Jaji Mstaafu, Joseph Warioba ambaye ni Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba akizungumza na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji
Mstaafu Damiani Lubuva (kulia) jijini, Dar es Salaam jana. Picha na
Juliana Malondo
mwananchi
MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec),
Jaji Mstaafu Damian Lubuva ametoa maoni mbele ya Tume ya Katiba
akipendekeza kuwa Katiba Mpya iunde Tume Huru ya Uchaguzi na kwamba
itambulike kwa jina la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Jaji Lubuva aliyekuwa akitoa maoni hayo kwa niaba
ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, alisema kuwa tume huru ni inayokubalika na
wadau wote wa uchaguzi na wananchi kwa jumla, ambayo katika utekelezaji
wa majukumu yake, itafanya kazi zake bila kuingiliwa.
“Uhuru wa tume utaanzia tangu kwenye jina la tume
yenyewe…; Kubadilishwa kwa jina na kuweka neno ‘Huru’ kunaweza kubadili
fikra za wadau juu ya Tume ya Uchaguzi,”alisema Lubuva.
Lubuva alifafanua kuwa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi, inapaswa kuanzishwa chini ya sheria mama ya nchi ambayo ni
Katiba, kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika.
Alizitaja baadhi ya nchi hizo zilizo na tume huru
za uchaguzi kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, Kenya, Ghana, Zimbabwe na
Botswana.
Alipendekeza pia uteuzi wa wajumbe wa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi ufanywe na wadau mbalimbali na kuteuliwa na rais
kabla ya kuthibitishwa na Bunge. “Na kwa kuboresha mazingira ya
upatikanaji wa wajumbe wa tume hiyo na viongzi wengine tumependekeza pia
Katiba Mpya itamke kwamba wadau mbalimbali watashiriki kupendekeza
majina, ambayo mwisho wake Rais atashiriki kuteua majina, lakini siyo
rais ateue moja kwa moja,” alisema Jaji Lubuva.
Mbali na hayo, Jaji Lubuva pia alipendekeza Katiba
Mpya itambue Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini akataka
isiunganishwe na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika utendaji wake wa
kazi.
“Pia tunapendekeza Katiba iipe Tume Huru ya Taifa
ya Uchaguzi mamlaka ya kugawa kata katika maeneo ya uchaguzi wa
madiwani,” alisema.
Alisema kuwa mamlaka hiyo hivi sasa iko chini ya
Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (Tamisemi), jambo
alilosema lina athari kipindi cha uchaguzi, kwa kuwa huathiri uchaguzi
wa madiwani, ambao hufanywa na Tume.
Ofisi ya Msajili wa Vyama
Akizungumzia utendaji kazi wa Ofisi ya Msajili wa
Vyama vya Siasa pamoja na NEC, Mwenyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi alisema: “Tumependekeza kwamba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa itambulike kikatiba. Tumetaka pia kazi za ofisi hiyo zifanyike kwa
kujitegemea na zisichanganywe na NEC.”
Tangu mwaka 1995 ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa
kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi uliorejeshwa mwaka 1992, NEC
imekuwa ikilaumiwa kuwa siyo huru na kwamba inaegemea chama tawala.
Madai hayo yamekuwa yakitolewa na vyama vya upinzani,
wanaharakati na baadhi ya asasi za kiraia, ambao kwa pamoja walikuwa
wakidai kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi itakayotoka katika mfumo
tofauti na ulivyo sasa ambapo inateuliwa na rais.
Katika hatua nyingine, Jaji Lubava alisema
wamependekeza pia mbunge akihama chama cha siasa, asipoteze haki yake ya
kuwa mbunge kwa sababu yeye amechaguliwa na wananchi.
Jaji Lubava alisema kwamba NEC pia imependekeza
Katiba Mpya iunde mahakama itakayokuwa ikipokea malalamiko kutoka katika
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo itafanya kazi ya kupokea
malalamiko hayo kabla ya uchaguzi kufanyika.
Wakati huohuo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
nayo imetoa maoni yake mbele ya Tume ya Katiba inayokusanya maoni kutoka
kwa taasisi mbalimbali.
Akizungumza baada ya kuwasilisha maoni yao jana,
Kamishna Mkuu TRA, Harry Kitillya alisema kuwa wamependekeza kuwa
misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali kwa kampuni na taasisi
mbalimbali nchini itambulike kikatiba, ili iwe wazi kwa wananchi.
Kitillya alisema kuwa hata taarifa za mawaziri
zinazopelekwa bungeni, zinapaswa kuonyesha matumizi ya wizara husika
zikiambatanishwa na taarifa za misamaha hiyo ya kodi.
‘’Hali hiyo itaongeza ufanisi katika suala la
ukusanyaji wa mapato kwa kuwa taarifa hizo za mawaziri
zilizoambatanishwa na misamaha ya kodi, zitaweza kukaguliwa na Ofisi ya
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serilkali (CAG),’’alisema Kitillya.
Aliongeza kuwa CAG anapaswa kuwa na nguvu kikatiba
ya kwenda kukagua taarifa za misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali
katika kampuni na taasisi binafsi, hali aliyosema italeta uwazi katika
misamaha hiyo kwa wadau mbalimbali.
Kitillya alisema kuwa TRA imependekeza mkwepa
kodi, mla rushwa na mtoa rushwa wapewe adhabu ya kifungo pamoja na
kutaifishwa kwa mali zao kama mkakati wa kujenga taifa la watu wenye
maadili na uaminifu.
Kamishna huyo pia alisema pia kwamba uteuzi wa
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) uendelee kufanywa na
rais, lakini uthibitishwe na Bunge ili kuleta ufanisi zaidi.
‘’Hatusemi kwamba rais apunguziwe madaraka yake,
ila tunaona sasa ni busura kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
akishateuliwa na rais, aweze kuthibitishwa bungeni,’’alisema Kitillya.
Kuhusu ukusanyaji wa kodi katika muungano, TRA
imependekeza katika Katiba ijayo kuwepo na chombo kimoja cha ukusanyaji
kodi katika Jamhuri ya Muungano, ambapo alisema kuwa kinachotakiwa ni
Katiba kuainisha kodi za muungano, ieleze nani atatoza, atazisimamia na
mgawanyo wake uwe wazi ili kuondoa malalamiko kwenye suala la mapato.
H Aidan Mhando, Daniel Wadau mbalimbali wakiwamo wabunge na
wachumi wamekuwa wakipinga misamaha ya kodi isiyo na tija kwa taifa,
ambayo Waziri wa Fedha alipewa mamlaka ya kuitoa aonapo inafaa.
Hatua hiyo imekuwa ikizua mjadala mara kwa mara, huku ikielezwa kuwa inatoa mwanya wa kulihujumu taifa kimapato.
Habari hii imeandikwa na Aidan Mhando, Daniel Mwingira na Matern Kayera
MWANANCHI
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment