Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisoma hotuba ya kuwahamasisha wananchi kushiriki Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2012.
Ndugu wananchi;
Imekuwa
ni mazoea yetu kuwa Rais huzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi.
Lakini, leo nazungumza nanyi siku saba kabla ya mwisho wa mwezi kwa
sababu maalum. Sababu yenyewe si nyingine bali ni Sensa ya Watu na
Makazi itakayofanyika kwa siku saba kuanzia kesho Jumapili tarehe 26
Agosti, 2012. Shabaha yangu ni kutaka kuwakumbusha Watanzania wenzangu
wote kuhusu wajibu wao wa kujitokeza kuhesabiwa siku hizo. Naomba kila
mmoja wetu ahakikishe kuwa anakuwepo kuhesabiwa na kujibu maswali yote
yatakayoulizwa na makarani wa sensa kwa ufasaha.
Ndugu wananchi;
Katika
historia ya nchi yetu, Sensa ya mwaka huu itakuwa ni ya tano tangu
Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12
Januari, 1964 na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 26
Aprili, 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa kwa upande wa Tanzania Bara wakati wa
ukoloni zilifanyika Sensa mwaka 1910, 1931, 1948 na 1957. Kwa upande wa
Zanzibar wakati wa ukoloni na utawala wa Sultan kulifanyika Sensa mara
moja mwaka 1958.
Ndugu Wananchi;
Kama
ilivyokuwa kwa Sensa zilizotangulia, madhumuni makubwa ya Sensa ya Watu
na Makazi ya mwaka 2012 ni kujua idadi ya watu, mahali walipo, jinsia
zao, umri wao, elimu, shughuli wazifanyazo, vipato vyao, upatikanaji wa
huduma mbalimbali pamoja na makazi. Taarifa hizi hutumiwa na Serikali
kupanga mipango ya maendeleo, kutengeneza programu mbalimbali na kubuni
miradi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini. Aidha, huisaidia
Serikali kupanga na kupeleka huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi
kwa kuzingatia mahitaji halisi ya maeneo yao wanayoishi kwa mujibu wa
idadi yao na mgawanyiko wao kijinsia, kiumri na huduma zinazohitajika.
Hivyo basi, idadi halisi isipojulikana kuna hatari ya wananchi kukosa
huduma wanazohitaji kwa kiwango kinachostahili. Vilevile, takwimu hizi
hutumiwa na Serikali katika kufikia uamuzi wa kugawa majimbo ya uchaguzi
na maeneo ya utawala kama vile mikoa, wilaya, kata, vijiji na vitongoji
vipya.
Ndugu wananchi;
Pamoja
na umuhimu huo wa jumla wa Sensa kwa maendeleo ya nchi yetu, Sensa ya
mwaka 2012 ina umuhimu wa aina yake. Taarifa zake zitatumika kufuatilia
na kutathmini utekelezaji wa Dira za Taifa za Maendeleo za Tanzania Bara
na Zanzibar; Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara
(MKUKUTA II); Mkakati wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA II); na
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2011/12 – 2015/16. Vilevile
taarifa zitakazopatikana zitatumika kupima maendeleo ya utekelezaji wa
Malengo ya Milenia (Millenium Development Goals) yaliyowekwa na Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2000. Kama tujuavyo, itakapofika mwaka
2015 ndicho kilele cha utekelezaji wa Malengo hayo hivyo kujua hatua
tuliyofikia sasa itasaidia kujipanga vizuri katika miaka mitatu
iliyosalia.
Ndugu Wananchi;
Pamoja
na faida hizo, taarifa za Sensa hii zitasaidia kufanikisha zoezi
linaloendelea sasa, la kuwapatia Watanzania vitambulisho vya taifa.
Baadhi ya maswali yatakayoulizwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi
yatasaidia katika kuhakiki maombi ya vitambulisho vya taifa. Bila ya
shaka sote tunatambua vyema manufaa ya vitambulisho vya taifa, hivyo
basi ndugu yangu, shiriki zoezi la sensa ili kuirahisishia Serikali kazi
ya utoaji wa vitambulisho kwa raia wake.
Ndugu wananchi;
Shughuli
yoyote kukabiliwa na changamoto mbalimbali ni jambo la kawaida. Lakini,
tofauti na miaka ya nyuma, Sensa ya mwaka huu imekabiliwa na changamoto
ambazo hazijawahi kuwepo. Kuna baadhi ya wenzetu wamekuwa wanafanya
jitihada za makusudi za kutaka kulivuruga zoezi la Sensa nchini.
Wamekuwa wanawashawishi watu wasishiriki kuhesabiwa, kwa sababu ambazo
baadhi yake hazina uhusiano wo wote na Sensa. Zipo sababu nyingine
ambazo hata haziingii akilini. Kwa mfano, wapo watu wanaodai kuwa
hawatashiriki Sensa mpaka mjusi aliyeko kwenye Jumba la Makumbusho kule
Berlin, Ujerumani atakaporudishwa. Kinachozungumzwa hapa ni mabaki ya
mifupa ya mnyama wa kale aliyekuwepo hapa nchini zaidi ya miaka milioni
200 iliyopita. Mwaka 1906 wana sayansi wa Kijerumani waliyagundua mabaki
hayo kule Tendaguru, Lindi, wakayafukua na kuyapeleka Ujerumani ambako
yamehifadhiwa tangu wakati huo.
Ndugu Wananchi;
Kudai
mifupa hiyo irejeshwe nchini si jambo baya, watu wataona wanyama wa
kale waliokuwepo wakati huo wanafananaje. Huenda pia kikawa kivutio cha
utalii. Hata hivyo, kugeuza kurejeshwa kwa mabaki hayo kuwa sharti la
kushiriki Sensa ni jambo ambalo mantiki yake siielewi. Watu wakisusia
Sensa kwa sababu hiyo itakuwa siyo tu haieleweki wala haielezeki, bali
hata watu wengine nchini na duniani watawashangaa. Lakini, jambo ambalo
ningependa wajiulize ni kuwa hivi hasa wanamsusia nani? Mjerumani au
wanajisusia wenyewe? Hivi kweli mtu uko tayari kuacha manufaa yako ya
maendeleo yapotee au yaathirike kwa sababu ya mjusi ambaye hata
akirejeshwa huna manufaa ya moja kwa moja? Hasara anapata nani sisi au
wao? Nawasihi, Watanzania wenzangu, tusiwasikilize watu wanaoeneza
maneno yahusuyo Mjusi au mambo mengine ya upotoshaji na uvurugaji wa
mambo yenye maslahi makubwa zaidi kwetu binafsi na nchi yetu. Tuachane
nao hawatutakii mema na wala hawaitakii mema nchi yetu. Nawaomba
tusitumie vibaya uhuru wa kutoa maoni.
Ndugu Wananchi;
Wapo
ndugu zetu wengine wanaotaka liongezwe swali la dini ya mtu katika
orodha ya maswali yatakayoulizwa katika Sensa ya mwaka huu. Wahusika
wakuu hasa ni baadhi ya viongozi na wanaharakati wa Kiislamu. Wao
wanasema bila ya swali hilo kuwepo, Waislamu wasikubali kuhesabiwa.
Wamekuwa wanafanya juhudi kubwa ya kuwashawishi Waislamu wawaunge mkono
katika msimamo wao huo. Nimesoma baadhi ya nyaraka na vipeperushi vyao
kuhusu madai hayo. Nilipata pia bahati ya kukutana na kuzungumza na
baadhi ya wanaharakati na viongozi wa harakati hizo. Nia yangu katika
kufanya hayo ilikuwa ni kutaka kuelewa kwa undani hoja na madai yao.
Yako mambo kadhaa yanayotajwa kama sababu, lakini ukweli ni kwamba jambo
linaloweza kuhusishwa moja kwa moja na Sensa, ni lile la takwimu za
idadi ya Waislamu, Wakristo na Wapagani zilizotolewa na Baraza la
Maaskofu Katoliki, Shirika la Utalii na Shirika la Utangazaji Tanzania.
Hawazikubali
taarifa hizo kwa hoja kwamba, Waislamu hawajawahi kuhesabiwa na watoaji
wa takwimu hizo. Kwa sababu hiyo hawaelewi ni kwa vipi watoe idadi ya
kuwa ni asilimia fulani Watanzania. Hawana ugomvi nao kuhusu takwimu za
Wakristo na Wapagani kwani huenda waliwahesabu. Kwa maoni yao, taarifa
hizo si za kweli na ni upotoshaji unaofanywa maksudi kwa sababu
wanazozijua watoaji wa taarifa hizo. Ili kuondoa upotoshaji huo,
wanaharakati na viongozi hao wa Waislamu wakataka swali la dini liwepo
katika Sensa hii ili ukweli ujulikane.
Katika
mazungumzo yangu na baadhi ya viongozi wa Waislamu niliwaambia kuwa
naelewa sababu na hoja za wao kukasirishwa na kutokuzikubali takwimu
hizo. Vile vile, niliwaeleza kuwa takwimu hizo si za Serikali bali ni za
mashirika hayo. Nilisisitiza kuwa takwimu za Serikali kuhusu idadi ya
watu hutolewa na Ofisi Kuu ya Takwimu na si chombo kingine chochote cha
Serikali. Bahati nzuri Ofisi Kuu ya Takwimu haijatoa takwimu hizo na
wala siyo chanzo cha takwimu zilizotolewa na mashirika hayo.
Walikozipata wanajua wenyewe. Taarifa hizo hazina ithibati yo yote na
ndiyo maana zinatofautiana. Niliwasihi waachane nazo, wazipuuze na
wakipenda watoe tamko la kuzikataa.
Ndugu Wananchi;
Niliwaambia
pia kuwa kuelekeza lawama kwa Serikali kwa ajili ya taarifa hizo ni
kuionea na kutoitendea haki. Vile vile kuibebesha dhima ya kuongeza
swali la dini ili kuyajibu mashirika hayo ni kuipa mzigo usiostahili.
Napenda, kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaotoa takwimu za namna
hiyo kutambua unyeti wake na kuepuka kufanya hivyo. Zinatuletea
mifarakano isiyokuwa ya lazima kama ilivyo sasa.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wetu, yaani Serikali, imekuwa vigumu kukubali maombi ya
kuliingiza swali la dini katika Sensa hii kwa sababu za kisera na
kiutekelezaji. Wakati wa ukoloni maswali ya rangi, dini na kabila la mtu
yaliulizwa katika Sensa. Baada ya uhuru, maswali hayo yaliulizwa katika
Sensa ya kwanza ya mwaka 1967 kwa vile ilikuwa bado inafuata misingi ya
kikoloni. Baada ya hapo ulifanyika uamuzi wa kisera wa kutokuuliza
maswali hayo kwani nia ya wakoloni kuuliza maswali yale ilikuwa ni kwa
sababu ya sera yao ya wagawe uwatawale. Walitoa huduma kwa ubaguzi, sera
ambayo Serikali zetu ziliachana nayo baada ya Uhuru na Mapinduzi.
Huduma hazikuwa zinatolewa kwa ubaguzi wa rangi, kabila wala dini, bali
kwa msingi wa haki ya uraia na ubinadamu wake.
Ndugu Wananchi;
Sera
hiyo pia ilikuwa na lengo la kudumisha umoja na mshikamano wa taifa
letu na watu wake. Badala ya watu kubishana juu ya watu wa dini ipi ni
wengi na hivyo kufarakana kwa kutokubaliana na takwimu zilizotolewa,
sera mpya inawataka watu wajivunie uwingi wao kama Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Nionavyo
mimi Sera hii ni nzuri na kwamba ulikuwa ni uamuzi wa busara na hekima
kubwa. Tuendelee kuidumisha na kuienzi. Kufanya vinginevyo, na hasa
kuingiza sera ya kutoa huduma kwa misingi ya dini zetu ni kuliingiza
taifa letu ambalo lina sifa ya amani, upendo na utulivu, katika migogoro
isiyokuwa ya lazima. Ni migogoro inayoweza kuepukika kwa kuenzi na
kudumisha sera yetu hii nzuri na sahihi.
Ndugu Wananchi;
Sababu
ya pili inayotupa ugumu kiserikali ni ya kiutekelezaji. Imechukua miaka
kadhaa ya maandalizi mpaka kufikia hatua hii ya sasa ya kuwa tayari
kutekeleza zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Isitoshe
Sensa ya majaribio imeshafanyika kwa kutumia vifaa, madodoso na maswali
yaliyopo na marekebisho kufanywa baada ya hapo. Kuingiza mambo au jambo
jipya sasa itakuwa viguku kiutekelezaji. Kutachelewesha zoezi zima na
kusababisha hasara kubwa kwa taifa.
Kwa
vile watu wote hawataulizwa swali la dini na kwa kuwa dini si kigezo
cha kutoa huduma kwa wananchi, hakuna ulazima wa kusisitiza swali hilo
liwepo. Napenda kuwasihi ndugu zangu wanaokereketwa na jambo hili waache
kuling’ang’ania na badala yake wajitokeze kuhesabiwa. Tujitokeze
kuhesabiwa ili na Waislamu nao wawemo katika idadi ya wananchi wa
Tanzania.
Ndugu Wananchi;
Sioni
ulazima wa kuunda Tume Huru ya Sensa yenye uwakilishi sawa wa Wakristo
na Waislamu. Tangu mwaka 1931 kazi ya Sensa imekuwa inafanywa na Ofisi
Kuu ya Takwimu nchini na ndipo ujuzi na maarifa yote yapo. Hata ukiamua
uiite Tume bado utawatumia watu hao hao, hivyo mabadiliko hayo hayana
sababu. Vile vile, sioni haja ya kuwa na mgao wa wafanyakazi wake kwa
msingi wa dini kwa sababu Sensa siyo kwa ajili ya kujua Wakristo na
Waislamu. Huduma hazitolewi kwa misingi ya dini za watu.
Ndugu Wananchi;
Katika
maelezo yao kwangu, hivi karibuni Kamishna wa Sensa, Hajat Amina Mrisho
Said na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Muungano, Mama Albina Chuwa
walinieleza kwamba kwa kawaida katikati ya Sensa moja na nyingine,
hufanyika utafiti wa kidemografia, yaani Demographic Survey. Huu ni
utafiti wa kina unaofanywa katika ngazi ya kaya ambapo taarifa za mambo
mengi yahusuyo watu ambazo hazikusanywi, katika Sensa hukusanywa. Mara
ya mwisho utafiti huo kufanyika ilikuwa mwaka 1973, yaani baada ya Sensa
ya mwaka 1967 na kabla ya ile ya mwaka 1978. Ni makusudio ya Ofisi ya
Taifa ya Takwimu kuanzisha tena utaratibu huo mwaka 2016 ambapo baadhi
ya masuala yaliyoachwa yanaweza kujumuishwa. Subira yavuta heri.
Ndugu Wananchi;
Nimehakikishiwa
na mamlaka zinazohusika kuwa maandalizi ya sensa yamefikia hatua nzuri
na zoezi liko tayari kuanza siku ya Jumapili, tarehe 26 Agosti, 2012.
Lakini, mafanikio ya zoezi lenyewe yatategemea sana ushiriki wa watu
ambao ndiyo walengwa na wadau wengine. Naomba nitumie fursa hii kuwataka
Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa
Halmashauri za Wilaya na Miji na wadau wengine wa kisiasa na kiutendaji
wa ngazi mbalimbali waendelee kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za
Sensa katika maeneo yao ya uongozi. Hawana budi kuhakikisha kuwa zoezi
linakuwa na mafanikio makubwa. Wale wote wanaofanya vitendo vya kuvuruga
zoezi hili wachukuliwe hatua stahiki za kisheria.
Nawaomba
viongozi wa kisiasa na kijamii nao waendelee kuwahamasisha na
kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa na
kushirikiana na Makarani wa Sensa watakapokuwa wanafanya kazi yao.
Wakumbusheni kukataa kuwasikiliza au kuwafuata watu wanaowashawishi
wasijitokeze kuhesabiwa. Watu hao si wema wao na wala hawaitakii mema
nchi yetu.
Ndugu wananchi;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama sitawapongeza Hajat Amina Mrisho Said, Kamishna
wa Sensa wa Tanzania Bara na Ndugu Mwalim Ameir, Kamisaa wa Sensa
Zanzibar kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya ya kutoa uongozi
wa kisiasa, kusimamia na kuratibu zoezi la Sensa nchini. Nawapongeza
pia Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Mtakwimu Mkuu wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na watendaji wengine wa Sensa
katika ngazi mbalimbali katika Mikoa, Wilaya, Majimbo, Tarafa, Kata,
Mitaa, Vijiji na Shehia kwa kazi nzuri ya matayarisho na uendeshaji wa
Sensa ya mwaka 2012. Nawatakia mafanikio mema katika kazi hii muhimu na
adhimu kwa nchi yetu na watu wake.
Ndugu
zangu, Watanzania wenzangu, nawaomba sote tuwaunge mkono ndugu zetu
hawa kwa kushiriki katika zoezi la Sensa kuanzia siku ya Jumapili tarehe
26 Agosti, 2012. Haya shime sote tujitokeze kuhesabiwa kwani kujitokeza
kwetu ndiyo ukamilifu na mafanikio ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka
2012. Ewe Mtanzania mwenzangu shiriki Sensa kwa maendeleo yako na ya
taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Asanteni kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment