YAFUATIA YA NYERERE,MKAPA NA MWINYI, ZITTO ASEMA WAJISALIMISHE
RIPOTI
ya utafiti wa utoroshaji wa fedha nchini kwenda kufichwa katika benki
za nchi za nje ikiwamo Uswisi uliofanywa na na Shirika la Global
Financial Integrity umeonyesha kuwa fedha nyingi kutoka Tanzania
zilitoroshwa kati kipindi cha utawala wa awamu ya nne kati 2005 na 2009.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo kuhusu utoroshwaji wa fedha kwa njia haramu
kutoka Afrika kwenda mataifa yaliyoendelea, ambayo gazeti hili
limeipata, katika kipindi hicho fedha zilizofichwa nje ya nchi ni Dola
za Marekani 7,967.4 milioni (sawa Sh12.7 trilioni).
Ripoti
hiyo pia imeonyesha kuwa katika kipindi cha utawala wa kwanza ulioishia
1985, fedha zilizofichwa nje zilikuwa Dola 3,493.3 milioni (Sh5.5
trilioni) na katika awamu ya tatu kati ya 1995 hadi 2005, zilikuwa Dola
2,108.8 milioni (Sh3.3 trilioni) wakati katika awamu ya pili
zilitoroshwa Dola 529.1 milioni (Sh846 bilioni).Utafiti huo wa Shirika
Global Financial Integrity unaonyesha pia nchi 20 za Afrika zinaongoza
kwa kuficha fedha nje ya nchi, Nigeria ikiongoza.
Jumla
ya Dola za Marekani 1.8 trilioni zimefichwa katika benki mbalimbali nje
ya nchi kutoka katika nchi za Kiafrika katika kipindi cha mwaka 1970
hadi 2009.
Mpina
Akizungumzia
ripoti hiyo jana, Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina alishauri mambo
mawili muhimu yafanyike ili kukabiliana na ufisadi wa kutorosha fedha na
raslimali za nchi kwenda nje ya nchi.Alisema kuwa hatua ya kwanza ni
kufanya marekebisho ya sheria za nchi na pili ni kujenga mfumo madhubuti
wa kukabiliana na mafisadi nchini. Kuhusu marekebisho ya sheria, Mpina
aliliambia Mwananchi Jumapili kuwa baadhi ya viongozi wasio na uchungu
na nchi wamekuwa wakitorosha kirahisi fedha na rasilimali za nchi
kutokana na udhaifu wa sheria. “Ni lazima kwanza sheria zetu ziwe na
nguvu ya kuweza kulinda fedha na rasilimali za nchi,” alisema mbunge
huyo ambaye hivi karibuni alionyesha kukerwa na tabia hiyo aliyosema
inazidi kuwadidimiza Watanzania kwenye wimbi la umaskini. Akizungumzia
hatua za kuchukuliwa dhidi ya wahusika, Mpina alielezea kusikitishwa
kwake na woga walionao baadhi ya viongozi kwa kuogopa kuwataja hadharani
mafisadi. “Mfano suala la Rada… limekuwa ni tatizo na hakuna nia ya
dhati ya kukabiliana na wahusika,” alilalamika.
Zitto: Tutawataja wahusika
Akizungumzia
suala hilo jana, Zitto alisema kuwa walioficha fedha nje ya nchi
wanapaswa kujisalimisha wenyewe kwa kuwa Serikali inaweza kupata orodha
yao kutoka mamlaka ya Uswisi. Alisema kuwa amekuwa akishauriana na mmoja
wa wabunge wa zamani wa Afrika Kusini ambaye ndiye aliyefanya naye
utafiti kuhusu fedha hizo za kifisadi zilizofichwa Uswisi. “Tutawataja
mmoja baada ya mwingine maana taarifa zetu ni za uhakika na hazina
mashaka,” alisema Zitto. Alisema fedha hizo zimetokana na rushwa kwenye
mikataba ya kutafuta mafuta, gesi na Kampuni ya Meremeta.
Kashfa
ya kuwapo kwa vigogo walioficha fedha zao nchini Uswisi iliibuliwa na
baadhi ya vyombo vya habari nchini mwezi Juni mwaka huu na baadaye
mwangwi wake kulitikisa Bunge katika mkutano wake wa nane uliomalizika
Alhamisi ya Agosti 16 mjini Dodoma. Habari hizo zilikuwa zikinukuu
taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Uswisi kuonyesha kuwapo kwa kiasi
cha Sh315.5 bilioni, zilizotoroshwa na Watanzania na kufichwa nchini
humo na vigogo ambao ni wanasiasa pamoja na wafanyabiashara.
Jumatano
wiki hii, tuhuma hizo ziliibuka tena bungeni pale Kambi ya Upinzani
ilipodai kwamba inawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja
ikiwa Serikali haitawataja.
Naibu
Kiongozi wa Upinzani bungeni, Zitto alipokuwa akiwasilisha hotuba ya
kambi yake kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha na Uchumi
alisema kuwa miongoni mwa wanaomiliki fedha hizo ni kiongozi wa juu
nchini, pamoja na aliyepata kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu
iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa.
Taarifa
hizo zinaeleza kuwa mbali na kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo
wengine wanne ambapo anayefuatia anamiliki Dola 30 milioni (Sh48
bilioni), mwingine dola 20 milioni (Sh32 bilioni) na wengine wawili kila
mmoja anamiliki dola milioni 10 (Sh16 bilioni).
Kwa
kuangalia fedha hizo ni dhahiri kwamba vigogo watano tu kati ya kundi
la Watanzania 27, wanamiliki dola milioni 126 (Sh201.6 bilioni) sawa na
asilimia 67.74 ya fedha hizo, wakati wengine 22 waliobaki wanamiliki
dola milioni 60 (Sh96 bilioni) sawa na asilimia 32.25. Kwa hesabu za
kawaida, kiasi cha Sh300 bilioni, kinaweza kugharimia ujenzi wa vyumba
vya madarasa zaidi ya 33,300, ikiwa chumba kimoja kinagharimu kiasi cha
Sh9 milioni. Katika orodha ya walioweka fedha nchini humo, pia wamo
wafanyabiashara wanaomiliki kiasi cha dola kati ya milioni mbili na
milioni saba.
Wamo
wawili waliowahi kuwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya
Mwalimu Julius Nyerere ambao akaunti zao zina kiasi kisichozidi dola
500,000 kwa kila mmoja.
CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz




No comments:
Post a Comment