Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea na jitihada zake za kuhamasisha na kuendeleza Taaluma ya Uhasibu nchini kwa kutembelea Baobab Institute of Tanzania iliyopo Mapinga, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, kwa lengo la kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu majukumu ya Bodi pamoja na fursa mbalimbali zilizopo katika Taaluma ya Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu.
Ziara hiyo iliyofanyika Juni 12, 2026, ni sehemu ya programu endelevu ya NBAA ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa vyuo, Taasisi za elimu na shule za sekondari nchini, ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kuhusu shughuli za Bodi, kuhamasisha vijana kujiunga na Taaluma ya Uhasibu na kuwaandaa kwa fursa zinazopatikana katika soko la ajira.
Katika ziara hiyo, maafisa wa NBAA walikutana na wanafunzi pamoja na walimu wa Baobab Institute of Tanzania, Taasisi inayotoa kozi mbalimbali zikiwemo Uhasibu na Fedha. Wanafunzi walipata fursa ya kujifunza kwa undani kuhusu majukumu ya NBAA katika kusimamia, kudhibiti na kuendeleza Taaluma ya Uhasibu na Ukaguzi wa hesabu nchini.
Akizungumza na wanafunzi hao, maafisa wa NBAA walisisitiza umuhimu wa Taaluma ya Uhasibu katika kukuza uchumi wa taifa na kuimarisha uwajibikaji katika Taasisi za umma na binafsi. Waliwahimiza wanafunzi kujenga msingi imara wa taaluma zao kwa kuzingatia maadili, weledi na kujituma katika masomo yao.
Aidha, wanafunzi walipatiwa elimu kuhusu njia mbalimbali za kufikia sifa za kitaaluma za uhasibu, taratibu za usajili wa wahasibu na wakaguzi wa hesabu pamoja na fursa za ajira na maendeleo ya taaluma zinazoratibiwa na NBAA.
Ziara hiyo pia ilitoa fursa kwa wanafunzi kuuliza maswali mbalimbali kuhusu taaluma ya Uhasibu, mahitaji ya soko la ajira, matumizi ya teknolojia katika taaluma hiyo na hatua za kufuata ili kufikia hadhi ya mtaalamu wa Uhasibu. Wataalamu wa NBAA walijibu maswali hayo na kuwahimiza wanafunzi kuendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuongeza ushindani wao katika soko la ajira.
Kwa upande wake, uongozi wa Baobab Institute of Tanzania umeishukuru NBAA kwa kutembelea Taasisi hiyo na kutoa elimu yenye manufaa kwa wanafunzi, ukieleza kuwa ziara hiyo imeongeza hamasa, maarifa na uelewa wa wanafunzi kuhusu taaluma ya uhasibu na mchango wake katika maendeleo ya taifa.
NBAA imeeleza kuwa itaendelea kutekeleza programu za uelimishaji kwa vijana katika taasisi mbalimbali za elimu nchini ili kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kuhusu taaluma ya Uhasibu na fursa zinazopatikana, sambamba na kuchangia upatikanaji wa wataalamu wenye sifa na weledi unaohitajika katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
Picha ya pamoja kati ya Watumishi wa NBAA pamoja na wakufunzi wa Baobab Institute of Tanzania.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya akitoa ufafanuzi kuhusu kazi zinazofanywa na Bodi hiyo wakati wa mafunzo kwa wanachuo wa Baobab Institute of Tanzania.
Mfanyakazi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), Sawa Ngendabanka akizungumzia kuhusu usajili, madaraja mbalimbali ya mitihani ya Taaluma ya Uhasibu na jinsi ya kufanya mitihani hiyo.



No comments:
Post a Comment