DOZI 35,000 kati ya 78,000 za dawa ya kutibu
malaria aina ya Artequick, zilizotolewa kama msaada kwa Tanzania na
Serikali ya China, zimepotea katika mazingira ya kutatanisha, Mwananchi
imebaini.
Imebainika kuwa dawa hizo zilizokuwa zigawiwe bure
kwa wagonjwa katika hospitali za Serikali nchini, sasa zinauzwa kwa
kati ya Sh9,000 hadi Sh12,000 kwenye maduka na hospitali binafsi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na
kuthibitishwa na vyanzo vya kuaminika zinabainisha kuwa, dawa hizo
zimeibwa, au zikisafirishwa kwenda Zanzibar au baada ya kufikishwa huko
na sasa zinauzwa mitaani.
"Dawa zilipofika dozi hizo 35,000 ilionekana
zipelekwe Zanzibar kwanza halafu zinazofuata zisambazwe mikoa ya
Tanzania Bara, lakini cha ajabu hivi sasa dawa hizo zinauzwa katika
maduka ya jumla ya dawa na ya rejareja," kimeeleza chanzo hicho.
Chanzo hicho kinabainisha kuwa, paketi za dawa
hizo zilikuwa zimeandikwa pembeni 'Not for Sale’ (siyo kwa ajili ya
kuuzwa) ambayo yamefutwa kwa kupakwa rangi nyekundu ili yasionekane.
Mkurugenzi wa Tiba katika Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA), akizungumza kupitia kwa Ofisa Uhusiano wa mamlaka hiyo,
Gaudencia Simwanza alikiri kukamatwa kwa dawa hizo za msaada kutoka
China ambazo zilikuwa zinauzwa mitaani na kueleza kuwa, wapo katika
uchunguzi.
Ni kweli tumekamata dawa hizo za msaada
zilizotolewa na China kwa ajili ya hospitali za Serikali nchini na
zilizoibwa ni zile zilizotakiwa kusambazwa Zanzibar," alisema Simwanza
na kuongeza kuwa, ni mapema mno kueleza kiasi cha dawa kilichokamatwa.
Simwanza aliongeza kuwa, kimsingi dawa hizo
zimekutwa katika eneo ambalo hazitakiwi kuwepo na kwamba hilo ni kosa
kisheria na hali hiyo inaashiria kufanyika kwa wizi.
“Kukutwa na mali ya wizi ni kosa kisheria, kwahiyo
tunafanya uchunguzi zaidi ili kubaini kiasi cha wizi ambao
umefanyika,”alisema Simwanza.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD),
Cosmas Mwaifwani alikiri kupokea dawa hizo za msaada kutoka China na
kwamba, boksi zote 88 zilizopokewa zipo salama.
“Ni kweli tumepokea dawa hizo boksi 88 sawa na
paketi 35,000 lakini dawa zote zipo salama na hatujaanza kuzisambaza,”
alisema Mwaifwani na kuongeza kuwa msaada huo ulipokewa Novemba 6 mwaka
huu.
Alisema hajui hizo ambazo zinauzwa zikiwa
zimefutwa maandishi zimetoka wapi na kusisitiza kuwa walizonazo zina
maandishi ya ‘Not for Sale’ pembeni ya paketi.
Dawa hizo kulingana na uchunguzi wa Mwananchi zinauzwa kwa bei
ya Sh3,500 kwa dozi katika maduka ya jumla na reja reja ni hadi Sh10,000
kwa dozi na zilibainika baada ya wasamaria kuitaarifu TFDA.
Chanzo hicho kilibainisha kuwa, dawa zenye jina
kama hilo zimekuwa zikisambazwa na Bahari Pharmacy Ltd na zikiwa
zimepakwa rangi nyekundu pembezoni mwa paketi kuliwatia shaka, hivyo
walitoa taarifa TFDA.
"Dawa kama hizo zipo madukani, lakini hazijafutwa
pembeni na hizo ni zile ambazo zimeingizwa nchini kihalali na sio zile
za msaada" kimebainisha chanzo hicho.
"Ni aibu watu, hususan watoto kufa kwa malaria
wakati dawa zinaibiwa," kilibainisha chanzo hicho na kuongeza kuwa, nia
njema ya Serikali ya China inataka kukwazwa na watendaji wa wizara na
wafanyabiashara wasio waadilifu.
Mkurugenzi wa Bahari Pharmacy Ltd, Churchill
Katwaza alipoulizwa kuhusiana na dawa hizo, alikiri kuwa kampuni yake
kuagiza aina hiyo ya dawa na alishangaa kusikia zile za msaaada kutoka
China zimeibwa.
"Hata mimi nimesikia kuwa, TFDA wamekamata dawa
zinazofanana na tunazosambaza sisi na zimefutwa pembeni kwa rangi
nyekundu," alisema Katwaza.
Ofisa Uhusiano wa Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii, Nsachriss Mwamaja alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alisema
kuwa, taarifa zilizotolewa na TFDA ndio hizo za wizara.
"Taarifa ya TFDA ndio ya wizara hivyo zitumieni hizo," alisema Mwamaja.
Kampuni ya Guangdong Med World Pharmaceutical ya
China kupitia serikali ya nchi hiyo, imeahidi kutoa msaada wa dozi
78,000 za dawa hiyo kwa hospitali za serikali ili kupunguza vifo
vinavyotokana na ugonjwa wa malaria."Taarifa ya TFDA ndio ya wizara hivyo zitumieni hizo," alisema Mwamaja.
CHANZO: MWANANCHI



No comments:
Post a Comment