Mkutano
wa 34 wa jumuiya ya Afrika ya Utawala wa Umma na Usimamizi Bora
(AAPAM) umeelezwa kuwa wa mafanikio makubwa zaidi tokea kuanzishwa kwa
Taasisi hiyo mwaka 1976.
Wajumbe
wa mkutano wa siku tano wa AAPAM wamesema idadi ya washiriki mwaka
huu wamekuwa wengi kupita mikutano mengine yote iliyofanyika kabla
kutokana na kila nchi kuwa na hamu ya kutuma wajumbe wake Zanzibar.
Wamesema
kuwa licha ya idadi kubwa ya wajumbe, wameridhishwa na maandalizi
mazuri yaliyofanywa na Serikali na wanategemea mkutano huo utaleta
mabadiliko makubwa ya utumishi ya umma kwa nchi za Afrika kutokana na
wataalamu wengi wa ngazi za juu kushiriki mkutano huo na kutoa mada
zao.
Wajumbe
hao ambao wamepata nafasi ya kutembelea sehemu mbali mbali za mjini na
mashamba wamesema Zanzibar inanafasi kubwa ya kupiga hatua katika
masuala ya kiuchumi na kijamii iwapo itaweza kutumia ipasavyo
rasilimali ilizonazo ikiwa ni pamoja na bandari, fukwe, matunda, bahari
na ardhi yenye rutuba.
Meneja
utawala wa kampuni kubwa nchini Lesothu, Majid Maan amesema
anashangazwa kusikia kwamba Zanzibar haisafirishi samaki wala matunda
nje ya nchi wakati sehemu zote walizopita zimezungukwa na miti ya
matunda.
“Sisi
kule Lesothu na baadhi ya nchi jirani tunahitaji sana maembe na
ndizi na Zanzibar matunda haya yapo ya kutosha kwanini Wafanyabiashara
wa hapa wasijitoe kutafuta soko sehemu hizi,” aliuliza Meneja Majid.
Alitoa
rai kwa Serikali kupitia Wizara inayohusika na Biashara kutumia Umoja
wa nchi za Kusini mwa Afrika SADDEC na Jumuia nyengine za Magharibi na
Kusini mwa Afrika kujitangaza na amesema anauhakika mazao ya Zanzibar
yananafasi kubwa ya kupata soko la uhakika.
Baadhi
ya wajumbe wameishauri Serikali kuanzisha uvuvi wa bahari kuu baada ya
kushuhudia wavuvi wengi wa Bandari ya Nungwi wakirudi kuvua wakiwa na
samaki wadogo huku visiwa vya Zanzibar vikiwa vimezungukwa na
bahari kuu yenye samaki wengi wakubwa.
Mkutano
huo unatarajiwa kufungwa kesho wakati wa mchana na kabala ya kufungwa
rasmi itatangazwa nchi itakayo kuwa mwenyeji wa mkutano ujao wa 35.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR



.jpg)
No comments:
Post a Comment