HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

TPA WASAINI MKATABA WA UPANUZI WA BANDARI YA DAR ES SALAAM.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Prof: Makame Mbarawa akiongea na wadau wa sekta ya usafirishaji kabla ya zoezi la utiaji saini wa mkataba wa upanuzi na uongezaji wa kina cha Bandari kati ya Serikali na Kampuni ya China Harbour Engineering. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA) Mhandisi Deusdedit Kakoko na kushoto ni Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Bw. Mkinga Mkinga. 
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Prof: Makame Mbarawa (katikati) akishuhudia makabidhiano ya mkataba wa upanuzi na uongezaji wa kina cha Bandari kati ya Serikali na Kampuni ya China Harbour Engineering. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA). Mhandisi Deusdedit Kakoko na kushoto ni Mtedaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. XU XINPEI. 
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini Tanzania (TPA). Mhandisi Deusdedit Kakoko kulia na Mtedaji Mkuu wa Kampuni ya China Harbour Engineering Bw. XU XINPEI wakionyesha mkataba wa makubaliano ya upanuzi na uongezaji wa kina cha Bandari kwa wadau wa sekta ya usafirishaji baada zoezi la utiaji saini wa mkataba huo kukamilika. (Picha na Benjamin Sawe- Maelezo).

Benjamin Sawe, Maelezo
Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), imesaini mkataba wa upanuzi na uongezaji wa kina cha bandari utakaowezesha bandari ya Dar es Salaam kupokea meli kubwa za mizigo na kushindana na bandari nyingine katika pwani ya bahari ya hindi.
Upanuzi huo  utakaofanywa na kampuni ya China Harbor Construction  ya China utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 336 na utadumu kwa miezi 36, ambapo  utahusisha uongezaji wa kina cha lango la bandari na uongezaji wa kina cha maji kati ya gati namba 0, 1 hadi 7.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hatua hiyo inalenga kuifufua upya bandari ya Dar es Salaam ili ifanye kazi kwa ushindani na kuhudumia wateja wengi kuliko ilivyo sasa. 
“ Kukamilika kwa upanuzi na uongezaji wa kina cha maji  katika gati namba 1 hadi 7 kutoka mita 8 hadi 15 kutawezesha meli kubwa na za kisasa zenye uwezo wa kubeba hadi makontena  elfu kumi na tisa kutia nanga katika bandari ya Dar es Salaam na kuongeza ufanisi na kukuza uchumi wa Tanzania”, amesema Prof. Mbarawa.
Aidha Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa pamoja na upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu wezeshi ya reli na barabara ili kuhakikisha mizigo haikai muda mrefu bandarini.
“Ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge toka Dare s Salaam hadi Kanda ya Ziwa na Kigoma na ufufuaji wa reli ya Tazara kutawezesha bandari ya Dar e s Salaam kufanya kazi kwa ufanisi na kuvutia wafanyabiashara wengi hivyo nawataka  wafanyakazi wote wa bandari kufanyakazi kwa bidii na uadilifu”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA Eng. Deusdedit Kakoko amesema kiasi cha dola za Marekani milioni 421, kitapatikana kwaajili ya ujenzi huo ambapo kati ya fedha hizo  Benki ya Dunia itatoa mkopo wa masharti nafuu wa dola milioni 345.
Kukamilika kwa ujenzi huo kutaondoa adha ya baadhi ya meli kusubiri kwa muda mrefu kupata nafasi ya kutia nanga na kutaongeza hadhi ya bandari ya Dar es salaam na kuvutia wasafirishaji wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.

UWANJA WA NDEGE DODOMA KUFANYA KAZI SAA 24

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho (kulia), mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa ajili ya kukagua Taa za Kisasa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), kwa ajili ya kuongozea ndege zilizowekwa uwanjani hapo.
Msimamizi wa mradi Bw. Samwel Mruma kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), akionesha Taa za Kisasa za Umeme Jua (hazipo pichani), kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), zilizofungwa kwa ajili ya kuongozea ndege katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa Msimamizi wa mradi Bw. Samwel Mruma kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), wakati alipokagua mfumo wa Kisasa wa Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), zilizofungwa katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho na kulia ni Meneja wa Uwanja huo Julius Mlungwana.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akionesha kifaa (Remote Controller) cha kuwashia Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), zilizofungwa katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa waandishi wa habari, wakati akikagua Taa hizo uwanjani hapo.
Muonekano wa Mfumo wa Kisasa wa Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), zilizofungwa katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma. Taa hizo zitatumika kuongozea ndege nyakati za Usiku na zina uwezo wa kuwaka masaa laki moja.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho (katikati), na Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Leonard Chimagu (kushoto), wakati alipokagua mfumo wa kisasa wa Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma.

Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi wa kufunga Taa za kuongozea ndege ili kuruhusu Uwanja wa Ndege wa Dodoma kuweza kutumika masaa 24. 

Akizungumza hayo mjini Dodoma mara baada ya kukagua Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light) zilizofungwa uwanjani hapo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa uboreshaji wa uwanja huo katika kuruhusu ndege za aina zote kutua masaa 24 kwa wiki. 

“Hii ni hatua ya pili ya uboreshaji wa uwanja huu ambapo hatua ya kwanza tumeimaliza ya upanuzi wa barabara za kuruka na kutua ndege (runway) hadi kufikia KM 2.5”, amesema Waziri Profesa Mbarawa. 

Aidha, ameongeza kuwa ufungaji wa taa hizo umegawanywa kwa hatua tatu ambapo awamu ya kwanza imekamilika kwa kujumuisha ufungaji wa Mfumo wa Kisasa wa Taa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), katika barabara za kuruka na kutua ndege na maeneo ya maegesho, hatua ya pili ni kufunga taa za kumsaidia Rubani kuweza kuona uwanja wote na hatua ya mwisho ni taa zitakazofungwa mita 400 kila upande uwanjani hapo. 

Amefafanua kuwa Taa hizo za kisasa (Aviation Solar Powered Light) zitapunguza gharama za uendeshaji uwanjani hapo ikiwemo matengenezo yake kwani zinadumu muda mrefu. 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara, Sekta ya Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho, amesema kuwa nia ya Serikali ni kuendelea kurefusha uwanja huo ambapo italipa fidia kwa nyumba zilizopo pembeni ya uwanja huo ili kuongeza usalama wa uwanja na ndege kwa ujumla. 

“Tutaweka uzio katika uwanja huu kulingana na matakwa ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege na pia kupitia uzio huu taa zitakuwa salama”, amesisitiza Dkt. Chamuriho. 

Naye, Msimamizi wa mradi Bw. Samwel Mruma kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), amesema mfumo wa taa hizo za kisasa za Umeme Jua (Aviation Solar Powered Light), zimefungwa kwa siku 14 na zina uwezo wa kufanya kazi kwa miaka 12 na kuwaka kwa masaa laki moja ukilinganisha na nyingine ambazo zinawaka kwa masaa elfu kumi. 

Mfumo wa uwekaji Taa za Kisasa ni mkakati wa Serikali katika kuhakikisha inaendelea kuboresha viwanja vyake vya ndege ili kukidhi viwango vianavyostahili katika usafiri wa anga.

BAJETI YA WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO YAPITISHWA

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati), akimsikiliza Katibu Mkuu (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga (Kulia), mara baada ya kumaliza kuwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2017/2018. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Eng. Deusdedit Kakoko.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akipongezana na Watendaji wa Wizara hiyo mara baada ya kumaliza kuwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2017/2018.
 Watendaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wakipongezana mara baada ya Bunge la Bajeti kupitisha Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2017/2018.
Mtendaji Mkuu Wa Shirika la Reli Nchini (TRL), akizungumza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju mara baada ya Bunge la Bajeti kupitisha Bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa Fedha 2017/2018.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

WAZIRI PROFESA MBARAWA AKAGUA KITUO CHA UTAFUTAJI NA UOKOAJI –MAGOGONI

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyekaa) akitoa maelekezo kwa wafanyakazi wa Kituo cha Utafutaji na Uokoaji, alipokitembelea kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na kituo hicho kilichopo eneo la Magogoni Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua Mfumo maalumu wa kompyuta unaotumika kuangalia uzito wa Meli zinazoingia nchini wakati alipokagua huduma hizo katika Kituo cha Utafutaji na Uokoaji, kilichopo katika eneo la Magogoni Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua takwimu mbalimbali za huduma zitolewazo na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika Kituo cha Utafutaji na Uokoaji kilichopo eneo la Magogoni Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Katikati) akikagua daftari linaloonyesha kumbukumbu za Meli zinazoingia nchini wakati alipokagua huduma hizo katika Kituo cha Utafutaji na Uokoaji kilichopo eneo la Magogoni Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Katikati) akikagua daftari linaloonyesha kumbukumbu za Meli zinazoingia nchini wakati alipokagua huduma hizo katika Kituo cha Utafutaji na Uokoaji kilichopo eneo la Magogoni Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akijaribu kutumia mfumo wa simu kuita Meli inayongia katika bandari ya Dar es Salaam, wakati alipokagua huduma zinazotolewa katika Kituo cha Utafutaji na Uokoaji kilichopo katika eneo la Magogoni Jijini Dar es salaam.

Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano-UUM 

PROF. MBARAWA: NEEMA YAJA WAFANYABIASHARA KANDA YA ZIWA

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati), akielekea kukagua Bandari ya Kemondo mkoani Kagera ili kujionea utendaji kazi wake.  Kulia ni Meneja wa Bandari Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo.
 Meneja wa Bandari Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo, akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Wa pili kushoto), njia ya reli katika bandari ya Kemondo mkoani Kagera, ambayo itaruhusu mizigo itakayokuja kwenye mabehewa kwa njia ya meli iweze kupakuliwa na kupelekwa kuhifadhiwa kwenye maghala.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akikagua sehemu ya maegesho ya meli katika Bandari ya Kemondo, mkoani Kagera. Bandari hiyo ina upana wa mita 100.
 Muonekano wa gati ya meli katika Bandari ya Kemondo, mkoani Kagera.
 Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani Kagera Eng. Zephrine Bahyona, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa nne kulia), alipokuwa akikagua Kivuko cha Kyanyabasa kinachotoa huduma katika mto Kyanyabasa, mkoani Kagera.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani Kagera Eng. Zephrine Bahyona, alipotembelea na kukagua kivuko cha Kyanyabasa kinachotoa huduma katika mto Kyanyabasa, mkoani Kagera.
Muonekeano wa kivuko cha Kyanyabasa kinachotoa huduma katika mto Kyanyabasa, mkoani Kagera. Kivuko hicho kina uwezo wa kubeba watu sitini au magari mawili madogo kwa wakati mmoja.

Imeelezwa kuwa kukamilika kwa ukarabati wa meli ya MV Umoja kutarudisha huduma ya usafirishaji wa mizigo katika kanda ya ziwa kupitia bandari ya Kemondo  iliyopo mkoani Kagera.
Kauli  hiyo imetolewa na  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati akikagua Bandari hiyo kuangalia maendeleo yake, na kuitaka Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA), Shirika la Reli Nchini (TRL), na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL),  kuanza kuandaa Mfumo mmoja wa kutoa Stakabadhi ili kuwarahisishia wateja wake huduma za usafirishaji wa mizigo.
Aidha, Waziri Mbarawa ameitaka TRL kukarabati njia za reli bandarini hapo haraka iwezekanavyo ili kuruhusu mizigo itakayokuja ikiwa kwenye mabehewa kwa njia ya meli iweze kupakuliwa pindi Meli hiyo itaposhusha.
"Serikali imefanya ukarabati wa meli ya MV Umoja ambayo itabeba mizigo ikiwa kwenye mabehewa na reli hii inahitaji ukarabati mapema ipasavyo nawaagiza TRL kufanya ukarabati wa reli ili kusiwepo usumbufu wowote wakati wa kushusha na kupakia mizigo hiyo" , amesema Profesa Mbarawa.
Ameiagiza Mamlaka hiyo kuanza kutafuta tena wateja ambao kwa muda mrefu walikuwa wamepotea kutokana na  bandari hiyo kusuasua kutoa huduma zake kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Meneja wa TPA Kanda ya Ziwa Bw. Abel Moyo, amemuahidi Waziri huyo  kutekeleza agizo lake kwa kushirikiana na TRL pamoja na MSCL na kuwahakikishia wafanyabiashara wa kanda ya ziwa  kuwa na matumaini mpya ya kupata usafiri bora na wa uhakika.
Katika hatua nyengine, Waziri Mbarawa ametembelea na kukagua Kivuko cha Kyanyabasa kinachotoa huduma katika mto Kyanyabasa na kumtaka Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoani humo, Eng. Zephrine Bahyona,  kutoa huduma bora sambamba na kukusanya mapato ili kuweza kutatua changamoto ndogondogo zinazowakabili.
Naye, Kaimu Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) mkoani humo Eng. Zephrine Bahyona, amezitaja baadhi ya changamoto zinazoathiri utendaji mzuri wa kivuko hicho kuwa ni kukatika kwa magugu maji na hivyo kupelekea kusombwa kwa kivuko.
Waziri Profesa Mbarawa pia amekagua barabara ya Uyovu- Bwanga yenye urefu wa kilometa 45 mkoani Geita na kuridhishwa na kasi ya Mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo ambapo ujenzi wake kwa sasa umefika asilimia 56.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WIzara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

SERIKALI YAONYA WAVAMIZI WA MIUNDOMBINU

 Mhandisi Mshauri wa Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TECU), Eng. Mushubira Kamuhabwa (kulia), akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 kwa kiwango cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiruka mtaro wa maji uliopo pembezoni mwa barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera.
 Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera. Barabara hiyo inajengwa na mkadarasi kutoka Kampuni ya CHICO na imegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 64.96.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mhandisi Jumanne Werema (wa kwanza kulia), kuhusu kukamilisha ujenzi kwa wakati wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo eneo la Mafumbo, wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera.
 Mhandisi Jumanne Werema kutoka Kampuni ya ujenzi wa CMG akimpa taarifa ya mradi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo eneo la Mafumbo, wakati alipokagua, wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati), akiongozana na Mhandisi Salum Chanzi (kushoto), kutoka Wakala wa Majengo nchini (TBA), pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawiro (kulia), kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya  Sekondari ya Wavulana ya Ihungo mkoani Kagera iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi takriban miezi sita iliyopita
Moja ya Jengo la Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Ihungo linalojengwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA), baada ya Shule hiyo kuathiriwa na tetemeko la ardhi takriban miezi sita iliyopita, mkoani Kagera.

Serikali imesema haitavumilia wala kusita kumchukulia hatua yeyote anayevamia na kujenga katika hifadhi za miundombinu ya barabara na reli kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Karagwe, mkoani Kagera mara baada ya kukagua barabara ya Kyaka hadi Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi kuacha dhana ya kuingilia miundombinu hiyo kwa imani ya kulipwa fidia na Serikali.
"Najua bado kuna watu wanaendelea kuvamia miundombinu ya usafirishaji, sasa nasema kuwa Serikali itaendelea kubomoa pasipo kulipa fidia kwa yeyote anayevunja sheria", amesema Profesa Mbarawa.
Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Waziri Profesa Mbarawa amekipongeza Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa (TECU), kinachosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kwa kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa kuzingatia viwango na  kuwataka kuendelea kuimarisha kitengo hicho ili kiweze kufikia hatua ya kujenga barabara nchini.
Aidha, amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuwahamasisha wananchi wake kuilinda na kuitunza barabara hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kama ilivyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo Eng. Mushubira Kamuhabwa, amesema kuwa kazi inaendelea vizuri kwani mpaka sasa mradi huo umefika asilimia 98 ambapo kazi iliyobaki ni uwekaji wa alama za barabarani.
Eng. Kamuhabwa ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria kutokana na barabara hiyo kuwa kiungo kati ya Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyaka hadi Bugene umejengwa na kampuni ya CHICO kutoka nchini China na kugharimu kiasi cha shilingi  bilioni 64.96.
Katika hatua nyengine Waziri Mbarawa ametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa shule ya  Sekondari ya wavulana ya Ihungo mkoani Kagera iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi takriban miezi sita iliyopita.
Akiwa katika shule hiyo Profesa Mbarawa ameridhishwa na kasi ya mkandarasi anayejenga shule hiyo na kusema nia ya Serikali ni kuijenga shule hiyo kwa ubora wa hali ya juu ili kukabiliana na majanga mbalimbali.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawiro pamoja na mambo mengine ameishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wake na kuijenga shule hiyo kwa ubora wa hali ya juu.
Ni takribani miezi sita tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani Kagera na kuharibu miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, madaraja, hospitali, shule pamoja na makazi ya watu.
Kutokana na uharibifu huo Serikali pamoja na wadau mbalimbali ilianza juhudi za  ukarabati na ujenzi wa miundombinu hiyo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano


WADAU WA BARABARA WATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA KUDHIBITI AJALI NCHINI

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wadau waliohudhuria mkutano wa siku mbili wa Usalama barabarani katika ukumbi wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB) Bw. Joseph Haule akitoa taarifa ya udhibiti wa ajali za barabarani kwenye mkutano wa wadau wa usalama barabarani uliofanyika jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akiongea na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano wa Namibia Mhe. Sankwasa James Sankwasa wakati wa mkutano wa siku mbili wa kutathmini usalama barabarani, Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa Chama cha Kimataifa kinachoshughulika na masuala ya barabara  Dkt. Kiran Kapila wakati wa mkutano wa siku mbili wa kutathmini usalama barabarani, Jijini Dar es salaam.
 Mmoja wa wanafunzi aliyeshinda tuzo ya uchoraji wa picha ya usalama barabarani Veronica Shirima akitoa maelezo kwa wadau wa usalama barabarani, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Wanne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Usalama barabarani mara baada ya kufungua mkutano huo, Jijini Dar es salaam.
Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wadau wa usafirishaji kuweka mikakati dhabiti ya kupunguza ajali za barabarani nchini ili kuokoa maisha ya watanzania wanaofariki dunia kila mwaka kutokana na ajali hizo.
Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo alipofungua mkutano maalumu wa kanda wa kujadili na kutathmini changamoto za usalama barabarani na jinsi ya kuzikabili unaofanyika jijini Dar es salaam.
Profesa Mbarawa amesema kuwa ajali za barabarani zimekuwa zikikatisha maisha ya watanzania wengi kila mwaka ambao wengi wao ni vijana na nguvu kazi ya taifa hivyo ni jukumu la wadau kubadilisha hali ya usalama barabarani.
“Kama tukijifunza vizuri na kuyafanyia kazi mafunzo haya tunaweza kubadili hali ya usalama barabarani kwani inaumiza kuona vifo vya watu wengi vinavyotokana na ajali za barabarani hivyo ni wakati wa Jeshi la Polisi, na  Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu na Majini SUMATRA kushirikiana kukomesha ajali hizi”. Amesisitiza Profesa Mbarawa.
Ameongeza kuwa Serikali itatoa kipaumbele kwa yale yatakayojadiliwa na kuamuliwa katika mkutano huo ili kuongeza kasi ya udhibiti wa ajali za barabarani hapa nchini na kupunguza idadi ya ajali zinazoepukika.
Naye Mwenyekiti wa Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule amesema kuwa Bodi hiyo inashirikiana na taasisi nyingine katika kuhakikisha ubora wa miundombinu ya barabara inakuwa salama na kupitika wakati wote.
Kwa upande wake Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani hapa nchini Mohamed Mpinga amesema kikosi cha usalama barabarani kitaendelea kuhakikisha kuwa ajali za barabara zinadhibitiwa.
“Suala la ajali za barabarani ni jukumu letu sote kwa pamoja hivyo tukiungana kwa pamoja na kushirikiana tutaweza kupunguza ajali hizi kwa kiwango kikubwa”.  Amesema Kamanda Mpinga.
Mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo jijini Dar es salaam umewakutanisha wadaau mbalimbali wa kimataifa wa masuala ya ujenzi na usimamizi wa usalama wa watu na mali wawapo barabarani .
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

WAZIRI MBARAWA AWATAKA TEMESA KUONGEZA UJUZI UTENGENEZAJI WA VIVUKO.

 Meneja Mradi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport inayojenga Kiuvko cha MV. Kazi, Bw. Major Songoro,   akitoa ufafanuzi wa mashine kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alipokagua Kivuko hicho jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia), akiangalia moja ya vifaa vilivyoko kwenye chumba cha kuendeshea kivuko katika kivuko cha MV. Kazi kinachojengwa jijini Dar es Salaam. Kivuko hicho kitakabidhiwa tarehe 15 Mwezi huu. Wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), Dkt. Musa Mgwatu.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia),  akifafanua jambo kwa Uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko kipya cha MV Kazi ambacho kinatengenezwa jijini Dar es salaam na Kampuni ya Songoro Marine Transport.
 Mafundi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport, wakiendelea na kazi ya kufunga mashine katika Kivuko cha MV Kazi. Kivuko hicho kitakamilika na kukabidhiwa wiki ijayo na kina uwezo wakubeba abiria 800 na magari 22 kwa wakati mmoja.
Kivuko cha MV. Kazi kikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake.Kiuvko hicho kitakamilika na kuanza tarehe 15 mwezi huu na kina uwezo wakubeba abiria 800 na magari 22 kwa wakati mmoja.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano