| Waandishi Wetu, Moshi na Mwanza |
SIKU chache baada ya gazeti hili kuripoti kuibuka kwa kundi la majambazi wanaoua kwa kutumia sindano za sumu, kkisha upora wananchi, olisi mkoani Kilimanjaro imejibu mapigo na kuua watu watano wanaotuhumiwa kuwa washirika wa kundi hilo.
Watuhumiwa
hao ambao walikutwa na sanduku (Briefcase) lenye mabomba ya sindano na
uzi wa kushonea majeraha makubwa, waliuawa usiku wa kuamkia jana katika
kile polisi walichoeleza kuwa ni katika harakati za kurushiana risasi na
majambazi hao.
Katika tukio hilo, polisi mmoja PC
Lameck mwenye nambar G406 alijeruhiwa mguu wa kushoto na chembechembe za
risasi zilizokuwa zikifyatuliwa na majambazi hao.
Tukio hilo lililotokea,
siku chache baada ya Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP) kuwataka
polisi kujibu mapigo kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya ujambazi
jimboni kwake, lilitokea Kijiji cha Kyala eneo la Marangu, wilayani Moshi Vijijini.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema licha ya kurushiana
risasi, polisi walilazimika kurusha bomu la machozi ndani ya nyumba
walimokuwa wamejificha washirika wa kundi hilo.
Boaz alisema baada ya kupekuliwa majambazi hao,
walikutwa na bunduki aina ya Shotgun Greener yenye namba 858356 ikiwa
na risasi nne na maganda ya risasi, bastola aina ya Browning na risasi
mbili na risasi 10 za bunduki aina ya SMG.
Licha ya
silaha hizo, majambazi hao walikutwa pia na mapanga na sime zilizokuwa
na damu, zana mbalimbali za kuvunjia, mali mbalimbali zinazodaiwa
kuporwa kwa watu na nyama za mbuzi na kondoo.
Waliouawa
wametambuliwa kuwa ni Paul Baltazar (25), mmiliki wa nyumba walimokuwa
wamejificha majambazi hao na Remius Msambure (30), Focaus Mtui (35) na
mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Elias, huku maiti moja ikiwa haijatambuliwa.
Akifafanua
kuhusu tukio hilo, Boaz alisema juzi saa 7:00 usiku wa kuamkia jana,
polisi walipokea taarifa kuwa Kijiji cha Kitowo Marangu, kundi la
majambazi watano lilikuwa limevamia duka la mfanyabiashara aliyetajwa
kuwa ni Gaudence Temu.
Katika tukio hilo, majambazi
hao walimjeruhi kwa mapanga mlinzi aitwaye Hamis Mnyaru (25) kabla ya
kuwashambuliwa walinzi wa jadi maarufu kama Sungusungu waliotajwa kuwa
ni, Richard Temu (33) na Erick Yuda (30) ambao walijitokeza kutoa msaada.
Kamanda Boaz alisema ufuatiliaji wa kina ulifanyika ili kubaini maficho yao na kugundua kuwa, walikuwa wakijificha katika nyumba Kijiji cha Kyala ndipo walipokwenda na kuvamia wakiwataka wajisalimishe lakini wakakataa.
Alisema
polisi walilazimika kujibu mapigo na kufanikiwa kuwaua kwa risasi
watuhumiwa watano wakati wakijaribu kutoroka kutoka katika nyumba hiyo.
Katika tukio linguine, Ofisa Uhamiaji
Mkoa wa Mwanza, Albert Buchafwe amenusurika kuuawa kwa risasi baada ya
kudaiwa kushambuliwa na Mkuu Msaidizi wa Kituo cha Polisi Nyakato,
Abubakar Zebo kwa madai kuwa walikuwa wakishambulia jambazi.
Tukio
hilo ambalo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,
Liberatus Barlow linadaiwa kutokea saa 4:13 usiku wakati ofisa wa
uhamiaji akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake, alikutana na gari ndogo
aina ya Suzuki lililomwashia taa likimuashiria kusimama.
Akielezea
mkasa huo, Buchafwe alisema baada ya kuwashiwa alipochunguza kwa makini
gari hilo alibaini kuwa ni lile linalotumika na ofisa huyo wa polisi,
hivyo alisimama na kujitambulisha kwake akiwa ndani ya gari lakini
aliamuriwa kuzima taa za gari lake na kutoka ndani.
“Nilitii
nikazima taa, lakini nilisita kutoka katika gari langu,
nilijitambulisha kwamba ni ofisa uhamiaji na kumtaja jina ofisa huyo (wa
polisi), ambaye aliendelea kunilazimisha kushuka ndani ya gari huku
nikiona akijiweka sawa ikiwamo kuandaa bastora tayari kushambulia,”
alisema.
Alisema wakati akiwa bado anajitambulisha,
alishuka askari aliyekuwa na sare katika gari hilo la ofisa wa polisi
akiwa na silaha ya SGM, hali ambayo ilimlazimu kugeuza gari haraka na
kukimbia huku gari lake likishambuliwa nyuma kwa risasi.
Buchafwe
alisema amepata na mashaka na tukio hilo kutokana na askari huyo
aliyehusika kuwa na uhusiano wa karibu na mkewe, ambaye wamekuwa na
ugomvi naye pamoja na kesi ya kutalikiana mahakamani na kwamba, huenda
halikuwa la bahati mbaya.
“Nina kesi na mke wangu
mahakamani,ofisa huyu wa polisi amekuwa na uhusiano wa karibu na mke
wangu ambaye tunashtakiana mahakamani, inanishangaza mtu ambaye
ananifahamu licha ya kujitambulisha bado alikuwa akishilikilia msimamo
wa kunitaka kushuka, nadhani hapa kuna jambo zaidi ya hali ilivyo,”
alieleza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Leberatus
Barlow alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba, ana uhakika ni bahati
mbaya kwani jeshi lake lilipata taarifa za Kiintelijensia za kuwapo kwa
majambazi wakidaiwa kutumia gari sawa na la ofisa huyo.
“Hili
ni tukio la bahati mbaya, jeshi letu lilipata taarifa za Kiintelijensia
juu ya kuwapo kwa majambazi na kuamua kuweka mtego, sasa ofisa huyu
alifika muda na wakati ambao askari wetu walikuwa eneo hilo na kuingia
mtego wetu, alikuja na gari ambalo ni sawa na lile ambalo tulielezwa
lingetumika, lakini bahati nzuri mauaji hayakutokea,” alisema.
Imeandikwa na Daniel Mjema, Rehema Matowo, Moshi na Frederick Katulanda, Mwanza
CHAZO: http://www.mwananchi.co.tz
|



No comments:
Post a Comment