HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

MASAUNI ATANGAZA MAJINA YA WATUHUMIWA 16 WA MAUAJI YANAYOENDELEA KIBITI, MKURANGA NA IKWIRIRI

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP), Simon Sirro, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), baada ya kufanya kikao kuhusiana na uhalifu katika maeneo ya Kibiti,Mkuranga na Ikwiriri,mkoani Pwani, ambapo Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(kushoto),alitangaza kutafutwa kwa watu 16 wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo.Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa polisi makao makuu,jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), baada ya kufanya kikao na viongozi wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi kuhusiana na uhalifu katika maeneo ya Kibiti,Mkuranga na Ikwiriri,mkoani Pwani, ambapo alitangaza kutafutwa kwa watu 16 wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo.Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP), Simon Sirro.Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa polisi makao makuu,jijini Dar es Salaam.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akionyesha baadhi ya picha za watuhumiwa wa uhalifu katika maeneo ya Kibiti,Mkuranga na Ikwiriri kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), baada ya kufanya kikao na viongozi wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi ambapo alitangaza kutafutwa kwa watu 16 wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo.Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini(IGP),Simon Sirro.Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa polisi makao makuu,jijini Dar es Salaam.

IGP Sirro afanya ziara Kibiti na Rufiji, Atangaza msako mkali

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro  jana alifanya mazungumzo na wazee pamoja na viongozi wa dini wilayani Kibiti mkoani Pwani ili kubaini waalifu wanaotekeleza mauaji ya watu wilayani humo na kusema vyovyote itakavyokuwa lazima watawarudisha kwenye msitari.

IGP Sirro alisema kupitia mazungumzo hayo tayari amepata taarifa za wahalifu hao ingawa ni mapema kuziweka wazi ila amewakikishia wananchi kuwa waalifu wao ni lazima watapatikana.

“Kubwa ni kwamba wazee wetu wa Kibiti wametueleza taarifa nyingi sana na mnavyojua hawa waalifu wanaishi ndani ya Kibiti, ndani ya Ikwiriri, kwa hiyo wazee wetu wamejaribu kutueleza ni wapi tunaweza kuwapata na chanzo cha mambo yote haya,” alisema IGP Sirro na kuongeza;

“Kwa hiyo kimsingi mambo mengine mengi ni ya kipelelezi ambayo siwezi kuyasema kwa sasa, lakini kikubwa wametupa dira, muelekeo kwa maana kwamba wale ndugu zetu au maadui zetu kwa lugha nyepesi tumepata njia nzuri ya kudeal nao. Kwa hiyo nitume salamu kwao kwamba waendelee kukimbia lakini njia ya muongo ni fupi na mwisho wa siku tutawarudisha kwenye mstari"

UPDATES: RAIS MAGUFULI AMTEUA KAMANDA SIMON SIRRO KUWA IGP


Wafanyakazi wa Mochwari Watiwa Mbaroni kwa Kuiba Kete 32 za Dawa za Kulevya

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro amefunguka kuwa wahudumu wa mochwari ya Mwananyamala wameiba jumla ya kete 32 za dawa za kulevya zilizokuwa kwenye mwili wa Raia wa Ghana aliyefariki dunia akiwa katika nyumba ya wageni.

Kamanda Sirro amesema wahudumu hao wanne wote wamekamatwa na kukiri kwamba  baada ya kifo cha raia huyo wa Ghana aliyefariki ndani ya 'Red Carpet' iliyopo Sinza Dar es Salaam walipasua mwili wa raia huyo na kutoa kete hizo kisha kuziuza, na kuongeza wametaja watu ambao wamewauzia ambao nao wamekamatwa na wapo chini ya ulinzi wa polisi

"Yule Mghana ambaye alikutwa amefariki dunia tarehe 14/ 03/ 2017 kwenye nyumba ya wageni ya 'Red Carpet' na alichukuliwa na kupelekwa mochwari Mwananyamala lakini inaonekana wale wahudumu wali[pata taarifa kuwa ule mwili una dawa za kulevya, kimsingi walikula njama wakampasua na kutoa kete 32 za madawa ya kulevya na baada ya kuyapata waliyauza hayo madawa" alisema Sirro

Kamanda Sirro aliendelea kusema kuwa mpaka sasa wanawashikilia watu wanne ambayo wamehusika katika jambo hilo.

"Mpaka sasa tunawashikilia watu wanne ambao wanakiri kupasua mwili huo ambao ni wahusika wakuu na ni wahudumu wa mochwari ya Mwananyamala lakini tumekwenda mbali zaidi baada ya kufanya upasuaji wamemuuzia nani naye amekatwa pia na anaeleza kuwa alinunua hayo madawa, lakini pia naye alichukua na kumuuzia mtu mwingine anayefahamika kwa jina la Ally Nyundo, huyu Nyundo tulishamkataga na kumpeleka kwa Mkemia Mkuu yeye alionekana ni mtumiaji, kimsingi tuna hao watuhumiwa wanne na huyo wa tano aliyekamatwa sasa tunaandaa jalada" alisisitiza Sirro

Jeshi la Polisi Lasema Linawashikilia Watu 3 Kwa Kuvamia Mkutano wa CUF na Kuwapiga Watu

Saa  tatu baada ya viongozi wa CUF kukutana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuhoji sababu za kutokamatwa watu waliofanya vurugu kwenye mkutano wa waandishi wa habari na viongozi wa chama hicho wa wilaya ya Kinondoni, Jeshi la Polisi limetangaza kushikilia watu watatu.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho Julius Mtatiro, viongozi hao waliwaeleza wanahabari kuwa ni ajabu kuona  Polisi haijachukua hatua huku ikijulikana wazi kuwa watu hao walijeruhi wanahabari na viongozi wa chama hicho katika tukio ambalo liliripotiwa na vyombo vya habari.

Viongozi hao walikutana na Sirro jana saa 5 asubuhi na kuzungumza kwa takribani saa moja, na kisha saa 8 mchana Kamanda huyo alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kukamatwa kwa watu hao, wakituhumiwa kuhusika katika tukio hilo.

Jumamosi iliyopita takribani watu watano wakiwa kwenye gari lenye nembo na bendera za CUF, walivamia mkutano huo uliokuwa ukifanyika kwenye hoteli ya Vinna, Mabibo wilayani Kinondoni na kufanya vurugu.

Miongoni mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso kininja alichomoa bastola na kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na wenzake, jambo lililosababisha wananchi wamzingire na kumshushia kipigo.

Katika ufafanuzi wake, Mtatiro alisema tukio hilo ni la 13 dhidi ya upande unaomwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad lakini vyombo vya Dola viko kimya.

“Baada ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa kimya ili kuona kama polisi watasema chochote ila imekuwa tofauti. Wako kimya tu,” alisema Mtatiro.

Akieleza kilichowapeleka kituoni hapo, alisema: “Tulitaka kujua yule mvamizi aliyekuwa na bastola mpaka sasa yuko wapi. Mvamizi mmoja tunajua alikamatwa na wananchi, akapigwa kidogo na kuokolewa. Tulitaka kujua alitoa maelezo gani.”

Alisema baada ya tukio hilo, Mkuu wa Upelelezi aliwapigia simu viongozi waliovamiwa akiomba waende kituo cha Polisi Magomeni  wakapatanishwe.

“Tulishangazwa na taarifa hiyo, kwa watu waliovamiwa kwenda kupatanishwa. Tulijihoji kama Jeshi la Polisi linaweza kupatanisha watu wenye makosa ya jinai, kwani mtu wa makosa hayo upelelezi unapokamilika hupelekwa mahakamani,” alisema Mtatiro.

Alisema sababu nyingine ya kwenda kituoni hapo ni kutaka kufahamu kama watu wanaofanya matukio hayo wako juu ya sheria.

“Tulimwonya Kamanda Sirro kwamba sisi (upande wa Maalim) tuna nguvu kuliko Lipumba na kuiomba Polisi kutekeleza majukumu yake kwa kuchukua hatua dhidi ya wavamizi hao,” alisema.

Katika mkutano wake na wanahabari, Sirro alisema Polisi inashikilia watu watatu wakituhumiwa kufanya vurugu kwenye mkutano huo.

“Tulipata taarifa ya kuvamiwa kwa mkutano wa wanachama wa CUF na watu wasiofahamika wakiwa na silaha. Baada ya taarifa hizo kupokewa askari walifuatilia na kukamata watu watatu,” alisema Sirro.

Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitafuatwa.

Alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa waliohusika watasakwa kokote watakokuwa.

KAMANDA SIRRO AWATAKA WANANCHI KUTOJICHUKULIA SHERIA MIKONONI

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Simon Sirro amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi badala yake waviachie vyombo husika ili viweze kufanya kazi yake.

Ameyasema hayo Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari. Amesema kuwa wananchi kujichukulia sheria mikononi pindi wawakamatapo watuhumiwa ni kinyume cha sheria hivyo wanatakiwa kuacha mara moja tabia hiyo.

“Ni vyema wananchi wakaacha  tabia ya kujichukulia sheria mikononi ili vyombo usika vifanye kazi yake,”amesema Sirro.

Aidha, amesema kuwa wananchi kuwauwa watuhumiwa ni kosa kisheria kwani watakao bainika kufanya hivyo sheria kali dhidi yao zitachukuliwa.

Hata hivyo, ameongeza kuwa ni bora wananchi waache tabia hiyo ya kujichukulia sheria mikononi kwani vyombo husika kama Polisi na Mahakama vipo kwa ajili ya shughuli hiyo.

SIRRO: MBOWE ASIPORIPOTI TUTAMFUATA

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limesema kama Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe hataripoti bila kutoa taarifa yoyote ya hudhuru atafuatwa kwa kuwa jeshi hilo linahitaji kumhoji.
Kamanda wa kanda hiyo, Simon Sirro amesema hayo leo muda mfupi baada ya Mbowe kueleza kuwa hataripoti polisi kutokana na wito wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Pia Sirro amesema askofu wa kanisa la ufufuo na uzima Josephat Gwajima na mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji walilala polisi kwa kuwa bado upelelezi dhidi yao unaendelea..
"Oparesheni ya dawa za kulevya bado inaendelea na kuanzia sasa hatutaruhusu mkusanyiko wa wananchi karibu na kituo cha polisi hiki watakaoonekana watashughulikiwa na asije akalaumiwa Kamishina Sirro kwa kuwa tayari nimeshatoa taarifa."

Chanzo: Mwananchi

MSAKO DAR WANASA WATUHUMIWA 590

Ndugu wasomaji wetu tunaomba support yenu kwa kutangaza nasi hapa kwenye hii blog kwa bei nafuu ili tuweze kuendelea kutoa habari bila tatizo lolote. Wasiliana nasi kupitia namba +255713363965 / +255755274953. Tunashukuru kwa ushirikiano wenu.


JESHI la Polisi katika Kanda Maalumu Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa 586 kwa makosa mbalimbali katika msako uliofanyika kwa siku kumi kuanzia Novemba 22 mwaka huu.

Hayo yalisemwa jijini humo na Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro.

Alisema watuhumiwa hao wamekamatwa maeneo mbalimbali kwa nyakati tofauti kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu, kuvunja nyumba usiku na kuiba, wizi kutoka maungoni, kucheza kamari, kubughudhi abiria, wizi wa magari, shambulio la aibu na la kawaida, kutengeneza, kuuza na kunywa pombe haramu ya gongo pamoja na uvutaji bangi.

Aliongeza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa baada ya operesheni iliyofanyika maeneo ya Buguruni na Magomeni ambapo walikamatwa jumla ya watuhumiwa 257, walikamatwa kwa makosa mbalimbali na jumla ya lita 405 za Pombe haramu za gongo zilikamatwa, mitambo miwili ya kutengenezea gongo na bangi.

Kamanda Sirro alisema baadhi ya watuhumiwa hao walikutwa na silaha ndogo ndogo za kufanyia uhalifu kama visu, nyembe, bisibisi. Katika tukio jingine , Polisi Kanda Maalum Dar es salaam kupitia kikosi kazi cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha, mnamo Novemba 29, mwaka huu majira ya saa nne na nusu Kijichi Neluka Mbagala lilifanikiwa kukamata gari lililobeba mali za wizi.

Sirro alisema gari hilo lilikamatwa baada ya majambazi watatu wakiwa na gari Toyota Noah lenye rangi ya fedha lililosajiliwa kwa namba za usajili T 129 DDS, kuvamia baa moja inayofahamika kwa jina la Whatsapp na kuvunja, kisha kuiba vitu mbalimbali vikiwemo seti ya televisheni aina ya Samsung, king’amuzi kimoja cha startimes kimoja, radio moja, spikambili aina ya Sony, na katoni tatu za glasi.