HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Aibua Ubadhirifu wa Kutisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)

UBADHIRIFU wa kutisha unaohusisha mabilioni ya fedha, umefichuliwa kwenye Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ukihusisha uongozi, wafanyakazi, watoa huduma na wazabuni. 

Wanaodaiwa kuhusika na utafunaji wa mabilioni hayo, walitumia mabadiliko mapya ya usajili wa vitambulisho, yaliyoigharimu serikali kupitia manunuzi yasiyo na tija huku wadanganyifu wakitumia mianya iliyopo kujinufaisha wenyewe kinyume na taratibu. 

Kutokana na hali hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad, aliagiza wale vote waliohusika na ubadhirifu na udanganyifu wa mabilioni ya fedha, wachukulie hatua kali. 

"Ukaguzi umejiridhisha kwamba, uongozi, wafanyakazi, watoa huduma na wazabuni wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika ubadhirifu na udanganyifu kwenye matumizi ya fedha katika mradi wa kuboresha vitambulisho vya taifa," alisema.
 
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)    imeonesha ubadhirifu katika eneo la usajili na utambuzi ambako Sh bilioni 1.2 zililipwa kwa huduma za bima kupitia dalali wa Bima M/s Aste Insurance Brokers Company Limited. Kiasi hicho kililipwa zaidi ya gharama halisi isivyostahili.

Huduma hizi zilipaswa kugharimu Sh milioni 450.2, lakini mamlaka ililipa Sh bilioni 1.7. CAG alibaini kuwa dalali huyo wa bima, alitumia akaunti za biashara katika kupokelea fedha za malipo ya bima ya Sh bilioni 1.7 badala ya akaunti ya amana isivyostahili.

Kwa hali hiyo, CAG amependekeza kampuni ya uwakala wa bima irejeshe Sh bilioni 1.2 zilizolipwa zaidi isivyostahili; na hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya Astery Ndege na kampuni hii kwa kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kutoka mamlaka. 

Ubadhirifu mwingine alioutaja ulikuwa ni manunuzi ya bima ya vifaa vya usajili na magari yaliyotumika katika mradi wa vitambulisho vya Taifa ya jumla ya Sh milioni 494, yaliyofanyika bila kukihusisha Kitengo cha Manunuzi.

CAG pia ameshauri hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya watumishi waliohusika katika udanganyifu, uliobainishwa na kutozingatia sheria za manunuzi ya umma na kuisababishia Mamlaka gharama zisizo na tija sanjari na kuhakikisha kuwa wahusika wanafidia hasara iliyopatikana, kisha kuhakikisha udhibiti wa vifaa. 

Uhakiki wa leja za mafuta, pia ulibaini kuwa lita 1,110 za mafuta ya dizeli yenye thamani Sh milioni 2.2 zilitumika kwa shughuli zisizo za Mamlaka.

Pia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilikopa Sh milioni 455.3 kutoka NIDA kwa ununuzi wa magari manne mwaka 2014, ambazo hadi ukaguzi unafanyika Oktoba 2016 fedha hizo hazikuwa zimerejeshwa. 

Uhakiki wa fomu zenye ‘Barcode’ zilizotengenezwa kupitia mpiga chapa binafsi M/s MFI Solution, ulibaini kuwa fomu 7,762,907 zenye thamani ya Sh bilioni 2.5 zilizopokelewa na mamlaka hazikutumika.

Kadhalika, ilibainika kuwa fomu 8,220,000 zenye thamani ya Sh milioni 519.6 zilizochapishwa tangu mwaka 2011/2012 hadi 2013/2014 hazikutumika; hivyo kutelekezwa katika stoo za TANITA. 

“Hali hii ilitokana na mamlaka kutokuwa na Mpangokazi, hivyo kuingia hasara ya Sh milioni 932.8,” ilisema ripoti hiyo.

Matengenezo ya magari 
Aidha, kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 mpaka 2015/2016, Mamlaka ilifanya matengenezo ya magari kupitia gereji binafsi yaliyogharimu Sh bilioni 1.3. 

Nida pia ilifanya matengenezo yaliyogharimu Sh bilioni 1.1 yaliyofanyika na kulipwa na Mamlaka bila kufanyika ukaguzi unaothibitisha kuwapo kwa ubovu wa gari na mahitaji ya matengenezo husika.

Pia kulikuwa na matengenezo yaliyogharimu Sh milioni 197.2, yaliyofanyika na kulipiwa na Mamlaka bila kufanyika ukaguzi wa awali wala ukaguzi baada ya matengenezo.

 Ripoti imeeleza kuwa ukaguzi ulibaini malipo ya Sh milioni 42.7 yalifanyika zaidi ya madai stahili kutokana na udanganyifu wa kuongeza tarakimu katika hati za madai na kutumiwa kwa hati moja ya madai zaidi ya mara moja katika malipo ya kuanzia mwaka 2012/2013 hadi 2015/2016.

Ajira za muda na za kudumu 
NIDA imegundulika kuwa ilikiuka sheria katika ajira za muda na za kudumu, zilizofanywa na mamlaka kuanzia mwaka 2012 hadi 2015, ambapo vibarua 1,071 walipatikana kwa kupigiwa simu bila kutangaza mahali popote kinyume na Sera ya mamlaka hiyo. Ukaguzi ulibaini kuwa NIDA iliomba kupatiwa vibarua kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Chuo cha Utumishi wa Umma wapatao 415.

Lakini baada ya kupatiwa vibarua hao, mamlaka haikuwatumia na kubainisha kwamba wangetumiwa siku za baadaye. Ripoti ilifafanua kuwa mamlaka iliamua kuajiri vibarua wengine wapatao 882 bila kutangaza mahali popote, tofauti na watumishi 415 ambao walikwishapatiwa. Pia Septemba 2015 Mamlaka iliajiri watumishi 213 licha ya kibali cha kuajiri kutoka Utumishi kuisha tarehe Aprili 2015.

NIDA pia inatuhumiwa kufanya malipo Sh milioni 16.6 ya kiinua mgongo kwa vibarua, kinyume na mkataba wa ajira ya muda na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004. 

Ubadhirifu mwingine uligundulika kwenye matumizi ya mafuta ya dizeli na petroli, yaliyonunuliwa na mamlaka yenye thamani ya Sh bilioni 2.3, yaliyotolewa kwenye magari na majenereta, ambapo hayakuthibitika matumizi yake kutokana na sababu mbalimbali.

CAG pia amebaini upotevu wa vifaa vyenye Thamani ya Sh milioni 93.7 katika stoo ya mamlaka. Ukaguzi umebaini kuwa hakukuwa na taarifa rasmi kutoka kwa mtunza stoo juu ya upotevu huo, licha ya kufahamu kuhusu upotevu wa vifaa hivyo. Vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 991.4 havikutumika tangu kununuliwa kwake katika vipindi tofauti kuanzia Machi 2013 hadi Oktoba 2016.

Udanganyifu mwingine ulifanyika katika ushindanishi wa wazabuni katika ununuzi wa vifaa vya TEHAMA. Nida ilifanya manunuzi ya Ipad zenye thamani Sh milioni 63.4 zilizonunuliwa kutoka kwa M/s Elite computers baada ya kuonekana kukidhi vigezo vya ushindani na kupewa zabuni saba (7) tofauti. Lakini taarifa za wazabuni ambao waliainishwa kuwa washindani katika zabuni hii, M/s Prudent Enterprise na M/s Morex General Enterprise zilighushiwa; na wazabuni hawa hawakuhusishwa wala kutoa nukuu za bei.

Upangishaji nyumba Mamlaka ilitoa zabuni ya kuipangisha Ofisi ya Mamlaka kwa Mary Mwema kupitia barua ya maombi ya tarehe 06.05.2012 ambapo tangazo la zabuni husika ni la tarehe 25.05.2012 baada ya tarehe ya kuomba.

 “Zabuni husika haikupitia Kitengo cha Manunuzi na haikuwa imeidhinishwa na Bodi ya Zabuni,” inasema ripoti hiyo. 

Pia ripoti ilifafanua kuwa mzabuni wa upangishaji wa jengo la ofisi ya John Masenga haukujumuishwa kwenye mchakato wa tathmini ya kitaalamu licha ya kukidhi vigezo.

NIDA kuanza kutoa namba za utambulisho Desemba

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesema kuanzia Desemba mwaka huu mpaka Januari 2017 itaanza kutoa namba maalum za utambuzi kwa wananchi.

Mkakati huo umetangazwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Nchemba alipokutana na uongozi na wafanyakazi wa NIDA, kwa lengo la kujadili mikakati mbalimbali ya kuboresha utendaji wa mamlaka hiyo.

Alisema tayari serikali imekamilisha kanzidata ya wananchi walizozipata kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC na kwamba, tayari taasisi zaidi ya 35 zimeanza kutumia taarifa za NIDA katika kufanya utambuzi wa wafanyakazi wao sawia na kupunguza usumbufu kwa wananchi kuhusu taarifa zinazowahusu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa NIDA Bw. Andrew Massawe alisema kwa zoezi la awali lililofanyika nchi nzima tayari wamefanya uhakiki wa kuwatambua watumishi wa serikali takribani laki tano na elfu sitini na tano.

KIKAO CHA MHESHIMIWA MWIGULU NCHEMBA NA WAKUU WA IDARA NA TAASISI ZA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.



 Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, akizungumza na wakuu wa Taasisi na Idara za wizara (hawapo pichani), wakati wa kikao cha  kujadili masuala mbalimbali ya mipango na maendeleo ya wizara. Kulia ni Naibu Waziri  Mhandisi Hamad Masauni. Kikao hicho kimefanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa wizara, jijini Dar es Salaam. (Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi)
 Wakuu wa Taasisi na Idara za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Idara ya Wakimbizi pamoja na wakuu wa vitengo wizarani hapo wakimsikiliza Waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba, wakati kikao cha kujadili masuala mbalimbali ya mipango na maendeleo ya wizara. Kikao hicho kimefanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa wizara, jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Ernest Mangu, akizungumza wakati  wa kikao cha  kujadili masuala mbalimbali ya mipango na maendeleo ya  Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Idara zake. Kikao hicho kiliongozwa na Waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba (hayupo pichani). Kushoto ni Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Minja. Kikao hicho kimefanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa wizara, jijini Dar es Salaam

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI-WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI.

KITANZI KINGINE WATUMISHI WA UMMA, SASA KUKAGULIWA VYETI KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


MWAROBAINI wa uwepo wa watumishi hewa katika sekta ya umma umepatikana ambapo kuanzia Oktoba 3, mwaka huu, utambuzi wa watumishi wote wa umma kwa kutumia mfumo mmoja wa kukusanya na kuhifadhi taarifa, utaanza huku watumishi wote wa umma, wakitakiwa kupeleka nyaraka muhimu ndani ya wiki mbili.
Utambuzi huo, utafanywa na serikali kwa kushirikisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huku uhakiki na utambuzi huo ukiwalenga watumishi wote wa umma walio kwenye wizara, idara za serikali zinazojitegemea na tawala za mikoa.
Wengine ni mamlaka za serikali za mitaa, wakala za serikali, taasisi na mashirika ya umma, ambapo watumishi wote wa umma wametakiwa kupeleka taarifa zote muhimu zinazowatambulisha katika mamlaka zilizotajwa.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu usajili wa vitambulisho vya taifa kwa watumishi wa umma.
Akifafanua lengo la utambuzi huo, Kairuki alisema lengo ni kuwa na mfumo mmoja wa taarifa sahihi za watumishi wa umma, ili kuondoa uwepo wa watumishi hewa, unaoigharimu serikali mabilioni ya fedha, ambazo zingetumika kufanya kazi nyingine za maendeleo.
“Tulikaa na NEC na NIDA, na tukaona tunaweza kuboresha mfumo wetu wa taarifa na tukaona tuchukue ile kanzi data ya NEC na tumeiingiza kwenye mfumo wa NIDA na kuangalia taarifa za watumishi wetu wa umma, na sasa tuna alama zao za vidole, tunahakikisha tuna taarifa zao sahihi hadi anuani yake,” alisema Kairuki.
Alisema kupitia mfumo huo wa utambuzi, watumishi wote wa umma wanaopaswa kupeleka taarifa zote muhimu kama vile hati ya malipo ya mshahara, cheti cha kuzaliwa, vyeti vya kitaaluma, kitambulisho cha kazi, kitambulisho cha Mzanzibari mkaazi, hati ya kusafiria na kadi ya mpiga kura.
Kufuatia uhakiki huo, Kairuki alizitaka ofisi zote na taasisi za serikali zilizobainishwa kuwasiliana na NIDA ili kupanga mpango kazi wa kufanya shughuli hiyo na kuandaa ratiba itakayowawezesha watumishi wa umma kufanya usajili bila kuathiri utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, ofisi na taasisi hizo zimetakiwa kuandaa mazingira wezeshi ya kufanikisha kazi hiyo kwa kuandaa ofisi mahususi zitakazotumika kuendesha kazi hiyo na kuteua Ofisa Mwandamizi atakayeshirikiana na maofisa kutoka NIDA, na Ofisi ya Rais Utumishi katika kutekeleza hayo.
Pia taasisi na ofisi hizo zimetakiwa kuainisha magari na madereva kwa ajili ya kufanya kazi hiyo kwenye mamlaka ya serikali za mitaa na kwamba kwa ofisi ambazo makao makuu yake yako mkoani Dar es Salaam, watumishi wake watasajiliwa katika ofisi hizo.
Waziri Kairuki alisema kwa watumishi ambao wako katika ofisi za matawi mikoani watafanya usajili katika vituo vya usajili kwenye halmashauri zilizopo ofisi husika.
Akizungumzia hatua zitakazochukuliwa kwa watumishi watakaokaidi agizo hilo ndani ya muda uliopangwa, Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma , Dk Lauren Ndumbaro alisema hilo ni kosa na adhabu zake zimeainishwa kwenye kanuni za utumishi wa umma.
“Kwa wale watakaokaidi kutekeleza agizo hilo ndani ya muda uliowekwa, wanafahamu kwamba ni kosa kisheria na wanaweza kujifukuzisha kazi wenyewe,” alisema Dk Ndumbaro.
Hata hivyo alisema kabla ya hatua hizo hazijachukuliwa nafasi ya utetezi itatolewa kwa watumishi walioshindwa kutekeleza ndani ya muda uliopangwa, ili kubaini wenye sababu za msingi na kwa wale wasio na sababu za msingi, sheria itachukua mkondo wake.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mifumo ya Tehama wa NIDA, Muhammed Hamis, alisema baada ya usajili huo kufanywa kwa watumishi wa umma watapewa vitambulisho vyenye saini, tofauti na vile vya awali ambavyo havikuwa na saini.
“Lakini tumeanza kusajili Septemba 14, mwaka huu kwa wale ambao hawakuwa na vitambulisho vya taifa, ila waliokuwa navyo ila havina saini watapewa baada ya wale ambao hawakuwa navyo kabisa kupata,” alisema Hamis.
Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alisema serikali itachukua hatua kwa watumishi hewa waliobainika katika Mamlaka ya Usimazi wa Bandari (TPA), ambao wameambiwa na mwajiri kuacha kazi wenyewe. “Nimesikia taarifa hiyo, ila sisi serikali hatuwezi kuliacha, ni lazima hatua zichukuliwe,” alisema Waziri Kairuki.

ALIYEKUWA MKURUGENZI MKUU (NIDA) AKOSA DHAMANA ARUDISHWA RUMANDE

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imetoa masharti ya dhamana kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Dickson Maimu na wenzake watano, wanaokabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 1.2.
Jaji Eliezer Feleshi, alitoa masharti hayo juzi baada ya kukubali hoja za maombi yaliyowasilishwa na washtakiwa hao. Hata hivyo baada ya kutolewa kwa masharti hayo, washtakiwa walirudishwa rumande baada ya kushindwa kuyatimiza.
Mbali na Maimu, washtakiwa wengine waliopewa masharti ya dhamana ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Joseph Makani, aliyekuwa Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, na aliyekuwa Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond.
Wengine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Bima ya Aste Insurance Brokers Company, Astery Mwita Ndege, aliyeingia mkataba na Nida wa kutoa huduma za bima na Xavery Silverius Kayombo, ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Gotham Internatianal Limited.
Akitoa masharti hayo, Jaji Feleshi alisema, Maimu alitakiwa kutoa dhamana ya Sh milioni 315.9, mshtakiwa wa pili Sh milioni 105.8, wa tatu Sh milioni 6.9, wa nne na watano kila mmoja Sh milioni 22.05.
Aidha, kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, wanaotakiwa kusaini hati ya dhamana ya nusu ya fedha zilizotajwa na Mahakama.
Aliongeza kuwa, washtakiwa hawaruhusiwi kusafiri nje ya Dar es Salaam bila kibali cha Mahakama pia wawasilishe hati za kusafiria kwenye ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kila mmoja anatakiwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa muda na tarehe kesi itakapopangwa.
Awali washtakiwa hao, waliwasilisha maombi hayo na Mahakama iliyatupilia mbali, hata hivyo waliwasilisha tena maombi hayo. Washtakiwa hao wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao wakati wakitekeleza majukumu yao, kutumia nyaraka za uongo na kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh bilioni 1.2.

VITAMBULISHO VYA TAIFA KUTUMIKA UCHAGUZI UJAO

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


VITAMBULISHO vya Taifa huenda vikatumika katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Rose Mdami wakati akitoa maelezo kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni mjini hapa katika hafla ya kumkabidhi kiongozi huyo wa Bunge kitambulisho chake cha taifa.
Mdami alisema tayari mamlaka hiyo imechukua taarifa za wapigakura kutoka kwenye kanzidata ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuzichakata na kuna uwezekano mkubwa vitambulisho vya taifa vikatumika katika uchaguzi ujao na kuirahisishia kazi tume hiyo kufanikisha uchaguzi huo wa Rais, Wabunge na Madiwani.
"Vitambulisho tunavyovitoa sasa vina saini ya mtu husika, hivyo vitatumika benki. Tumewashirikisha pia NEC ambao wametupa 'database' (kanzidata) yao, tumezichakata na tunaendelea na taratibu ili ikiwezekana Vitambulisho vya Taifa vitumike katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 badala ya vile vya tume," alisema Mdami.

Akishukuru, Ndugai aliipongeza mamlaka hiyo kwa kuwa na mipango mizuri, lakini akaishauri serikali kuweka sharti kuzilazimisha benki kutoruhusu mtu kufungua akaunti bila kuwa na kitambulisho cha taifa.
Spika pia alihoji sababu za Nida kuwa na vitambulisho vyenye rangi tatu tofauti na kujibiwa na Mdami kuwa kitambulisho cha kwanza ni cha raia mzawa, cha pili cha raia wa kigeni anayeishi nchi na cha mwisho kwa ajili ya wakimbizi.
"Kwa sasa si rahisi mkimbizi kujichanganya mitaani huko na kupatiwa kitambulisho cha taifa. Tunashirikiana na Tamisemi kuhakikisha hakuna udanganyifu tena. Mtu anayejaza fomu ya kupatiwa kitambulisho anatakiwa kupitia vipengele 72 ambavyo si rahisi kuvighushi kama si mzawa," alisema Mdami.

CHANZO: HABARI LEO

NIDA KUANZA KUGAWA VITAMBULISHO VYA TAIFA VYENYE SAINI KWA WANANCHI KUANZIA JUMATANO SEPTEMBA 14, 2016

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) itaanza kutoa Vitambulisho vipya vya Taifa vyenye saini kwa wananchi wote waliokamilisha taratibu za usajili na utambuzi na kuchukuliwa alama za kibaiolojia (Alama za vidole, Picha, Saini ya Kielektroniki).

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA Bw. Andrew Massawe; utekelezaji wa zoezi hilo utaanza rasmi Jumanne tarehe 14 Septemba 2016 katika ofisi zote za NIDA zikiwemo ofisi za Wilaya zilizoanza usajili Tanzania Zanzibar na mikoa ya Dar-es-salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, na Ruvuma) pamoja na waheshimiwa Wabunge Dodoma.

Waombaji wote ambao Vitambulisho vyao viko tayari watatumiwa ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) katika simu zao za kiganjani (mkononi) kufahamishwa kufika katika vituo vya Usajili kuchukua Vitambulisho vyao.

Kuhusu wananchi ambao tayari wana Vitambulisho visivyo na saini; Bw. Massawe amesema…. “ Mamlaka inakusudia kubadilisha vitambulisho vyote vya zamani visivyo na saini, ila kwa sasa vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika sambamba na vipya wakati taratibu za kuendelea kuvibadilisha zikiendelea” alisisitiza.
Amesema kutokana na uwepo wa njia nyingi na salama za kusoma taarifa za mwombaji zilizomo ndani ya kifaa maalumu kilichofichwa kwenye kadi ya mtumiaji (chip); ndiyo maana vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika katika huduma mbalimbali zinazohitaji kumtambua mtumiaji kabla ya kupata huduma.

Akizungumzia wananchi ambao hawakuwahi kusajiliwa, Bw. Massawe amesisitiza kwamba wananchi wote ambao hawakuwahi kusajiliwa na wana umri wa miaka 18 na kuendelea; kwa mikoa ambayo tayari kuna ofisi za usajili, kuendelea kujitokeza kwa wingi kusajiliwa ili kupata Vitambulisho vya Taifa kwani zoezi la usajili ni endelevu.
“Kwa wale wananchi ambao walisajiliwa kupitia Daftari la Mpiga kura NEC; NIDA iko mbioni kuanza kutoa nambari za utambulisho wakati tukiendelea kukamilisha taratibu za usajili ili kupata utambulisho kamili na kuanza kunufaika na matumizi mapana ya Utambulisho wa Taifa wakati taratibu za uzalishaji wa Vitambulisho zikiendelea”.


Wananchi wanakumbushwa kutunza vizuri Vitambulisho vyao ili kuepuka gharama kwani kitambulisho cha Taifa kwa mara ya kwanza kitatolewa bure na iwapo kitapotea, ili kupata kingine lazima mtumiaji akilipie.

Kwa sasa vitambulisho vya Taifa vimeanza kutumika katika baadhi ya huduma nchini hususani kwenye mabenki kwa ajili ya kufungua akaunti na kuthibitisha taarifa za mtu kabla ya kupatiwa huduma.  Taratibu za kupanua wigo wa matumizi ya Vitambulisho kielektroniki kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali zinaendelea.

WATANZANIA MILIONI 23 KUPATA NAMBA YA UTAMBULISHO WA VITAMBULISHO VYA URAIA IFIKAPO DESEMBA 31, 2016.

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imeeleza kuwa ifikapo Desemba 31 mwaka huu jumla ya watanzania milioni 23 watakuwa na namba za utambulisho wa vitambulisho vya Uraia.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Bi. Rose Mdami amesema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo Rais, Dkt. John Pombe Magufuli la kuitaka Mamlaka hiyo kuweka saini ya mwombaji na mtoaji wa vitambulisho hivyo.

“Tumeanza kutekeleza agizo la Mhe. Rais tangu mwezi Juni mwaka huu, hii inamaanisha kwamba vitambulisho vyote tulivyochapisha kuanzia mwezi Juni mpaka leo vina saini ya muombaji, saini ya mtoaji na tarehe ya kuzaliwa muombaji” amefafanua Mdami.

Ameeleza kuwa kazi ya ugawaji wa vitambulisho hivyo inasubiri kuzinduliwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli atakayekabidhiwa  kitambulisho cha uraia namba moja na baadaye vitambulisho hivyo kugawiwa kwa wananchi  wengine.

Mdami amesema ifikapo Desemba 31 mwaka huu NIDA itakuwa imetoa namba za utambulisho wa vitambulisho hivyo  kwa watanzania milioni 23 kwa kutumia taarifa za Tume ya Uchaguzi (NEC) zilizo katika vitambulisho vya kupigia kura na kuziamishia katika kanzi data ya NIDA.