|
VITUKO
vimeendelea kutawala uchaguzi wa ndani ya CCM katika wilaya na mikoa
mbalimbali huku baadhi ya maeneo ya uchaguzi yakiingia dosari, na
makada kushutumiana kwa sababu mbalimbali.
Habari kutoka Morogoro zinasema Mwenyekiti Mstaafu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ( UVCCM), Mkoa wa Morogoro, Jonas Nkya amewalalamikia viongozi wa CCM mkoani wakiwamo wabunge, wajumbe wa Nec na Mawaziri kwa kutowajali vijana wanapokuwa na shida. Akizungumza mbele ya waandishi wa habari wakati uchaguzi wa viongozi wa UVCCM mkoa ukiendelea, Nkya alisema viongozi hao wanaitelekeza jumuiya wakati wa shida. Pia alizungumzia kasheshe ya vijana kutoka wilaya mbili za Ulanga na Kilombero waliogomea uchaguzi kwa saa zaidi ya mbili kwa madai ya kukosa chai. Nkya alisema uchaguzi huo ulikuwa mgumu kutokana na viongozi mbalimbali waliokuwapo mkoani hapa wakiwamo wabunge kutowachagia katika uchaguzi huo pamoja na kutoa ahadi zao wakati walipoombwa kuchangia kabla ya uchaguzi huo. Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa mkutano huo walizungumzia kuwapo kwa watu wenye umri mkubwa unaopingana na katiba ya mwanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM. Ilielezwa kwamba katiba hiyo inasisitiza kwamba wanachama wote watakuwa chini ya uimri wa miaka 35, lakini katika mkutano wa uchaguzi walikuwapo wajumbe wenye umri wa miaka 50. Mwandishi wa habari alifanya mazungumzo na Anna Fednandi (50) ambaye ni mjumbe wa UVCCM kutoka Wilaya ya Morogoro vijijini akiwa kama mpiga kura juu ya uchaguzi ambapo alisema uchaguzi ulikuwa mzuri na kwamba umefanyika kwa huru na haki. Akizungumzia suala la umri kwa wanachama wa UVCCM, Anna alisema kuwa pamoja na UVCCM kuweka kigezo cha umri kwa wanajumuiya wake, lakini kinachosababisha wenye umri mkubwa waendelee kuongoza ni vijana wengi kutojitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali. Katika hatua nyingine habari kutoka Dodoma zinasema uchaguzi wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Dodoma juzi ulimalizika kwa Salome Kiwaya kuibuka mshindi baada ya kumshinda mgombea mwenzake Judith Muyeya. Kiwaya alitangazwa kuwa mshindi baada ya kujizolea kura 553 huku Myeya akiambulia kura 206 katika uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa Chuo Cha Mipango nje kidogo ya Mji wa Dodoma. Akitangaza matokeo hayo kwa waandishi wa habari jana, Katibu wa UWT Mkoa wa Dodoma Kaundime Kasase alisema kuwa uchaguzi ulikuwa huru na haki na kwamba hakuna manung’uniko yaliyojitokeza. Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu kutoka Arusha anaripoti kwamba mabadiliko yameendelea kukikumba Chama Cha Mapinduzi(CCM), Mkoa wa Arusha, baada ya jana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake(UWT) wa Mkoa wa Arusha, Nebris Kimbele kushindwa kutetea nafasi hiyo. Kimbele ambaye ni mmoja wa vigogo wa CCM mkoa huo, alishindwa na Frola Zolote ambaye alipata kura 254 dhidi ya kura 201 za Kimbele. Uchaguzi huo, uliofanyika kituo cha mikutano cha Arusha(AICC) na kusimamiwa na Katibu wa CCM, Mkoa wa Arusha Mary Chatanda na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela. Akitangaza matokeo hayo, Chatanda alisema jumla ya wapigakura walikuwa ni 462 na kura moja tu ndiyo iliyoharibika. Awali akiomba kuchaguliwa tena, Kimbele aliahidi kujenga jengo la ghorofa la jumuiya hiyo na kuahidi kutoa semina zaidi kwa wanawake wa Arumeru ili kuwajengea uwezo. Naye Zolote alitumia maneno ya Biblia kujinadi na kujifananisha na Daudi ambaye alitumwa kuwakomboa wana wa Mungu huku pia akiwapigia magoti wajumbe na kuwaomba wamchague. Katika uchaguzi huo, Katibu mkuu wa zamani wa UWT, Halima Mamuya alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu Taifa, Lucy Bongele alichaguliwa kuwakilisha mkutano wa Wazazi . Mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Arusha, Namelok Sokoine akichaguliwa kuwakilisha jumuiya hiyo katika mkutano wa vijana (UVCCM) Habari hii imeandaliwa na Lilian Lucas,Morogoro, Habel Chidawali, Dodoma, |
Uchaguzi Ndani ya CCM Wazua Vituko Kulaumiana Kwingi
Tag:




No comments:
Post a Comment