HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Yaliyojiri Afrika mwaka huu wa 2012

LEO katika ukurasa huu wa habari za Afrika tunakuletea matukio muhimu ambayo yalitawala katika vyombo mbalimbali vya habari ndani ya mwaka huu kuanzia mwezi Januari.
Ikiwa wewe ni mfuatiliaji wa habari za Afrika hakika utakuwa umesikia  mambo mengi yaliyotokea katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwa ni pamoja na mauaji katika nchi zilizoingia katika machafuko ya muda au muda mrefu.
Mengine yaliyotokea ni baadhi ya wanajeshi kuamua kuwaondoa kinguvu viongozi waliopo madarakani na kuzitawala nchi hizo kimabavu.

Afrika Kusini
Miongoni mwa matukio ambayo yalijiri katika nchi hizo tukianzia na Afrika ya Kusini, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alitangaza maombolezo nchini humo kutokana na mauaji ya wachimbaji madini 38 yaliyosababishwa na polisi wakati wakiandamana kudai kuongezewa mishahara, tukio ambalo lilihuzunisha watu wengi Afrika.
Pia Ellinah Wamukoya ameteuliwa kuwa askofu wa kwanza wa kike wa Kanisa la Anglikana barani Afrika.
Akiongea muda mfupi baada ya kuteuliwa Ellinah Wamukoya alisema kwamba uamuzi huo umeonesha heshima kubwa kwa kina mama.
Tukio lingine kubwa kwa Afrika ni kuhusu mwana mama Ellinah Wamukoya (61) sasa atakuwa  kama askofu mpya wa kanisa hilo katika ufalme wa Swaziland, moja wapo ya nchi zinazokisiwa kufuata siasa za kihafidhina.
Kutawazwa kwake kumejiri huku Kanisa la Anglikana, likitarajiwa kujadili ikiwa kina mama wataruhusiwa kuapishwa kuwa maaskofu wa kanisa hilo.
Askofu wa Jimbo la Captetown, nchini Afrika Kusini, amesema kuwa wamechukua uamuzi huo ili wawe mfano kwa wengine na pia kuwatakia, viongozi wa kanisa hilo, faraja na hekima ili kujadilia suala hilo kwa haraka.
Kwa mujibu wa ripoti aliyotuma kwa vyombo vya habari, askofu huyo wa Jimbo la Capetown, Revd. Thabo Makgoba, amesema wimbi kwa sasa linavuma na kuwa wameshuhudia tukio la kihistoria ambao ni sawa na mbingu kufunguka.
David Dinkebogile aliongoza sherehe hizo na kukariri kuwa nia yao kuwa ilikuwa kumwapisha askofu na wale siyo mtu mweusi, mwafrika na raia wa Swaziland.
Askofu Wamukoya ni meya wa zamani wa mji mkuu wa Swaziland Manzini.

Somalia
Mwaka huu Wabunge wa Somalia waliandika historia ya nchi hiyo, baada ya kufanya uchaguzi uliotawaliwa na amani na kumchagua Hassan Sheikh Mohamud kuwa Rais wa nchi hiyo.
Waliopiga kura hizo ni wabunge pekee ambapo kulikuwa na wagombea 12 wa kinyanganyiro hicho cha kuongoza taifa hilo ambalo linakabiliwa na machafuko ya amani.
Licha ya Mataifa mbalimbali kuipongeza Serikali ya Somalia, kwa kufanya uchaguzi wa amani baada ya kipindi kirefu, Kundi la Al-Shabaab limesema kwamba haliwezi kuitambua serikali hiyo.
Pia  Al-Shabaab wameanza kuuza nyama ya fisi katika mji wa Bandari Kusini mwa Somalia, kama njia ya kukusanya pesa kwa ajili ya kuendesha oparesheni zake za kijeshi.

Nigeria
Pia mwaka huu nchini Nigeria mengi yaliweza kutokea miongoni mwa hayo ni kuhusu wapiganaji wa Boko Haram, waliwaua Wanafunzi 40 kwa kuwapiga kwa risasi. Mauaji hayo ya kusikitisha yalifanyika katika eneo la Mubi, Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Tukio jingine la kuvunja amani nchini humo ni lile watu wenye silaha waliokuwa wamepanda pikipiki, kushambulia nyumba ya Makamu wa Rais wa Nigeria, Namadi Sambo eneo la  Zaria katika jimbo la Kaskazini la Kaduna.  Pia Zaidi ya watu milioni mbili nchini Nageria mwaka huu waliathiriwa na mafuriko ya mvua ambayo ilinyesha katika nchi hiyo.
Mafuriko hayo mabaya ambayo kwa mara ya mwisho yalitokea miaka 50 iliyopita, yalisababisha wananchi kuhama makazi yao na kutafuta maeneo mengine ya kujihifadhi.

Mali
Tukio jingine la kihistoria nchini Mali ni lile la wanajeshi nchini humo walipozingira Ikulu ya nchi hiyo na kumwondoa Rais wao madarakani.
Baada ya kufanya hivyo walipitisha Serikali ya mpito ambayo waliikabidhi madaraka.
Kutokana na hali hiyo Shirika la Kimataifa la Amnesty  lilisema kwamba sasa Mali inaelekea kuingia kwenye mgogoro wa haki za binadamu.
Shirika hilo lilisema kwamba Jeshi limekuwa likijihusisha na uamuzi wa mauaji, mateso na udhalilishaji wa kijinsia tangu mapinduzi ya mwezi Machi.

Guinea- Bissau
Biashara ya dawa za kulevya imedaiwa kushamiri katika nchi ya Guinea Bissau, tangu kufanyika kwa  mapinduzi  mwezi Aprili 12,  mwaka huu.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilionyesha wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa biashara ya hiyo nchini hapo.
Baraza hilo liliwataka  viongozi nchini humo kurejesha utawala wa kikatiba ili kuinusuru na janga la dawa kuzagaa kwa dawa hizo nchini hapo.

Sudan
Wizara ya Afya nchini Sudan ilitangaza kuwa homa ya Manjano ilisababisha vifo vya  watu zaidi ya 32 nchini humo.
Ugonjwa huo ambao awali haukujulikana kama ndiyo ulikuwa chanzo cha vifo hivyo ulisambaa katika miji mikuu ya nchi hiyo ya Darfur na Khartoum.

Ivory Coast
Rais wa Ivory Coast Alassane Outtara, alilivunja Baraza la Mawaziri la nchi hiyo kutokana na mzozo wa sheria ya ndoa.
Chama cha Rais Outtara, kiliunga mkono sheria hiyo lakini viongozi wa upinzani walioko serikalini waliupinga.

KONGO
Wapiganaji wa Kundi la M23 katika Jumhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, waliuthibiti Uwanja wa Ndege wa  Kimataifa wa Goma.
Wapiganaji hao walifanikiwa kuuthibiti uwanja huo baada ya mapigano makali yaliyofanyika dhidi ya vikosi vya jeshi la nchi hiyo.
Katika mapigano hayo ambayo yalisababisha vifo vya watu na baadhi yao kuyakimbia maeneo yao na kuelekea kusikojulikana wakihofia usalama wao.

Algeria
Rais mstaafu wa  Algeria ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa kwa miaka mingi, Chadli Bendjedid, amefariki dunia.
Chadli  ambaye anasifika kwa kuanzisha mfumo wa utawala wa kidemokrasia katika taasisi za kiserikali nchini humo, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 83. Kwa mujibu wa taarifa  Bendjadid, aliaga dunia kutokana na maradhi ya saratani baada ya kulazwa katika Hospitali ya kijeshi ya Ain Naajda mjini Algiers.

Zimbabwe
Taarifa kutoka nchini Zimbabwe zilisema kwamba mchakato wa  kuandaa maoni ya kura mpya huenda usifanikiwe kutokana na kutokuwa na pesa za kutosha nchini Zimbabwe.
Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe ZEC licha ya kwamba iko mbioni kuandaa kura ya maoni kuhusu katiba mpya imekiri kwamba huenda isifanikiwe kutokana na uhaba mkubwa wa fedha.
Pia mwaka huu Waziri Mkuu wa nchini humo  Morgan Tsvangirai sasa ameweka wazi kuwa ndoa yake na Elizabeth Macheka itafungwa Septemba 15.

Ethiopia
Kufariki kwa  Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi, ambapo Mamia ya waombolezaji walijitokeza kuupokea mwili wa kiongozi wao uliowasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia, ukitokea Brussels, Ubelgiji.


Zambia
Rais wa msaafu wa Zambia Keneth Kaunda amelazwa hospitalini wakati mkewa akiwa bado hajazikwa.
Taarifa kutoka kwa familia ya Kaunda zilisema kwamba Kaunda alizidiwa ghafla wakati wa maombolezo ya mkewa Betty, Taarifa zilisema kwamba Kaunda alikimbizwa hospitalini huku mkewe akiwa hajazikwa na huku  bado watu wakiwa katika maombolezo kanisani.

Liberia
Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, amemsimamisha kazi mmoja wa watoto wake wa kiume kutoka ngazi ya unaibu gavana wa benki kuu ya nchi hiyo  na vigogo wengine watano kwa kushindwa kuorodhesha mali zake katika tume ya kuzuia rushwa nchini humo.
Rais huyo alilazimika kumfuta kazi mtoto wake huyo anayefahamika kwa jina la Charles Sirleaf, aliyetajwa kuwa  ni miongoni mwa maofisa 46 walioshindwa kuorodhesha mali zao.

Mexico
Rais mpya wa Mexico Enrique Pena Nieto ameanza kazi ya kuongoza nchi hiyo Juzi Jumamosi, akitoa uwezekano wa kukisafisha chama chake cha Institutional Revolutionary Party PRI, ambacho kimetawala nchini humo kwa muda mrefu.

Malawi
Malawi inapata Rais mpya wa kike  ,Joyce Banda ambaye baada ya kupata wadhifa huo alimfuta kazi Waziri wa Mambo ya nje Peter Mutharika, kaka yake Marehemu Rais Bingu Wa Mutharika aliyefariki dunia mwaka huu.

Ghana
Rais wa Ghana John Atta Mills amefariki ghafla wakati akipata matibabu. Taarifa kutoka ofisi ya rais zilisema kuwa alifariki ghafla baada ya kupelekwa hospitali.
Kwa sasa nafasi yake hiyo imechukuliwa na John Dramani Mahama Kiongozi mpya wa Ghana John Dramani Mahama ameahidi kuimarisha hali ya utulivu nchini humo.

Burkina Faso
Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso amesema nchi yake iko tayari kushiriki katika oparesheni ya kijeshi Kaskazini mwa Mali. Waziri huyo Jibril Bassole alisisitiza juu ya kukombolewa eneo la kaskazini mwa Mali na kusema kuwa wanajeshi wa Burkina Faso wako tayari kushiriki kwenye operesheni hiyo.
Burkina Faso, Niger na Mauritania ni nchi jirani na Mali ambazo zimeathirika zaidi na  mgogoro wa kisiasa, kibinadamu na kiusalama huko kaskazini mwa nchi hiyo.
Kamisheni ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa ilitoa mamilioni ya dola kwa ajili ya kuwahifadhi wakimbizi tangu mwanzoni mwa mwaka huu baada ya raia wa kaskazini mwa Mali kulikimbia eneo hilo na kuelekea katika nchi jirani.


MWANANCHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: