Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
26/8/2012, Lilongwe, MALAWI.
Tanzania
imeitaka Malawi kusitisha shughuli za utafiti katika eneo la ziwa Nyasa
lenye mgogoro na kusisitiza nia yake ya kuendelea kuzungumza na nchi
hiyo kuhusu mgogoro wa mpaka licha ya nchi hiyo kuendelea na msimamo
wake wa kumiliki eneo lote la ziwa hilo.
Hayo
yamebainishwa katika mkutano wa wataalam na viongozi kutoka serikali
ya Malawi na Tanzania kushindwa kufikia muafaka uliokusudiwa kuhusu eneo
halali la mpaka unaotenganisha nchi hizo.
Akizungumza
wakati wa kuhitimisha kikao cha usuluhishi kilichohusisha timu za
wataalam na viongozi wa wizara husika wa nchi hizo kilichomalizika jana
usiku mjini Lilongwe Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa
wa Tanzania Bernard Membe amesema Tanzania bado inaamini katika
mazungumzo ili kufikia muafaka wa kudumu wa mgogoro huo.
Amesema
kuwa pamoja na sababu mbalimbali zilizotolewa na upande wa serikali ya
Malawi juu ya umiliki wa eneo lote la ziwa Nyasa ,msimamo wa Tanzania
juu ya mpaka unaozitenganisha nchi hizo uko wazi kwa kwa kuzingatia
vielelezo vya historia vilivyoachwa na wakoloni na sheria za kimataifa
kuhusu mpaka kuwa katikati ya ziwa hilo.
Ameeleza
kuwa licha ya serikali ya Malawi kuonyesha kila dalili za kukwamisha
mazungumzo hayo yaliyoanza kupitia vikao mbalimbali nchini humo viongozi
wa nchi hizo kupitia mkutano wa kutafuta suluhu uliomalizika jana
usiku wameamua kuunda timu za wataalam
“Licha
ya kuwasilisha vielelezo kuonyesha uhalali wa mpaka hatukuweza kufikia
muafaka tumefika mahali pa kuhitaji msaada tuzitume tume za nchi zetu
zitoe mapendekezo ya nini kifanyike maana kuna kila dalili kwamba sisi
wenyewe tutashindwa kuendelea zaidi “
Amesema
kuwa wataalam kutoka Malawi na Tanzana watakutana mwezi Septemba jijini
Dar es salaam ili waweze kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuwapata
wasuluhishi wa mgogoro huo pamoja na kutoa mapendekezo ya faida na
hasara ya njia watakazozipendekeza.
“
Sasa tumefika mahala pa kuhitaji msaada,tutazituma timu zetu zikae
pamoja na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike maana inaonyesha wazi
kabisa sisi wenyewe hatutaweza kuendelea tena sasa timu zitatoa
mapendekezo juu ya kesi hii tuwaite wazee wenye busara barani Afrika
tunaowaamini watuamulie” amesema.
Amefafanua
kuwa timu za wataalamu zitakazoundwa zinatarajia kukutana mwezi
Septemba jijini Dar es salaam ili kutoa mapendekezo ambayo yatapelekwa
kwa marais wa nchi hizo katika kuelekea hatua ya pili ya utatuzi wa
mgogoro huo ikiwemo kumtafuta msuluhishi au kwenda kwenye mahakama ya
Kimataifa.
Aidha
, Tanzania imeitaka Malawi kusitisha shughuli za utafiti katika eneo la
Tanzania katika ziwa Nyasa lililo na mgogoro na kukisisitiza kuwa
mchakato wote wa kutafuta suluhu utaendeshwa kwa amani na utulivu huku
akiwaomba watanzania kuendelea kuiombea nchi amani ili suala hilo
limalizike kwa amani ,utulivu na undugu.
Kwa
upande wake waziri wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya kimataifa wa Malawi
Bw. Ephraimu Chiume katika maelezo yake wakati wa kuhitimisha mkutano
huo amesisitiza kuwa licha ya mgogoro huo kuhitaji busara zaidi bado
serikali yake inaamini kuwa mpaka kati yake na Tanzania uko upande wa
mashariki mwa ziwa Nyasa na unatenganishwa na ardhi ya Tanzania.
Amesema
kutokana na unyeti wa suala lenyewe na eneo hilo pamoja na historia ya
nchi yake anapenda kuona ufumbuzi ukipatikana haraka ili wananchi wa
nchi mbili waweze kuendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.
“Ni
matumaini yangu mkutano wa Dar es salaam utaofanyika mwezi Septemba
utazaa matunda ili suala hili lipatiwe ufumbuzi na ikiwezekana tupate
msaada wa sheria za kimataifa kwa sababu suala hili liko kisheria zaidi”
alisisitiza Bw. Chiume.
Ujumbe
wa wataalam kutoka Tanzania uliokuwa ukitafuta suluhu ya mgogoro huo
uliwahusisha makatibu wakuu Patrick Lutabanzibwa (Ardhi),John
Haule(Mambo ya nje) na mawaziri wa wizara ya Ardhi Prof. Anna Tibaijuka
na Bernard Membe wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa, balozi wa
Tanzania nchini Malawi Patrick Tsere pamoja na wataalam wanaotoka eneo
la ziwa Nyasa akiwemo Prof.Hemphrey Kamisama ambao nao walitoa maelezo
kueleza hisia za wananchi wa eneo hilo na uhalisia wa ziwa hilo.



No comments:
Post a Comment