Diwani Gwae Mbua wa kata ya Mwankoko akimlalamikia mhandisi wa ujenzzi manispaa
Singida Robert Massoro kwenye baraza la madiwani ktk ukumbi wa FDC na kufikia
azimio la kumkataa
Mkurugenzi wa manispaa Singida, Mathias Mwangu akijibu hoja anazolalamikiwa
mhandisi wa ujenzi Robert Massoro,kutoka kushoto ni naibu meya Hamisi Mkata,
meya Salum Mahami na kulia kabisa ni DAS wa Singida Celestin Onditi..
Pantaleo Sorongai, Diwani wa Mitunduruni akimlalamikia mhandisi wa manispaa
Singida Robart Massoro kutokana na utendaji mbovu wa kazi zake
BARAZA la madiwani
manispaa ya Singida limekataa kufanya kazi na mhandisi wa ujenzi wa halmashauri
hiyo, Robert Masoro kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kugombana na
wakandarasi, pia kutomudu usimamizi wa miradi ya ujenzi.
Azimio hilo
lilifikiwa jana na baraza hilo, lililokutana kwa muda wa siku mbili katika
ukumbi wa chuo cha maendeleo mjini hapa.
Akitangaza azimio
hilo, meya wa manispaa Singida, shekhe Salum Mahami alisema kutokana
na tuhuma mbalimbali dhidi ya mhandisi Masoro, kwa pamoja baraza limeamua
kutoendelea kufanya naye kazi kutokana na madhaifu mbalimbali.
“Baada ya baraza
kubadilika na kukaa kama kamati ya baraza, injinia Masoro hahitajiki tena
hapa…kumekuwa na matatizo na manyanyaso makubwa kati ya idara na wakandaras,
madiwani wamekosa imani naye, suala hili halikuletwa hapa ili afufukuzwe kazi
wala kusimamishwa kazi, bali imeleta pendekezo la kutohitahika tena katika
manispaa yetu,”alisema Shekhe Mahami.
Baada ya baraza
kusomewa taarifa hiyo, kwa pamoja madiwani wote waliunga mkono hoja hiyo, hivyo
kumaanisha mhandisi Masoro hahitajiki tena katika manispaa ya
Singida.
Awali baraza hilo
lilielezwa kati ya sababu zilizopelekea mhandisi Masoro akataliwe kufanya kazia
katika halmashauri hiyo ni, kushindwa kusimamia ujenzi wa daraja la Unyambwa kwa
mwaka mmoja sasa, pia daraja la Mwankoko.
Madiwani hao
wakiongozwa na Gwae Mbua, Shabani Sattu, Pantaleo Sorongai, Baltazar Kimario na
Khadija Simba,walimshutumu wazi mhandisi huyo kutokana tuhuma mbalimbali,
ikiwemo usimamizi mbovu ujenzi wa barabara ya Msufini, inayojengwa kwa lami.
Tuhuma zingine ni
ujenzi duni wa barabara ya Peoples Club iliyogharimu zaidi ya Sh. Milioni 39,
huku madaraja na mifereji ikiwa imejengwa chini ya kiwango.
Dosari zingine ni
ujenzi wa miundo mbinu ya barabara (madaraja) na kutoa vibali ovyo vya ujenzi
hata katika miradi ambayo yeye hahusiki, lakini akiwa na nia ya kuwekea
mazingira fulani yanayokwenda kinyume na maadili ya utumishi wa
umma.
Hata hivyo mhandisi huyo alipoulizwa na NIPASHE
kwa njia ya simu kuhusiana na tuhuma hizo alidai kuwa hawezi kufanya kazi na
watu wenye majungu na kwamba 'Singida siyo mwisho wa reli', anaweza kufanya kazi
sehemu yoyote nchini, siyo lazima iwe Singida.



No comments:
Post a Comment