HABARI

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

MATUKIO

MICHEZO

SIASA

» »Unlabelled » Watu 21 wafa maji Kigoma

Ziwa Tanganyiko 

WATU 21 wanahofiwa kufa maji katika Ziwa Tanganyika, baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupasuka na kuzama baada ya kupigwa na mawimbi.
Taarifa za tukio hilo lililotokea juzi usiku zinaeleza kwamba boti hiyo inayojulikana kwa jina la Yarabi Tunusuru, ilikuwa imebeba abiria 85, ambapo 64 kati yao waliokolewa.
Katika harakati za uokoaji, miili ya watu tisa waliokufa maji iliopolewa na watu 12 hawajulikani walipo huku hofu ikitanda kuwa wamefariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Frasser Kashai alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo akisema ilitokana na uzembe wa kiongozi wa boti, kutosikia malalamiko ya abiria.
Nahodha wa boti hiyo, Akilimali Seif, alisema kuwa walianzia safari yao katika Kijiji cha Kipili mkoani Rukwa, Jumatano iliyopita, kuelekea Mji wa Uvira uliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Alisema kuwa ikiwa njiani, boti hiyo ilikuwa ipitie mji wa Rumonge nchini Burundi, ambako ingeshusha sehemu ya mzigo iliyobeba ambayo idadi kubwa ilikuwa ni chakula.
“Tulianza safari salama tukienda Uvira, DRC kupitia Burundi katika mji wa Rumonge, kupeleka mizigo ya wafanyabiashara. Lakini, hali ilianza kubadilika juzi (Alhamisi),” alisema nahodha huyo na kuongeza:
“Saa nane mchana tukiwa Kijiji cha Kalilani (kilichopo jirani kabisa na Hifadhi ya Taifa ya Mahale), mvua kubwa ilinyesha na mawimbi yakawa makubwa. Kwa kweli siamini kama baadhi yetu tumeokoka.”
Alifafanua: “Kilichosababisha boti yetu ipasuke ni ubishi wa aliyekodi; … Licha ya abiria kumlalamikia wakitaka aegeshe boti ufukweni, yeye alikataa na kulazimisha tuendelee na safari. Matokeo yake mawimbi yakazidi, hadi ilipofika saa nne na nusu usiku injini ya boti ilizimika, ndipo maji yakawa yakiingia.”
Seif aliendelea kuhadithia kuwa maji yaliendelea kutanda kwenye boti na muda mfupi baadaye ilipasuka na kuzama.
Alisema kwamba kabla ya kupasuka, boti hiyo ilikuwa ikisukumwa na mawimbi kuelekea eneo la ufukweni mwa ziwa, ambapo abiria walianza kuweweseka na kila mmoja akawa anatafuta cha kumwokoa.
Kwa mujibu wa Seif, wachache walibahatika kuvaa majaketi ya uokoaji yaliyokuwapo na wengine ilibidi wajaribu kutumia mapipa ya mafuta, matenga ya samaki na magunia ya mihogo.

Alifafanua kwamba abiria waliokuwa wakienda Kigoma, walitakiwa kuteremshiwa eneo la Lubengera, lililopo katika Kijiji cha Kirando wilayani Uvinza, ili wapande mabasi kuelekea Kigoma mjini.
Baadhi ya watu waliookolewa walidai kuwa boti hiyo ilikuwa imebeba zaidi ya tani 45 za bidhaa mbalimbali.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Herembe wilayani Uvinza, Paschal Mpampi, alisema kuwa walisikia kelele kutoka ziwani na kubaini ajali imetokea.
“Tulifanikiwa kuwaokoa watu hao kwa kuwavuta kila walipokaribia ufukweni, ingawa tunasikitika kuona wengi kati ya hao walikufa,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali mstaafu, Issa Machibya, amewataka wananchi wa mkoa huo kuwa na umoja kwa kukataa kusafiri wanapoona hali ya hewa siyo nzuri.
Aidha, amewataka wamiliki kuacha tabia ya kujaza mizigo kupita kiasi na kuzidisha abiria.

 MWANACHI

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments: