HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

KAMATI YA KUDUMU YA UTAWALA NA SERIKALI ZA MITAA KUTOKA BUNGE LA MSUMBIJI YATEMBELEA OFISI ZA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI JIJINI DAR ES SALAAM

 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) Jaji (R) Mhe. Semistocles Kaijage (kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa ya Bunge la Msumbiji, Mhe. Lucas Chomera Jeremiah (kushoto) Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015 wakati Kamati hiyo ilipotembelea Ofisi za Tume leo jijini Dar es salaam.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R) Mhe. Semistocles Kaijage (katikati) akitoa ufafanuzi kuhusu majukumu ya Tume kwa  Wabunge wa Bunge la Msumbiji ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa waliotembelea Ofisi za NEC jijini Dar es salaam kujifunza namna Tume hiyo inavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Lucas Chomera Jeremiah na Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Bw. Hamis Mkunga.


Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Emmanuel Kawishe (kushoto) akiwaeleza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa ya Bunge la Msumbiji namna Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania inavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa ya Bunge la Msumbiji, Mhe. Lucas Chomera Jeremiah (kushoto) akifafanua jambo wakati wa kikao cha Wajumbe wa Kamati hiyo kutoka Msumbiji na watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania leo jijini Dar es salaam, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa ya Bunge la Msumbiji wamezitembelea Ofisi za NEC kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala ya Uchaguzi.Kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage.

 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) Jaji (R) Mhe. Semistocles Kaijage (Kulia) akisalimiana na Wabunge wa Bunge la Msumbiji na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa wa nchi hiyo waliotembelea Ofisi za NEC kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu uendeshaji wa chaguzi mbalimbali.

NEC yaanza kutekeleza mpango wa Elimu ya Mpiga Kura kupitia Redio

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani akitoa elimu ya mpiga kura kupitia redio A FM ya mkoani Dodoma leo Mei 9 mwaka huu huku akifuatiliwa kwa makini na watangazaji wa redio hiyo.

Hussein Makame, NEC 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa wito kwa wananchi walioko kwenye halmashauri mbalimbali nchini, kuitumia vyema fursa ya utoaji wa elimu ya mpiga kura kupitia redio za kijamii kwenye halmashauri zao ili kuondoa manung’uniko kwenye chaguzi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Bw. Kailima Ramadhani wakati akizungumzia mpango wa kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima ulioanza kutekelezwa Mei 8 mwaka huu hii katika mikoa kumi nchini.
Alisema kupitia mpango huo wananchi wanaosikiliza redio za kijamii kwenye halmashauri nchini, watapata fursa ya kujifunza elimu ya mpiga kura na kuelewa masuala yote muhimu yanayohusu mfumo mzima wa kupiga kura. 

“Tumepanga mpango, Tume itasambaa nchi nzima kuzungumzia elimu ya mpiga kura kwenye redio za kijamii zilizoko kwenye halmashauri zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” alisema Bw. Kailima.

Alisisitiza kwa kutoa wito kwa wananchi walioko maeneo ambayo Tume itakwenda kutoa elimu ya mpiga kura, wasikilize na kuuliza maswali ili waweze kuelewa.

“Hii ni fursa kwa wananchi ambayo muda mrefu hawajawahi kuipata, hivyo nawaomba wafuatilie ili waweze kuelimika zaidi ili yale manung’uniko ya kura yatakuwa yamekwisha na tutakuwa na uchaguzi mzuri zaidi ya ile ambayo tumeifanya.” Alifafanua Bw. Kailima.

Utekelezaji wa mpango huo umegawanyika katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza limeanza kutoa elimu hiyo elimu hiyo kwenye mikoa ya Kagera,Mwanza, Kilimanjaro, Morogoro, Mbeya na Dodoma.

Mikoa mingine itakayojumuishwa kwenye kundi hilo ni Ruvuma, Mara, Pwani na Mtwara ambapo elimu hiyo itatolewa kuanzia tarehe 8 Mei hadi tarehe 20 Mei mwaka 2017.

Kundi la pili linatarajiwa kutoa elimu hiyo kuanzia tarehe 24 Mei hadi tarehe 7 Juni mwaka huu katika mikoa ya Geita, Tanga, Singida, Shinyanga, Lindi, Arusha, Tabora, Kigoma, Iringa, Manyara, Rukwa, Katavi, Songwe, Njombe na Simiyu.

Bw. Kailima alisema kuwa utoaji wa elimu hiyo utajikita kwenye mada kuu ya Elimu ya Mpiga Kura iliyogawanywa kwenye vipindi vitano, itakaytoolewa kwenye redio hizo kulingana mada husika na wananchi kuuliza maswali na kujibiwa na wawasilishaji wa mada hizo kutoka Tume.

“Ni mada ambayo imejumuisha masuala yote muhumu yatakayofanya mpiga kura yeyote au mdau yeyote wa uchaguzi kuisoma au kuisikiliza na akaelewa mfumo mzima wa masuala ya kupiga kura” alisema.

Mbali na kutoa elimu ya mpiga kura kupitia vituo vya redio za kijamii katika halmashauri nchi nzima, Tume pia inatoa elimu hiyo kwa njia ya magazeti na vyombo vingine vya habari na mitandao ya kijamii, kushiriki kwenye mikutano na maonesho mbalimbali nchini.

NEC YATOA UFAFANUZI UTARATIBU WA KUMPATA MBUNGE NA DIWANI VITI MAALUM.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeeleza kuwa nafasi za Wabunge wa Viti Maalum wanaoteuliwa zipo kwa mujibu wa Sheria na zimeainishwa katika  Ibara ya 78 (1) na (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Akitoa ufafanuzi huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani amesema kuwa Ibara ya 78 (1) na (4) ya Katiba inaeleza utaratibu mzima wa kuwapata Wabunge wanawake wa Viti maalum.

Amesema  kila Chama cha Siasa kinachoshiriki katika Uchaguzi Mkuu na kupata angalau asilimia 5 ya Kura zote halali za wabunge kitapata Wabunge wa Viti Maalum kulingana na Kura ambazo chama husika kimepata. 

Amefafanua kuwa Chama kinachopata asilimia 5 ya Kura zote halali za Wabunge katika Uchaguzi Mkuu kinatakiwa kuwasilisha orodha ya wanachama wanaopendekezwa kuwa wagombea wa Viti Maalum ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Aidha, ameeleza kuwa endapo inatokea nafasi wazi ya Mbunge wa Viti Maalum katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na sababu mbalimbali, Spika wa Bunge humtaarifu Mwenyekiti wa Tume juu ya uwepo wa nafasi hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Amesema kuwa  Mwenyekiti wa Tume hukiandikia barua chama husika kukitaarifu juu ya uwepo wa nafasi wazi ya viti maalum ili kiweze kuwasilisha pendekezo la jina katika orodha kiliyowasilishwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi mwaka 2015,  ikiambatanishwa na Fomu namba 8 D ya kuomba jina lililopendekezwa  liteuliwe na Tume katika nafasi ya Ubunge kulingana na sifa zilizoainishwa kwa mujibu wa Sheria.

NEC YATANGAZA NAFASI WAZI YA KITI CHA MBUNGE WA VITI MAALUM CHADEMA MHE. DR. ELLY MARKO MACHA

  Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kuwepo kwa nafasi wazi ya Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA,  kufuatia kifo cha Mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho Mhe. Dr. Elly Marko Macha aliyefariki tarehe 31 Machi 2017.

Akitoa taarifa ya nafasi hiyo kuwa wazi Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage amesema kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameijulisha Tume juu ya kuwepo kwa nafasi wazi ya Mbunge huyo.

Amesema taratibu za kujaza nafasi hiyo zinaendelea kwa kuzingatia Ibara ya 78 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

VIDEO : TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI YAFAFANUA HATMA YA UBUNGE WA SOPHIA SIMBA LEO


Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kuutarifu Umma kuwa; kwa mujibu wa Kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemjulisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa; kufuatia Mbunge wa Viti Maalum, SOPHIA MNYAMBI SIMBA kufukuzwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi tarehe 11 Machi, 2017 kiti cha Mbunge huyo wa Viti Maalum Wanawake kwa tiketi ya CCM kiko wazi.

Kwa mujibu wa Ibara ya 67 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ili mtu ateuliwe au achaguliwe katika nafasi ya Ubunge ni lazima awe mwanachama aliyependekezwa na Chama chake husika cha Siasa.

Kwa kuwa Ndg. SOPHIA MNYAMBI SIMBA amefukuzwa uanachama wa Chama kilichomdhamini, Ibara ya 67 (2) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaelekeza kuwa Mbunge huyo amepoteza sifa za kuteuliwa au kugombea Ubunge.

Kutokana na kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge wa Viti Maalum, taratibu za kujaza nafasi hiyo zinaendelea kwa kuzingatia kifungu cha 86A (8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Jaji (R) Semistocles Simon Kaijage
Mwenyekiti
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI
12 Aprili, 2017

NEC: KUIZUIA KADI YA KUPIGIA KURA YA MTU MWINGINE NI KINYUME CHA SHERIA

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji (R) Semistocles Kaijage (kulia) akisalimiana na mwenyeji wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Jaji Richard Kibela baada ya mwenyeji wake kumpokea wakati akiwasili mkoani Shinyanya kutoa Elimu ya Mpiga Kura mkoani humo.Kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kanda ya Shinyanga Sekela Mwaiseje.


Hussein Makame, NEC aliyekuwa Bukoba
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewatahadharisha watu wanaochukua kadi za kupigia kura za wenzao na kuzizuilia au kubaki nazo kuwa ni kinyume cha Sheria.

Hayo yamesema na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe wakati akitoa elimu ya mpiga kura katika halmashauri ya manispaa ya Bukoba na Shinyanga hivi karibuni.

Alisema kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinasema kuwa ni kosa la jinai kwa mtu kuchukua kadi ya mpiga kura mwingine na kuiziulia, kukataa kuirudisha au kubaki nayo kwa uzembe.
Bw. Kawishe alifafanua kuwa kumekuwa na malalamiko kwamba inapofikia karibu na kipindi cha uchaguzi, baadhi ya watu wanachukua kadi za wapiga kura wengine na kuzizuia kinyume cha Sheria.

Hata, hivyo alisema kutokana na kutoa elimu ya mpiga kura kupitia mikutano na kuhudhuria maonesho mbalimbali, baadhi ya wananchi wameelewa umuhimu wa kadi hizo na kuahidi kutoampa mtu kadi zao za kupigia kura.

“Kwa hiyo katika jambo hilo tumekuwa na mrejesho ambo ni chanya lakini tunachowaomba ukiandikishwa tunza kadi yako ya mpigia kura” alisema Bw. Kawishe na kuongeza kuwa; “Jambo la pili mwananchi usikubali mtu achukue kadi yako ya mpigia kura na wala usitumie kadi yako ya mpiga kura kwenye kuchukulia dhamana sehemu yoyote”
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Tiafa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe, akisamiliana na Mkurugenzi wa Halamashauri ya Manispaa ya Shinyanga Bw. Geofrey Ramadhani Mwangulumbi baada ya kuwasili kwenye Halmashauri hiyo kutoa Elimu ya Mpiga kura.

“Kwa sababu itakwenda kuchukulia dhamana alafu utashindwa kwenda kupiga kura unapofika wakati wa kupiga kura, mwananchi ajue kwamba kupiga kura ni haki yake” Alisema mtu aliyejiandikisha asipokwenda kupiga kura anakosa haki ya kuchagua kiongozi anayemtaka na badala yake anawaacha wenzako wakuchagulie kiongozi.

“Unaacha kupiga kura alafu baadaye anakuja kulalamika unasema huyu kiongozi simtaki kumbe kura moja inatosha kubadilisha matokeo ya eneo zima” alisema.

Hivyo aliwasihi wananchi waendelee kuzingatia amani katika uchaguzi na kuwashukuru kwa jinsi uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na uchaguzi mdogo uliofanyika Januari 22 mwaka huu kwa jinsi ulivyokuwa na amani na utulivu.

”Kwa kweli Watanzania tutambue kuwa amani ni yetu sisi sote na sisi ndio tutakaoilinda hiyo amani tuiweke Tanzania yetu kwanza alafu sisi baadaye” aliwakumbusha Watanzania.

Akijibu swali la mmoja wa wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Bukoba aliyehoji anayepoteza kadi ya mpiga kura anachukuliwa hatua gani kumuwajibisha, Bw. Kawishe alisema hakuna hatua yoyote inayochukuliwa dhidi yake.

Alifafanua kuwa wale wote wanaopoteza kadi ya mpiga kura wanatakiwa wafike kwenye kituo cha uboreshaji wa daftari la wapiga kura na kujieleza na watapatiwa kadi nyingine.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Tiafa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe, akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro wakati alipomtembelea ofisini kwake mkoani humo.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe akitoa Elimu ya Mpiga kura kupitia Kituo cha redio Faraja Fm cha mkoani Shinyanga mwishoni mwa wiki hii.Kulia kwake ni mtangazaji wa redio hiyo Faustin Kasala.
Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Tiafa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe, akitoa Elimu ya Mpiga kura kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Old Shinyanga iliyopo manispaa ya Shinyanga. Picha na Hussein Makame, NEC

MWENYEKITI MSTAAFU WA NEC AKABIDHI TAARIFA YA UTENDAJI WAKE WA KAZI WA MIAKA 5 KWA MWENYEKITI MPYA

Mwenyekiti Mstaafu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Damian Lubuva (kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa sasa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage (kushoto) taarifa ya utendaji Kazi wake kwa kipindi miaka 5 alichokuwa madarakani.
Mwenyekiti Mstaafu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva akizungumza na Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Sekretarieti ya Tume hiyo mara baada ya kukabidhi taarifa ya utendaji Kazi wake kwa kipindi miaka 5 alichokuwa madarakani.
Mwenyekiti wa sasa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage akizungumza na Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Sekretarieti ya Tume hiyo mara kupokea taarifa ya utendaji Kazi wa Mwenyekiti Mstaafu wa Tume hiyo Jaji Damiani Lubuva jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Ramadhan Kailima akizungumza jambo wakati wa makabidhiano hayo jijini Dar es salaam.Katikati ni Mwenyekiti Mstaafu wa Tume Jaji Mstaafu Damian Lubuva na Kulia ni Mwenyekiti wa Sasa wa NEC, Jaji wa Rufaa, Semistocles Kaijage.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti Mstaafu wa Tume Jaji Damiani Lubuva , Wajumbe wa Tume na Secretarieti ya Tume hiyo.

Picha na Aron Msigwa - NEC.

WANANCHI JIMBO LA DIMANI, ZANZIBAR WAPIGA KURA KWA AMANI NA UTULIVU

Wananchi wakiangalia majina yao kabla ya kupiga kura katika kituo cha Bweleo katika jimbo la Dimani leo.


Hatimaye wananchi wa Jimbo la Dimani visiwani Zanzibar waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Mpiga leo wamejitokeza kwa wingi katika vituo mbalimbali kupiga kura kumchagua Mbunge atakayewawakilisha kwa kipindi cha miaka miaka 4.

Zoezi la upigaji wa Kura katika vituo mbalimbali lilianza majira ya saa 1 asubuhi  likifanyika kwa hali ya Amani na Utulivu huku baadhi ya wananchi waliojitokeza kupiga kura wakipongeza maandalizi mazuri yaliyofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzine (NEC)  kufanikisha Uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa, Mhe. Semistocles Kaijage akizungumza kuhusu mwenendo wa Uchaguzi huo mara baada ya kutembelea vituo  vya kupigia kura katika jimbo hilo na  kuzungumza  na Mawakala wa Vyama vya Siasa waliokuwepo vituoni, Waangalizi wa Uchaguzi na Wasimamizi wa Uchaguzi  huo amesema Tume imeridhishwa na kazi nzuri  iliyokuwa ikiendelea katika vituo mbalimbali vya kupigia Kura. 
“ Viongozi wa Tume tumetembelea vituo mbalimbali vya kupigia Kura katika jimbo la Dimani; tumeona wenyewe upigaji wa Kura unaendelea vizuri, tumewauliza Mawakala, Watazamaji na Wasimamizi wa Vituo vya Uchaguzi  kila mmoja amesema Uchaguzi unakwenda vizuri, nachoweza kuwaambia watanzania Uchaguzi Dimani unakwenda Vizuri” Amesema Jaji Kaijage.

Amesema Wasimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo hilo wanaendelea kufanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili pia kushughulikia kwa haraka changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika  baadhi ya vituo vya kupigia Kura.

Ameeleza kuwa zoezi zima la upigaji wa Kura linaendeshwa kwa uwazi mkubwa, Utulivu na Amani na kuwawezesha wananchi kupiga kura bila vikwazo vyovyote.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage (Katikati) akizungumza na Msimamizi kituo cha Dimani Bi. Abdu Simai Haji leo wakati zoezi la upigaji kura likiendelea katika jimbo la Dimani.

Aidha, Mhe. Kaijage amebainisha kwamba endapo yatajitokeza malalamiko yoyote wakati zoezi la upigaji wa Kura likiendelea katika vituo mbalimbali , Mawakala wa Vyama vya Siasa ambao ni wasimamizi wa Maslahi ya Wagombea na Vyama vyao Vituoni watajaza fomu  ya malalamiko  Na. 14 kwa mujibu wa Sheria ambayo inatoa fursa ya kushughulikiwa kwa malalamiko hayo.

Aidha, amebainisha kuwa mara baada ya zoezi la upigaji wa kura kumalizika leo saa 10 jioni kazi ya kuhesabu Kura itafuata ili hatimaye wamnanchi wa Jimbo la Dimani waweze kupatiwa matokeo ya maamuzi waliyoyafanya kupitia Kura zao.

Mhe. Kaijage amesisitiza kuwa Wasimamizi wote wa Uchaguzi huo wamepewa mafunzo ya kuzingatia ili kuhakikisha wanaendesha zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa na kuwezesha matokeo kutangazwa kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kumjua mshindi wa Uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage (wa pili) akiwa ameambatana na Baadhi ya Watendaji wa NEC na Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Bi. Idaya Selemani Hamza (wa Kwanza) akiwasili katika kituo cha Kupigia Kura cha Kombeni katika jimbo la Dimani kuangalia maendeleo ya Upigaji wa Kura leo.

“ Endapo taratibu zote za Uchaguzi zitakuwa zimekamilika kwa mujibu wa Sheria, hakutakuwa na sababu yoyote ya kuchelewesha matokeo,mpaka sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi tumeridhishwa na mwenendo mzima wa zoezi la upigaji wa Kura na matokeo yatatolewa kwa wakati” Amesisitiza.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe akizungumzia zoezi la Upigaji wa Kura amesema kuwa Wapiga Kura wanaoruhusiwa kupiga kura ni wale waliokidhi Sifa na Vigezo vilivyoainishwa kisheria kuwawezesha kupiga Kura.

Amesema  kwa mujibu wa Sheria Msimamizi wa Kituo ndiye mwenye mamlaka ya maamuzi katika kituo cha kupigia Kura ikiwa ni pamoja na kuamuru kuondolewa kwa mtu yeyote atakayeonekana kufanya fujo au kuzuia zoezi la uchaguzi kuendelea kituoni.

Katika Uchaguzi Uchaguzi huo mdogo wa Ubunge wa jimbo la Dimani jumla ya Wapiga Kura 9,280 wanatarajiwa Kupiga kura katika Vituo 29 huku vyama vya Siasa vyenye wagombea vinavyoshiriki Uchaguzi huo ni 11 huku Waangalizi wa Uchaguzi waliojitokeza kushiriki katika Uchaguzi huo ni zaidi ya 300.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage (Katikati) akizungumza na waandishi wa Habari wa Zanzibar kutoa tathmini ya hali ya Uchaguzi mara baada ya kuetembelea vituo mbalimbali vya kupigia kura katika jimbo la Dimani leo.
Baadhi ya Wangalizi wa Uchaguzi katika jimbo la Dimani wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Dimani leo.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Rufaa Mhe. Semistocles Kaijage (Kushoto) akizungumza na Mawakala wa Vyama vya Siasa waliokuwepo ndani ya kituo cha kupigia Kura cha Kombeni katika jimbo la Dimani leo. Wengine wanaochukua taarifa ni Watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Mmoja wa Wananchi katika jimbo la Dimani akipiga Kura yake kumchagua Mbunge katika jimbo la Dimani leo. Picha na Aron Msigwa –NEC.