MAUAJI YAENDELEA KULITIKISA JIJI LA MWANZA

Mauaji yenye utata yanayohusishwa visasi au umafia yanadaiwa kulitikisa Jiji la Mwanza katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi kadhaa sasa.
 Mauaji hayo yanahusisha vifo vya mfanyabiashara Seni Manumbu (42) na mwandishi wa habari, Richard Masatu pamoja na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Lyimo Barlow (55) ambaye hata hivyo, watuhumiwa wa mauaji yake wamepelekwa mahakamani.

 Marehemu Barlow aliuawa kwa kupigwa risasi shingoni na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, saa 7:30 usiku katika eneo la Minazi Mitatu, Kitangiri, Ilemela jijini hapa wakati akimsindikiza mwalimu Dorothy Lyimo Moses (42) wakitokea kwenye kikao cha harusi.


 Wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti lakini kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, wananchi kadhaa waliliomba jeshi la polisi kurejea kufanya uchunguzi na upelelezi wa kina kuhusiana na mauaji ya Masatu na Manumbu kwani yanachafua sifa ya Jiji la Mwanza.

 Walisema kama imewezekana kuwatia mbaroni watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika kumuua Barlow, inashindikanaje kwa jeshi hilo kuwatia nguvuni watuhumiwa wa mauaji ya marehemu Masatu na Manumbu?


 Walisema ipo haja jeshi la polisi kurejea kufanya upelelezi upya na wa kina kutokana na mazingira ya mauaji hayo.


Kwamba mauaji hayo yanatia shaka ukizingatia vifo vyote vilitokea usiku na mauaji ya Barlow na Manumbu kufanana, kwani wote waliuawa kwa kupigwa risasi na wauaji waliyatekeleza kwa ustadi mkubwa bila ya kujulikana kirahisi.


 Wakati mauaji ya Masatu na Manumbu yanatokea, Barlow alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ambapo awali akitoa taarifa ya kifo cha Masatu, alikiri kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani, kabla ya kubadilisha kauli yake na kudai marehemu huyo aligongwa na gari.

Taarifa hiyo ilikuwa ikipingana na aliyoitoa awali Agosti 10, 2011 pamoja na taarifa ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Masatu.


 Lakini hadi Barlow  anafariki, gari linalodaiwa kumgonga Masatu aina ya Toyota Hiace, halikuwahi kukamatwa mahali popote, jambo linalozidisha imani kwa wananchi kwamba mauaji hayo ni ya kulipiza kisasi.


Masatu alikutwa akiwa hoi hajitambui katika mtaro wa Barabara ya Mwanza -Musoma, eneo la Igoma jirani na Baa ya Ndama. Alivunjwa mguu wa kushoto, alipasuliwa bandama na kifua na wauaji hao, ambapo hakuna kitu kilichochukuliwa kutoka kwa marehemu huyo.

Alifariki akiwa katika hospitali ya mkoa wa Mwanza, Sekou Toure akipata matibabu Agosti 9, mwaka jana.


Kufuatia kifo hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi  Evarist Ndikilo, aliunda tume ambayo pamoja na kuhitimisha uchunguzi wake, hakuna majibu wala taarifa iliyotolewa ni nini ilibaini katika mauaji ya Masatu. 

 
 Aidha, mfanyabiashara Manumbu, aliuawa kwa kupigwa risasi Julai 21, mwaka jana, saa 7:00 usiku katika eneo la nyumbani kwake  Mecco Nyakato, Wilaya ya Ilemela jijini hapa, wakati akirejea nyumbani kwake.


Imeelezwa kuwa marehemu Manumbu  siku ya tukio  aliongozana na mwanaye Manumbu John (21) kwenye gari, baada ya kufika katika lango la nyumba yake, ghafla risasi zilipigwa na kumjeruhi upande wa shavu la kulia, akafariki wakati anakimbizwa kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC).


Mtu au  watu waliohusika kufanya kitendo hicho hawajafahamika hadi leo, hali inayofanya wananchi waamini pia kwamba mauaji hayo ni ya kulipiza kisasi.

 Hata hivyo, kuhusiana wa mauaji ya marehemu Barlow, polisi wamefanikiwa kuwatia mbaroni watu 8 akiwemo mwanamke mmoja na wamepelekwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mwanza.

Mwingine anayekumbukwa kufanyiwa unyama ni aliyekuwa Mbunge wa Mwanza, marehemu Saidi Somari ambaye alimwagiwa tindikali na watu wasiofahamika.


Wakati mauaji hayo yakitajwa kuwa ni ya kulipiza kisasi, wabunge wawili wa Chadema, mwaka jana nao walipewa mkong’oto kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kisasi cha kisiasa.
Wabunge hao ni Mbunge wa Ilemela, Samson Highness Kiwia na Salvatory Machemli wa Ukerewe, ambapo walidai kuwa waliowapiga nia yao ilikuwa ni kuwaua.


Mauaji mengine yanayokumbukwa ambayo watu wanadai ni ya kulipiza kisasi ni ya aliyekuwa dereva teksi, Karoli aliyekuwa akiendesha gari namba T406 BCX, ambaye aliuawa kwa kuchomwa kisu. Alikutwa akiwa anavuja damu mwaka juzi katika mtaa wa Makongoro karibu na Kanisa la KKKT.


Mwingine aliyeuawa kwa kuchomwa kisu Mei 15, 2010 ni aliyekuwa Katibu wa CCM, Kata ya Isamilo, Nyamagana, Bakari Stephano.

No comments

Powered by Blogger.