Wanachana wa CUF wanaomuunga mkono mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba walijikuta wakizozana wao kwa wao muda mfupi baada ya mwenyekiti huyo kumaliza mkutano wake na waandishi wa habari.
Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumza na waandishi wa habari leo (Jumamosi) kuhusu kamati mpya ya maadili ya nidhamu iliyozinduliwa katika ofisi za chama hicho Buguruni.
Baada ya kumaliza kutoa maelezo yake, mwenyekiti aliketi chini na kisha Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Abdul Kambaya amesimama na kuwataka waandishi kutoka nje.
Lakini waandishi hao walisita kutii agizo hilo wakitaka kupata ufafanuzi wa baadhi ya hoja.
“ Ndugu waandishi tunaomba mtoke nje tuendelee na kikao chetu maswali mtauliza baada ya kamati kumaliza majukumu yake,” amesikika akisema Kambaya.
Hata hivyo, waandishi wameendelea kusisitiza kutaka kupata fursa ya kuuliza maswali kwa mwenyekiti ghafla kulisikika sauti toka nyuma ya ukumbi zikiwashinikiza waandishi hao watoke.
Mmoja wa mwanachama aliyekuwa amevalia fulana na kofia zenye nembo ya chama ndiye aliyeamsha zogo pale alipodai; “waondoke hawa waandishi kila siku wanakuja hapa hawaandiki habari zetu.”
Matamshi yake hayo yalidakwa na wengine waliokoleza mjadala hatua iliyofanya baadhi ya wanachama kusimama na kupinga hali hiyo.
“ Wewe ebu jiheshimu...acheni mambo yenu haya..ahaa hatutaki,” wamezozana wanachama hao.
Mzozo huo uliodumu kwa dakika tano umemalizika baada ya waandishi kutoka nje. Wakati wote wa malumbano hayo waandishi hawakuchangia neno lolote.
Mzozo huo ulihamia nje kwa dakika kadhaa huku baadhi ya wanachama wakivitaja na kuvituhumu vyombo vya habari kwa kutoandika habari zao.
Chanzo: Mwananchi
Profesa Lipumba: Akanusha Kutumiwa na CCM Kuivuruga CUF
By: VIJIMAMBO on May 04, 2017 / comment : 0 CUF, Habari, Profesa Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti wa CUF anayetambulika na msajili wa Vyama vya Siasa Prof. Ibrahim Lipumba leo May 4, 2017 kupitia kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na Clouds TV amesema hakuwa na namba ya Edward Lowassa wakati anajiunga UKAWA.
Aidha, kwenye mahojiano hayo Prof. Lipumba amesema kuwa amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha anaiongoza CUF katika kudai haki za wananchi tofauti na Maalim Seif ambaye mara kadhaa ikitokea suala hilo haonekani akisema:
“Mwaka 2000 baada ya Uchaguzi Mkuu tuliingia kwenye maandamano Zanzibar, lakini Maalim Seif alikwenda Uingereza nilikuwa mstari wa mbele.
Prof. Lipumba amesema pia kuwa Maalim Seif amekuwa akidai kila anapokosana na mtu kisiasa kuwa mtu huyo anatumiwa na CCM akitolea mfano wa Ahmad Rashid, akisema:
“Ni kawaida ya Maalim Seif, akikosana na mtu kisiasa anasema anatumiwa na CCM. Rejea mgogoro na Ahmad Rashid".
Akizungumzia kuhusu kumpokea na kumtambulisha kwa viongozi wa UKAWA aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Edward Lowassa wakati anatoka CCM, Prof. Lipumba alisema:
“Mbatia ndiye aliyeniunganisha na Lowassa. Sikuwa na namba zake, na wakati anakuja, nilisema wazi suala la rushwa ni mfumo siyo mtu.
“Mzigo mzito anapewa Mnyamwezi, lakini huu wa kumnadi Edward Lowassa ulinizidi uzito, nisingeweza kuubeba."
Wakai huo huo Prof. Lipumba amebainisha kuwa hakuwa na nia ya kurejea katika nafasi yake ya Uenyekiti wa CUF baada ya kujiuzulu, lakini aliombwa na wanachama wa chama hicho.
“Sikuwa na nia ya kurudi kuwa Mwenyekiti CUF ila wanachama waliniomba nirudi baada ya uchaguzi kumalizika na hali kutulia”
PROFESA LIPUMBA ATINGA MAHAKAMANI
By: VIJIMAMBO on April 21, 2017 / comment : 0 CUF, Habari, Maalim Seif, Profesa Ibrahim Lipumba
Mgororo wa ruzuku ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) unazidi kupamba moto baada ya mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kwenda kuitetea mahakamani.
Profesa Lipumba na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa chama hicho, Thomas Malima wamefungua maombi Mahakama Kuu wakiomba waunganishwe kwenye kesi iliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa CUF, walio upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katika kesi ya msingi ya ruzuku namba 21 ya mwaka 2017, wadai wanaiomba Mahakama imzuie msajili kutoa ruzuku kwa CUF na imuamuru Sh360 milioni alizozitoa kwa kina Profesa Lipumba zirejeshwe kwenye akaunti rasmi ya chama.
Wadaiwa katika kesi hiyo ni Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lakini Profesa Lipumba na Malima wamewasilisha maombi mahakamani nao waunganishwe kwenye kesi hiyo upande wa wadaiwa.
Maombi hayo yalitajwa jana na Malima aliieleza mahakama wakiwa viongozi halali wa chama hicho, wanaomba kujumuishwa kwenye shauri hilo kwa kuwa wana masilahi na shauri hilo.
Wakili wa CUF upande wa Katibu Mkuu, Juma Nassoro na Wakili wa Serikali, Hang Chang’a waliieleza mahakama kuwa bado hawajapewa hati za maombi hayo.
Jaji Wilfred Dyansobela aliamuru waombaji hao (kina Lipumba) kuwapatia nyaraka hizo na amepanga kusikiliza maombi hayo Juni 6, siku ambayo kesi ya msingi itatajwa.
Maalim Seif: Hakuna CUF ya Maalim wala CUF ya Lipumba
By: VIJIMAMBO on April 10, 2017 / comment : 0 CUF, Habari, Maalim Seif, Profesa Ibrahim Lipumba
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema chama hicho kitaendelea kufanya mambo kiungwana kwa kuwa Tanzania ni nchi ya amani na kuwa hakuna CUF ya Maalim Seif wala CUF ya Lipumba.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Maalim Seif alisema CUF inatimiza wajibu wa kutunza amani na iwapo kingetaka kuleta machafuko basi kingefanya hivyo tangu zamani.
“CUF ni moja. Ni kweli sisi tumekuwa wapole na waungwana, sisi si tunaambiwa hii nchi ya amani, sisi tunatimiza wajibu wetu wa kutunza amani. Hakuna chama kinachotunza amani kama CUF” alijibu mara baada ya kuulizwa na waandishi wa habari.
“The struggle we continue, mtatia ndani Maalim Seif, mtatia ndani Mtatiro lakini there are so many Maalim Seif’s. Kuna Maalim wengine ni vichaa,” alisema
Wakati huhuo Maalim Seif aionyooshea kidole Rita
Katibu Mkuu wa CUF , Maalim Seif Sharif Hamad amezungumza na waandishi wa habari leo na kusema Wakala wa Usajili wa vizazi na vifo, (RITA) utakuwa umekiuka sheria iwapo utaisajili na kuitambua bodi ya wadhamini iliyoundwa na Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba.
“Sisi tumekuwa wapole sana, tunaona katiba inavunjwa, lakini niseme kwamba, kama Rita wataisajili bodi ya Lipumba, watakuwa wamekiuka sheria yao wenyewe. Bodi ipo na imesajiliwa 1993 na tunacho cheti cha kusajiliwa” alisema
Alisema ni utaratibu kuwa kila kipindi fulani marekebisho hufanywa lakini bodi haifi.
Alisema bodi ya CUF ipo na kama ofisa Mtendaji mkuu wa Rita ataisajili basi ajue anavunja sheria.
MAALIM SEIF: LIPUMBA HANA UWEZO WA KUNIVUA UKATIBU MKUU CUF
By: VIJIMAMBO on April 02, 2017 / comment : 0 CUF, Habari, Maalim Seif, Profesa Ibrahim Lipumba
Sarakasi za kisiasa zinaendelea kutawala ndani ya chama cha CUF baada ya Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, kudai kuwa Profesa Ibrahim Lipumba anatumiwa kukihujumu chama hicho.
Maalim Seif alimtuhumu Profesa Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF, anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuwa anakihujumu chama ili kishindwe kudai haki waliyoipata katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka juzi.
Aliyasema hayo jana katika kijiji cha Tumbatu Mkoa wa Kaskazini Unguja alipozungumza na wanachama wa chama hicho, ikiwa ni ziara maalumu ya uimarishaji wa chama katika mikoa yote ya Kisiwa cha Unguja.
Maalim Seif alisema pamoja na Profesa Lipumba kupata nguvu kutoka vyombo vya dola na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika kukihujumu chama hicho, lakini hawataweza kufikia malengo hayo.
Alisema taasisi hizo kwa pamoja zimekuwa zikimuunga mkono Lipumba kwa kumpa kila nguvu anayohitaji ili kuona anafanikisha malengo ya CCM ya kuitawala nchi bila ya kuwepo kwa chama kikuu pinzani, ila nguvu zao hizo zitagonga mwamba.
“Nashangaa sana kuona Lipumba amekubali kutumika na CCM kwa kukihujumu chama kwa masilahi binafsi, lakini nataka muelewe wananchi kuwa pamoja na nguvu zao zote hizo katu hawataweza kuwakatisha tamaa Wazanzibari ya kudai haki yao waliyoipata katika uchaguzi uliopita,” alisema.
Alishangazwa kuona Ofisi ya Msajili kwa kushirikiana na vyombo vya dola badala ya kufuata Katiba na sheria za nchi, wao wamekuwa wakikihujumu chama hicho.
“Pamoja na hujuma hizi zinazofanywa na Lipumba katika chama chetu, lakini nashangaa Rais (John) Magufuli anatumbua watendaji wabovu, lakini humu mrajisi (Msajili) wa Vyama vya Siasa anamuachia,” alisema.
Kuhusu kuondolewa kwenye nafasi yake, Maalim Seif alisema kwa mujibu wa katiba ya CUF, Lipumba hana uwezo wa kumvua nyadhifa hiyo hata kama angekuwa ni mwenyekiti halali.
Alisema kwa mujibu wa katiba yao ili Katibu avuliwe wadhifa wake lazima mkutano mkuu uhudhuriwe na zaidi ya nusu ya idadi wajumbe.
Alisema kikao kilichofanyika chini ya Profesa Lipumba kilihudhuriwa na wajumbe wasiokuwa na ujumbe kihalali, ambao walipandikizwa kuonesha kama kikao hicho kilikuwa halali.
“Ikiwa mimi nimefukuzwa chama kutokana na madai kuwa sihudhurii vikao vinavyofanywa na ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam, mbona yeye Lipumba tangu mwaka 2015 hawajawahi kuja ofisi kuu ya chama ambayo ni mtendeni hadi leo, kwa hiyo naye alitakiwa kufukuzwa,” alihoji.
Maalim Seif alisema kuwa kinachosikitisha ni kuona Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nayo kuidhinisha kuwa wamekubaliana na mageuzi hayo yaliyofanywa na Lipumba kwa kushirikiana na wajumbe wake.
“Ninachokifahamu mimi ndani ya katiba yetu inasema kuwa ili uamuzi wa kuvuliwa nafasi ya uongozi ni lazima anayedaiwa kufanya kosa aitwe na uongozi kujieleza, lakini mimi sijaitwa kujieleza,” alihoji Maalim Seif.
Akizungumzia madai ya kushinda Uchaguzi Mkuu uliopita, Maalim Seif alisema waliwataka wananchi wa Zanzibar kutokata tamaa na haki yao, huku akidai hivi karibuni dola ya Zanzibar itakuwa chini ya CUF.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema uongozi wa CUF unasikitika kuona vyombo vya dola vikiingilia mamlaka ya chama hicho na kusahau wajibu wao.
Alisema kuwa wajibu wa vyombo hivyo ni kusimamia amani ya wanachama na viongozi wake, lakini ni jambo la kushangaza kwa viongozi wa vyombo hivyo kuwa ni miongoni mwa wanaongoza kuonesha chuki dhidi ya CUF.
Alisema pamoja na hujuma hizo, lakini viongozi wakuu wa chama hicho chini ya Maalim Seif, hawatosita kudai haki yao hadi kieleweke.
Akijibu tuhuma hizo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara na anayemuunga mkono Profesa Lipumba, Magdalena Sakaya alimtuhumu Maalim Seif kuwa ndiye anakula njama za kukidhoofisha chama.
Alisema Seif amekataza ruzuku zisifike kwenye wilaya, hakuna mikutano na hakuna hata pikipiki huku wenzao Chadema waliokuja juzi wamekuwa chama kikuu cha upinzani kutokana na kuwa wamoja.
“Malalamiko anayotoa ajikite kwenye katiba, aichambue kifungu kwa kifungu atabaini anakosea wapi.
“Hii ni taasisi ya chama, siyo kampuni ya mtu, lazima tufuate katiba tuliyojiwekea ambayo ipo wazi inatoa maelekezo ya kila kitu, anayekengeuka anafanya makusudi na sisi hatuwezi kukaa kimya bila kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuteua watakaofanya kazi alizotakiwa kufanya yeye,” alisema Sakaya.
Alieleza kuwa badala ya kujenga chama, ameamua kukidhoofisha na anatumiwa kufanya hivyo akijificha kwenye mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Amekuwa bwana kesi, kila kukicha anafungua mpya, mimi nina kesi, Lipumba ana kesi, Msajili wa Vyama ana kesi, mwanasheria ana kesi, akae kimya asubiri ziishe, ”alisema Naibu katibu mkuu huyo.
MAHAKAMA KUU YAMWAMURU MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KUTOTOA RUZUKU KWA PROF. LIPUMBA NA KUNDI LAKE MPAKA SHAURI LITAKAPOAMULIWA
By: VIJIMAMBO on April 01, 2017 / comment : 0 CUF, Habari, Mahakama, Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba
Mahakama Kuu imemuamuru Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kutotoa ruzuku kwa Prof. Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi, CUF, na kundi lake.
Zuio hilo ni mpaka shauri dhidi ya Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu kutoa fedha za ruzuku shilingi milioni 369 kwa njia za wizi na udanganyifu litakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.
Uamuzi huo umefikiwa na Jaji Dyansobela baada ya kukubaliana na hoja zilizowasilishwa kwa hati ya dharura.
Jopo la Mawakili wa CUF, liliiomba Mahakama Kuu kutoa amri hiyo kwa kuwa fedha zilizotolewa awali shilingi milioni 369 hazijulikani zimetumika vipi, na hazikuwa katika mikono salama wala hakuna udhibiti wowote wa chama kuhusu fedha hizo ikizingatiwa kwamba, Prof. Lipumba alishavuliwa uanachama.
Mawakili hao akiwemo Juma Nassor , wamesisitiza kwamba, mazingira yaliyopo ni vyema na busara kwa fedha za umma zilizopaswa kutolewa kama ruzuku kwa chama cha CUF kwa sasa ziendelee kubakia serikalini.
Aidha, wameiomba Mahakama Kuu kwamba amri hiyo pia ifungamane na kesi ya msingi namba 23/2016 ya kuhoji maamuzi ya msajili kumtambua Prof Lipumba kwa nafasi ya uenyekiti iliyopo mbele ya Jaji Kihijo ambayo kwa sasa imekatiwa rufani ya kufanyiwa marejeo mbele ya Mahakama ya Rufani Tanzania.
Lipumba Amtumbua Maalim Seif
By: VIJIMAMBO on March 07, 2017 / comment : 0 CUF, Habari, Maalim Seif, Profesa Ibrahim Lipumba
Mgogoro wa Uongozi wa Chama cha Wananchi CUF umeendelea kufukuta ambapo Mwenyekiti wa Chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili Vyama vya Siasa nchini Prof. Ibrahim Lipumba amemteua Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad baada ya Maalim Seif kukaidi wito wa Mwenyekiti wake kwenda Ofisi kuu Buguruni kwa zaidi ya mara nne
Prof. Lipumba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam pamoja na wafuasi wa chama hicho, amesema Maalim Seif amekaidi wito wa kwenda Makao Makuu Buguruni tangu Septemba 23 mwaka jana kwa ajili ya kusimamia mkutano wa kamati ya Utendaji ambao ulitakiwa kujadili mambo kadhaa ya chama hicho
Aidha, Prof. Lipumba amewavua madaraka wakurugenzi kutoka Zanzibar akiwemo Salim Bimani aliyekuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, Omar Ali Salehe Mkurugenzi Mipango na Uchaguzi, Abdalah Bakar Khamis Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, Pavu Juma Abdallah - Haki za Binadamu, Mahima Ali Mahima Katibu Mtendaji JUVICUF pamoja na Yusuph Salim Naibu Mkurugenzi Ulinzi na Usalama CUF wote kutoka Zanzibar.
Chama cha Wananchi CUF kimekumbwa na Mgogoro wa uongozi tangu Prof. Lipumba alipotangaza kujiuzulu uongozi wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambapo baadaye alitangaza kurudi na kufanyika mkutano mkuu ambao ulivurugika na kusababisha mpasuko kati ya CUF bara na CUF Zanzibar.
CUF YA PROFESA LIPUMBA YAJIBU MAPIGO KUHUSU RUZUKU WALIYOPEWA NA HAZINA
By: VIJIMAMBO on January 31, 2017 / comment : 0 CUF, Matukio, Profesa Ibrahim Lipumba
Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa) wa Chama cha Wananchi (CUF), Thomas D.C Malima (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama hicho jijini Dar es Salaam leo kuhusu ruzuku ya chama hicho iliyopokelewa kupitia akaunti namba 2072300456 ya Benki ya NMB Tawi la Temeke. Kulia ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Mneke Jafar na Katibu Jumuiya ya Wanawake (JUKE), Salama Masoud.
Meza Kuu. Kutoka kulia ni Kamanda Mkuu, Athumani Hamadi,Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Mneke Jafar, Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa) wa Chama cha Wananchi (CUF), Thomas D.C Malima, Katibu Jumuiya ya Wanawake (JUKE), Salama Masoud na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Masha Amour.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
| Mkutano ukiendelea. |
The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) chini ya Uongozi thabiti wa Mwenyekiti wake Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kinaishukuru na kuipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa kwa kukipatia Chama chetu Ruzuku yake inayopatikana kwa Mujibu wa Sheria ya vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992.
Pamoja na Ruzuku ya CUF kuzuiwa kwa Muda wa miezi mine (4) kuanzia mwezi Septemba, 2016 hadi Desemba 2016 kutokana na sintofahamu ya uongozi wa Kitaifa wa CUF, Msajili hakuona haja ya kuendelea kuizuia wakati shughuli za chama zinafanyika kila siku. Kuendelea kuizuia Ruzuku halali ya chama ni kukizuia kufanya kazi zake halali za kisiasa ikiwa ni pamoja na kushiriki katika chaguzi mbali mbali za kiserikali zinazoendelea nchini.
Waheshimiwa wanahabari, Baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014 alijiridhisha kuwa Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba ndiye Mwenyekiti halali wa CUF kwa kuwa mchakato wa kukamilisha kujiuzulu kwake haukukamilika kabla yeye kutengua barua yake ya kujiuzulu.
Mnamo Tarehe 23 Septemba 2016 , Msajili aliandika barua kwa Katibu Mkuu wa CUF kumjulisha msimamo na mwongozo wa wake kuwa “Mwenyekiti wa Taifa wa CUF ni Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba”
Baada ya Katibu Mkuu kupokea barua hiyo aliamua kupinga Uamuzi huo wa Msajili wa Vyama vya Siasa uliotokana na Malalamiko ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wapatao 324 kati ya 343 ambao walilalamikia uvunjifu wa Katiba ya CUF unaofanywa na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Maaalim Seif na timu yake walienda mbali kwa “kuikimbia ofisi yake” iliyoko hapa Ofisi Kuu ya CUF Buguruni na kukimbilia Mafichoni kusikojulikana na kusababisha kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kiutendaji. Hivyo, Mwenyekiti wa Taifa aliamua kufanya mabadiliko ya Kurugenzi za Chama kwa kumujibu wa ibara ya 91(1)(f) ya katiba ya CUF, nainukuu:
“Mwenyekiti wa Taifa atateua kutoka miongoni mwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa au wanachama wajasiri kuwa wakurugenzi na manaibu wakurugenzi wa Chama pamoja Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama baada ya kushauriana na Makamu Mwenyekiti na kufikisha uteuzi huo mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa kuthibitishwa”.
Kwa mujibu wa Ibara ya 95(3) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014, Nainukuu:-
“Naibu Katibu Mkuuatakayemfuatia Katibu Mkuu kwa madaraka ni Yule anayetoka upande tofauti wa Jamhuri ya Muungano na upande anotoka Katibu Mkuu”. Kwa kifungu hicho, Katibu Mkuu anaposhindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu yoyote ile, Naibu Katibu Mkuu Bara ndiye anakaimu Ukatibu Mkuu mpaka atakaporejea ofisini kuendelea na majukumu yake.
Hii inatokana ukweli wa kikatiba uliowekwa kwenye ibara ya 105 (1) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014, Nainukuu:-
“Pale ambapo mwanachama yeyote wa Chama mwenye madaraka kwa mujibu wa masharti ya katiba hii, kwa sababu yeyote ile, hawezi kutekeleza kazi zake kwa muda, mwanachama anayemfuata kwa madaraka kwa mujibu wa katiba atakaimu nafasi yake”.
Hivyo, kwa mujibu wa ibara hii na ile ya 95(3) Ni suala la kikatiba lisilo na shaka kwa Mheshimiwa Magdalena Sakaya (Mb) ambaye ndiye anayemfuata Katibu Mkuu kwa Madaraka kukaimu ofisi ya Katibu Mkuu mpaka atakaporejea ofisini kwake Buguruni. Kwa hiyo, Mhe Sakaya ataendelea kufanya majukumu yote ya Katibu Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya CUF. Na Katibu Mkuu hapaswi kulalamika.
Kuhusu masuala ya fedha, Kwa mujibu wa kanuni ya jfedha ya mwaka 2014, ibara ya 22(2)(a) (B):-“Masuala yote ya fedha yanasimamiwa na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi na ndiye Mshauri Mkuu wa Katibu Mkuu kuhusu Masuala ya Fedha”.
Na kwa kuwa Katibu Mkuu ni Ofisi siyo mtu, anapokuwa hayupo ofisini Naibu Katibu Mkuu Bara atatekeleza majukumu yote ya ofisi ya Katibu Mkuu kama Kaimu Katibu Mkuu. Ni aibu kwa Mwalimu Seif kulalamika wakati anaijua katiba ya CUF na anajua kuwa amekimbia ofisi mwenyewe ndiyo maana Mhe Sakaya anafanya kazi alizozikimbia kwa kushirikiana na wakurugenzi walioteuliwa na Mwenyekiti wa Taifa kwa mujibu wa Katiba.
Waheshimiwa wanahabari, Chama Chetu kimepokea sehemu ya malimbikizo ya ruzuku ya CUF Kiasi cha Tsh. 369,366,671/=. Tumepokea Ruzuku hiyo kupitia Akaunti namba 2072300456 ya The Civic United Front (CUF-Chama cha Wananchi) NMB Tawi la Temeke. Hii siyo akaunti Mpya ya Chama kama inavyodaiwa Maalimu Seif na genge lake.
Akaunti hii ilifunguliwa zaidi ya miaka Kumi iliyopita na Katibu Mkuu kwa ajili ya kupokea na kutoa fedha za CUF kwa wilaya ya Temeke. Na kwa mujibu wa Kanuni ya Fedha ya CUF ya mwaka 2014, ibara ya 23(1)(f) Nainukuu: -
“Chama ngazi ya Taifa kinaweza kufungua akaunti tofauti au kubadili matumizi ya akaunti iliyopo kwa ajili ya kazi au shughuli maalum kadri itakavyoona inafaa. Akaunti hizo zilizofunguliwa utawekwa utaratibu maalum wa kuzihudumia”.
Kwa kuzingatia hali iliyopo, Tuliona kubadilisha matumizi ya Akaunti ya The Civic United Front (CUF-Chama cha Wananchi), Tawi la Temeke itumike kupokelea Ruzuku ya Chama toka serikalini ili iweze kufikia katika mikono salama kwa ajili ya uendeshaji wa Shughuli za Chama.
Waheshimiwa wandishi, Baada ya kuipokea Ruzuku hiyo, tayari tumeshaitumia katika harakati za Kiuchaguzi katika Chaguzi za marudio ya Udiwani katika kata 14 ambapo CUF imefanya vizuri sana katika kata tatu (3) ambazo ni Nkome (Geita), Malya (Kwimba) na Kijichi (Temeke).
Waheshimiwa wandishi, Ikumbukwe kuwa Tangu Mwalimu Seif na Genge lake wakimbie Ofisi Kuu Buguruni Tarehe 23 Septemba 2016, shughuli za chama zilikuwa zikiendelea kufanyika japokuwa hatukuwa tunapata ruzuku toka Serikalini. Wanachama wetu walikuwa na ari zaidi ya kukichangia chama ili kuendeleza harakati za ukobozi wa Haki sawa kwa Wote. Kwa mapenzi makubwa ya Chama chake Mheshimiwa Mwenyekiti wetu Profesa Ibrahim Haruna Lipumba alikuwa Msitari wa mbele kukisaidia chama kwa kujitolea na hata kukikopesha chama ili tutekeleze Majukumu ya ujenzi wa chama.
Waheshimiwa wanahabari, Hii si mara ya kwanza Mhe Profesa kukisaidia chama Chetu. Ipo mikataba kadhaa ambayo Mwenyekiti wetu amewahi kukikopesha chama fedha zake mwenyewe.
Waheshimiwa wandishi, Ni jambo la kusikitisha kuwa kwa takribani mwaka mmoja hasa baada ya Mhe Profesa Lipumba kuwa nje ya uenyekiti wa Taifa wa CUF, Wilaya zote za Tanzania Bara zilisitishiwa Ruzuku toka Ofisi kuu wakati wilaya zote za Zanzibar zikiwa zinaendelea kupokea ruzuku. Kwa kweli huu ni uonevu mkubwa kwa wanaCUF wa Tanzania Bara na huu ni mpango wa Makusudi wa Maalim Seif na genge lake.
Baada ya kupokea Ruzuku hiyo, Tumeamua kuzipelekea ruzuku Wilaya zote za Tanzania Bara alau ruzuku ya miezi mitatu mitatu kwa kila wilaya. Mpaka sasa tumeshatuma ruzuku katika wilaya 82 ambapo Tsh. 66,300,000/= zimetumika.
Ikumbukwe kuwa Wilaya zinazotakiwa kupokea ruzuku ni wilaya zote zilizofanya uchaguzi wa ndani ya Chama ambapo Jumla ya wilaya 104 zina uongozi halali wa chama. Kwa mantiki hiyo, wilaya 22 bado hazijapewa Ruzuku kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo Akaunti zao kuwa dormat kwa muda mrefu, na nyingine kutowasilisha akaunti namba zao ofisini.
Hivyo, tunatoa wito kwa viongozi wa Wilaya zote wa CUF kwenda benki kuangalia taarifa ya fedha ya akaunti zao kisha kutupa taarifa. Lakini pia ni wajibu wao kufanya matumizi ya fedha hizo kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni ya Fedha za CUF kwa kuwa hizo ni fedha za umma.
Waheshimiwa wandishi, tumesikitishwa na tamko la inayojiita Bodi ya wadhamini ya CUF eti fedha zimeibwa na wanazuia viongozi wa wilaya wasichukue fedha zilizoko kwenye akaunti zao. Kwa mujibu wa ibara ya 98(1) nainukuu:-
“ Kutakuwa na Bodi ya wadhamini itakayoteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa mujibu wa sheria za nchi kwa kipindi cha miaka mitano (5) na mjumbe anaweza kuteuliwa tena baada ya muda kumalizika”.
Ndugu wandishi, Bodi ya CUF iliteuliwa kwa mara ya mwisho Januari 2010, hivyo ilimaliza muda wake Januari 2015. Haijawahi kuteuliwa tena na haijawahi kulipiwa Mchango wa kila mwaka RITA tangu 2013. Kutokana, sheria za nchi na katiba ya CUF, Bodi hiyo ni mfu kwa hiyo haina uwezo wa kushughulikia na kusimamia masuala yoyote ya fedha za CUF. How can a dead body talk about financial matters?.
Wakiwa wanajua ukweli huo, bado wanakubali kutumika kwa maslahi ya Maalim Seif. Hii ni kuthibitisha kuwa “Mbwa mzee hafundishwi mbinu mpya za kuwinda”. Ni kweli Maalim Seif, Bashange na Katau wamezeeka, ni sawa mbwa wazee wasioweza kutumia mbinu mpya za kujijenga kwa wanachama wa CUF bali wanazidi kujifedhehesha.
Ndevu zao ni ishara ya kupitwa na wakati. Ni bora watuachie vijana tujitanabahishe kwa mbinu za kisasa za kuiweka kweli ndani ya CUF na Watanzania kwa ujumla. Kama Maalim Seif alikuwa simba wa vita vya miaka 1980, kamwe hawezi kuwa simba wa vita ya 2016/2017. Huwezi kuwa Katibu Mkuu ambaye unapeleka Ruzuku Zanzibar kupitia Michango ya Wabunge lakini ukawa hutaki Wilaya za Tanzania Bara zipate Ruzuku. Huu ni ubaguzi uliokithiri na sisi hatutaukubali.
Tunaiomba ofisi ya Gavana wa Benki kuu kutupilia mbali ombi la Bodi ya wadhamini ya CUF isiyo halali kwa kuwa imepitwa na wakati na inakiuka hata katiba ya CUF ibara ya 98(1) na (2) inayotaka bodi iundwe na jumla ya wajumbe 9 ambapo 3 kati yao lazima wawe wanawake lakini bodi feki ya Mwalimu Seif ina wanaume watupu ndiyo maana wanailalamikia RITA eti wametoa siri za ufeki wao.
Na kama wanahisi RITA wameghushi nyaraka, waende Polisi wakafungue mashitaka dhidi ya RITA, japokuwa nalo ni jambo gumu kwao maana wao ni Bodi mfu, hawana uwezo wa kushitaki wala kushitakiwa.
Waheshimiwa wanahabari, kwa sasa Maalim Seif anamlaumu kila mtu. Anamlaumu Jaji Mutungi kwa kusema ukweli, anawalaumu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kwa kuupinga udikiteta wake Mkutanoni, anamlaumu Gavana wa Benki, anailaumu RITA, anamlaumu Jaji Kihiyo, anamlaumu Rais Shein, anamlaumu Jecha, anamlaumu Profesa Lipumba eti anakuja kuzuia asipewe urais wa Zanzibar lakini cha ajabu hajilaumu mwenyewe kwa udikiteta wake ndani ya CUF na tamaa yake ya kupenda fedha za Lowasa kuliko utu na thamani yake kwa jamii.
Mwisho, tunamtaka Mwalimu Seif na Genge lake waende kwa amani watuachie CUF yetu. Hata Mapalala ailianzisha CUF lakini alipoonekana anaisaliti aliamua kuiacha CUF kwenye mikono salama. “Yeye sasa ni Simba mzee hawezi mawindo ya wakati huu”.
Imeandaliwa na;-
Thomas D.C Malima
Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa)
Subscribe to:
Posts (Atom)
PAMOJA BLOG
WANAOTUTEMBELEA
ZINAZOSOMWA ZAIDI
-
Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tati...
-
Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi kwa kushiriki Maonesho ya...
-
Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tati...
-
Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tati...
-
Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tati...
-
WAZIRI DKT. BASHIRU AIAGIZA BODI MPYA YA TAFICO KUIGEUZA TAFICO KUWA INJINI YA UCHUMI SEKTA YA UVUVIWaziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ameitaka Bodi mpya ya pili ya Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) kuhakikis...
-
Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tati...
-
Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tati...
-
Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kutoa elimu na mafunzo kwa vyuo vikuu pamoja na shule za sekondar...
-
Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tati...
BLOGU MARAFIKI
KUMBUKUMBU
HABARI ZINGINE
MPYAA: TAZAMA HAPA MATOKEO YA DARASA LA SABA 2014
November 07, 2014








