HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

Lowassa aachiwa kwa dhamana

Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa ameachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa kwa saa nne katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Lowassa ameondoka makao makuu ya polisi saa 8.15 na kuelekea nyumbani kwake.
Akizungumza baada ya mahojiano hayo, Mwanasheria wa Chadema, Peter Kibatala amesema Lowassa amejidhamini mwenyewe na ametakiwa kuripoti tena Alhamisi saa 6.00 mchana.
Kibatala amesema Lowassa amehojiwa kwa kosa la uchochezi na ameandika maelezo ya onyo juu ya kauli aliyoitoa wakati wa futari iliyoandaliwa na mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.
"Mzee amehojiwa kwa kile wanachokiita kauli ya uchochezi aliyoitoa Juni 23, mwaka huu wakati wa futari iliyoandaliwa na Waitara. Baada ya kuhojiwa ameandika Maelezo ya Onyo na atatakiwa kuripoti tena Alhamisi, Juni 29," amesema.

Jinsi mauaji ya kutisha ya polisi nane yalivyofanyika

Wakati Taifa likiwa katika simanzi na taharuki baada ya askari wanane kupoteza maisha katika shambulizi lisilo la kawaida dhidi ya Jeshi la Polisi, mashuhuda wa tukio hilo wanasema wauaji walijipanga katika maeneo matatu tofauti katika eneo la tukio kabla ya kufanya shambulizi hilo.
Habari za shambulio hilo la aina yake lililotokea juzi ziliripotiwa na gazeti hili pekee jana na hali ya simanzi ilitawala jana wakati Jeshi la Polisi likitoa taarifa kuhusu tukio hilo, huku Rais John Magufuli akiongoza waombolezaji.
“Baada ya kusikia hili tukio nilikaa kama dakika kumi natafakari bila kupata majibu. Hivi haya matukio yanafanywa na kina nani? Wanafanya kwa malengo gani?” alihoji Othman Juma, aliyekuwa anafuatilia mkutano huo wa Jeshi la Polisi katika ukurasa wa Mwananchi.
Wauaji hao walimshambulia kwa risasi tano dereva wa gari aina ya Toyota Landcruiser (pickup) na wakati askari walipokuwa wanajariku kuruka kujinusuru, watu hao waliwatungua kwa risasi wakati gari likienda kunasa pembeni ya barabara.
Watu hao walilifuata gari hilo liliposimama na kuwavua fulana za kuzuia risasi kisha kuwamalizia tena kwa risasi kabla ya kuchukua silaha saba walizokuta, tatu zikiwa za masafa marefu.
Waandishi wetu waliofika eneo la tukio wamesema hofu imezidi kutanda kwenye vijiji vya Wilaya ya Kibiti, na hasa Kijiji cha Jaribu ambako viongozi wao hawaonekani na wakazi hupotea inapofika nyakati za usiku kuhofia maisha yao.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, aliyeomba jina lake lihifadhiwe, aliiambia Mwananchi kuwa washambuliaji hao walikuwa watatu na walijificha katika maeneo matatu kando ya Barabara ya Dar-Kibiti kuhakikisha hawawezi kulikosa kwa risasi gari hilo la Jeshi la Polisi.
Alisema wakati gari hilo likipita kwa mwendo wa kasi majira ya saa 12 jioni eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa, likiwa limetokea Jaribu Mpakani, kijiji kilichopo takriban kilomita tatu kutoka eneo la tukio, washambuliaji hao walianza kufyatua risasi mfululizo, hasa kumlenga dereva.
“Wauaji hao walifanya mashambulizi hayo wakitokea vichakani kwa kuwa eneo hilo ni pori. Lakini eneo walipouawa askari hao lilikuwa limefyekwa vizuri kwa miti yote na majani kukatwa,” alisema.
Alisema baada ya dereva kushambuliwa, gari lilianza kuyumba na kupoteza mwelekeo na askari waliokuwa ndani walianza kuruka nje ya gari ili kujiokoa au kurudisha mashambulizi na kila waliporuka walikumbana na risasi.
Shuhuda huyo alieleza kuwa baada ya gari kusimama, watu hao walienda kwenye gari hilo lililokuwa limeegemea kwenye ukingo ulio kando ya barabara na kuwamalizia kwa risasi askari hao wanane na mmoja alijeruhiwa mkono wake wa kushoto.
Askari huyo alimudu kuwatoroka wavamizi hao baada ya kutambaa kupanda gema lililokuwa karibu na eneo ambalo gari liligota na kuibukia upande wa pili ambao una mtaro.
“Sielewi. Ni Mungu tu,” alisema askari huyo aliyetambulishwa kwa jina la PC Fredrick ambaye amejeruhiwa mkono wa kushoto.
Lakini dereva wa gari hilo, ambaye pia alijaribu kutoroka eneo hilo, alionekana kirahisi na washambuliaji kwa kuwa alikimbia kunyoosha njia kulingana na mwelekeo wa barabara hiyo na hivyo kushambuliwa kwa risasi nyingine.
Waandishi wetu waliofika eneo la tukio kuanzia jana asubuhi wameeleza kuwa wananchi walisikia milio ya silaha nzito majira ya saa 12:15 jioni, lakini walishindwa kusogelea kutokana na vitendo vya mauaji vinavyoendelea maeneo yao.
Wakazi wa eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa walisema walisikia milio ya silaha nzito tofauti na milio ya bunduki za kawaida na hivyo kuamua kutotoka nje.
Mkazi wa Mkengeni, Rashid Mohamed alisema hofu imezidi kijijini hapo na wanashindwa kufanya biashara zao kama walivyokuwa wakifanya awali, na hivyo maisha yanazidi kuwa magumu.
Mohamed alisema juzi walisikia milio ya bunduki na risasi moja iliangukia kwenye paa la duka lake. Alisema ana hofu kwa sababu biashara yake haiendi vizuri kwa kuwa watu hawaendi kazini kwa kuhofia usalama wao.
“Leo watu wengi hawajaenda kabisa mashambani. Kila mtu ana hofu. Unaweza kwenda halafu ukakutana na hao wauaji. Hali si nzuri kabisa, sijui hatima yangu ni nini,” alisema mfanyabiashara huyo.
Mkazi mwingine wa Kijiji cha Bungu, ambako kuna kambi maalumu ya polisi, Mwajuma Said alisema kwa sasa hawana viongozi kwa kuwa wote wamekimbia baada ya kutishiwa maisha.
Alisema kutokana na kukosa serikali tangu Februari mwaka huu, walianza kupeleka matatizo yao Kituo cha Polisi cha Bungu. Alisema baada ya tukio la juzi hawajui watapeleka wapi shida zao kwa sababu polisi ambao wanawategemea nao wanauawa.
“Walikuja wakatupa vipeperushi kwenye ofisi ambavyo waliandika kwamba wamefika kijiji chetu kwa ajili ya kumuua mwenyekiti, mjumbe na mtendaji wa kijiji. Baada ya vitisho hivyo, viongozi hao walikimbia kijiji hiki, mpaka sasa hatuna serikali,” alisema mwanamke huyo.
Mwalimu mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema wauaji hao wamekuwa wakielekeza mashambulizi yao kwa watumishi wa umma, jambo ambalo linampa hofu.
“Hatujui hatima yetu itakuwaje. Baadhi ya walimu wanaomba uhamisho ili waondoke eneo hili. Polisi tunao wa kutosha lakini yanapotokea mauaji kama haya tunashindwa kujua ni nguvu gani waliyonayo wauaji hao,” alisema mwalimu huyo mkazi wa Kijiji cha Bungu.
Hali ilivyokuwa jana
Mwananchi ilikuta polisi wakiwa eneo la tukio majira ya saa 4:30 asubuhi, wakichukua vipimo, huku baadhi yao wakiwa wameficha sura kwa kuvaa kinyago kinachoruhusu macho pekee kuonekana.
Eneo hilo ni kilomita tatu kutoka kituo cha ulinzi ambako askari hao walibadilishana lindo na kuanza safari ya kurudi kambini Bungu.
Eneo la tukio hilo ni mteremko uliopo Kijiji cha Mkengeni kilichopo kati ya Mkuranga na Rufiji.
Askari mmoja wa kambi maalumu iliyopo Bungu aliiambia Mwananchi kuwa risasi tano zilipigwa mfululizo upande wa dereva kabla gari hilo halijaacha njia na kwenda kuegemea kwenye ukingo wa bonde dogo lililo pembeni ya barabara.
“Sehemu lilipotokea tukio ni kama ina kichaka na askari aliyenusurika alitambaa kwa tumbo kwenye kichaka cha upande wa kulia kama unaelekea Rufiji na kufanikiwa kujinusuru, ingawa alikuwa ameshapigwa risasi ya mkono,” alisema askari huyo.
Alieleza zaidi kuwa baada ya gari kupinduka na askari hao kupigwa risasi, bado walivuliwa vikinga risasi na kupigwa risasi nyingine.
Akizungumza eneo la tukio Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alimwambia Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba kuwa washambuliaji hao walijipanga maeneo matatu na walikuwa wanafahamu wanachofanya.
“Wangemkosa hapa, wangempata pale au pale. Lengo lao ilikuwa kumshambulia dereva,” alisema Ndikilo huku akionyesha kwa mikono aliposimama mshambuliaji mmoja baada ya mwingine.
Wananchi katika kijiji cha Mkengeni walikuwa wamesimama katika makundi na wengine wakiwa kwenye vibanda vya kahawa wakijadiliana kuhusu tukio hilo na wengi hawakutaka kuongea na waandishi wakionekana kuhofia maisha yao.
Baada ya Waziri Mwigulu kuwasili eneo la tukio na kupokea maelezo kutoka kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga, msafara huo ulielekea Kijiji cha Bungu kuona kambi hiyo maalumu.
Kambi hiyo imetengenezwa kwa maturubai sita ambayo wanaishi askari hao.
Shambulio hilo ni mwendelezo wa matukio kadhaa dhidi ya askari wa Jeshi la Polisi ambayo yamekuwa yakitokea tangu mwaka juzi. Januari 20, 2015, watu wasiojulikana walivamia Kituo cha Polisi cha Ikwiriri wilayani Rufiji na kuua askari wawili waliokuwepo kituoni hapo na kuondoka na silaha walizokuta.
Uvamizi kama huo ulifanyika Februari 3, 2015 wakati kundi la watu wasiojulikana lilipovamia Kituo cha Polisi cha Mgeta wilayani Kilombero na kuchukua bunduki aina ya SMG iliyokuwa na risasi 30.
Tukio jingine lilitokea Julai mwaka juzi wakati watu wasiojulikana walipovamia Kituo cha Polisi Sitakishari, Ukonga, Dar es Salaam na kuua askari wanne na raia watatu na baadaye kupora silaha ambazo idadi yake haikuwekwa bayana.
Katika shambulizi jingine lililofanyika Agosti mwaka jana, polisi wanne waliuawa wakiwa Benki ya CRDB, Mbagala, Dar es Salaam ambako walikuwa wakibadilishana lindo. Watu wasiojulikana waliowasili eneo hilo kwa pikipiki tatu, waliwafyatulia risasi askari hao na kuwaua baadaye kuondoka na bunduki mbili.
Polisi pia wameuawa katika matukio ambayo walijaribu kupambana na watu hao, likiwamo la Vikindu ambako ofisa wa polisi wa cheo cha ASP, Thomas Njuki alipigwa risasi wakati polisi ilipoenda kukamata watuhumiwa wa ujambazi.
“Tumeshapoteza askari zaidi ya 10. Ninaamini wanatosha. Sasa tunaenda kwenye operesheni maalumu, hatutakuwa na mzaha wala msamaha,” alisema kamishna wa operesheni na mafunzo wa Polisi, Nsato Marijani alipoongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
“Tutawapata popote walipo, tutawashughulikia kikamilifu hakuna atakayebaki. Mapambano haya hayana mwisho, huu ni mwanzo usio na mwisho,”alisema.
Alisema baada ya mauaji hayo ya polisi, operesheni kali ilifanikisha kubaini maficho ya muda ya watu hao.
Kamishna Marijani aliwataja askari waliouwawa katika shambulio hilo kuwa ni Peter Kigugu, ambaye ni mkaguzi msaidizi wa polisi, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zacharia, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub.
Alisema katika msako huo, polisi waliwaua watu wanne wanaosadikiwa kuwa ni majambazi na kukamata bunduki nne, mbili zikiwa zile zilizoporwa kwa askari.
Alisema watu hao walifanikiwa kuua askari wengi kwa sababu walikuwa pamoja ndani ya gari, na si kwa sababu wana ujuzi wa kipekee.
Alipoulizwa kuhusu uhusiano wa shambulio hilo na ugaidi, Kamishna Marijani alisema: “Wale ni majambazi, hawana lolote. Si chochote. Hatuwezi kuweka kanda maalum kwa sababu yao. Wameamua kupambana na Jeshi la Polisi kwa sababu tunawazuia. Huu si ugaidi, ni ujambazi.”
Alisema matukio ya uhalifu yametawala mkoani Pwani kutokana na kuwa na mapori yanayowavutia wahalifu na kuweka maficho yao.
Kamishna Marijani aliwataka wananchi kuliunga mkono Jeshi la Polisi katika operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa.
Kamishna pia alipiga marufuku pikipiki kuonekana Kibiti, Mkuranga na Rufiji kuanzia saa 12:00 jioni.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema watu hao waliiba silaha saba, nne zikiwa ni bunduki aina ya SMG na bunduki tatu za masafa marefu.
Alisema bunduki nyingine mbili aina ya SMG zilizokuwa sehemu ya mbele ya gari la polisi zilipatikana kwa kuwa washambuliaji hao hawakuziona.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alitembelea eneo hilo na kusema wanaofanya mauaji hayo watashughulikiwa.
“Hatukubaliani na jambo hilo, halina nafasi. Mkuu wa Mkoa pokeeni pole na fungeni mikanda upya ili tuunganishe nguvu kukabiliana na uhalifu huu,” alisema Mwigulu akiwa katika kambi maalumu ya Bungu muda mfupi baada ya kuwasili eneo la tukio saa 7:00 mchana.
Waziri Mwigulu aliwapa pole polisi na kuwataka kusonga mbele ili kuhakikisha silaha zilizoibwa zinarudishwa.
Akizungumzia zaidi tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ndikilo alisema ni tukio zito kwa mkoa kupoteza askari wanane wakati mmoja. “Ni tukio zito na mtihani mkubwa kwa wananchi, hasa wanapoona askari walioletwa kuwalinda nao wamefariki,” alisema Ndikilo.
Aliwataka wananchi wawe na subira wakati serikali ya mkoa ikiendelea kulifanyia kazi suala hilo.


Chanzo: Mwananchi

MAJAMBAZI YALIYOUA POLISI 8 KWA RISASI NAYO YAMEUAWA

Jeshi la Polisi Tanzania limesema limewaua majambazi wanne ambao walikuwa ni sehemu ya kundi la majambazi lililowashambulia na kuwaua askari 8 wilayani Kibiti mkoani Pwana jana usiku.

Akizungumza na wanahabari leo, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Nsato Marijani amesema kuwa mara baada ya kundi hilo kuwashambulia askari, kikosi kingine cha askari kilifanya msako na kubaini maficho ya majambazi hao.

Amesema baada ya kuwabaini, yalifanyika mashambulizi ya kurushiana risasi, ambapo majambazi wanne waliuawa pamoja na kukamata bunduki 4 zikiwemo SMG mbili zilibainika kuwa kati ya zile zilizoporwa na majambazi hao.

Akielezea tukio hilo lilivyokuwa, Kamishna Marijani amesema kundi la waharifu walikuwa na silaha za moto na ambao idadi yao haikujulikana liliweka mtego na kufanikiwa kuishambulia kwa risasi gari iliyokuwa na askari 9 waliokuwa wakitoka katika malindo kurudi kambini, na kuwaua askari 8 kati yao huku mmoja akijeruhiwa mkononi.

Amewataja askari waliuawa kuwa ni pamoja na Mkaguzi Msaidizi Peter Kiguu, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub, ambapo pia walipora bunduki 7 zikiwemo SMG 4.

Kufuatia tukio hilo, Kamishna Marijani ametangaza vita na waharifu wote katika maeneo hayo, ambapo amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinaanza oparesheni maalum katika mkoa wa Pwani, kuhakikisha vinawasaka na kukomesha mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua.

"Mpaka sasa jeshi limekwisha poteza skari zaidi ya 10, inatosha…. Tunakwenda kwenye oparesheni maalum, hatutakuwa na mzaha, tutawasaka popote walipo na kuwashughulikia kikamilifu, ,,, watajua tofauti ya moto na maji… mpaka jana idadi ilikuwa ni 8 kwa nne, lakini nawahakikishia kuwa ndani ya wiki moja idadi hiyo itakuwa imebadilika, na tutakuwa na hesabu tofati” amesema Marijani

Kuhusu hofu ya ugaidi, Kamishna Marijani amesema tukio hilo siyo la kigaidi bali ni uhalifu wa kawaida, huku akibainisha kuwa Tanzania hakuna ugaidi

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limepiga marufuku uendeshaji wa pikipiki katika maeneo yote ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji zaidi ya saa 12:00 jioni. Amesema usafiri wa boda boda utaruhusiwa kati ya saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.

CHANZO: EATV 

Askari 152 Wafukuzwa Kazi.

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Jumla ya askari 152 wamefukuzwa kazi mwaka huu na Jeshi la Polisi kwa sababu ya kukiuka Sheria, Taratibu na Kanuni ya Jeshi hilo kama zilivyoainishwa katika Kanuni za Kudumu za Polisi (PGO) namba 103.

Idadi ya askari hao waliofukuzwa kazi imetolewa jana mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Msabaha aliyehitaji kufahamu juu ya idadi ya askari waliochukuliwa hatua kwa sababu ya utovu wa nidhamu.

Mhandisi Masauni alisema kuwa kazi ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama ni kulinda raia, mali zao pamoja na mipaka ya nchi lakini kuna baadhi ya askari hao wanakwenda kinyume na Sheria kwa kuwapiga wananchi na kuwasababishia ulemavu pamoja na vifo hivyo Jeshi hilo limewachukulia hatua za kinidhamu.

“Jeshi la Polisi hufanya kazi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo lakini kuna baadhi ya askari wamekuwa wakikiuka maadili na mwenendo mwema wa Jeshi letu hivyo kuanzia Januari 2015 hadi Juni 2016 tuliwachukulia hatua za kinidhamu askari 200”, alisema Mhandisi Masauni.

Naibu Waziri huyo alifafanua kuwa baada ya askari hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu, walifanyiwa uchunguzi wa kina na jumla ya askari 152 kati ya 200 walikutwa na hatia hivyo hatua iliyofata ni kuwafukuza kazi.

Akizungumzia kuhusu mpango wa Serikali juu ya kujenga nyumba za askari Polisi, Mhandisi Masauni alisema kuwa wanatambua tatizo la makazi ya Askari Polisi katika maeneo mbalimbali nchini hususani kwenye mikoa mipya hivyo Serikali ina nia ya kutatua tatizo hilo kwa kuanza ujenzi wa nyumba kwa ajili ya askari hao.

“Serikali imedhamiria kupunguza tatizo la upungufu wa makazi ya askari polisi kwa kujenga nyumba kwa awamu kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba 4,136 nchi nzima ambao utaanza kutekelezwa baada ya taratibu za mkopo wa kuwezesha ujenzi huu kukamilika”, aliongeza Mhandisi Masauni.

MTANDAO WA WIZI WA BAJAJI NA BODABODA WANASWA MBEYA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashali akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya kuhusiana na tukio la kuunasa mtandao wa wizi wa Bajaji na Pikipiki (BodaBoda) Mkoani Mbeya.(JamiiMojaBlog)
Mkutano wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya na Waandishi wa habari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashali akionesha baadhi ya Bjajai na Pikipiki ziizokmatwa katika msako uliofanywa na jeshi hilo la POLISI Mbeya. 
Askari Polisi wakiwa wamebeba moja ya bajaji iliyokamatwa mara baada ya Jeshi la Polisi Kufanya masako .
Bajaji zilizokamatwa na Jeshi la Polisi mara baada ya kufanya msako. 
JESHI la Polisi Mkoani Mbeya limefanikiwa kuunasa mtandao uliokuwa ukihusika na matukio mbalimbali ya wizi wa bajaji na Pikipiki (bodaboda) katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya.

Mtuhumiwa anayehusika na matukio hayo imefahamika kwa jina la Getruda Mwakyusa Mkazi wa Mtaa wa Manga Veta jijini hapa.

Akizungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Dhahiri Kidavashari amesema jeshi la polisi limeendelea kufanya misako katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya ili kudhibiti uhalifu .

Amesema Octobar 13 katika misako hiyo jeshi hilo la polisi lilifanikiwa kuunasa mtandao wa wizi wa bajajai na pikipiki ambapo mtuhumiwa wa matukio hayo alifanikiwa kutoroka ambapo nyumba yake mara baada ya kufanyiwa upekuzi zilikutwa pikipiki 3,bajaji 3,bodi 7 za bajaji .

Amesema kati ya mali hizo pikipiki mbili tayari zimekwisha tambuliwa na wamiliki wake kuwa ziliibiwa wilayani Chunya septemba25 mwaka huu katika kijiji cha Isenyela kata ya Mbugani.

Aidha Kamanda wa Polisi Mkoani humo ametoa wito kwa jamii husasani vijana kuacha tabia ya kutaka mali kwa njia ya mkato badala yake wafanye kazi kihalali ili kijipatia kipato sanjali na kutumia fursa zilizopo ili kujitafutia ajira.

POLISI ALIYEREKODIWA AKIPOKEA RUSHWA KUCHUKULIWA HATUA

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Jeshi  la Polisi visiwani Zanzibar, limesema litamchukulia hatua za kinidhamu ofisa wake mwenyewe cheo cha Sajenti ambaye alionekana hivi karibuni akipokea rushwa kutoka kwa raia wa kigeni.

Hatua hiyo, imekuja baada ya picha za video kusambaa katika mitandao ya kijamii, zinazomwonyesha askari huyo akipokea fedha ambazo hadi sasa hazijajulikana kiwango chake kutoka kwa raia huyo wa kigeni, ambaye alikuwa na kosa la kutofunga mkanda.

Katika video hiyo, raia huyo anaokana kutoa fedha na kumkabidhi askari huyo huku akiahidi kumsaidia ili asikamatwe mbele ya safari.

Tukio hilo lilitokea eneo la Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ingawa askari huyo alitaja eneo la Mahonda akionyesha nia ovu ya kutenda kosa hilo bila kujijua kama anachukuliwa video.

Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame alisema jeshi hilo linampongeza raia huyo wa kigeni kwa kutoa taarifa hiyo.

“Jeshi la polisi linachukua nafasi hii kulaani kosa hili, licha ya kua ni kosa la jinai linalifedhehesha jeshi na kulitia doa kutokana na dhamana kubwa lililokabidhiwa,” alisema.

Alisema kwa mujibu  wa taratibu za jeshi hilo, tayari limeanza uchunguzi mara moja na kwamba litachukua hatua zinazostahili.

Kutokana na hali hiyo, Kamishina Hamdani amewataka wamiliki wa makampuni ya simu za mikononi kufufua mfumo wa upigaji simu kutumia namba za dharura ambazo ni 111 na 112 ili kuwarahisishia wananchi kutoa taarifa.

ALIYEMUUA TRAFIKI AFIKISHWA MAHAKAMANI

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Mkazi wa Mbezi Africana Dar es Salaam, Amani Elikana (32), amefikishwa   katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni akituhumiwa kumuua Askari wa Usalama Barabarani, Sajenti Mensali wa Kituo cha Polisi Mabatini – Kijitonyama.

Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu, Caroline Kiliwa, Wakili wa Serikali, Amani Mghamba alidai  mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 22 mwaka huu eneo la Kijitonyama.

“Mtuhumiwa inadaiwa kwamba siku hiyo kwa makusudi  ulimuua askari mwenye namba D. 8254 Sajenti Mensali kinyume cha sheria ya Jamhuri ya Muungano,” alidai Mghamba.

Hakimu Kiliwa alisema mtuhumiwa hapaswi kujibu kitu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo hivyo shtaka hilo liliahirishwa  hadi Oktoba 4 mwaka huu litakapotajwa tena.

KORTINI KWA KUIDHALILISHA POLISI KWA WHATSAPP

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


Zikiwa zimepita siku tano tangu wakazi watano wa Dar es Salaam walipopandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Kisutu kwa kosa la kumdhalilisha Rais John Magufuli na Jeshi la Polisi kwa kutumia mitandao ya Facebook na Whatsapp, mkazi mwingine ameongezeka.
Jana, mfanyabiashara Christon Mbalamula (28), alifikishwa katika mahakama hiyo akikabiliwa na shtaka la kutumia mtandao wa Whatsapp kwa kulidhalilisha jeshi hilo.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Dk Yohana Yongolo, Wakili wa Serikali Winifrida Sumawe alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Agosti 26, 2016 eneo la Kigamboni.
Alidai siku ya tukio, mshtakiwa huyo alilidhalilisha Jeshi la Polisi baada ya kusambaza ujumbe uliosema, “Natangaza ndoa na askari yeyote atakayejipendekeza kwangu siku hiyo ataolewa bila mahari.” Baada ya kusomewa shtaka hilo alikana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi haujakamilika.