Waziri wa Nishati na Madini,Sospeter Muhongo
SERIKALI imetoa msimamo wake kwamba bei ya umeme
haitapanda kama Shirika la Umeme nchini (Tanesco) lilivyopendekeza,
huku ikiahidi kufanya mabadiliko makubwa ndani ya shirika hilo kuanzia
Januari mwakani.
Imesema lengo la mabadiliko hayo ni kuhakikisha
yanaenda sambamba na kutafuta kampuni nyingine za kuzalisha umeme
nchini ili kuboresha huduma hiyo kwa wateja.
Akizungumza na wadau wa umeme katika Ukumbi wa
Halmashauri wa Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara jana, Waziri wa Nishati
na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema kwamba mapendekezo ya
Tanesco kupandisha gharama za umeme na ambayo Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (Ewura) iliyapokea, hayalengi kutatua matatizo ya
shirika hilo.
Alisema kuwa tatizo ndani ya Tanesco siyo pesa,
bali ni mfumo mbovu wa uendeshaji, ambao unalifanya shirika hilo kuwa
mzigo na kushindwa kutoa huduma bora kwa wateja wake, ikiwa ni pamoja na
kuongeza idadi ya wateja.
“Msimamo wa Serikali ni kwamba, bei haitapanda kwa
kuwa matatizo ya Tanesco yanaeleweka kuwa ni mfumo mbovu,” alisema
Profesa Muhongo na kuongeza:
“Tunategemea kuifumua Tanesco na kuangalia
uwezekano wa kupata kampuni zaidi ya mbili za kuzalisha umeme, maana
mfumo wa menejimenti ni mbovu na umepitwa na wakati.”
Alifafanua kuwa kuanzia Januari mwakani watabadilisha muundo huo ili kupata kampuni ya kuzalisha na ya kusambaza umeme nchini.
Waziri huyo aliongeza kwamba baada ya mabadiliko
hayo, ndipo Tanesco inaweza kutoa maoni ya kuomba kuongeza gharama za
nishati hiyo.
Alisema kutokana na mfumo mbovu ulio ndani ya
shirika hilo sasa, wananchi wengi wameshindwa kutumia nishati ya umeme
na kwamba hali hiyo inachangia kutokukua kwa uchumi.
“Huwezi kutegemea kupanda kwa uchumi kama
uzalishaji wa umeme ni mdogo kwa kuwa hata uzalishaji viwandani
utapungua na wananchi wa kawaida nao hawapati umeme kama inavyotakiwa.
Tunataka kuliboresha shirika hili,” alisema Profesa Muhongo.
Waziri Muhongo pia ametangaza azma ya kuwafukuza kazi vigogo wa shirika hilo watakaoshindwa kutekeleza agizo la Serikali la kuwaunganishia umeme wateja kwa bei ya punguzo.
“Kuanzia Januari mosi mwakani bei ya kuunganisha
umeme inaanza kutumika ya punguzo kutoka 455,108 hadi 177,000 sawa na
asilimia 61.11, kinyume na hapo mtakuwa mmejiachisha kazi,” alisema.
Alisema kuwa watakaoshindwa kutekeleza watafukuzwa kazi bila
barua ya onyo wala kesi na nafasi zao zitazibwa na vijana wasomi ambao
wanazunguka kila kona ya nchi wakitafuta ajira.
“Nasisitiza kwamba asiyeweza kazi awapishe
wanaoweza mapema, maana umeme ni uchumi…, kama Mkoa wa Mara unawatu
takribani 2 milioni, lakini wanaotumia umeme ni watu 18,911 sawa na
asilimia 6 tu,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza:
Katika mkutano huo Profesa Muhongo alishangazwa na
kitendo cha wananchi kutoalikwa wakati wao ndiyo wadau wakubwa wa
nishati hiyo, badala yake walialikwa viongozi wa vijiji, madiwani na
watumishi wa Halmashauri.
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment