Ngwila Daudi
NGWILA Daud (62) ni mkazi wa Kijiji cha Uhambule, Kata ya Igulusi wilayani Mbarali mkoa wa Mbeya ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa ajabu alioupata miaka 15 iliyopita na kusababisha uso wake kuvimba.
Ugonjwa huo uliomuanza mwaka 1997, umefanya watu wake wa karibu wakiwamo ndugu na jamaa kumkimbia kutokana na muonekano wake.
“Kabla sijapata ugonjwa huu nilikuwa nikifanya
shughuli mbalimbali na kujipatia kipato change. Niliweza kuitunza
familia yangu na kuwasaidia ndugu zangu ambao leo wamenikimbia” anasema
Ngwila.
Anasema ugonjwa huo ambao uliumiza vichwa vya
madaktari katika Hospitali tatu; Hospitali ya Rufaa Mbeya, Ilembula
wilayani Njombe na Hospitali ya Igogwe wilayani Rungwe kuutibu, bado
haujapata tiba yake hivyo kumfanya aonekana wa ajabu mbele ya watu
wengine.
“Ulianza kama upele chini ya mdomo,” anaeleza mwanaye Ayoub Mwalugaje kutokana na yeye mwenyewe kushindwa kuzungumza vizuri.”
Kutokana na kushindwa kuzungumza kwa ufasaha,
mwanae Ayoub Mwalugaje ambaye ni mtoto wake pekee alitoa maelezo ya
tangu kuanza kuugua kwa mama yake.
Anasema baada ya mama yake kuanza kuugua, ndugu
zake walimtenga. “Kilichotusadia kuweza kuendesha maisha ni mali na
mifugo iliyoachwa na marehemu baba,” alisema.
Aliendelea “Wajomba zangu wamenitenga mimi na
mama. Inaniuma sana kwa kuwa nyakati za usiku mama yangu huwa na maumivu
makali, anapumua kwa shida, anatokwa damu puani na mate kwa muda mrefu”
anasema Ayoub.
Akisimulia namna anavyohangaika na matibabu ya
mama yake, Ayoub anasema mwaka 2002 alimpeleka katika Hospitali ya
Ilembula, ambako madaktari walidai kuwa wasingeweza kufanya upasuaji
kutokana uvimbe huo kushikana na mishipa.
Anasema baada ya kupata maelezo hayo , alikata
tamaa na kuamua kurudi kijijini. Lakini, mwaka 2005 kuna baadhi ya
marafiki wa marehemu baba yake walimshauri ampeleke katika tiba za jadi.
Anasema alikwenda katika mji wa Mbalizi ambako
alionana na mganga huyo wa tiba za asili (Jina tunalihifadhi).
Alimnywesha dawa mama yake na baada ya wiki moja, uvumbe ulipasuka.
“Baada ya uvimbe kupasuka ilitoka damu nyeusi
zaidi ya lita mbili, aliendelea kuuguza jeraha na baada ya wiki mbili
alipona na kurudi nyumbani huku akiendelea kunywa dawa hizo za
kienyeji”.
CHANZO: MWANANCHI
Anasema uvimbe huo ulipotea kabisa kwa zaidi ya miaka mitatu,
lakini cha kushangaza mwaka 2008 dalili za kuanza upya zilianza
kujionyesha na baadaye ulianza kuvimba upya.
“Kwa kweli hali ile ilitushtua sana, mara moja
tulienda Mbalizi, lakini tulipofika hatukumkuta yule mganga wa kienyeji
na tulipojaribu kuuliza watu wake wa karibu hawakuwa na taarifa sahihi
alipokuwa amekwenda,” anasema Ayoub.
Anasema wakati akiwa katika harakati za kuokoa maisha ya mama yake, baba yake alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Anasema baada ya kumaliza msiba wa baba yake
waliendelea na harakati za kunusuru maisha ya mama yake na safari hii
walimpeleka katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Anasema baada ya uchunguzi wa kina, madaktari
walidai kuwa uvimbe ule umesababisha saratani. Lakini hawakuwa na uwezo
wa kutibu na kumshauri atafute hospitali zenye uwezo wa kufanya kazi
hiyo.
Auza Ng’ombe kupata fedha za matibabu
Anasema baada ya kuuza zaidi ya ng’ombe 10,
alimpeleka mama yake katika Hospitali ya Igogwe wilayani Rungwe na
walipomfanyia uchunguzi walidai uvimbe huo ni tezi na si saratani hivyo
matibabu yake yanahitaji umakini mkubwa.
Anasema maelezo hayo ya wataalamu katika hospitali
hizo, yamefanya kubaki njia panda, kwa kuwa licha ya kuona uvimbe huo
ukimtesa mama yake, ni ugonjwa gani na matibabu yake ni yapi.
“Tumehangaika sana sehemu mbalimbali lakini
hatujapata suluhu, na kwa kuwa tumekuwa tukisikia kuwa Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili kuna watu wanaweza kuifanya uchunguzi wa kina tumeona
tuombe msaada kwa jamii,” anasema Ayoub na anaongeza;
“Naomba Watanzania wenzangu wanisaidie kunichangia
chochote naamini kwa msaada wao nitaweza kujua mama yangu anaumwa nini,
ili aweze kupatiwa matibabu na kupona kabisa.”
Mtu yeyote aliyeguswa na mada hii na anahitaji
kumsaidia, anaweza kuwasiliana kwa simu yake namba 0768 75 37 24 au
kutuma mchango wake wowote.
CHANZO: MWANANCHI



No comments:
Post a Comment