|
KAMATI iliyoundwa na
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi kuchunguza kifo cha
mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daud
Mwangosi juzi ilikabidhi ripoti yake kwa waziri huyo, lakini kwa
mshangao wa wengi ripoti hiyo ilibakia kuwa siri ya Serikali kwa maelezo
kuwa, kesi ya mauaji hayo tayari iko mahakamani na kwamba kuiweka
hadharani kungegusa mambo ambayo yangeingilia mwenendo wa kesi hiyo. Badala yake vyombo vya habari vilipewa kile Kamati hiyo ilichokiita Muhtasari wa Uchunguzi wa Kifo cha Mwangosi wenye kurasa 10 za maelezo ya jumla tu na yenye kujirudiarudia, tena mara nyingine kwa mafumbo. Kwa mfano, katika muhtasari wake, Kamati hiyo iliyokuwa chini ya Jaji mstaafu Steven Ihema ilipendekeza nafasi za wakuu wa wilaya na mikoa ‘ziangaliwe upya’ kwa maelezo kwamba zinatumika kisiasa. Hapa maana ya nafasi hizo kuangaliwa upya ni kama fumbo analofumbiwa mjinga. Hata hivyo, pamoja na muhutasari wa ripoti hiyo kuelekeza lawama kwa baadhi ya watu wasiohusika, sehemu ya muhtasari wa ripoti hiyo imetenda haki. Kwa mfano, pamoja na mambo mengine, sehemu hiyo inasema nguvu iliyotumiwa na polisi kuwatawanya wafuasi wa Chadema siku ya tukio ilikuwa kubwa kupita kiasi na kuwa, licha ya kwamba utumiaji wa mabomu haukufanywa kwa weledi, pia matumizi ya silaha hizo hayakuwa ya lazima. Hali hiyo iliamsha ghadhabu ya wananchi wengi ambao kupitia katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii waliituhumu Serikali kwamba ilikuwa inaficha ukweli kuhusu kifo hicho kwa kuzingatia kwamba kesi za aina hiyo hutumia miaka nyingi kutolewa hukumu. Kwa maana hiyo, wananchi walihisi kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wa matumaini yao ya kupata undani wa kifo cha mwanahabari huyo aliyeuawa akiwa mikononi mwa polisi. Lakini ghadhabu ya wananchi ilichochewa na ripoti za kamati nyingine tofauti zilizoundwa katika nyakati tofauti kuchunguza mazingira ya kifo cha mwandishi huyo kutokana na vurugu zilizotokea Septemba 2 mwaka huu katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi mara baada ya polisi kuwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakifungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho. Baraza la Habari Tanzania (MCT), nalo juzi lilianika ripoti yake kuhusu kifo hicho ambayo ilisema mauaji hayo yalifanywa na polisi kwa makusudi kutokana na uhasama ambao umekuwapo kwa muda mrefu baina ya waandishi na polisi mkoani Iringa. Pia ripoti hiyo ilisema mwandishi huyo aliuawa mikononi mwa polisi chini ya usimamizi wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na kwamba hiyo inathibitishwa na maelezo pamoja na ushahidi uliokusanywa kwa kutumia picha za video na ushahidi mwingine muhimu wa taarifa za vyombo vya habari. Wakati hayo yakitokea, Tume ya Haki za Binadamu jana ilizindua ripoti yake kuhusu mauaji ya mwandishi huyo na kumlaumu Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda na kusema kupitia kwa mwenyekiti wake, Jaji Kiongozi mstaafu, Amiri Manento kwamba alikosea kisheria kutengua amri ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi ambaye awali alikuwa ametoa kibali kwa Chadema kufanya shughuli ya kufungua matawi ya chama hicho pasipo kufanya maandamano. Taasisi nyingi zimetoa kauli za kukosoa Serikali na Kamati ya Jaji Ihema kwa kuficha ripoti hiyo. Kwa mfano, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema kukataa kutoa ripoti hiyo hadharani na badala yake kutoa muhtasari wake ni makosa makubwa ambayo hayasahameki. Pamoja na kukiri kwamba Kamati hiyo iliyoteuliwa na Waziri Nchimbi imefanya kazi nzuri katika baadhi ya maeneo, tunalazimika kusema kwamba ilipaswa kuishauri Serikali kuitoa ripoti hiyo hadharani badala ya kuishauri kuificha kabatini kwa kisingizio cha kesi iliyopo mahakamani. Tunadhani kwamba hatua hiyo imewanyima wananchi fursa ya kupata habari na hakika huo siyo utawala bora.
CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz
|
Kifo cha Mwangosi bado ni kitendawili
Tag:




No comments:
Post a Comment