HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

Yussuf Manji Ajiuzulu Uenyekiti Club ya Yanga

Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji amejiuzulu wadhifa  huo akidai kuwa anatoa nafasi kwa watu wengine kuiongoza.

Kupitia barua yake, Manji amesema kuwa anaondoka akiamini ameiacha Yanga ikiwa timu yenye mafanikio kisoka nchini.

"Muda wangu wa kutangaza kuwa ninakaa pembeni kutoka kwenye nafasi ya uenyekiti ni sasa. Tayari tumekuwa mabingwa watetezi mashindano tena tuna kizuri cha wachezaji na makocha. Tumeungana kwa pamoja haijawahi kutokea, " imesema sehemu ya barua hiyo.

Akizungumza kwenye kipindi cha Sports Headquarters kinachoendeshwa na kituo cha radio cha EFM, Manji amekiri kujiuzulu.

"Hiyo taarifa ni sahihi na sababu za kujiuzulu zipo humo, " amejibu Manji kwa kifupi.

Kwa mujibu wa barua ya Manji iliyoisaini Mei 22, inasema amejiuzuru uenyekiti na sasa majukumu yote hadi pale uchaguzi mpya utakapofanyika wa kujaza nafasi yake majukumu yote ya timu yatakuwa chini ya Makamu wa Rais, Sanga.
 
Sanga alithibisha kupokea barua ya Manji kujizuru akisema ni kweli nimepokea barua ya mwenyekiti juu ya uamuzi wake wa kupumzika kwa sasa.
 
Katika barua Manji aliisema huwa kunafika muda tukiwa tunafuata wito fulani, wakati mimi nikiwa sehemu ya Yanga ilinibidi nijitokeze mbele kwa ajili ya umoja wa klabu yetu tuipendayo na kuongoza. Kulikuwa na wanachama waliokuwa wakigombana, ndipo ilikuwa muda wangu wa kutoa msaada kwa Yanga.
 
"Sisi sote ni sehemu ya ukoo mkubwa wa Yanga na ukweli mnaufahamu, imani ndiyo jambo ambalo tulilihitaji ndani ya Yanga kuturudisha katika mwelekeo sahihi wa miaka 11 iliyopita."
 
Taarifa hiyo iliendelea kusema "Kama Mungu alivyotuonyesha kwa kubadili jiwe kuwa mkata, hivyo msaada wangu kwa uwezo wa neema zake, naamini ulifanya mabadiliko chanya na klabu iko imara na huru. Lakini umefikia wakati wangu wa kuachia wengine na wengeni wasifikirie nilikuwa kiongozi aliyetaka cheo chochote au umashuhuri, ila ni upendo uliomgusa kuitumikia Yanga yetu. Pamoja tulifanikiwa mengi sana, na kuandika historia ndani ya Yanga na nilipolea baraka zenu mimi binafsi na familia yanga kupitia furaha japo ndogo, iliyoweza kuwaletea, ambao ninawashukuru sana.
 
"Nilisema tangu mwaka 2014, kuwa sitagombea katika uchaguzi wa uongozi kwenye nafasi yoyote ndani ya klabu na nikaonyesha mfano kuwa klabu yetu siyo mtu mmoja ila ni yetu sote, na uongozi ni lazima utoke kutoka kwenye kizazi kimoja kwenda kingine.
 
Iliongeza taarifa hiyo kuwa "Lakini mwaka jana tulikuwa katika mashindano ya mabara na kuacha pengo isingekuwa sahihi, hivyo kinyume na msimamo wangu niligombea uenyekiti wa Yanga na kupata ushindi bila ya kupigwa, lakini kama nikiendelea, nitakuwa ninaonyesha mfano upi kwa watoto wetu ambao wanaipenda Yanga kwa sababu yetu? Kwani Yanga siyo klabu yao kama ilivyokuwa yenu na mimi?"
 
Muda wangu wa kutangaza kuwa ninakaa pembeni kutoka kwenye nafasi ya mwenyekiti wa Yanga ni sasa, tayari tumekuwa mabingwa wa mashindano tena, tuna kikosi kizuri na wachezaji na makocha, tumeungana kwa umoja haijawahi kutokea, tumerudisha heshima ya kuwa washindano wa ukweli katika klabu Afrika, na kuwa imara zaidi kiuchumi na mkataba wa ufadhili  ya Sportspesa.
 
Nafahamukuwa bado kuna mengi yanayohitajika kutimizwa, lakini barabar ya mambo yanayotakiwa kutimizwa haiwezi kuisha, na siwezi kuwa mroho wa kuamini kuwa ni mimi pekee nitakayeweza kutufikisha mwisho wa safari.
 
Muda wangu kama mwenyekiti wa klabu yetu ulikuwa umeongezwa tu na haikumaanisha katika demokrasi yetu uwe ni ule usiokuwa na kikomo.

SERIKALI YAKANA KUMSHIKILIA YUSUF MANJI

Sakata la kushikiliwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Yusufu Manji limeendelea kuchukua sura mpya, safari hii yakiibuka mabishano Mahakama Kuu baada ya Serikali kukana kumshikilia.

Mabishano hayo yameibuka jana kati ya mawakili wa Serikali na mawakili wa Manji baada ya mfanyabiashara huyo kufungua maombi juma lililopita akihoji uhalali wa kushikiliwa na Uhamiaji.

Manji aliyefungua maombi hayo mahakamani hapo kupitia Wakili wake Hudson Ndusyepo, anaiomba mahakama iiagize Uhamiaji afikishwe mahakamani ili mahakama iamue uhalali wa kushikiliwa kwake na kisha iamuru aachiwe huru.

Kutokana na maombi hayo, Jaji Ama-Isario Munisi, aliwaamuru wajibu maombi kuwasilisha hati zao za kiapo kinzani dhidi ya maombi hayo na kupanga kuyasikiliza jana mchana.

Wajibu maombi ni Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam.

Hata hivyo jana Serikali katika majibu yake kupitia  hati ya kiapo kinzani cha Ofisa Uhamiaji, Anorld Munuo, ilikana kumshikilia mfanyabiashara huyo. Mbali na kiapo hicho, Wakili Mkuu wa Serikali, Oswald Tibabyekoma, alisisitiza kuwa mfanyabiashara huyo hashikiliwi na yuko huru.

Maelezo hayo ya Serikali yalipingwa vikali na mawakili wa Manji, Alex Mgongolwa na Hudson Ndusyepo, ambao kwa nyakati tofauti walisisitiza kuwa hadi jana mfanyabiashara huyo alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, kwa matibabu, akiwa chini ya ulinzi wa maafisa Uhamiaji.

AFYA YA MANJI YAANZA KUIMALIKA

Taarifa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikolazwa zinasema hawezi kuruhusiwa kwa sasa.
Msemaji wa JKCI, Anna Nkinda alisema jana kuwa baada ya vipimo, madaktari wameshauri aendelee na mapumziko mpaka watakapoona inafaa kumruhusu.
Mkurugenzi wa Tiba wa JKCI, Dk Peter Kisenge alisema mgonjwa huyo anahitaji vipimo zaidi hivyo ataendelea kubaki katika hospitali hiyo.
Wiki iliyopita, Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Msumule aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kumtaka kuripoti katika idara hiyo kwa madai kwamba kampuni yake imeajiri wageni 25 wasiokuwa na vibali halali vya kuishi nchini.
Katika mkutano huo Msumule alisema, “Tumekamata pasipoti 126, tumechambua pasipoti 25 hawana vibali vya kufanyia kazi, kwa hiyo wanafanya kazi kinyume na taratibu. Wote hawa hatua zitachukuliwa watapelekwa mahakamani.
“Lakini niseme ukweli, hawa hawatapelekwa peke yao mahakamani, lazima Yusuf Manji ambaye ndiye mwajiri wa watu hawa, ambaye ndiye mmiliki wa kampuni hii lazima afikishwe mahakamani kujibu shtaka la kuajiri wageni wasio na vibali,” alisema.
“Jana ilikuwa tumkamate alale mahabusu na leo tumpeleke mahakamani, bahati mbaya wakati tunafanya zoezi la kwenda kumkamata tukapewa taarifa kwamba amelazwa hospitalini hadi sasa. Mara tu akitoka aripoti haraka ofisi hii ili tumuunganishe kwenye kesi hii ya kuajiri watu wasio na vibali.”
Hata hivyo, katika tangazo lililotoka katika gazeti la The Citizen, Aprili 13, 2016, Manji aliutangazia umma kwamba atastaafu uongozi katika kundi la kampuni za Quality kuanzia Julai 15, 2016 na kubaki kuwa mwenyekiti na mshauri mkuu mwenye uamuzi wa mwisho katika Baraza la Uongozi na Ofisa Mtendaji Mkuu.
Pia, katika gazeti hili lilitolewa tangazo jingine Desemba 20, 2016 kumpongeza Arif Sheikh kuwa msimamizi wa ofisi za Quality Group katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Manji.
Tangazo hilo lilieleza kwamba Manji atakuwa akizunguka kusimamia kampuni za Quality Group zilizo katika nchi 28 akiendelea na cheo chake cha mwenyekiti na mshauri mkuu mwenye uamuzi wa mwisho katika Baraza la Uongozi na Ofisa Mtendaji Mkuu.
Tofauti na alipofikishwa hospitalini hapo kwa mara ya kwanza Februari 12 ambako kulikuwa na ulinzi mkali wa askari kanzu na waliokuwa wamevaa sare na hata Februari 16 baada kupata dhamana na kuwa chini ya maofisa wa Uhamaji, jana hapakuwa na ulinzi wowote.

AFYA YA MANJI YAIMARIKA, VITA DAWA ZA KULEVYA YAENDELEA

Afya ya mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji inaendelea vizuri baada ya jopo la madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kuendeleza matibabu yake baada ya kupata dhamana akitokea mahakamani.
Hii ni mara ya pili kwa Manji kuugua ghafla na kulazwa hospitalini hapo, mara ya kwanza ilikuwa polisi alipokuwa akihojiwa ambako aliugua ghafla jioni na alipelekwa JKCI.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mkurugenzi wa Tiba wa JKCI, Dk Peter Kisenge alisema walimpokea Manji akitokea mahakamani na kwamba anaendelea na matibabu na afya yake inazidi kuimarika.
“Tunaendelea kumpatia matibabu yanayohitajika kwake kwa sasa na anaendelea vizuri,” alisema Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya moyo katika taasisi hiyo.
Taarifa za ndani zaidi zilidai kuwa Manji kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo. Hata hivyo, madaktari wa JKCI bado wameendelea kusita kuzungumzia tatizo linaloisumbua afya ya Mwenyekiti huyo wa klabu ya Yanga.
Hata hivyo, mara baada ya kufikishwa hospitalini hapo, Manji alikutana na wingi wa wagonjwa kiasi cha kumfanya alazwe na wagonjwa wengine baada ya vyumba vya wagonjwa mashuhuri kujaa.

Vita dawa za kulevya
Vita dhidi ya dawa za kulevya imeendelea kupamba moto nchini hasa baada ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kukabidhiwa majina 97 ya wauzaji wakubwa, pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzindua Baraza la Taifa kukabiliana na uhalifu huo.
Ni vita ambayo haipiganwi Tanzania pekee, Kenya kuna watuhumiwa wamefikishwa mahakamani nchini Marekani, Rais Donald Trump ameanza mapambano hayo huku nchini Ufilipino Rais wake, Rodrigo Duterte aliishaanza kwa kuwapiga risasi watumiaji na wauzaji.
Kinachotokea sasa nchini ni mwendelezo wa kilichoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliyeanza na wasanii na baadaye akataja watu 65 na hivi karibuni alikabidhi majina 97 kwa Kamishna Mkuu Rogers Sianga akisema wanaweza kuwa na taarifa zinazoweza kusaidia katika vita hiyo.
Pia, wakati Makonda akikabidhi majina 97 kwa Kamishna Sianga, alitoa amri ya kukamatwa Chid Mapenzi (Rashid Said) na kesho Jumatatu kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro watuhumiwa watatu wa dawa za kulevya, Agnes Gerald ‘Masogange, Chid Mapenzi na Walid Nasher watafikishwa mahakamani.
Wakati Makonda akikabidhi majina hayo, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alitangaza vita dhidi ya Makonda baada ya kumtaja kwenye orodha ya wanaojihusisha na uhalifu huo.
Askofu Gwajima alisema hayo katika ibada ya Jumapili iliyopita iliyofanyika kanisani kwake Ubungo, baada ya kuachiwa na polisi, alitumia fursa hiyo kuwaeleza waumini wake na Watanzania kilichotokea tangu aliporipoti polisi.

Ilivyokuwa Jumatatu
Akizungumza katika kikao alichokiita cha awamu ya tatu ya kutaja majina wanaojihusisha na dawa za kulevya, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, Makonda alisema ana majina mengine 97 baada ya majina ya wasanii na yale 65.
Awamu ya kwanza ilikuwa mapema mwezi huu, Makonda alitangaza hadharani majina ya wasanii aliodai wanajihusisha na dawa za kulevya akiwataka wafike kituo cha polisi cha kanda maalumu kwa ajili ya mahojiano huku awamu ya pili akiwataja wanasiasa na viongozi wa dini akiwataka pia wafike katika kituo hicho.
Makonda alisema kundi hilo la tatu, limewahusisha baadhi ya watu ambao wako ndani ya nchi aliodai wana mtandao na watu wa nje ambao kuingiza kilo 2,000 au 5,000 siyo jambo gumu kwao.
Siku hiyo hiyo, Kamishna Sianga alitumia fursa hiyo kusema kuwa atawaagiza maofisa wa Serikali waliopitisha tani 21 za viuatilifu vya kutengeneza dawa za kulevya kukamatwa na kuhojiwa na wakibainika watachukuliwa hatua.

Jumanne
Jina la Makonda lilitawala kila kona nchini ikiwamo kutajwa katika mkutano wa Bunge uliomalizika hivi karibuni na kujadiliwa zaidi katika mitandao ya kijamii, ikiwamo makundi ya WhatsApp na mingine.
Wakati mkuu wa mkoa huyo akitawala kila kona, mfanyabiashara Manji aliyekuwa yupo hospitali kwa ajili ya matibabu akiwa chini ya ulinzi, alikumbwa na mkasa mwingine baada ya Kampuni ya Quality Group kudaiwa kuajiri wageni 25 wasiokuwa na vibali vya kufanya kazi nchini.
Ofisa Uhamiaji wa Dar es Salaam, John Msumule aliwaeleza wanahabari kuwa uchunguzi uliofanywa na idara hiyo ulibaini watu 128, waliajiriwa katika kampuni tofauti ambazo ni miongoni mwa kampuni 20 zilizo chini ya Quality Group.
Msumule alisema kutokana na hali hiyo, wamepanga kumshtaki Manji kama mmiliki wa Quality Group kutokana na tuhuma za kuajiri raia wa kigeni wasio kuwa vibali, na kutoa wito kumtaka kuripoti uhamiaji baada ya kutoka polisi

Jumatano
Manji alitoka hospitali Jumatano saa 10.00 jioni baada ya kupatiwa matibabu kwa siku tatu, ingawa haikufahamika alikwenda nyumbani au polisi. Mbali na hilo, siku hiyo vyombo vya habari viliripoti kukamatwa kwa mwanadada anayetamba katika video za nyimbo mbalimbali za bongo fleva, Agnes Gerald ’Masogange’ kwa tuhuma za kujihusisha na dawa za kulevya.

Alhamisi
Manji alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu, akitokea hospitalini alikokuwa amelezwa baada ya kuugua ghafla akiwa katika kituo cha polisi.
Manji alipandishwa kizimbani kwa tuhuma za kutumia dawa za kulevya aina ya heroin, hata hivyo mfanyabiashara huyo alikana shtaka hilo.
Katika kesi hiyo, Manji aliwakilishwa na mawakili watatu ambao ni Alex Mgongolwa, Hudson Ndusyepo na Jeremiah Mtobeya wakati upande wa Serikali uliwakilishwa na Osward Tibabyekoma , Kishenyi Mutalemwa (Wakili Mwandamizi wa Serikali) na Shedrack Kimaro.
Tibabyekomwa alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika.
Wakili Mgongolwa kwa niaba ya jopo la mawakili wa Manji aliomba Mahakama kumpa dhamana mteja wao kwa sababu shtaka linalomkabili kisheria linadhaminiwa na kwamba apewe masharti nafuu.
Hata hivyo, Tibabyekoma aliiambia mahakama hiyo kuwa hawana pingamizi kwa sababu shtaka hilo linadhaminika kisheria.
Baada ya maelezo hayo, Manji alitakiwa kutimiza masharti ya dhamana kwa kuwa na mdhamini mmoja anayeaminika ambaye atasaini hati ya dhamana ya maneno ya thamani ya Sh10 milioni.
Manji alidhaminiwa na Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ambaye aliikamilisha kazi hiyo na Manji kuachiwa huru.

Ijumaa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka wakuu wa mikoa nchini na wilaya kutotangaza majina ya watuhumiwa kabla ya kufanyika uchunguzi na kujiridhisha.
Majaliwa alitoa kauli wakati akizindua Baraza la Taifa la Dawa za Kulevya, hafla iliyofanyika ofisini kwake Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wakuu wa mikoa mbalimbali wakiwamo wakuu wa majeshi ya ulinzi na usalama. Aliwataka wakuu wote wa mikoa kushiriki vita hiyo kwa kuwa wao ni wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama kwenye maeneo yao ya kazi, pia kwa kuzingatia sheria na kanuni wana uwezo huo.

MANJI ALAZWA TENA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE

Baada  ya kupata dhamana ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu juzi, mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, amelazwa tena kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Ofisa Uhusiano wa Taasisi hiyo jana, Anna Nkinda, Manji alifikishwa hospitalini hapo juzi jioni ikiwa ni muda mfupi baada ya kupata dhamana dhidi ya kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin inayomkabili.

“Ni kweli Manji yupo hapa, aliletwa jana jioni (juzi) kwa matibabu ambapo hadi leo (jana) ninavyoongea na wewe bado yupo hapa amelazwa anaendelea na matibabu kama kawaida,” alisema Anna.

Hii ni mara ya pili kwa Manji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, kulazwa kwenye taasisi hiyo.

Mara ya kwanza ilikuwa ni Februari 12, mwaka huu alipolazwa hapo akitokea katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alipokuwa ameshikiliwa tangu Februari tisa akifanyiwa mahojiano.

Mfanyabiashara huyo alifika mwenyewe kwenye kituo hicho cha polisi kutokana na wito uliotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliyetaja majina 65 ya watu aliodai wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Mbali na Manji, baadhi ya watu wengine waliotajwa na Makonda na kutakiwa kufika kituoni hapo ni Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan ambao tayari wamehojiwa polisi huku Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, akiwa bado hajahojiwa licha ya kutajwa kwenye orodha hiyo.

Juzi Alhamisi, Manji alifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo shauri lake lilisikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha.

Karani wa mahakama hiyo, Sarah Mulokozi, alimsomea mshtakiwa shtaka lake ambapo alidai kuwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu eneo la Upanga Sea View jijini Dar es Salaam, Manji alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.

Mtuhumiwa huyo alikana shtaka hilo na Mkurugenzi wa Mashtaka Msaidizi (ADPP), Osward Tibabyekomya, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Upande wa mawakili wa utetezi ambao ni Alex Mgongolwa na Hudson Ndusyepo, waliiomba Mahakama kumpa mshtakiwa dhamana  kwa sababu ya mashtaka yanayomkabili yanadhaminika.

Hakimu Mkeha alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kutakiwa kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni 10 pamoja na mdhamini mmoja wa kuaminika ambapo Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, Charles Mkwasa, alimdhamini Manji, ambaye aliachiwa kwa dhamana hadi Machi 16.

Mara baada ya kupata dhamana, Manji aliondoka mahakamani hapo saa 9:40 akiwa kwenye gari yenye namba T670 BBX aina ya Hummer.

YUSUFU MANJI AFIKISHWA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI KISUTU MCHANA HUU.

Mfanyabiashara maarufu nchini na mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusufu Manji amefikishwa mahakamani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hivi sasa ameingizwa katika mahabusu ya mahakama, akisubiri kupandishwa kizimbani kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Manji amefikishwa mahakamani leo ikiwa ni siku ya nane tangu alipojisalimisha na kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alopoitikia wito wa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda ili kuhojiwa.

Umati mkubwa wa watu wanaodhaniwa kuwa ni mashahabiki wa Klabu ya Yanga, ndugu jamaa na marafiki wamefurika katika chumba cha mahakama, wakimsubiri apandishwe kizimbani.


Kwa taarifa zaidi zinakuijia hivi punde

BREAKING NEWS: MANJI ATOKA POLISI KWA GARI LA KUBEBEA WANGONJWA

Mfanyabiashara maarufu wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Club ya soka ya Yanga Yusuph Manji ni miongoni mwa Watu 65 waliotajwa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda kwenye orodha ya sakata la dawa za kulevya.

Manji ambaye alikwenda Polisi toka Alhamisi iliyopita, leo jioni ameonekana na Waandishi wa habari nje ya kituo cha Polisi kati Dar es salaam akichukuliwa na gari la Wagonjwa lenye namba za usajili za DFP na kuondoka nae.

Kwenye msafara huo ulioondoka gari lake aina ya Range Rover lilikuwepo pia lakini yeye alichukuliwa na gari la Wagonjwa lenye namba za usajili za DFP. Manji alikuwa amevaa fulana, suruali na viatu vya wazi vyote vya rangi nyeusi.

GWAJIMA NA YUSUF MANJI WAKESHA NA POLISI DAR

Ni kama shughuli zilisimama kwa saa kadhaa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam wakati watu wawili maarufu nchini, Askofu Josephat Gwajima na mfanyabiashara Yusuf Manji waliporipoti kituoni hapo wakitaka wahojiwe.
Wawili hao, pamoja na wengine 63 walitakiwa waripoti kituoni hapo leo kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu biashara ya dawa za kulevya, utumiaji au kama wana taarifa zinazoweza kusaidia Jeshi la Polisi kukomesha biashara hiyo haramu.
Wito huo ulitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye juzi aliita waandishi ofisini kwake na kutaja orodha ya watu 65, wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara na viongozi wa dini.
Lakini, Manji, ambaye ni mwenyekiti wa moja ya klabu kubwa nchini ya Yanga, na Askofu Gwajima, anayeongoza kanisa la Ufufuo na Uzima, walienda kituoni hapo jana na walisikindikizwa na mashabiki na waumini wao.
Manji, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Quality Group, alifika kituoni hapo saa 4:54 asubuhi akiwa wa kwanza na alifika akiwa ndani ya gari aina ya Range Rover ya rangi nyeusi, akifuatana na watu wawili alioingia nao kituoni.
Dakika chache baada ya kuingia, Manji alitoka ndani na akawa anazungumza na watu waliovalia sare na wengine kiraia na baada ya muda aliingia tena ndani ya kituo.
Ilipotimu saa 6:10 mchana, Manji alitoka na kuonekana anaondoka, lakini alipofika getini askari walimfuata na wakarudi naye ndani.
“Mzuie, mzuie, mzuie,” alisikika mmoja wa polisi akisema wakati Manji akionekana kuondoka. Mfanyabiashara huyo alitii amri na kurudi kituoni.
Wakati Manji akiwa ndani ya kituo hicho, saa 7:33 mchana Askofu Gwajima aliwasili akiambatana na watu wapatao 10 walioonekana kuwa ni viongozi wa kanisa hilo na wote wakaingia kituoni.
Wakati viongozi hao wakiwa ndani, saa 8:00 mchana waumini takribani 20 walionekana kuwa ni wa kanisa la Ufufuko na Uzima walifika wakiwa wamevalia suti nyeusi. Waumini hao wa kike na kiume walikusanyika nje ya kituo hicho na kujipanga mstari nje ya geti la kuingilia kituoni, lakini askari waliwazuia na kuwataka kukaa mbali na eneo hilo ili wasubiri hatma ya askofu wao.
Taarifa kutoka ndani ya kituo hicho zilisema kuwa watuhumiwa hao hawakutoa maelezo yoyote kwa sababu Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alikuwa kwenye kikao ofisini kwa Makonda.
Eneo hilo pia lilifurika mashabiki kadhaa wa klabu ya Yanga waliokuwa wakifuatilia hatma ya Manji.
Baada ya ukimya uliotawala eneo hilo huku waandishi wa habari wakifuatilia matukio hayo kwa mbali kutoka nje, Manji na Gwajima walionekana wakitoka kituoni saa 10:27 jioni na wote kupanda gari dogo jeupe aina ya Toyota Land Cruiser na kuondoka.
Baada ya kurejea, Kamanda Siro aliwaambia waandishi wa habari kuwa hangeweza kuzungumzia suala hilo jana.

Gwajima amvaa Makonda
Awali, Gwajima alizungumza na waumini wa kanisa lake na kumuomba Rais John Magufuli ambadilishe kazi Makonda, akimsifu kuwa ni mchapakazi, lakini hawezi kazi ya utawala kutokana na ama kutokomaa au kutokuwa na uzoefu.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kuongea na waumini, Askofu Gwajima alisema kitendo cha Makonda kumtaja hadharani akihusishwa na dawa za kulevya kinaonyesha ana nia ovu na kanisa hilo.
“Sisemi Magufuli amfukuze kazi, hapana, Makonda ni jasiri na mchapakazi, lakini kazi ya utawala, kuongoza watu imemshinda atamharibia Rais,” alisema.
“Usalama wa Taifa watakuwa wanafahamu kama Askofu Gwajima anahusika au hahusiki kwa namna moja ama nyingine na dawa za kulevya. Kitendo cha Makonda kunitaja kupitia vyombo vya habari kinaonyesha ana chuki na mimi na hajui masuala ya utawala.
“Hivi hafahamu kwamba nina waumini zaidi ya 70,000, nina makanisa 400 na maaskofu 25. Ameshindwa vipi kuchunguza na kuniita hadi atangaze kwenye vyombo vya habari?”
Alisema sababu nyingine ya kutaka Rais Magufuli ambadilishe kazi ni kutokana na viongozi wa Serikali hivi sasa kufanya kazi kwa hofu.
“Mawaziri, wakuu wa mikoa wanaogopa wanaposikia sauti ya Makonda, wanadhani kila anachofanya ametumwa na Rais Magufuli. Si kweli anawatisha tu huyo,” alisema.
“Magufuli amekuwa akimpongeza Makonda kwa kazi nzuri anazozifanya, lakini si kila anachofanya anatumwa na Rais.”
Aliwataka viongozi wengine kutokuwa na hofu na Makonda kwa kuwa anachokifanya ni kuwatisha wenzake kwa kutumia jina la Rais.
“Nimekuwa nikijiuliza sifahamu chochote kuhusu dawa za kulevya, huyu Makonda ananipakazia hivi ili kumfurahisha nani?” alihoji.

Wivu na chuki binafsi
Askofu Gwajima alisema hivi karibuni walikuwa kwenye mechi ya soka kati ya viongozi wa dini na wa serikali ambayo yeye na Makonda walicheza timu moja.
“Kwa kuwa nilichelewa, niliamua kutumia helikopta hadi uwanjani lakini wakati tukicheza mpira, Makonda alikuwa ananiangalia kwa jicho la chuki mpaka nikawa nashangaa. Sasa leo nimeamini kijana mwenzangu ana chuki binafsi,” alisema.
Alisema Makonda anatakiwa kufahamu kwamba si kila anayefanikiwa kiuchumi anakuwa anajihusisha na dawa za kulevya.
Askofu Gwajima alisema ana shahada ya uzamivu ya filosofia (PhD) na hulipwa dola 1,000 za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh2.2 milioni) kwa saa anapofanya uhadhiri vyuoni.
“Nimetoka Japan ambako nilikaa miezi mitatu, unadhani nitachuma kiasi gani?” alihoji.
“Sasa kijana mwenzangu Makonda asiwe na chuki binafsi, bali angeniuliza unapataje fedha, lakini si kuvunja heshima yangu niliyoijenga siku nyingi.”
Alisema hajawahi kunywa pombe, kuvuta sigara na wala hajui dawa za kulevya zikoje.

Makonda kanisani
Gwajima alisema Makonda akiwa na spika wa zamani wa Bunge, Marehemu Samuel Sitta waliwahi kufika kanisani kwake kuombewa.
“Nilimkaribisha Makonda madhabahuni na akazungumza na waumini akisema ni heshima kubwa kupata nafasi ile na tulisali pamoja. Je, kipindi kile hakuhofia kuwa nahusika na dawa za kulevya?” alihoji.
Nisirudishwe kwa Lowassa
Alipoulizwa kama patashika anazopata zinatokana na kuwa karibu na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, mchungaji huyo alisema anashangaa kuona anarudishwa kwa mtu aliyeona anafaa kuwa Rais.
“Wakati wa uchaguzi kila mtu aliona mtu aliyefaa kuwa Rais na mimi niliona Lowassa ndiye aliyekuwa anafaa kuwa Rais,” alisema Gwajima.
“Lakini bahati nzuri Lowassa hakuchaguliwa na badala yake amechaguliwa Magufuli ambaye anafanya kazi ambayo ingeweza kufanywa na wapinzani. Kwa hiyo namuunga mkono. Nashangaa kwamba mimi namuunga mkono, lakini wanazidi kunirudisha kwa yule.
“Mimi si mnafiki. Wakati Rais Jakaya Kikwete akiwa madarakani niliikosoa sana Serikali yake, lakini nashukuru sasa Magufuli anafanya kazi zilizotarajiwa na Watanzania wengi, ndiyo maana mara nyingi nampongeza.”