MKUU
WA MKOA WA DAR ES SALAAM ATOA TAMKO NA KUSEMA SHERIA NA KANUNI ZA NCHI
LAZIMA ZIFUATWE, MIHADHARA IMESIMAMISHWA MPAKA HALI ITAKAPOKUWA SALAMA
NA JESHI LA POLISI LIMEJIPANGA VEMA KATIKA KUKABILIANA NA VURUGU
ZITAKAZOJITOKEZA.
Na Adrophina Ndyeikiza-Ofisi ya Mkuu wa Mkoa DSM
19/10/2012
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Said Meck Sadiki amekutana na waandishi wa habari leo asubuhi katika Ofisi yake na kutoa tamko kuhusu vurugu zinazoendelea kujitokeza katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mhe.Mkuu wa Mkoa amesema kuwa kumeibuka vitisho vya hapa na pale katika
Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kukamatwa kwa Sheikh Issa Ponda ambaye
anajulikana kama Katibu wa Baraza kuu na Taasisi za Jumuiya ya Kiislamu.
“Mpaka sasa wametoa taarifa kuwa kutakuwepo na maandamano ya kuelekea
Ikulu ili kushinikiza kuachiwa huru kwa Sheikh Issa Ponda na wafuasi
wake”.Alisema Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Maandamano hayo hayana kibali chochote kile ni kutaka kuibua vurugu na
uvunjifu wa amani kwa wana Dar es Salaam.
Hivyo basi nawaomba wananchi wa
Dar es Salaam kutokushiriki katika maandamano hayo kwani kwa kufanya
hivyo sheria kali zitachukuliwa dhidi ya waandamanaji kwani maandamano
hayo ni Haramu na hayana kibali wala tija kwa Taifa letu.Alisisitiza
Mkuu wa Mkoa.
Aidha,Mkuu wa Mkoa alisema kuwa lazima tufike mahali tuishi kwa kufuata
misingi ya taratibu na sheria za taifa letu kwani Sheikh Ponda
hakukamatwa kama Sheikh bali kama mchochezi wa vurugu na kuwashawishi
wafuasi wake kuidharau Serikali na vyombo vya usalama.Hivyo amekamatwa
kama mtuhumiwa mwingine yoyote anayeweza kukamatwa.
Hivyo basi yatupasa tuwe na subira na kufuata taratibu husika kwani kama
Sheikh Issa Ponda hana hatia basi ataachiwa na kama ana hatia basi
atahukumiwa kama ilivyo kawaida kwa mtuhumiwa yoyote yule akipatikana na
hatia.Hivyo basi lazima tujue kuwa nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya
taratibu na sheria na hakua aliye juu ya sheria.Sheria ipo na lazima
ifuatwe.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema Mihadhara yote ya
kidini kwa sasa imesimamishwa kwa kipindi hiki kigumu mpaka hapo hali
itakapokuwa shwari.
NAYE SHEIKH WA MKOA WA DAR ES SALAAM- Sheikh Alhadi Mussa amewataka
waumini wa dini ya kiislamu kuwa na subira katika kulitatua suala hili
na wasijipange kufanya vurugu ya aina yoyote kwani suala hilo
limeshafika katika vyombo vya sheria hivyo tuviachie vyombo hivyo
vifanye kazi yake na haki itakuja kujulikana.
Aidha Sheikh huyo amesema kuwa ameridhishwa na maneno ya maaskofu katika
kuwataka waumini wao kuwa na utulivu na si kulipiza kisasi kwani.Lakini
pia amewataka waislamu nao watulie katika hilo.
NAYE PADRI ANTHONY MAKUNDE –Katibu Mkuu wa Balaza la Maaskofu(Tech)
amesema kuwa anaungana na viongozi wengine wa makanisa katika
kuwasisitiza viongozi wa Dini ya Kikristo kuendelea kuwa na subira
katika kipindi hiki kwani njia pekee na sahihi ya kutafuta suluhu na
amani ni njia ya mazungumzo.
KWA UPANDE WA KAMANDA WA POLISI WA MKOA WA DAR ES SALAAM- Suleimani
Kova amesema kuwa Jeshi la Polisi limeungana na Mhe.Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam katika kukabiliana na vurugu zitakazojitokeza katika Mkoa wa
Dar es Salaam.Aidha mtu yeyote akifanya kosa anachukuliwa kama mharifu
kwa sababu sheria haibagui wala kuchagua yenyewe inakata kotekote
haiangalii kama ni Padri au Sheikh.
Kuhusu maandamano hayo yaliyopangwa
Kamanda kova amesema kuwa Jeshi la
Polisi limejipanga vema katika kukabiliana na hilo hivyo mtu yeyote
akitaka kuandamana ajitahidi kutafakari mara mbili mbili itakuwaje baada
ya hapo kwa yeye na familia yake.
Mwisho kabisa kamanda Kova amewataka watu hawa wajisalimishe wenyewe kwa
jeshi la polisi ama sivyo sheria itachukua mkondo wake.Nao ni kama ifuatavyo;
- Mukadam Salehe
- Kondo Juma
- Saaban Mapeo
- Jaffary Mneke -
- Rajabu Katimba -
- Amani Moshi



No comments:
Post a Comment