SHONZA, MCHANGE, MWAMPAMBA WATIMULIWA BAVICHA
MBUNGE wa
Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), amekalia kuti kavu kutokana na
kutajwa kuwa anafadhili baadhi ya viongozi wa Baraza la Vijana Taifa la
CHADEMA (BAVICHA) kuleta mgogoro ndani ya chama hicho.
Siri hiyo
ilifichuliwa juzi na baadhi ya vijana hao walipokuwa wakijitetea mbele
ya kikao cha BAVICHA ili kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zikiwakabili za
kutumika kuwachafua viongozi wakuu wa CHADEMA.
Taarifa za
uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zilisema kuwa mmoja wa vijana hao,
Fred Hatari, ambaye ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanachama wa CHADEMA
Vyuo Vikuu (Chaso), alitoa ushuhuda mbele ya Kamati Tendaji ya BAVICHA
kuwa Shibuda amewahi kumwita mara kadhaa na kumpa fedha ili atoe matamko
ya kuchafua viongozi wa chama.
Huku
akionesha ujumbe kadhaa wa simu yake ya mkononi (sms) aliyodai kutumiwa
na Shibuda, mwenyekiti huyo aliiambia kamati kuwa amekutana zaidi ya
mara mbili na mbunge huyo na kupewa fedha ili akatoe matamko sehemu
tofauti ya kumpinga Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, na kusema kuwa ana
kadi ya CCM.
“Fred
aliamua kusema ukweli mbele ya kamati yetu, akaomba asamehewe kwa
maelezo kuwa alifukuzwa Chuo Kikuu kwa kutetea haki, na kwamba alikuwa
akiishi kwa kutangatanga, ndiyo maana alikubali kupokea fedha ya
Shibuda, lakini alikataa kumkashifu Katibu Mkuu,” kilisema chanzo chetu.
Mwenyekiti
wa BAVICHA Taifa, John Heche, alipoulizwa jana kuhusu sakata hili,
alikataa kusema chochote kuhusiana na kikao chao, akisisitiza kuwa
anapanga mkutano na waandishi wa habari ambao atautumia kuweka wazi
ukweli na ushahidi wote alionao.
BAVICHA
iliunda kamati ndogo ya kuchunguza mgongano uliokuwepo baina ya viongozi
wake na hivyo kumteua Mwenyekiti wa baraza hilo Mkoa wa Singida,
Josephat Isango, kuwa mwenyekiti.
Baada ya
kamati hiyo kuwasilisha ripoti yake juzi, baraza hilo lilifanya uamuzi
mgumu wa kuwafukuza baadhi ya viongozi wake akiwemo Makamu Mwenyekiti wa
BAVICHA Taifa, Juliana Shonza na kuwasimamisha baadhi ya wanachama.
Katika kikao
hicho ambacho kilijumuisha wenyeviti wa mikoa yote ya kichama nchi
nzima, Shonza hakuhudhuria badala yake alituma barua akidai kuwa nje ya
Dar es Salaam kwa shughuli za kifamilia.
Makamu
mwenyekiti huyo amekuwa akidaiwa kusigana kimaamuzi na viongozi wenzake,
na hivyo kutoa matamko ambayo wakati mwingine yalikuwa yakikinzana na
msimamo wa chama.
Chanzo chetu
kilifafanua kuwa, baada ya ripoti ya kamati ya uchunguzi kusomwa,
sekretariati ya BAVICHA ilitoa mapendekezo yake kuunga mkono mapendekezo
ya kamati na kisha wakaletwa mashahidi wengine waliokuwa nje ya kikao
ili kuthibitisha kama yaliyosemwa ni ya kweli au la.
Katika
ushahidi uliotolewa, Shonza alibainika kuwa huwa anatumiwa na Shibuda
kutafuta vijana wengine wapokee fedha ili watoe matamko ya
kukifedhehesha chama.
Baada ya
tuhuma hizo kuthibitishwa na kujadiliwa na wajumbe, kura zote ziliazimia
kuwa aondolewe uongozi na kusimamishwa uanachama wa BAVICHA.
Wengine
waliotuhumiwa kushirikiana na Shonza ni waliokuwa wagombea ubunge mwaka
2010 katika majimbo ya Kibaha Mjini (Habib Mchange) na Mbozi Mashariki
(Mtera Mwampamba) ambao pia wamefukuzwa uanachama wa BAVICHA.
Kikao hicho
pia kilichukua uamuzi mgumu wa kuwasimamisha uanachama kwa muda wa mwaka
mmoja, Gwakisa Mwakisando (Mbeya), Wilson Makala (Babati) na Joseph
Kasambala (Mbeya).
Alipotafutwa
na gazeti hili jana jioni kwa simu, Shibuda alikanusha kuhusika na
tuhuma hizo akisema kuwa hata kijana huyo (Fred) hamfahamu.
“Hivi wewe
nikikwambia Shibuda ni baba yako utakubali? Mnapaswa kujiridhisha na
uzushi huo, mimi sijui mambo ya BAVICHA maana si mjumbe huko na sikuwahi
kutumia fedha kumchafua Dk. Slaa kwani sina ugomvi naye,” alisema.
Aliongeza
kuwa hapendi siasa za udaku na chuki, na akaahidi kulifuatilia suala
hilo, huku akidai kuwa kuna watu wanataka kumchafua bila sababu.
Tanzania Daima




No comments:
Post a Comment