Katika
mkutano wa Kumi wa Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Spika wa Bunge ndugu Anna Makinda alitangaza mabadiliko kadhaa ya muundo
wa Bunge katika Kamati mbalimbali za Bunge. Moja ya maamuzi ya Spika
yalikuwa ni kufutwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma
ambayo inajulikana kifupi kama POAC.
Maamuzi haya
yameleta sintofahamu kwa wananchi wengi na wafuatiliaji wa masuala ya
Bunge na Uwajibikaji katika nchi yetu. Ni muhimu tufahamu uundwaji wa
POAC ulitokana na misingi gani na kwamba Uamuzi wa Spika unarudisha
nyuma maendeleo makubwa ya kujenga Bunge imara na lenye meno. Maamuzi ya
Spika ni kinyume cha kanuni za Bunge, sheria ya Ukaguzi na Katiba ya
nchi. Maamuzi ya Spika yanavuruga Bunge,ni ya hovyo na yanapaswa
kupingwa na kila mdau wa Uwajibikaji nchini.
Baada ya
Tanzania kuingia kwenye zoezi la Ubinafsishaji, mashirika mengi ya Umma
yaliuzwa na mengine kufa kabisa. Wakati huo kulikuwa na chombo kinaitwa
SCOPO (Standing Committee on Parastatal Organisations) kwa madhumuni ya
kusimamia uendeshaji wa Mashirika ya Umma. Bunge lilikuwa na Kamati ya
Bunge ya Mashirika ya Umma na kamati hiyo ilifutwa mwaka 1997 kufuatia
hatua za ubanifsishaji na ukweli kwamba Mashirika ya Umma hayatakuwapo
na hivyo hapakuwa na haja ya kuwapo kwa kamati hiyo. Mwenyekiti wa
mwisho wa Kamati hiyo alikuwa ni Mzee William Shelukindo wakati huo
akiwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Mwaka 2007,
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alifanya mkutano wa
Uwajibikaji na kueleza Taifa kuwa kimsingi Mashirika ya Umma bado yapo
na mahesabu yao, kwa kuwa hayaangaliwi, ni mabaya sana nafedha za umma
zinapotea. Pia alieleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ibara ya 143(5) inamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
kutoa taarifa za Ukaguzi za Mashirika ya Umma (Public Authorities and
Other Bodies). Hivyo aliomba Bunge liunde Kamati ya Bunge ya Mashirika
ya Umma ili liweze kupokea, kujadili na kutoa maelekezo kuhusu mahesabu
ya Mashirika ya Umma na kusimamia ufanisi wa Mashirika ya Umma.
Vile vile
alishauri Kamati hiyo isimamie sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya
Umma. Spika wa Bunge wa wakati huo, kupitia Kamati aliyoiunda chini ya
Job Ndugai (wajumbe wengine walikuwa dkt Willibrod Slaa, Beatrice
Shelukindo, Hamad Rashid Mohammed na Nimrod Mkono) wakaunda Kamati ya
Bunge ya Mashirika ya Umma kwa mujibu wa Kanuni za Bunge za Mwaka 2007.
Kamati ya
POAC iliundwa rasmi mwaka 2008 mwezi Februari. Nilipewa dhamana ya kuwa
Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati hii. Sababu za kuanzishwa kwa kamati ya
POAC bado zipo na kimsingi sababu hizo ni za maana sana sasa kuliko
ilivyokuwa kabla.
Majukumu ya
POAC yaliainishwa na sehemu ya tatu ya nyongeza ya nane ya Kanuni za
Bunge toleo la mwaka 2007, kanuni ya 115 (13)(a-e). Majukumu hayo ni
pamoja na kushughulikia mahesabu yaliyokaguliwa ya Mashirika ya Umma,
kuainisha maeneo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za Umma, kutathmini
ufanisi wa Mashirika ya Umma na kufuatilia utekelezwaji wa sera ya
ubinafsishaji wa mashirika ya Umma. Kuanzia mwaka 2008 Mdhibiti na
Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali amekuwa akitoa taarifa za
mahesabu ya mashirika kama Katiba ya nchi inavyomtaka na sheria ya
ukaguzi ya mwaka 2008. Sheria hii imeitaja kamati ya POAC kama moja ya
kamati zenye majukumu ya kuwasilisha Bungeni taarifa ya mwaka ya
mahesabu ya Mashirika ya Umma.
Katika
kipindi cha miaka mitano POAC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa
umahiri na kwa kweli kwa uwazi sana kuliko kamati nyingine zote za
Bunge. Taarifa ya mwisho ya POAC katika Bunge iliyowasilishwa katika
mkutano wa saba wa Bunge, mwezi Aprili mwaka 2012 ulipelekea kutolewa
kwa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ambayo ilisababisha
mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri. Hatua hii ilikuwa ni hatua
muhimu sana katika kuweka mizizi ya utamaduni wa uwajibikaji nchini
kwetu. Wakati Kamati inajiandaa na Taarifa yake ya Mwaka 2012 kwenye
Mkutano wa Kumi na Moja, Spika ameivunja. Ikumbukwe maagizo ya mwisho ya
Kamati ya POAC yalikuwa ni kuzuia mifuko ya hifadhi ya jamii kutoa
mikopo kwa Serikali bila ya kuwapo kwa mikataba. Hivi sasa Serikali
imekopa zaidi ya shilingi 1.2 trilioni kutoka mifuko ya Hifadhi ya Jamii
kwa ajili ya miradi mbalimbali, mikopo hiyo ya fedha za wafanyakazi
haina mikataba yeyote na POAC iliona hatari ya fedha za wafanyakazi
kupotea na kuleta madhara makubwa kwa wastaafu nchini.
Katika
maelezo yake Spika amesema nchi nyingine duniani hazina kamati kama ya
POAC. Nadhani waliomshauri Spika waliamua kumdanganya na yeye
akadanganyika. Nchi zote za Afrika Mashariki zina Kamati ya kusimamia
Mashirika ya Umma. Kenya inaitwa Public Investments Committee, Uganda
inaitwa State Corporations Committee na hata nchi nyingine kama India
ambazo zinafuata utamaduni wa kibunge kama wetu wanayo na wanaita Public
undertakings Committee. Nchini Afrika Kusini sio tu kuna Kamati ya
Mashirika ya Umma bali pia kuna Wizara inayosimamia Mashirika ya Umma
(Ministry of Public Entreprises). Kimsingi Kamati ya POAC ilipaswa
kuongezewa nguvu zaidi ili kufikia uwezekaji wa Serikali kwenye
makampuni binafsi badala ya kuifuta. Uwezekaji wa Serikali kwenye
makampuni kama BP, AirTel, Kilombero Sugar, SonGas nk hauna uangalizi
wowote.
Uamuzi wa
Spika wa Bunge kuifuta Kamati ya POAC ni uamuzi unaorudisha nyuma juhudi
za nchi kujenga asasi za uwajibikaji, ni kinyume cha sheria ya ukaguzi
wa umma inayotaja Kamati tatu za Bunge za kusimamia fedha za Umma na ni
kinyume cha Katiba ya nchi. Spika wa Bunge anasema kazi za Kamati ya
POAC zitafanywa na Kamati ya PAC; Tanzania ina jumla ya Mashirika ya
Umma 258 yenye thamani ya shilingi trilioni 10.2 mpaka mwezi Juni mwaka
2012, hata kamati ya POAC ilikuwa haiwezi kushughulikia Mashirika yote
ya Umma katika mwaka mmoja, PAC itawezaje kusimamia Wizara za Serikali,
Mikoa na wakala za Serikali na wakati huo huo Mashirika ya Umma 258?
Kwa vyovyote
vile Taifa linarudi miaka ya kabla ya 2008 ambapo Mashirika ya Umma
yalikuwa kichaka cha kuiba fedha za Umma. Hivi karibuni Kamati ya POAC
iligundua mtindo wa Wizara za Serikali kupeleka fedha Serikali kwenye
Mashirika na kutumia kifisadi ili kukwepa ukaguzi kwenye Wizara (Wizara
ya Utalii ilipeleka zaidi ya shilingi 600 milioni Bodi ya Utalii mwaka
2010/2011). Ikumbukwe pia wizi wa EPA, MEREMETA na hata uuzaji holela wa
baadhi ya mali za Serikali kupitia ubinafsishaji ulifanyika nyakati
ambazo Bunge halina kamati inayosimamia Mashirika ya Umma.
Kwa vyovyote
vile Spika wa Bunge amedhihirisha namna ambavyo anafanya maamuzi bila
kuzingatia maslahi ya nchi wala kuzingatia historia ya uwajibikaji
katika nchi. Namna mijadala ya Bunge inavyoendeshwa, namna anavyobeba
ajenda za Serikali katika kujenga Bunge kibogoyo na namna anavyofanya
maamuzi kwa kukurupuka, inahitaji hatua za kuokoa misingi ya uwajibikaji
wa nchi. Ni lazima Spika wa Bunge adhibitiwe kwa kuondolewa katika
nafasi hiyo haraka iwezekanavyo. Spika lazima ajue kwamba Mamlaka yapo
kwa wananchi na yeye ni msimamizi tu wa vikao vya Baraza la wananchi
liitwalo Bunge.
Anna Makinda lazima adhibitiwe, vinginevyo nchi yetu itaumia!
No comments:
Post a Comment