HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

NBAA YAWANOA WATAHINIWA MITIHANI CPA


Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendesha warsha kwa njia ya mtandao pamoja na mafunzo ya ana kwa ana kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi, ikilenga kuongeza ufanisi na maandalizi bora kwa watahiniwa wake.

Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo kwa niaba ya  Mkurugenzi Mtendaji, Peter Lyimo, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo, , alisema kuwa warsha hiyo imelenga kuwanoa wanafunzi wa ngazi mbalimbali kupitia mbinu bora za kujibu mitihani, hasa kwenye maeneo yenye changamoto kubwa kwa watahiniwa.

“Yapo masomo ambayo kiwango cha ufaulu kimekuwa kidogo. Hivyo tumewaleta walimu kutoka vyuo na Taasisi mbalimbali ili watoe uzoefu na mbinu sahihi kwa watahiniwa, ili waweze kujiandaa vizuri,” alisema Lyimo.

Aidha, Lyimo alifafanua kuwa mbali na wanafunzi waliounganishwa kupitia mtandao, pia kulikuwa na kundi la wanafunzi waliofika moja kwa moja katika ofisi za Bodi (NBAA) kupata mafunzo hayo ya kitaalamu ana kwa ana. Hatua hii inalenga kuongeza ufanisi na kuwawezesha wanafunzi kuuliza maswali kwa urahisi zaidi na kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa walimu.

Aliwasisitiza wanafunzi kuepuka kujiandaa kwa mazoea au kiholela na badala yake kutenga muda wa kutosha kujifunza, akibainisha kuwa kuna tofauti kubwa kati ya mitihani ya vyuoni na mitihani ya Bodi.

“Tumewasisitiza sana namna ya kujiandaa. Waweke muda wa kutosha kwenye kujifunza kwani mitihani ya Bodi inahitaji umakini mkubwa na maandalizi ya kitaalamu zaidi,” aliongeza.

Kwa mujibu wa Lyimo, NBAA imejipanga kuhakikisha kiwango cha ufaulu kinapanda katika mitihani yake mbalimbali, sambamba na kuongeza uelewa wa watahiniwa, ili baada ya kumaliza mitihani waweze kuwa wataalamu waliobobea kwenye uhasibu na ukaguzi.

Bodi hiyo imesisitiza kuwa hatua hii ni sehemu ya mkakati wake wa kuhakikisha kila mtahiniwa anapata maandalizi stahiki na changamoto zinazowakabili zinapatiwa suluhisho la kudumu.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo Peter Lyimo akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha kwa njia ya mtandao pamoja na mafunzo ya ana kwa ana kwa wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi
Mfanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), Sawa Ngendabanka akiwakaribisha wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani mbalimbali ya Bodi ambao walikuwa wakisikiliza Warsha hiyo kwa njia ya mtandao.
Mkufunzi CPA Rashid Mganwa akitoa elimu kuhusu namna ya kujiandaa na kufanya masomo ya B2 na C1 kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi waliokuwa wanafuatilia kwa njia mtandao.
Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, CPA Dkt. Emmanuel Christopher akitoa elimu kuhusu namna ya kujiandaa na kufanya masomo ya B1 na C3 kwa wanafunzi wanaotegemea kufanya mitihani ya Bodi waliokuwa wanafuatilia kwa njia mtandao.


Baadhi ya  wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya Bodi wakifuatilia mada pamoja na kuuliza maswai kwa wakufunzi

MABLOGA WASHUKURU UAMUZI WA SERIKALI KUWAPIGA MSASA KUIMARISHA WELEDI WAO



Na Mwandish wetu, Dar es Salaam.

CHAMA cha Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) kimeshukuru uamuzi wa serikali ya kuwapatia mafunzo maalumu ya kunoa weledi na uzalendo wa wanachama wake kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu. Mabloga zaidi ya 200 wakiwemo wa diaspora walioanzisha Mtandao huo mwaka 2015 watapata mafunzo hayo. 

“Tumekuwa na mazungumzo na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambao kimsingi ndio wasimamizi wakuu wa maudhui na wametuthibitishia kwamba wapo hatua za mwisho za kutekeleza maagizo ya serikali ya kutoa mafunzo kwa mabloga wote nchini,” alisema Mwenyekiti wa TBN , Beda Msimbe. 

Akifafanua kuhusu mafunzo hayo, Msimbe alisema kwamba lengo kuu la mafunzo ni kuwajengea mabloga weledi, uzalendo, na umakini katika kutambua na kupambana na habari feki, huku wakiwezesha usambazaji wa taarifa sahihi zitakazowawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi mkuu ujao. 

“ Tunahitaji kukumbushana kuhusu nchi hii, katiba yetu, amani na umuhimu wa uchaguzi katika demokrasia ya aina yetu.Uamuzi huu wa serikali wa kutupiga msasa ni muhimu sana” alifafanua.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Mwenyekiti huyo wa TBN, Beda Msimbe, alieleza kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na serikali kufanikisha mafunzo. Alisema wameomba mafunzo hayo kipindi cha sasa kwa kuwa wapo wanablogu ambao ni mara ya kwanza kuelekea katika uchaguzi mkuu, na kurejea ombi lao tena wakati wa mkutano wa wadau ulioandaliwa na Wizara ya Habari,Utamaduni,sanaa na michezo. 

Alisema kwamba uongozi wa TBN kwa sasa unafanya kazi kwa karibu na serikali kuhakikisha kuwa zaidi ya wanachama 150 wa chama hicho waliotawanyika nchini kote wanafaidika kikamilifu na mafunzo haya muhimu. 

Msimbe aliwataka mabloga wote nchini kuhakikisha wanawasiliana na Mratibu wa TBN, Bw. Gadiola Emanuel ili kuthibitisha anwani zao na kuhakikisha taarifa zao ziko sahihi kwa ajili ya ushiriki. Pia alitumia fursa hiyo kuwaalika wale wote ambao bado hawajajiunga na TBN kufanya hivyo sasa ili waweze kunufaika na fursa hii muhimu ya mafunzo. 

Chama cha Mabloga Tanzania (TBN) kinajumuisha mabloga wanaotengeneza aina mbalimbali za maudhui, ikiwemo michezo, habari za siasa, afya, uchumi, na habari mchanganyiko. Mafunzo haya yanatarajiwa kuimarisha uwezo wao wa kutoa taarifa zenye ukweli na uhakika, hivyo kuchangia katika mazingira ya uchaguzi yenye uwazi na uwajibikaji. 

NBAA YAZINDUA MFUMO WA KUKUSANYA TAARIFA ZA FEDHA ILI KUSAIDIA WADAU KUFANYA MAAMUZI SAHIHI


Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imezindua rasmi mfumo mpya wa kukusanya taarifa za fedha zilizokwisha kukaguliwa na Wakaguzi wa Hesabu, ambao utaanza kutumika rasmi kuanzia Julai 1, 2025.

Mfumo huu unalenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za kifedha kwa matumizi ya mamlaka ya mapato (TRA), taasisi za kifedha, wadau wa mikopo, taasisi za serikali na binafsi, na mashirika mbalimbali, kwa ajili ya kufanya maamuzi muhimu ikiwemo utoaji wa mikopo na tenda kwa wazabuni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam alipotembelea banda la NBAA katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu, alisema mfumo huo ni hatua kubwa katika kuhakikisha taarifa za fedha zinakuwa na uwazi, uaminifu na uhalali wa kitaaluma, hasa kwa wale wanaohitaji kuzitumia katika maamuzi ya maendeleo ya kiuchumi na kibiashara.

“Kuanzia sasa, taarifa zote za fedha zilizokaguliwa zitakuwa zinaletwa moja kwa moja kwenye mfumo wa NBAA. Hii itasaidia taasisi kama TRA, taasisi za fedha, na wadau wengine kuhakikisha taarifa wanazozipokea ni sahihi, zimetolewa na wakaguzi walioidhinishwa, na zinaweza kutumika kama msingi wa kufanya maamuzi makubwa kama utoaji wa mikopo au kandarasi,” alieleza Prof. Temu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika wa NBAA, CPA Kulwa Emmanuel Mandeleja, alisema mfumo huu utarahisisha sana mchakato wa uthibitishaji wa taarifa kwa taasisi mbalimbali, hasa zile zinazohitaji uthibitisho wa hali ya kifedha ya kampuni au taasisi kabla ya kutoa huduma au mikopo.

“Mfumo huu utahakikisha taarifa zote za kifedha zilizokaguliwa zinahifadhiwa sehemu moja salama na ya kuaminika. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kufanya tathmini, kuzuia taarifa za kughushi na kuimarisha mchakato wa maamuzi ya kifedha katika taasisi nyingi,” alisema CPA Mandeleja.

NBAA imetoa wito kwa taasisi zote, watoa huduma za ukaguzi, na wahasibu kuhakikisha wanatumia mfumo huo mpya ipasavyo na kuhakikisha taarifa zote zinaingizwa kwa wakati kama sehemu ya uwajibikaji na weledi wa kitaaluma.

Kwa maelezo zaidi, wadau wanakaribishwa kutembelea banda la NBAA katika jengo la Wizara ya Fedha na Mipango katika viwanja vya Sabasaba au kutembelea tovuti ya NBAA: www.nbaa.go.tz.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Sylvia Temu akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Bodi hiyo lililopo ndani ya  jengo la Wizara ya Fedha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Sylvia Temu akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Bodi hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Prof. Sylvia Temu akiwa kwenye picha ya pamoja na wafanyakazi wa NBAA alipotembelea banda la Bodi hiyo lililopo ndani ya jengo la Wizara ya Fedha. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Huduma za Shirika kutoka NBAA CPA Kulwa Malendeja.

NBAA YASHIRIKI MAONESHO YA 49 YA KIMATAIFA YA BIASHARA YA SABASABA 2025



Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) inashiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 49 yanayoendelea kwenye Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam, ikiwa ni jitihada za kuonyesha huduma mbalimbali zinazotolewa na Bodi hiyo pamoja na kutoa elimu kwa wananchi.

Banda la NBAA lipo ndani ya jengo la Wizara ya Fedha linawahudumia wananchi kwa kutoa maelekezo ya usajili wa mitihani katika ngazi mbalimbali za taaluma ya uhasibu, pamoja na kutoa maelekezo kuhusu ulipaji wa ada na huduma nyingine muhimu.

Akizungumza na Michuzi Blog, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya alisema kuwa katika kipindi hiki cha Sabasaba Bodi imewasogezea wananchi huduma karibu kwa kutoa huduma zote kama vile usajili wa watahiniwa wa mitihani ya Bodi, usajili wa wanachama wa ngazi mbalimbali, usajili wa Makampuni, usajili wa kozi mbalimbali zinazoendeshwa na Bodi mfano 'Certificate na Diploma ya IPSAS', 'Professional Diploma in Internal Auditing' ambayo ni kozi mpya kwa wanaofanya kazi kwenye idara za ukaguzi wa ndani ili kuwasaidia kuwa na uelewa kwenye masuala ya ukaguzi.

Aidha, Bi. Kageya aliongeza kwamba NBAA kwa sasa inatumia mifumo ya kidijitali kutoa huduma zake, ambapo wananchi wanaweza kufikia huduma hizo kupitia tovuti rasmi ya Bodi ambayo ni www.nbaa.go.tz.

Maonesho haya ya Sabasaba ni fursa kubwa kwa Bodi ya NBAA kuwasiliana moja kwa moja na wananchi na wadau mbalimbali wa taaluma ya uhasibu na ukaguzi, ili kuboresha utoaji wa huduma na kuelimisha kuhusu umuhimu wa taaluma hiyo katika maendeleo ya taifa.

Wafanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) wakiwa kwenye picha ya pamoja katika banda la Bodi hiyo lililopo ndani ya jengo la Wizara ya Fedha.


Huduma zikiendelea kwenye banda la NBAA

NBAA YATANGAZA MATOKEO YA MITIHANI YA MEI, 2025


Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) katika kikao chake cha 198 kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wake CPA. Prof. Sylvia S. Temu imeidhinisha matokeo ya mitihani ya 101 ya Bodi kwa Watahiniwa waliofanya mitihani hiyo iliyofanyika mwezi Mei 2025 katika ngazi mbalimbali za masomo ya Bodi hiyo ya NBAA.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo Peter Lyimo amesema kuwa matokeo hayo yameidhinishwa kufuatia mitihani iliyofanyika katika vituo 12 vilivyopo Tanzania Bara na Visiwani.

Amesema Jumla ya watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 8,100 kati ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mitihani watahiniwa 845 sawa na asilimia 10.4 hawakuweza kufaya mitihani hiyo kwa sababu mbalimbali hivyo idadi ya watahiniwa waliofanya mitihani hiyo walikuwa 7,255 sawa na asilimia 89.6, kati ya hao watahiniwa 3,726 sawa na asilimia 51.4 walikuwa wanawake na watahiniwa 3,529 sawa na asilimia 48.6 walikuwa Wanaume.

Lyimo amesema jumla ya watahiniwa 466 wamefaulu mitihani ya Shahada ya Juu ya Uhasibu nchini yaani CPA (T). Kati ya watahiniwa hao wanawake ni 227 sawa na asilimia 48.7 na wanaume ni 239 sawa na asilimia 51.3 ambapo idadi hii inafanya jumla ya watahiniwa waliofaulu mitahani ya CPA kufikia 14,399 tangu mitihani hiyo ianze mwaka 1975.

Kati ya watahiniwa 466 waliofuzu kutunukiwa Cheti cha Taaluma ya juu ya Uhasibu wengi wao wametoka katika vyuo mbalimbali ambapo watahiniwa 95 sawa na asilimia 20.8 wametoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), watahiniwa 72 sawa na asilimia 15.8 wametoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), watahiniwa 66 sawa na asilimia 14.5 wametoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, watahiniwa 60 sawa na asilimia 13.2 wametoka Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) na watahiniwa 19 sawa asilimia 4.2 wametoka Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Amesema jumla ya watahiniwa 11 wamefaulu mitihani ya CPA(T) linganifu (Equivalent Qualification) kati ya hao wanawake ni 04 sawa na asilimia 36.4 na wanaume ni 07 sawa na asilimia 63.6 ambapo mpaka sasa jumla ya watahiniwa waliofaulu mitihani hii wamefikia 341 tangu mitihani hii ianze Novemba 2014.

Pia amesema katika ngazi ya awali ya Uandishi na Utunzaji wa Hesabu(ATEC I) watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 101 kati ya hao watahiniwa 07 sawa na asilimia 6.9 hawakuweza kufanya mitihani hiyo kwa sababu mbalimbali na hivyo watahiniwa waliofanya mitihani walikuwa 94 sawa na asilimia 93.1.

Pia ameeleza kuwa kati ya watahiniwa 94 waliofanya mitihani katika ngazi hii watahiniwa 78 ambao ni asilimia 83.0 wamefaulu mitihani yao na kati ya hao watahiniwa 30 sawa na asilimia 31.9 wanastahili kutunukiwa barua za ufaulu na watahiniwa 48 sawa na asilimia 51.1 wamefaulu baadhi ya masomo na watahiniwa 16 sawa na asilimia 17.0 hawakufaulu mitihani yao.

Aidha amesema katika hatua ya pili ya Cheti yaani ngazi ya uandishi na Utunzaji wa Hesabu(ATEC II) waliojisaliwa walikuwa 173 kati ya hao watahiniwa 19 sawa na asilimia 11.0 hawakuweza kufanya mitihani kutokana na sababu mbalimbali. Hivyo watahiniwa waliofanya mitihani walikuwa 154 sawa na asilimia 89.0.

“Kati ya watahiniwa 154 waliofanya mitihani katika ngazi hii watahiniwa 93 ambao ni asilimia 60.4 wamefaulu mitihani yao ambapo kati ya hao watahiniwa 31 sawa na asilimia 20.1 wanastahili kutunukiwa Barua za Ufaulu na watahiniwa 62 sawa na asilimia 40.3 wamefaulu baadhi ya masomo katika ngazi hii na watahiniwa 61 sawa na silimia 39.6 hawakufaulu mitihani yao” Alisema Lyimo

Amesema katika ngazi ya taaluma hatua ya awali watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 1,077 kati ya hao watahiniwa 127 sawa na asilimia 11.8 hawakuweza kufanya mitihani hiyo kwa sababu mbalimbali hivyo watahiniwa waliofanya mitihani walikuwa 950 sawa na asilimia 88.2.

Pia ameeleza kuwa kati ya watahiniwa 950 waliofanya mitihani katika ngazi hii watahiniwa 730 ambao ni asilimia 76.8 wamefaulu mitihani yao ambapo kati yao watahiniwa 259 sawa na silimia 23.7 wanastahili kutunukiwa barua za ufaulu wa mitihani na watahiniwa 471 sawa na asilimia 49.6 wamefaulu baadhi ya masomo hivyo watahiniwa 220 sawa na asilimia 23.2 hawakufaulu mitihani yao.

Aidha amesema katika hatua ya kati waliojisaliwa walikuwa 4,094 kati ya hao watahiniwa 471 sawa na asilimia 11.5 hawakuweza kufanya mitihani kutokana na sababu mbalimbali. Hivyo watahiniwa waliofanya mitihani walikuwa 3,623 sawa na asilimia 88.5, kati ya watahiniwa hao 3,623 waliofanya mitihani katika ngazi hii watahiniwa 2,430 sawa na asilimia 67.1 wamefaulu mitihani yao kati ya hao watahiniwa 563 sawa na asilimia 14.8 wanastahili kutunukiwa barua za ufaulu na watahiniwa 1,894 sawa na asilimia 52.3 wamefaulu baadhi ya masomona watahiniwa 1,193 sawa na asilimia 32.9 hawakufaulu mitihani yao

Katika hatua ya mwisho, waliosajiliwa walikuwa 2,655 kati ya hao watahiniwa 221 sawa na asilimia 8.3 hawakuweza kufanya mitihani hiyo kwa sababu mbalimbali. Hivyo watahiniwa waliofanya mitihani walikuwa 2,434 sawa na asilimia 91.7. Kati ya watahiniwa 2,434 waliofanya mitihani katika ngazi hii watahiniwa 1,575 sawa na asilimia 64.7 wamefaulu mitihani mitihani yao ambapo kati ya watahiniwa 479 sawa na silimia 19.7 wanastahili kutunukiwa barua za ufaulu na watahiniwa 1,096 sawa na asilimia 45.0 wamefaulu baadhi ya masomo na watahiiwa 859 sawa na asilimia 35.3 hawakufaulu mitihani yao.

Lyimo amesema Bodi ya Wakurugenzi wa NBAA inatoa pongezi kwa wale wote waliofuzu mitihani yao na kuwataka wale ambao hawajafuzu kutokata tamaa badala yake waongeze bidii zaidi katika masomo yao ili wawezo kufuzu mitihani ijayo.

Pia amesema Bodi inawashauri watahiniwa kutumia vitabu vilivyotayayarishwa na Bodi katika kujiandaa kwa mitihani yao na pia wanashauriwa kusoma vitabu vingine vya ziada ili kuongeza ufahamu zaidi katika masomo hayo.

Mitihani ya muhula wa kati (Mid- session Examinations) itafanyika kuanzia Jumatatu tarehe 25 hadi Ijumaa tarehe 29 Agosti 2025 na mitihani ya Novemba itafanyika Jumanne tarehe 04 hadi Ijumaa tarehe 07 Novemba 2025 na pia matokeo ya mitihani ya 101 ya Bodi yanapatikana kwenye tovuti ya NBAA ambayo ni www.nbaa.go.tz.
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Elimu ya Taaluma na Mafunzo wa NBAA  Peter Lyimo

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWASISITIZA WATUMISHI WA UMMA KUTOA HUDUMA BORA, TCAA YATOA ELIMU KUHUSU USAFIRI WA ANGA

WAZIRI MKUU MAJALIWA AWASISITIZA WATUMISHI WA UMMA KUTOA HUDUMA BORA, TCAA YATOA ELIMU KUHUSU USAFIRI WA ANGA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amewataka watumishi wa umma kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na maadili ya utumishi wa umma.

Mhe. Majaliwa aliyasema hayo Juni 23, 2025, katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.

Akizungumza mbele ya viongozi wa serikali, watumishi wa umma na wananchi waliojitokeza kushuhudia maadhimisho hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kazi kwa watumishi wa umma, huku akiwasisitiza kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo kwa kutoa huduma zenye tija na huruma kwa wananchi.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema ni vyema kuimarisha mikakati ya kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kutumia fursa za uwepo wa maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma ili wajitokeze kwa wingi na  kupata huduma zinazotolewa na Serikali kwa haraka zaidi.

Awali,  wakati akizindua mfumo wa Kidijiti Mhe Majaliwa, alizitaka Taasisi zote za umma kutekeleza agizo la Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kuwa Taasisi zenye mifumo na zinazoendelea kubuni mifumo inayosomana na zinazoweza kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo ili kuboresha huduma ndani ya Serikali.

“Mamlaka ya Serikali Mtandao eGA hakikisheni kwamba mifumo iliyounganishwa inaendelea na majukumu yake ya kubadilishana taarifa lakini pia kila anayeingia mjiridhishe kuwa ana uwezo wa kuwasiliana na yeyote aliye kwenye mfumo’’. Alisema Mhe. Majaliwa.

Vile vile Mhe. Majaliwa aliwaasa watumishi wa umma kote nchini kujisajili katika mfumo wa kidijitali wa e – wezesha, ambao unawezesha watumishi wa umma kuwekeza moja kwa moja kupitia makato ya mshahara au mapato mbalimbali ya biashara.

Katika kuunga mkono maadhimisho hayo, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeungana na taasisi mbalimbali za umma kushiriki katika maonesho yanayofanyika kwa wiki nzima katika viwanja hivyo. Kupitia maonesho hayo TCAA inatoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake ya msingi, ikiwa ni pamoja na udhibiti wa shughuli zote za usafiri wa anga nchini.

Maeneo yaliyopewa kipaumbele na TCAA mwaka huu ni pamoja na usimamizi wa matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones), ambao ni uwanja unaokua kwa kasi na unahitaji uangalizi wa karibu kwa ajili ya kulinda usalama wa anga, faragha ya wananchi na kuzuia matumizi mabaya ya vifaa hivyo katika maeneo yaliyokatazwa kama vile taasisi za serikali, kambi za kijeshi, na miundombinu nyeti.

Aidha, TCAA inatumia jukwaa hilo kutoa taarifa kuhusu huduma za uongozaji ndege, pamoja na kuhamasisha vijana na wadau kuchangamkia fursa za mafunzo zinazotolewa na Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), ambacho kinamilikiwa na mamlaka hiyo.

Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu: “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijiti Ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji”, kaulimbiu inayolenga kuhimiza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha uwajibikaji wa watumishi wa umma.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka barani Afrika kuanzia Juni 16 hadi 23, yakihusisha taasisi mbalimbali za umma kuonesha huduma na mafanikio yao kwa wananchi kupitia maonesho ya wazi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza alipomwakilisha  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma  kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Juni 23, 2025.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakiendelea kutoa elimu katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya Utumishi kwa Umma.

NBAA KUANZISHA KANZI DATA ( DATABASE) YA WANAFUNZI WA UHASIBU VYUONI


Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeweka mikakati ya kuanzisha kanzi data (database) ya wanafunzi wanaosomea masomo ya uhasibu katika vyuo mbalimbali nchini, ili kuwezesha ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo yao kitaaluma na kuwasaidia katika maandalizi ya mitihani ya Bodi hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno, Afisa Tawala na Rasilimali Watu wa NBAA, Bi. Gloria Kaaya, alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi katika usimamizi wa taaluma ya uhasibu na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata taarifa sahihi kwa wakati kuhusu masuala ya kitaaluma.

"Tumeanzisha mpango huu ili kuwatambua na kuwafuatilia wanafunzi wote wanaosomea uhasibu vyuoni. Kupitia "database" hii, tutawawezesha kupata taarifa muhimu kuhusu taratibu za mitihani, masharti ya kupata misamaha "exemptions", na muda sahihi wa kuanza mitihani ya kitaaluma baada ya kuhitimu," alisema Bi. Kaaya.

Aliongeza kuwa baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikosa fursa ya kufanya mitihani ya Bodi kwa wakati kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi, au kuchelewa kujiandikisha ndani ya muda unaotakiwa, hasa pale inapozidi miaka mitano tangu kumaliza masomo yao.

Kwa mujibu wa NBAA, "database" hiyo pia itarahisisha mawasiliano kati ya Bodi, vyuo vya elimu ya juu na wanafunzi wenyewe, hivyo kuongeza uwazi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kitaaluma nchini.

"Tunataka wanafunzi wote waelewe fursa walizonazo na wajue hatua wanazopaswa kuchukua ili kufikia malengo yao ya kitaaluma. Mfumo huu utasaidia kuongeza idadi ya wataalamu wa uhasibu waliothibitishwa, ambao ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa," alisisitiza.

NBAA imetoa wito kwa taasisi za elimu ya juu kushirikiana na Bodi hiyo katika utekelezaji wa mpango huu kwa kuhakikisha taarifa za wanafunzi zinasajiliwa kwa usahihi, huku ikiwataka wanafunzi kufuatilia matangazo rasmi ya Bodi hiyo kupitia tovuti na mitandao yake ya kijamii.

Afisa Tawala na Rasilimali watu NBAA, Gloria Kaaya akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno kuhusu mikakati ya kuanzisha kanzi data (database) ya wanafunzi wanaosomea masomo ya uhasibu katika vyuo mbalimbali nchini kwa wakuu wa Idara za Fedha na Uhasibu vyuoni.







Baadhi ya wakuu wa Idara za Fedha na Uhasibu vyuoni pamoja na watumishi wa NBAA wakifuatilia mada

Picha ya pamoja