambo linalohatarisha usalama wao na mali zao.

“Kama walijua wanasafirisha kiasi kikubwa hicho cha fedha kwa nini wasingeomba hata ‘escort’ (kusindikizwa kwa ulinzi) ya polisi? Hili ni tatizo, hasa katika kipindi hiki kigumu cha upatikanaji wa fedha, watu wanatakiwa kuchukua tahadhari mapema.” alisema askari huyo.

WATU WANAODAIWA KUWA MAJAMBAZI WAVAMIA DUKA MWANZA, WAMUUA MAMA WA KIHINDI KWA RISASI

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za moto, wamevamia duka moja lililopo Mtaa wa Nkurumah (Katikati ya jiji la Mwanza) na kumuua kwa kumpiga risasi mama mmoja mwenye asili ya Kihindi kisha kupora kiasi cha pesa ambacho hakijajulikana bado.

Duka hilo linauza bidhaa mchanyanyiko Mini Supermarket pia hutoa huduma za miamala ya kifedha kwa njia ya mitandao ya simu za mkononi.

Imeelezwa kuwa wakati majambazi hao wakiwa kwenye harakati hizo, aliingia mama mmoja mwenye asili ya Kihindi kwa ajili ya kununua dawa za kutuliza maumivu, panadol, ndipo majambazi hayo yalipomfyatulia risasi tatu na kusababisha afariki dunia papo hapo kisha yenyewe kutoweka kusipojulikana.

Tukio hili limetokea kwenye duka na matukio ya kuporwa kwa watoa huduma za miamala ya pesa kwa njia ya simu imekuwa sugu kwenye Jiji la Mwanza huku majambazi wakitekeleza uharifu huo kwa hutumia silaha za moto hivyo kuleta hofu na amani kutoweka miongoni mwa wakazi wa Mwanza.

MAJAMBAZI MENGINE YAUAWA KATIKA MAPAMBANO MAKALI MKURANGA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Temeke limeua watu wanne wanaodhaniwa kuwa ni majambazi katika wilaya ya Mkuranga mkoa wa Pwani.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Gilles Muroto alisema tukio hilo ni la Oktoba 21 baada ya polisi kupata taarifa za kuwepo kwa kundi la watu wanaodhaniwa ni majambazi.

Alisema baada ya taarifa, kikosi kazi cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kilifanya ufuatiliaji na kubaini nyumba ambayo haijakamilika imezungushiwa uzio na muda wote mlango wa uzio huo ulikuwa umefungwa.

Aliongeza kuwa uchunguzi wa kina, ulifanyika na kubaini kuwa kweli kundi hilo, lipo ndani ya nyumba hiyo na kwamba muda mwingi mlango wa uzio, hufungwa na kuongeza kuwa majira ya saa tano askari wa kikosi kazi cha mkoa huo na mkoa wa Pwani, kilizingira nyumba hiyo.

“Baada ya kujipanga mlango wa uzio huo uligongwa na kutoa amri ya kuwataka walioko ndani ya nyumba hiyo wafungue mlango na kujisalimisha, lakini tulishangaa baada ya amri hiyo ghafla milio ya risasi ilianza kutoka ndani ya nyumba hiyo,” alisema Muroto.

Aliongeza kuwa baada ya milio hiyo, askari ambao walikuwa makini na wakiwa wamezingira nyumba hiyo wakiwa wamejipanga katika miundo ya mapigano, walianza mashambulizi kujibu mashambulio hayo.

Alisema majibizano yaliendelea na watu hao waliokuwa wanashambulia kutoka ndani, walivunja uzio na watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya watano walitoka huku wakiwa wanashambulia.

Muroto alisema askari waliendelea kupambana nao na kufanikiwa kuwajeruhi baadhi yao, na wengine walifanikiwa kutoroka na silaha zao.

“Mashambulizi kutoka ndani yalitulia na askari waliingia ndani ya uzio, kwa kuwa yalikuwa mapambano ya nguvu walikuta majambazi watatu wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 na 30 wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi na hali zao zilikuwa mbaya na tuliwapeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini walibainika kuwa tayari wameshakufa na miili yao imehifadhiwa hapo ikisubiri kutambuliwa,” alisema.

Alisema baada ya kufanya upekuzi, polisi walikuta silaha moja aina ya short gun pump action yenye MV.51516 R na namba ya usajili TZ car 99987 na risasi tano ndani ya magazini yake.

Risasi nyingine sita za short gun zilikutwa ndani ya mfuko wa plastiki pamoja na risasi nane za pistol.

Aidha alisema katika tukio hili, ilibainika kuwa kuna askari mmoja alijeruhiwa bega lake la kushoto na lilikuwa jeraha kubwa la risasi, hivyo alipelekwa katika Hospitali ya Muhimbili ambako amelazwa na anaendelea kupata matibabu akisubiri kufanyiwa upasuaji.

Muroto alisema ufuatiliaji wa majambazi, walitoroka eneo la mapambano uliendelea kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Mtambani, ambapo majira ya saa tatu asubuhi jambazi mmoja alipatikana akiwa mahututi na juhudi za kumfikisha hospitali zilifanyika. Hata hivyo, alikufa akiwa njiani.

”Tunawashukuru wananchi wote wema kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha kwa Jeshi la Polisi, kwa kuliunga mkono katika kufichua wahalifu na kupambana na wahalifu, nitoe tahadhari kuwa mkoa huu ukifanya tukio ujue utashughulikiwa kabla hujakamilisha na ukifanikiwa kukamilisha azma yako haitachukua muda utakamatwa,” alisisitiza.