HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

Nape Amvaa Tena Makonda kuhusu Sakata la Kuvamia Kituo cha Clouds

Miezi michache ikiwa imepita tangu kutokea tukio la uvamizi wa kituo cha Clouds Media Group na kuundwa kwa kamati ya kuchunguza tukio hilo, hatimaye aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye  amemvaa  tena  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusema kwamba hakuunda kamati ya kumchunguza yeye, bali aliunda kamati ya kuchunguza tukio la kuvamiwa kwa kituo cha utangazaji cha Clouds Media Group.

“Niliunda kamati kuchunguza tukio la kuvamiwa kituo cha utangazaji sio kumchunguza RC. Kama RC alikuwa mmoja wa wavamizi, hayuko juu ya sheria,” ameandika Nape kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Alipoulizwa kwanini Waziri wa Habari aunde kamati ya uchunguzi wa tukio la uvamizi badala ya kamati hiyo kuundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Nape alijibu kwa kuuliza swali kama kila kamati inaundwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Majibu haya ya Nape yamekuja ikiwa ni saa chache baada ya kuulizwa ni yapi maoni yake kuhusu kauli ya Makonda kwamba hakuwa akifahamu mipaka yake ya kazi ndio sababu alikwenda kuunda tume ya kumchunguza.

Kauli ya Nape kuhusu kuunda kamati imekuja ikiwa ni takribani saa 24 tangu Makonda aliposema kuwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliunda kamati ya kumchunguza.

Makonda alisema hayo jana, ambapo alidai kuwa kamati iliyoundwa na Waziri isingeweza kumhoji kwa sababu haikuwa na uwezo huo kutokana na wajumbe wa kamati hiyo kutofahamu mambo yanayohusiana na masuala ya uvamizi.

Mawaziri Waliotemwa Wageuka MWIBA Kwa Serikali

Mawaziri  wa zamani, Nape Nnauye na Charles Kitwanga, wamegeuka kuwa mwiba kwa kutoa hoja za kukosoa utendaji wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli.

Mwenendo wa makada hao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuikosoa Serikali, umeanza kuibuka siku za hivi karibuni baada ya wote kwa nyakati tofauti kuenguliwa katika nafasi zao za uwaziri.

Kwa hatua yao ya sasa, wanasiasa hao wanadhihirisha ukweli kwamba wabunge wengi hushindwa kueleza matatizo ya majimbo yao pindi wanapopewa nyadhifa serikalini na wanapotenguliwa wanadai wanapata nafasi zaidi za kuwatumikia wapigakura wao.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa wanadai kuwa makada hao walikosa ujasiri wa kuikosoa Serikali walipokuwa wanashikilia nyadhifa zao kutokana na kubanwa na hoja ya uwajibikaji wa pamoja.

Nape Nnauye
Nape ambaye alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kabla uteuzi wake kutenguliwa Machi, mwaka huu baada ya kupokea ripoti ya tukio la kuvamiwa kwa Kituo cha Televisheni cha Clouds, amesikika mara kadhaa nje na ndani ya Bunge akiikosoa Serikali.

Akiwa jimboni kwake Mtama alikoenda kuzungumza na wapigakura wake baada ya kutenguliwa, alisema kama matukio ya kuteka watu yataachwa yaendelee, basi CCM itakuwa na kazi ngumu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Nape alitoa kauli hiyo wakati huo kukiwa na tukio la kutekwa kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ibrahim Mussa maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki.

Wakati akichangia hotuba ya makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji wiki iliyopita, Nape alisema kuwa kama CCM isipotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 kwa kutowapatia maji wananchi, inaweza kuondoka madarakani.

Kauli nyingine ya Nape aliitoa wiki hii alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, aliposema kuwa wananchi wa mikoa ya Kusini hawatakubali kuona ujenzi wa kiwanda cha mbolea Lindi unakwama kutokana na kile alichodai vita iliyopo kati ya mataifa makubwa.

Aliitaka Serikali isikubali kuona vita hiyo inaendelea kuwaumiza wananchi hao na kuongeza kuwa kama itashindwa kusimamia, wao hawatakubali.

Pia kupitia kurasa zake za mtandao wa kijamii wa twitter, Nape, amekuwa akiandika baadhi ya kauli zenye mwelekeo wa kuikosoa Serikali

Charles Kitwanga
Kitwanga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alianza kuikosoa Serikali baada ya kutenguliwa mwaka jana, kutokana na ununuzi wa ndege mbili mpya aina ya Bombardier kutoka Canada ili kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Alisema ndege hizo, si tu hazina mwendo, lakini pia ilikuwa ni ajabu kununuliwa kwa fedha taslimu wakati duniani kote ndege hununuliwa kwa kulipa kidogo kidogo wakati mteja akiendelea kuzitumia.

Kitwanga aliibuka tena wiki iliyopita wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji Gerson Lwenge kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, akisema atawahamasisha wapigakura wake wakazime mtambo ulioko katika chanzo cha maji cha Iherere.

Alisema jimboni kwake hakuna maji ya uhakika na tangu mwaka 2008 wananchi wamekuwa wakiyasubiri bila mafanikio.

“Kwa hiyo, nitakachokifanya safari hii, sitatoa shilingi kwenye bajeti, bali nitakwenda kuwahamasisha wananchi wa Misungwi wapatao 10,000, twende tukazime mtambo katika kile chanzo cha maji ili wote tukose.

 “Mshukuru nilipokuwa waziri nilikuwa siwezi kusema kitu, sasa nimetoka, tutapambana kwa sababu lazima tuwe na mipango mizuri ya kuwapelekea wananchi wetu maji kama inavyofanyika katika umeme kupitia REA (Wakala wa Umeme Vijijini),” alisema.

Kauli hiyo iliibua hasira za Waziri Lwenge wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, ambaye aliita kuwa ni sawa na uasi.

Kutokana na kauli hiyo, alimtaka ahame chama kama haoni jitihada za kupeleka maji jimboni kwake zinazofanywa na Serikali.

“Kitwanga anaposema atakwenda kuhamasisha wananchi wakabomoe mtambo wa Iherere maana yake analeta uasi au hathamini kazi iliyofanywa na chama chake?

“Kama ni hivyo, sasa ajitoe kwenye chama kwa sababu Serikali imepeleka fedha na kwa maendeleo yaliyofanyika, ni lazima tuwahamasishe wananchi kutunza miundombinu iliyopo badala ya kwenda kuibomoa.’ alisema.

Khamis Kagasheki
Mbali na kina Kitwanga, baadhi ya waliokuwa mawaziri katika Serikali ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete nao pia wamegeuka kuwa wakosoaji wa Serikali.

Mmojawapo ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, anayeikosoa Serikali kupitia akaunti yake ya twitter.

Kagasheki aliyeangushwa katika ubunge wa Bukoba Mjini na mpinzani wake wa siku nyingi, Wilfred Lwakatare (Chadema), aliwahi kusema kuwa kama nguvu ya Ukawa ingemchagua mgombea makini, basi CCM ingekuwa na kazi ngumu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Kada huyo wa CCM aliyejiuzulu nafasi yake kutokana na sakata la Operesheni Tokomeza, aliwahi kuandika katika ukurasa wake wa twitter: “Kuikosoa Serikali yoyote ile ni jambo la kawaida. Ni vema kuchagua maneno na kulenga hoja bila matusi.”

Philip Mulugo
Naye Philip Mulugo aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakati wa utawala wa Kikwete, pia amekuwa akiikosoa Serikali ya Magufuli.

Mulugo ambaye kwa sasa ni mbunge wa Songwe, amesikika bungeni wiki iliyopita akiikosoa Serikali alipochangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.

Akichangia bajeti hiyo, Mulugo aliishangaa Serikali kuruhusu vitabu vyenye makosa vitumike shuleni wakati kuna uwezekano wa kuviondoa.

Katika maelezo yake, Mulugo alivitaja vitabu vya jiografia vya kidato cha tatu na kiingereza kidato cha nne, kuwa vina makosa yanayoweza kuharibu misingi ya wanafunzi.

“Haiwezekani mbili mara mbili mtu aseme ni sita wakati sisi tunajua ni nne. Kwa hiyo, hili suala la vitabu mliangalie vizuri kwa sababu haliko vizuri,” alisema Mulugo.

Pamoja na hayo, Mulugo alizungumzia michango inayotozwa na Serikali katika shule binafsi na kusema ni mingi na kwamba inatakiwa kupunguzwa kwa kuwa inawakatisha tamaa wamiliki wa shule hizo.

NAPE NNAUYE AFUNGUKA KUHUSU UKIMYA WA KINANA, MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE PAMOJA POLISI KUTUMIA NGUVU KUBWA

Na Regina Mkonde 
Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye amefunguka kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo, ukimya wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, muenendo wa shughuli za Bunge pamoja na tukio lililotokea hivi karibuni la Askari Polisi mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufyatua risasi hewani mbele ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima baada ya kutokea majibizano yaliyosababishwa na dereva wa Malima kuegesha gari vibaya.

Nape amefunguka hayo jana  jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wanahabari ambapo alisema, Kinana ambaye baadhi ya watu wanadai kuwa ukimya wake umetokana na kujiuzulu, yuko katika wadhifa wake wa ukatibu mkuu na anaendelea kufanya kazi za chama.

“Mimi sio msemaji wa chama, lakini Katibu Mkuu yupo na anafanya kazi yake kama kawaida…., mimi bado ni mwanachama na muumini mzuri wa CCM inayopenda haki, na nina amini hiki ndicho chama pekee bora kitakachoweza kuwakomboa watanzania pamoja na kuamiwa ikiwa kitatekeleza mkataba wake na wananchi ambao ni wa kutimiza ahadi zake ilizo ziahidi,” alisema.

Kuhusu tukio la Askari Polisi kufyatua risasi hewani, ambalo Kamishna wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda Simon Sirro alisema ulikuwa uamuzi wa busara wa kuondoa taharuki katika tukio hilo, na mbinu ya kuwatia nguvuni watuhumiwa.

Nape alishauri vyombo vya dola kutotumia nguvu kwani kitendo hicho kitajenga hofu na chuki baina ya serikali na wananchi na hata kwa chama tawala CCM, huku akiisihi serikali kuondoa vitendo vinavyotia hofu wananchi.

“Ni vizuri vyombo vya dola vikatimiza majukumu yake kwa kuwa ni vyombo vya wananchi, si vizuri vikitumia nguvu kubwa pale isipostahili. Ifikie hatua raia asiye na silaha Polisi wasitumie nguvu kushughulika naye kwa kutumia silaha. Nimeona ile video ikionyesha Malima alikuwa anauliza chanzo cha tatizo,” alisema na kuongeza.

“Kuna nchi tamaduni zake ni kutumia mabavu na nyingine zinatumia demokrasia, nchi yetu utamaduni wake si wa kutumia nguvu, tumezoea kuelewana kwa mazungumzo. Vyombo vya dola visitumie nguvu kwa kuwa tunajenga usugu usio na maana. Na kama kuna mazingira hatarishi basi nguvu itumike.”

Kuhusu mienendo ya shughuli za Wabunge Bungeni, aliwataka wabunge kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuwawakilisha na kusimamia vema masilahi ya wananchi wanaowawakilisha, pamoja na kuisimamia serikali kutekeleza vizuri majukumu yake.

“Bunge ni mkutano wa wananchi, na wabunge wapo kwa niaba ya wananchi katika kupitisha na kushauri mipango ya serikali. Ni vizuri wasimame katika maeneo yao, wasiwe wapiga makofi, pale serikali inapofanya vizuri ipongezwe na inapofanya vibaya ikosolewe,” alisema.

Kuhusu Uhuru wa Vyombo vya Habari, alisema ifikie hatua wananasiasa wawe na ngozi ngumu ya kuvumilia kukosolewa  na watu kupitia vyombo vya habari. Pia ameshauri wananchi wanaotaka maonesho ya vikao vya bunge moja kwa moja, kuuomba mhimili huo kubadilisha sheria zake ambazo zimeipa mamlaka ya kuamua namna ya kuendesha shughuli zake.

“Naamini uamuzi wa siku ile wa kuzuia shughuli za bunge live ulikuwa sahihi sababu sheria zinasema Bunge litaendeshwa kwa sheria zake. Wananchi wanaozungumzia Bunge live, waliombe libadilishe sheria zake ili lianze kuonyeshwa live,” alisema

Nape, Kitwanga wageuziwa kibao

Wabunge wawili waliokuwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tano, Nape Nnauye (Mtama) na Charles Kitwanga (Misungwi) jana waligeuziwa kibao, wakidaiwa kukiuka maadili ya uongozi baada ya kuzungumza kwa hisia dhidi ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Nape alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kabla ya kuachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, wakati uteuzi wa Kitwanga ulitenguliwa baada ya kuingia bungeni akiwa amelewa.
Wawili hao juzi walizungumza kwa hisia kuhusu kiwango kidogo cha fedha kilichowekwa wakisema hakiwezi kutatua tatizo la maji katika maeneo yao; Kitwanga akisema yuko tayari kuhamasisha wananchi wake 10,000 kwenda kufunga bomba la maji linalopita eneo lake.
Nape , ambaye pia alionekana kuwa na hisia kali, alisema sera ya Tanzania ya viwanda haitawezekana kama suala la maji halitapewa kipaumbele na kutengewa fedha za kutosha.
Jana, mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku, maarufu kwa jina la Msukuma, alisema wakati akichangia hoja ya bajeti hiyo kuwa kauli za wawili hao zinaonyesha kuwa kuna haja ya kazi ya uhakiki kufanyika pia kwa mawaziri.
“Kazi zilizoahidiwa katika Ilani ni nyingi si moja. Hizi hela ni nyingi tuunge mkono na wala tusiwasumbue kwa kuzikataa. Tuwape nafasi ili wakafanye kazi,” alisema Msukuma.
“Lakini suala langu, nataka kuwazungumzia wana-CCM wenzangu ambao jana nilisikiliza mchango wa mmoja, Kitwanga analalamika anasema atawamobilize (atawashawishi) wananchi 10,000 wakazime mashine ya maji Iherere.
“Nataka niwaulize nyinyi mawaziri wa Magufuli hivi vile viapo mnavyokula mnajua maana yake? Kama hamvijui basi sina hakika kama mko sawasawa na kama hamko sawasawa, (Waziri wa Elimu, Joyce) Ndalichako hebu pitisha operesheni ya vyeti feki, huenda hapa penyewe kuna feki za kutosha.”
Alihoji sababu za mtu aliyekuwa waziri kusimama bungeni na kusema kuwa alivyokuwa waziri alibanwa kuzungumza.
“Kwahiyo sisi mambo (ambayo) hatuzungumzi kwa kuwasaidia nyinyi tumebanwa na nani? Mnasimama mnasema sasa nazungumza na nakwenda kuwahamsisha wananchi 10,000 wakazime mtambo?” alihoji.
“Hebu ngoja niwakumbushe tukio la mwaka 2014. Wakati Mheshimiwa Kitwanga akiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, alikuja Geita . Mimi kama mwenyekiti wa CCM wa mkoa nikawaambia wananchi wasitoke mpaka walipwe na mzungu, yeye akaja akamwambia mkuu wa mkoa hata kama kuna mwenyekiti wapigwe mabomu na kweli kesho yake tulipigwa mabomu.
“Kwa hiyo nataka nimwambie Waziri wa Mambo ya Ndani siku akienda kuunganisha wananchi palepale Misungwi naye apigwe mabomu aonje joto ya jiwe. Haiwezekani waziri uliyekula kiapo, ukitimuliwa unakuja humu kutuchanganya, wakati hatujui mambo mliyokuwa mnazungumza kwenye cabinet (baraza la mawaziri).”
Baadaye alimgeukia Nape.
“Nape ambaye alikuwa mwenezi wangu wa (CCM) Taifa, jana (juzi) alizungumza mambo mazuri lakini kuna moja alisema ‘tusipowatekelezea suala la maji wananchi hawataturudisha tena madarakani’.”
Alisema hilo haliwezekani kwa sababu wananchi wanawategemea kwa mambo mengi na si maji pekee yake na wamewafanyia vizuri.
Alisema ilani hazijaanza kuandikwa katika Serikali ya Awamu ya Tano na suala si kumaliza ahadi zote.
Awali alimpongeza Rais John Magufuli na wizara hiyo kwa kazi aliyoiita kuwa nzuri, akisema ameona mabadiliko makubwa. “Mimi niko tofauti kidogo na wabunge wenzangu wanaosema tusipitishe bajeti kwa sababu hela ni ndogo. Binafsi naona hizi hela ni nyingi sana, tatizo ni zitoke zote tofauti na bajeti ya mwaka jana.”

Nape Nnauye: Watanzania hawawezi kutuelewa, na Tusipokuwa Makini Haataturudisha 2020

Mbunge wa Mtama, Mh Nape Nnauye amefunguka na kusema hatua mbalimbali zilizochukulia na serikali ikiwepo kubana matumizi, kufukuza wafanyakazi hewa, kuongezeka kwa mapato kama hazita tafsiriliwa kwa maboresho ya huduma za jamii ni sawa na kazi bure.

Nape Nnauye alisema hayo jana wakati akichangia katika bajeti ya Wizara ya Maji na kusema serikali inapaswa kufanya mambo kwa kuwafurahisha wananchi kwa kuwapa huduma bora na si vinginevyo.

"Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani ilianzakuchukua hatua kadhaa za kuongeza mapato ya serikali, ikiwa ni pamoja na kubana mianya ya wakwepa kodi lakini kupunguza matumizi ikiwemo kupunguza safari, kupunguza sherehe na matumizi ambayo kiukweli kwa namna nyingine yalionekana si ya lazima, ikiwemo kushughulika na wafanyakazi hewa. 

"Lakini pia kwa takwimu tunaambiwa uchumi unakuwa kwa asilimia 7.2 haya yote hayatakuwa na maana kama hayata tafsiriliwa kwenye maboresho ya huduma za jamii na hasa maji. 

"Hatua hizi lengo lake lilikuwa kuongeza uwezo wa serikali sasa kama hatua hizi zimechukuliwa na matokeo yake ni chanya tunapaswa tuyaone kwenye ongezeko la huduma za jamii, tusipofanya hivi hatua tulizochukua zitakuwa hazina maana hata kidogo, bajeti iliyopita tulitenga bilioni mia tisa bajeti hii tukiwa tumesimamimia hatua tulizochukua ambazo kiukweli zingeongeza uwezo wa Serikali tunatoka mia tisa na kwenda mia sita, kwa vyovyote vile Watanzania hawawezi kutuelewa" alisema Nape Nnauye

Nape Nnauye aliendelea kusisitiza kuwa wananchi hawawezi kuielewa serikali kama hatua inazochukua haziendi kubadilisha maisha yao ya kila siku, lakini Mbunge huyo alisema tatizo la maji lipo katika kila jimbo nchi hii sema kinachotokea wanapishana ukubwa wa tatizo.

"Ilani hii ya Chama Cha Mapinduzi ndiyo mkataba wetu kati ya CCM na wananchi tusipoitekeleza wananchi hawatoturudisha na huu ndiyo ukweli kwa sababu tuliwaahidi Mh Naibu Spika na bahati mbaya tatizo la maji pamoja na kuwaathiri watu wote lakini wakina mama ambao ndiyo wapiga kura wakubwa wa CCM ndiyo waathirika wakubwa wa tatizo hili ndiyo maana sina mashaka kwamba serikali itasikiliza na kwenda kuongeza pesa" alisema Nape Nnauye 

Nape Atema Cheche Kwa Wapiga Kura Wake

Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Mtwara kupitia tiketi ya CCM, Mhe. Nape Nnauye amtaka Rais Magufuli aunde tume huru ambayo itaweza kuchunguza matukio ya uhalifu ya uvamizi wa studio unaoendelea nchini.

Hatua hiyo inatokana na matukio ya kiuhalifu yanayoendelea Tanzania na kuacha maswali mengi vichwani mwa wananchi kushindwa kufahamu kuwa watu hao na vikundi hivyo vya kihuni vinavyofanya vitendo hivyo vinapata wapi mamlaka hayo kuwa na nguvu kushinda Dola.

“Ombi langu kwa Rais namuomba aunde tume huru ichunguze matendo haya yasijirudie tena kwa sababu yasipochukuliwa hatua yataharibu sura ya Tanzania pia yataweza kuibuka makundi ya wahuni kuanza kuteka watu nao kwa kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa. Tumsaidie Rais Magufuli kwa kumwambia ukweli naimani atasikia na atafanyia kazi kwa kuwa Rais wetu anapenda kusikiliza watu”. Alisema Nape

Aidha Mbunge huyo amesema watu wanaofanya mambo hayo wanalengo la kuwagombanisha wananchi na Rais wao jambo ambalo sio zuri kwa taifa.

 "Juzi amepotea msanii Roma Mkatoliki na wengine lakini mpaka sasa haifahamiki wapo wapi, yaani kama vile amepotea Nzi, tulisikia kijana mmoja wa CHADEMA anaitwa Ben Sanane amepotea saizi miezi mitano imepita, matendo haya ya kina Ben Sanane, Roma Mkatoliki, na wengine yanajenga chuki ya wananchi kwa Rais, lakini pia yanajenga chuki kwa wananchi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ". Alisema Nape Nnauye

Vile vile Nape amesema yeye mpaka sasa haamini yule mtu aliyemtolea silaha siku ya mkutano wake na wanahabari kama alitumwa ila shida aliyokuwa nayo ni kutaka kujua vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya nini mpaka matukio yote yanatokea.

Haya ni Maneno ya Nape
1.usema kuwa nilifanyakazi kubwa CCM haimaanishi kuwa wengine hawakufanya. Wote tunajua tulivyokipigania chama

2..Nilipopewa Uwaziri kwa miezi 15, sina mashaka, nilifanya kazi kwa umakini mkubwa kwa kutumia uwezo wangu wote

3.Kama ambavyo siku ya kuteuliwa hatukujadiliana, miezi 15 ilipopita aliyeniteua aliamua kufanya mabadiliko ya baraza.

4.Kama ikibainika kuwa alivamia kituo cha Clouds, alafu nisipochukua hatua, sitakuwa na sababu ya kuendelea kuwa waziri.

5.Nilipogundua ni kweli alivamia Clouds, niliamua kuchukua hatua na kusimamia maneno yangu nisionekane mpumbavu ni mimi.

6.potishiwa kwa bastola, nilimwambia yule mtu taratibu, unaharibu sababu tukio lile lilikuwa likirushwa mubashara.

7. yule aliyenitisha walisema si Polisi, mara hajulikani.Lakini mtu mwingine akinyanyua bastola hapa, Polisi hawatakuacha.

8..RPC alikuwa pale, kama hakuwa Polisi kwanini wasimkamate? Na mtu yule si kweli kwamba hajulikani, anajulikana.

9. Mazingira ya kupotea kwa Ben Saanane yanautata mkubwa sana. Watu wengi sana wanatishiwa sasa. Juzi studio wametekwa wanne.

10.Matukio yanayoendelea sasa nchini yanawafanya watu kuwa na hofu. Hawaamini kama wakitoka watarudi majumbani mwao salama.

11. Namuomba Rais wangu aunde tume huru ya kuchunguza matendo haya ili impelekee taarifa kamili aweze kuchukua hatua.

12.Tusipochukua hatua, yatajitokeza makundi ya wahuni nao watapitia mlango huo huo kwa sababu hakuna hatua zinazochukuliwa.

13.Matendo haya yasipokomeshwa haraka, CCM tutapata tabu sana kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.

NAPE AMKABIDHI RASMI OFISI WAZIRI MWAKYEMBE

 Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Prof Elisante Ole Gabriel akiwakaribisha Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison George Mwakyembe na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Nape Moses Nnauye kwa ajili ya makabidhiano rasmi ya Ofisi yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mjini Dodoma.
  Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura akitoa neno kwa Waziri mpya na Waziri aliyepita wakati wa makabidhiano rasmi ya Ofisi yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mjini Dodoma.
 Mhe. Nape Moses Nnauye aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo akitoa shukurani zake kwa watendaji wa Wizara kwa muda wote aliotumikia Wizara katika makabidhiano rasmi ya Ofisi yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mjini Dodoma.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison George Mwakyembe akimshukuru aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye kwa kuitumikia Wizara kwa muda wote aliokuwepo.

 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison George Mwakyembe na aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye wakitia saini hati za makabidhiano  rasmi ya Ofisi yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mjini Dodoma akishubudia utiaji wa saini ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo  Prof Elisante Ole Gabriel.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison George Mwakyembe na aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye wakikabidhiana hati za makabidhiano  rasmi ya Ofisi yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mjini Dodoma.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt Harrison George Mwakyembe na aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Waziri Mhe. Anastazia Wambura ,Katibu Mkuu wa Wizara hiyo  Prof Elisante Ole Gabriel, Naibu Katibu Mkuu Bibi Nuru Millao na watendaji wa Wizara mara baada ya mkabidhiano rasmi ya Ofisi yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara Mjini Dodoma.

Picha zote na Raymond Mushumbusi WHUSM Dodoma.

CHADEMA WAFUNGUKA KUHUSU NAPE

 Makamu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuhusu chama hicho kuwateuwa Lawrence Masha na Ezekia Wenje kugombea Ubunge wa Afrika Mashariki pamoja na mambo mbalimbali yayoendelea nchini. Kulia ni Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.

Na Dotto Mwaibale
CHAMA cha Demokrasia  na Maendeleo (Chadema) kimemtaka Rais Dk. John Magufuli kuueleza umma wa Watanzania sababu za kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Katika hatua nyingine kimesema wabunge wa vyama pinzani kwa kushirikiana na wabunge wa Chama cha Mapinduzi wanatarajia kuwasha moto katika Bunge la Bajeti linalo tarajia kuanza mapema mwezi ujao kulingana na mambo mbalimbali yautendaji wa Serikali ya awamu ya tano.

Aidha chama hicho kimemtaka Rais Magufuli kumchukulia hatua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutii matakwa ya wananchi na kuepuka hali ya kuonekana kutumia vibaya madaraka kwa kuwahukumu baadhi ya watu kwa kuwalinda watu wenye makosa ya wazi wazi.

Akizungumza Makao Makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam leo siku moja baada ya kutenguliwa kwa uteuzi huo Naibu Katibu Mkuu wa chama cha Chadema Bara, John Mnyika alisema kutokana na taarifa ya Ikulu kutoeleza sababu za kutenguliwa kwa nafasi ya Nape hivyo ipo haja kwa Rais kueleeza wazi sababu ya kumuondoa.

"Rais anapaswa kujitokeza kutoa sababu kwanini katika kipindi hichi ambacho kamati iliyoundwa na Waziri kutoa taarifa iliyoeleza wazo makosa yaliyofanywa na Makonda katika siku chache baada ya Rais kumkingia kifua," alisema.

Alifafanua kuwa hatua ya Rais Mgufuli kumuondoa Nape ni matumizi mabaya na ya wazi ya madaraka katika kuwahukumu baadhi ya watu na kuwalinda watu ambao wanafanya makosa ya wazi wazi.

"Chimbuko la matatizo haya ni Mkuu wa Mkoa huo na kauli za Rais Magufuli katika kipindi cha siku za karibuni kuhusiana na Makonda kwa gharama yeyote ya kumlinda Makonda ni wazi kwamba ni matumizi mabaya madaraka," alisema.

Hata hivyo alisema kuwa matumizi hayo mabaya ya madaraka kwa sasa yamejipenyeza zaidi hali ambayo kwa sasa hayamuhusu Rais Pekeake bali hata watendaji wa vyombo vya dola ambavyo pia vimejidhihirisha kutokana na matukio yanayoendelea ikiwemo matumizi ya silaha kwenye maeneo ambayo hayakuhitajika.

Alisema ipo haja kwa Rais Magufuli kuwaeleza watanzania kuhusiana na baadhi ya maofisa wa ulinzi na usalama waliovamia kituo cha Luninga cha Clouds wakiwa na silaha na walio mtishia bastola Nape kama amewatuma na kama hakuwatuma pia aeleze hadi sasa ameelekeza wachukuliwe hatua gani, akiwa yeye ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.                                                    
Aidha alitumia nafasi hiyo kumpa pole kwa wanahabari na Nape kutokana na mambo mbalimbali yanayowakuta, na kuwataka Watanzania kutarajia kuwashwa moto katika Bunge la Bajeti linalotarajia kuanza hivi karibuni katika kujadili mambo mbalimbali yanayotokana na utendaji wa Serikali.

"Naamini safari hii hatutakuwa wabunge wa Chadema au wa vyama vya upinzani pekee bali naamini safari hii Bunge litakuwa kitu kimoja katika kuchukua hatua wakiwemo wabunge wa CCM," alisema.

Kuhusu wabunge walioteuliwa kushiriki katika uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, aliwataja walioteuliwa kutoka katika chama hicho kuwa ni Lawrence Macha na Ezekia Wenje.

Alibainisha kuwa wagombea hao walipatikana kutokana na vikao vya siku mbili vya Kamati Kuu ya Chadema vilivyo fanyika hivi Machi 22 na 23 mwaka huu.